Ndoa Yangu

Ndoa Yangu

Hakika yaani inabidi usali na kufunga sana.
Ila wakati mwingine one anakera natamani angekuwa karibu nimpige makofi akili ifunguke kidogo.
Sema mapenzi upofu,one kapofuka kwa atu
mwanaume kama one kumpata kwa dunia ya sasa yataka ufunge na maombi maalum walah
 
Aliambiwa na sultan akamuona hamtaki mema, alipenda vibaya na wivu wake alokua nao
Sasa hivi kampata rose atasahau machungu sipat picha kuhusu atu
halafu ana ma baby kama kumi hivi.
Ila kinachoniuma ni kumsingizia one eti mlevi na anampiga jamani.

Ila one ajifunze mchumba hasomeshwi
 
SEHEMU YA 26

Nilikataa katakata siku hiyo ingawa walinisisitiza lakini sikuwa tayari kabisa. Nilipanga kuishi maisha mapya kabisa ambayo niliamini ingekuwa poozo la maisha yangu. Niliondoka na kurudi kwangu. Lakini kila nilipoingia ndani kwangu nilihisi kumuona Atuganile. Aliniganda kichwani hakunitoka kabisa. Hata nilipolazimisha usingizi ilikuwa tabu kunichukua na uliponivaa basi ndoto kuhisi ndoa yangu na maisha ya Atuganile hazikukoma. Hali ilikuwa hivyo mpaka mwezi unakatika. Niliteswa na fikra zangu kwa mateso ambayo sikuyatarajia. Niliamua kubadilisha hata line ya simu kwani Atu hakukoma kunikebehi kwa jumbe za mapenzi na kunikumbuka mara kwa mara mbali ya kumkalia kimya na kumbrock lakini aliweza kutumia namba tofauti tofauti na kunizidishia kero. Alijua wazo tayari nimemchukia na sipo pamoja naye tena kama alivyonithibitishia kutokuwa pamoja nami. Lakini nilishindwa kuelewa kipi alichokuwa anakitafuta zaidi kwangu? Au aliitaka roho yangu kabisa? Alinikera mno.
Katika mwezi huo wa kwanza sikuweza kabisa kulala kitandani zaidi niliishia kulala kwenye sofa. Hata kwenye ofisi yangu nilishindwa kufungua na kufunga kwa wakati. Nilijikuta nafungua mchana sana kama saa nane na kufunga saa kumi na moja ama kumi na mbili muda ambao ndio biashara ilianza kuchanganya lakini nilijikuta kelele za watoto ambao ndio walikuwa wateja wangu zaidi, zikinipasua kichwa na kunivuruga. Nilijihisi kuuhitaji utulivu wa muda mlefu pasipo gubudha. Sikupenda kabisa kumfikiria Atuganile na nilitamani sana kumsahau haraka lakini nilishindwa sijui kwanini. Kichwa changu kilijikuta kwenye dimbwi la mawazo 'automatic'.
Sulu alijitahidi kunitembelea mara kwa mara na kunishauri niachane na mawazo ya mke kwanza niyatazame maisha yangu lakini nilishindwa kabisa. Mara nyingi moyo ulinipasua na kuuma kila niliposikia sauti ya mwanamke ama kukutana na binti aliyeendana endana na Atuganile iwe kiumbo, sura hata kimuonekano.
