Kama sheria zinamnyima mtoto kupiga kura au kuajiriwa, kwanini zimkubalie kuingia kwenye ndoa?

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
Ndoa ni mzigo mzito sana kwa mtoto.jpg


Sheria katika nchi nyingi, ikiwemo Tanzania, zimeainisha umri wa chini wa miaka 18 kama kipimo cha mtu kutostahili kupiga kura. Dhana hii inatokana na imani kwamba hawajakomaa kifikra na kimawazo vya kutosha kufanya maamuzi ya kisiasa. Kwa mtazamo huu, ni kwamba kuna wasiwasi kuhusu uwezekano wa watoto kushawishiwa na watu wazima katika kupiga kura, hivyo kusababisha maamuzi yasiyoendana na maslahi yao.

Vilevile, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 hawapaswi kuingia katika ajira kwani wanahitaji muda wa kujifunza, kukua, na kujenga ujuzi kabla ya kujihusisha katika majukumu ya kazi. Sababu nyingine ni kuhusu hatari ya kudhuriwa au kunyonywa katika mazingira ya kazi, kwani watoto wanaweza kuwa na uwezo mdogo wa kujilinda dhidi ya mazingira yasiyo salama.

Kwa hoja hizi, tunaona kuna suala muhimu la kuzingatia – kuwa tuna jukumu la kuwalinda watoto wetu dhidi ya majukumu mazito kabla ya wakati. Hivyo basi, tukikubali kuwa watoto hawawezi kufanya maamuzi ya ajira au kushiriki katika uchaguzi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kutosha, tunapaswa pia kutekeleza kanuni hii katika suala la ndoa kwa watoto.

Ndoa ni suala linaloweza kuwa na athari za kudumu kwa watoto kwani ni dhahiri kuwa hawana utayari wala uelewa wa kufanya maamuzi kuhusu ndoa, kutekeleza majukumu ya ndoa na ku-deliver matarajio ya ndoa. Ikiwa tuko makini kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya kujihusisha na masuala ya kazi, kwa mfano, pia tunatupaswa kuwalinda dhidi ya hatari ya kuingia kwenye ndoa katika umri mdogo.

Kwa nini tusifikirie umuhimu wa kumpa mtoto muda wa kutosha akue ili aweze kufanya maamuzi ya busara kuhusu ndoa? Kwanini tunaona kuwa binti wa miaka 14 anaweza kuingia kwenye taasisi ya ndoa inayohitaji utashi na uelewa mkubwa wakati anakatazwa mambo mengine yenye uhitaji huohuo? Je, hatuoni hatari ya mtoto huyu kutumiwa vibaya kwa maslahi ya mtu mzima, pengine anayemzidi kwa miaka 30, ambaye tunamuita mume wake?

Kwa muktadha huu, ni dhahiri kuwa ndoa ni uamuzi mkubwa unaoweza kuathiri maisha ya mtoto. Kwa hivyo, ni wajibu wetu kama jamii kuwa na ufahamu wa kina na kutambua kuwa watoto wanastahili kulindwa, kuwezeshwa kukua, na kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao.

Suala la wazazi au walezi kuamua kuwaoza watoto wao kwa sababu zozote zile si sahihi. Ndoa na majukumu yake ni mzigo mzito sana kwa mtoto ambaye tunajua kuwa hana uwezo wa kufanya baadhi ya maamuzi kwa kuwa bado yupo kwenye hatua za ukuaji.

Tanzania, kama nchi nyingine duniani, imeridhia Mkataba wa Haki za Mtoto wa Umoja wa Mataifa. Mkataba huu unalenga kulinda haki na maslahi ya watoto, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata elimu, afya, na kulindwa kutokana na unyanyasaji na unyonyaji. Ni wakati sasa wa kutathmini desturi zisizoendana na haki hizi na kuchukua hatua madhubuti kuondoa changamoto hizi.
 
Una hoja usikilizwe ila nadhani suala la umri liwe miaka 16,hapa itakua imekaa vyema.
 
Back
Top Bottom