Nilijitahidi sana kupambana na hali hii mwilini mwangu na kujikuta nikikonda zaidi siku baada ya siku. Nguo na vitu vyote vilivyomuhusu Atuganile nilivihifadhi sehemu moja na kuvisokomeza uvungu wa kitanda ili nisivione na nivisahau kabisa. Kuna muda nilijikuta nauza mpaka tv, deki na meza yake kwaajili ya kumsahau Atuganile nikiamini nitanunua vyengine vipya vyenye muonekano tofauti. Sijui wazimu gani ulikuwa unanikumba. Niliuza vitu na kushindwa kununua vipya huku ile pesa nikiitumia ovyo pasipo kutimiza kusudio la lengo. Nilipokumbuka tayari pesa iliisha na bado haikuwa sababu ya kunifanya nisahau chochote zaidi ya kukiona chumba changu mwenyewe kama kituo cha polisi. Nilihisi sauti ya Atuganile ikinizomea na kunicheka kila niingiapo. Siku nyengine niliwaota wakinitisha na mamaake usingizini huku wakinicheka. Hapo ndipo nilipojikuta natumbukia kwenye unywaji wa pombe na uvutaji wa bangi tabia ambayo nilikuwa sina kabisa. Niliamini pombe na bangi vitanisaidia kwa namna moja ama nyengine kupata usingizi mzuri usio na mang'amung'amu. Lakini ndio kwanza nilizidi kupoteza uhalisia wangu pasipo kujijua. Dada zangu walikuja mara kwa mara lakini kunipata ilikuwa ngumu hata siku moja walikuja na mama na kunisubiria hadi mishale ya saa tano usiku ambapo nilikuwa narudi nikiwa bwi chakali nayumba. Hakika siku hiyo niliropoka maneno ya aibu na kumuumiza sana mama.
"Mama weeee wee nakupendaa lakiini ume..umeeenipooonzaa mama. Umeeenilazimiiishaaa kuoooaaaa shetaaa...nii eeeh si naweee eeweee dadaaaa mkuuuu? ha ha haaaa" Yalinitoka maneno ya kiloevi na kuwalaumu ndugu zangu. Hata mwenye nyumba naye alinisikitikia sana. Walinijua tabia yangu ilikuwa tulivu mwenye kujali na mcheshi muda mwingi. Walionijua walinionea huruma sana na kunisikitikia. Atuganile alinibadilisha na kuniaibisha kwa kweli.
Sikumbuki siku hiyo muda gani mama waliondoka ama walilala pale lakini nilipokuja kukurupuka saa sita mchana nilishngaa kukuta maombi yakiendelea ndani. Aliletwa mtumishi wa Mungu na kufanya ibada fupi na kukemea mapepo. Kichwa kiliniuma na upole kunivaa. Majuto yalinichukua baada ya maombi ya muda mrefu sana nilihisi kama kuna vitu vinang'oka kichwani mwangu. Mchungaji aliponiwekea mkono na kunikemea nilihisi hali tofauti na kuanza kukiona kichwa kikiwa chepesi mara kizito nakadhalika.
"Onesmo, wewe ni kijana mzuri sana lakini usimuweke Mungu mkono wa kushoto. Inapaswa muda wote Mungu awe mkono wa kuume panapo matatizo ama furaha Mungu ndie awe kimbilio lako. Inabidi jumapili hii ufike kanisani tufanye maombi maalum ya kukemea mapepo yote na vifungo vya kishetani vilivyokuzunguka." alisema mtumishi yule baada ya maombi na kuondoka. Siku hiyo hta mimi nilipashangaa ndani kwangu. Kila kitu kilikuwa shaghala baghala, sikuwa na Tv, deki, meza, hata kapeti la manyoya na sofa kumbe navyo nilishaviuza pasipo kuwa na kumbukumbu lini na nani nilimuuzia. Hakika niliyumba kwa kweli.
Mama alinikumbatia na kusema.
"One mwanangu, dawa kubwa kwako ni kuoa tu baba. Mungu mwenyewe naamini atakuwa radhi kwa hilo. ona mwanangu ulivyobadilika! na vipi kuhusu ofisi yako ya game?"
swali la mama lilinikumbusha na kunifanya nikurupuke muda huohuo kwenda ofisini kwangu ambako tayari ilikatika wiki na siku kadhaa tokea nilipofungua mara ya mwisho.
Asaaaalaaalee! moyo ulistuka kabla ya kufika ofisini kwangu baada ya kukuta watu wengi wamejaa mtaa mzima huku wakitazama ilipo frem yangu na nyenginezo. Walionijua baada ya kuniona walininyooshea vidole huku wengine wakisikitika. Mapigo ya moyo yalizidi kunienda kasi na nilipofika kabisa ndipo sikuamini macho yangu. Ofisi ilikuwa nyeupe pee! fremu ilivunjwa lango wazi na kila kilichokuwa ndani yake mashine zangu za 'game na tv zote walibeba wakiviacha viti pekee. Nilijikuta nikilia kama mtoto kwa hamaniko na staajabiko kuu. Kwanini wamenifanyia hivi? kina nani hao walionitumbukiza kwenye dimbwi kuu la dhiki? ofisi hiyo pekee ndiyo ilikuwa tegemezi na tumaini langu. Ilinisaidia mimi na ndugu zangu pia. Aaaaagh!
Kipindi nikiwa katikati la hamaniko na kilio cha kwikwi ndipo mama mwenye nyumba alipofika na kunisihi kunyamaza na kunipasha habari kuwa si mimi tu kumbe usiku wa jana yake walivamia majambazi na kuvunja kila frem mtaa ule na kuchukua pesa na baadhi ya vitu walivyoona vingewafaa huku wakiwaua watu wawili na baadhi yao wakiwajeruhi na kukimbizwa hospitalini akiwemo baba mwenye nyumba ambaye alijaribu kutete frem yangu isivunjwe. Baada ya maelezo ya mama mwenye frem pia nilitakiwa kufika kituoni kwa agizo waliloacha polisi waliofika asubuhi na kuondoka.
Sikuwa na budi nami nilijumuika polisi na kutoa maelezo kwa vile walivyonihoji na kurudi nyumbani nikiwa mnyonge nimechoka mwili na akili. Nilitamani hata kufa kwa kweli niliona maisha nishayashindwa tena. Yoote haya yasingelinikuta kama si ndoa yangu na Atuganile. Daaah! niliumia na hata nilipofika na kuwasimulia mama na ndugu zangu waliumia pia lakini hawakuacha kunipa moyo wa ushindi.
"Dawa ndio kama alivyosema mama. One kaka huna budi ili kichwa chako kiwe sawa inakupasa uoe tu pia Rose atakufaa amini hivyo."
safari hii kidogo ushauri wao ulianza kuniingia akilini na kutamani kumjua huyo Rose. Jumapili yake nilifika kanisani na familia yangu kwaajili ya maombezi.
Hakika maombi yalianza kunisaidia na kunipa mwangaza wa kujitambua na kupaona kule kubaya nilipokuwa naelekea. Nililaani na kuacha matumizi ya bangi na pombe. Kanisa la yule mchungaji ambaye alikuwa ananifanyia maombi ingawa lilikuwa mbali na tulipokuwa tunaishi kumbe pia ndipo walipokuwa wanasali kina Rose. Na hiyo yote ilikuwa mbinu za wazazi. Kati ya mamaangu na mama Rose pasipo Rose wala mimi kujua.
Miezi mitatu zaidi ilikatika nikiwa sina kazi lakini nikiipata neema ya bwana iliyonijengea tumaini jipya la ushindi maishani. Pale nilipokuwa naishi nilihama na kuhamia uswahilini zaidi tena nyumba ya kiza kwa kukosa uwezo wa kulipia gharama za umeme pia sikuwa na vitu vya matumizi ya umeme. Kanisani nilijikuta naingia katika bendi ya kanisa ya kumuimbia na kumsifu bwana. Sikuwahi kujijua awali kama nilikuwa na kipaji cha kuimba lakini hata mimi nilishangaa kila nilipoimba na kuambwa nina sauti nzuri yenye baraka ndani yake. Niliimba kwa hisia sana hata waumini walionisikiliza walitokwa machozi ya furaha na kumshukuru Mungu kwa hisia kuu. Rose naye alikuwa miongoni mwa waimbaji wazuri sana na kujikuta tukijenga urafiki. Kwa wakati huo tayari mimi nilishamjua kuwa yule ndiye mke ninayeandaliwa na hata mamaake Rose aqlishatambulishwa na kunikubali ingawa babaake Rose bado hakuwa anajua chochote ama kama alishajua kitu basi hakuonesha kwetu wala kusema chochote. Sikuwahi kumtongoza Rose kwa kweli. Lakini siku baada ya siku nilihisi kuanza kumpenda kweli ingawa nilishindana na upendo moyoni mwangu nikidhani yasije jirudia yale yaliyonitokea.
Katika hali ya kushangaza babaake Rose ambaye pia alikuwa kiongozi wa kanisa alizidi kunipenda siku baada ya siku na kutaka kufahamu mengi kuhusu maisha yangu na ndoto zangu. Kitu kikubwa ambacho mama alinisisitiza siku zote ni kusema kweli lakini kasoro kitu kimoja tu! NDOA. Alinikumbusha na kunisisitiza kuwa kamwe nisije mwambia mtu yeyote kama niliwahi kuoa hususani wazazi wa Rose hata marafiki wangu wapya kule. Na hiyo ilikuwa moja ya sababu ya kusali kanisa la mbali zaidi ya kule tulipoishi ambapo tungesali na majirani zetu ambao walikuwa wanajua habari zangu na hivyo ingekuwa kazi nyengine kuweza kumuoa Rose wala isingekubalika kwani mke wangu bado alikuwa hai.
Sijajua kama ulikuwa mpango ama nini lakini nilishangaa kuona baba Rose akizidi niweka karibu hata kuniajiri katika duka lake moja kubwa la jumla la kuuza simu na laptop. Ilikuwa kama ndoto kwangu kwa mshahara wa shilingi laki sita kwa mwezi. Nilishangaa sana mbali ya kuniajiri lakini pia sikuwa mfanyakazi wa kawaida zaidi ya kunipa nafasi za juu za uongozi pale dukani chini ya meneja. Siku ziliposonga ndani ya miezi michache nilihama kule uswazi na kupanga maeneo ya afadhali kidogo ambapo nilianza kuyafufua maisha yangu ya nyuma kwa kununua vitu vya ndani upya.
Na ndipo siku moja baba Rose alifanya tukio lengine la kushangaza zaidi baada ya kunikabidhi kiasi kikubwa cha pesa na kuniambia nitumie kwa kufanya jambo ambalo lipo ndani ya nafsi yangu litalonipa furaha ya maisha yangu ya kidunia.
Alinichanganya sana baba yule. Ilikuwa zaidi ya shilingi milioni tatu za kitanzania. Nilihisi kama ndoto. Mbali na pesa hizo pia aliniahidi kama nikifanya kitu ha kumpendeza Mungu katika jambo hilo basi ataninunulia na gari ya kutembelea.
Sikuwa na wazo lolote akilini mwangu zaidi ya kumpenda zaidi bintiye.
Ingawa kisura na umbo hakuwa mzuri kama Atuganile lakini usoni mwake kila nilipomtazama niliiona nuru ya faraja na upendo wa kweli ambao hakuwahi kunambia. Niliona jambo kubwa la kunifurahisha moyo ni ndoa tu. Ndoa yangu na Rose hakika ndilo nililofikiria. Lakini nilijiuliza je kama nitataka kufanya hivyo je litamfurahisha Mungu ikiwa tayari nilishaoa huku nikisema uongo kuwa sijawahi kuoa? Je, baba Rose naye atakubaliana nami kumuoa bintiye? Kwanini ananisaidia sana na kuniamini huyu baba ikiwa amenijua hata miezi sita bado? Au kuimba tu kanisani? Mmmh! Je, Rose naye atakuwa tayari kuolewa nami? aaaaaaaaah NDOA YANGU
 
SEHEMU YA 27

Mawazo yalitafuna kichwa na mtu niliyejitahidi kumshirikisha siri zangu alikuwa ni Sulu. Ingawa nae kipindi hiko hakuwa jirani na Dar baada ya kusafiri katika biashara zake alizozianzisha alipochukua mafao yake ya mradi wa umeme.
Nilimwambia hali halisi Sulu na kunishauri kuwa niwe makini katika hilo.
"Inaweza kuwa heri kwa namna moja ama ukawa mtihani mwengine endapo uongo mnaoutengeneza ukashindwa kufanya kazi mwisho wa siku. Kuwa makini sana One rafiki yangu nakuombea heri upate maisha ya furaha na mwezi wako lakini usiitengeneze furaha batili kaka." Alinisisitiza zaidi Sulu. Nilikata shauri na nilipomthibitishia mama nia yangu ya kumuoa Rose alifurahi sana na ndipo aliponipasulia kila kitu ambacho nilikuwa sikijui.
"One, mwanangu. Wazazi wote wa Rose wanakupenda. Baba Rose tayari anatamani uwe mkwe wake kabisa na hawana mtoto zaidi ya Rose. Mkewe alimshawishi na kumshauri muda mrefu na anajua mengi kuhusu maisha yako kasoro suala la kuwahi kuoa ambalo usije thubutu kuliropoka kwani ikijulikana hilo hutoweza tena kumuoa Rose wala hakuna kanisa litalokufungsha ndoa mwanangu. Cha msingi hapa tutafute wazee na washenga tufanye taratibu hizo na usisite kumwambia kuwa suala litaloupendezesha moyo wako ni ndoa. Hata yeye atafurahi ingawa haitakuwa vyema umwambie wewe kuwa unataka kumuoa bintiye."
Mama alisema nami nilimuelewa na kumuahidi kuzingatia.
Nyota njema niliiona kuniwakia kila siku ziliposonga. Kanisani nilizidi kuwa maarufu na kupendwa na viongozi mbalimbali wa dini na waumini wenzangu. Sauti yangu ya kumsifu Mungu ilizidi nipandisha chati na kunirahisishia njia kwa Rose hata siku nilipounyanyua ulimi wangu kumueleza ya moyoni mwangu kabla hata hatujapeleka washenga kwao kwa niaba ya kumchumbia na kumuoa kabisa. Mambo yalikuwa mepesi zaidi ya tarajio langu.
"One! usemacho ni kweli katika bwana?"
"Kweli kabisa Rose, nakupenda sana nahitaji uwe wangu wa maisha. Tufunge ndoa tuwe mwili mmoja katika maisha yetu ya hapa duniani mpaka pale kifo kitapotutenganisha. Naomba unikubalie sina janja ya kukwepa wala sina ufundi wa kuzungumza kama mwanasiasa. Nakupenmda sana Rose na nakuhitaji uwe wangu wa maisha. Huo ndio ukweli."
Yalikuwa ni maneno yangu ya ushawishi yaliyomtoa kifungoni Rose ambaye kumbe hata mwenyewe alishanipenda moyoni mwake ingawa ilikuwa ngumu kwake kusema. Kitambo alisubiri na kutamani siku hiyo ifike.
Mawazo kuhusu Atu mchana yalikoma ingawa usiku ndoto kuhusu Atuganile hazikukoma. Sikulitia maanani sana suala la kumuota mara kwa mara Atu mara mamaake zaidi nilipuuzia na kumshukuru Mungu kwa kuanza msahau kwani hakuniumiza kichwa tena na ilishapita miezi sita toka nimuone mara ya mwisho. Sikutaka kujua nini kiliendelea huko kwao wala kujua habari zao. Nilishasamehe kila kitu na kuanza yatengeneza maisha yangu mapya. Kichwani mwangu mwanamke niliyemuweka sasa alikuwa ni Rose ingawa kiukweli hakufikia kile kiwango cha Atuganile moyoni mwangu lakini nilimpenda.
Washenga walienda barua ilipokelewa. Majibu yalirudi kama tulivyotaraji huku nikiwa siamini. Baba ake Rose alikuwa mtu mwenye hekima sana na hakunichukulia kama mkwe tu bali kama mwanae wa kumzaa. Siku hiyo baada ya ibada ya jumapili alinituchukua sote kama familia. Mimi, mama, mkewe na Rose. Safari yetu ilikomea kwenye hoteli moja ya kifahali na hapo tulikula na kunywa kabla hajatwambia kile alichotupelekea pale.
"Kunapo mapenzi ya bwana sisi sote hapa ni wa ndani ya familia moja siku chache zijazo. One kijana wangu na Rose binti yangu. Sisi ni wazazi na zama za leo si zile za zamani. Kipindi mimi namuoa mamaenu hali ni tofauti na hivi sasa. Mambo yamebadilika sana ndio maana nimeshawishika leo kuwaleta hapa ili kama wazazi tujadili mustakabali wenu kabla ya tukio la kuwaunganisha halijafanywa hadharani."
Aliongea baba mkwe mtarajiwa na kutushauri mambo mengi ya msingi huku akiahidi kutununulia nyumba nzuri maeneo ya Mbezi. Hakuwa na mtoto wa kiume na alikuwa na mali nyingi baba Rose. Mimi kuwa mkwewe aliona ni njia sahihi kunizoesha mali zake kwa niaba ya mwanae Rose ambae ndiye mrithi wa haki. Siku hiyo moyo wangu ulibubujikwa machozi ya furaha baada ya dhiki na mateso ya muda mrefu toka kwa mke nyoka Atuganile. Kweli baada ya dhiki faraja. Hatimaye nimepata wakwe wakarimu waso chembe za unafki. Wakwe wacha Mungu. Wakwe wenye pesa. Yaani nilijuta hata sijui kwanini nilikataa habari za Rose mapema na kung'ang'ana kumuoa Atuganile. Tulizungumza tulifurahi na kila mmoja nafsi yake ilijaa matumaini.
Kila nilipofikiria sikuamini kama mimi leo hii naenda kuwa na maisha mazuri ambayo sijawahi kuyaota awali. Ulikuwa ni zaidi ya muujiza kwangu.
Mambo mswano, harusi ilitangazwa na kadi kuchapishwa. Kama alivyoahidi baba mkwe kipindi akinikabidhi zile milioni tatu siku za nyuma kuwa endapo nitafanyia jambo la kumfurahisha Mungu basi ataninunulia gari ya kutembelea. Na ndivyo ilivyokuwa. Gari nzuri aina ya Toyota Rav 4 nilinunuliwa kama zawadi. Yaani naweza sema Rose alikuwa ni mke niliyekuwa napewa bure kabisaaa. Kwani hata mahali iliyoandikwa pesa zilizunguka tui lakini zilitoka kulekule kwa baba mkwe mtarajiwa.
Mungu ni mwema kwa kweli. Maandalizi ya ndoa yakapamba moto na hatimaye tarehe rasmi ya ndoa yangu na Rose ilitangazwa.
********
"One, mimi ndie mkeo lakini mbona kuna kitu unanificha mume wangu?"
"Nakuficha? kitu gani tena?"
"Kwahiyo unajifanya hujui eeh! yaani kukuuguza kote leo hii umepata nguvu ushapanga kuniacha na kwenda kumuoa mwanamke mwengine?"
"Mh! Atuganiole mke wangu mbona unanichanganya?"
"Sio nakuchanganya One! au kwa kuwa sisi masikini eeh! unaniacha kwa kuwa umempata mwanamke toka familia ya kitajiri si ndio?"
"Atuganilee?"
Ndio jina langu. Sasa kaa ujue hakuna mwanamke yeyote wa kumuoa kwa kunificha. Sasa kama unajifanya unayajua sana muoe huyo Rose halafu utaona kitachotokea."
"Wee mpuuzi Atuganile unikome. Si ulinikataa wewe mimi mlevi?!"
"ha ha ha ha haaaa! sasa kama nimekuwa mpuuzi ndio utauona upuuzi wangu."
Nilikurupuka usingizini usiku mkubwa baada ya ndoto mbaya.
Ndoto niliyojiona niko nazungumza na Atuganile katika mazingira yale ya zamani baada ya kuzinduka usingizini na kujiona tuko pamoja. Mazingira ambayo nilikuwa bado sijamuoa Atuganile kiukweli. Mazingira ambayo yalikuwa si ya ulimwengu wa kawaida na mara ya mwisho kuyahama nilijikuta niko hospitalini Kyela.
Nilishika tama na kukaa kitandani baada ya ndoto ile mbaya. Ilikuwa imebaki siku moja tu kabla ya kufunga ndoa na Rose. Nilimlaani shetani na kumuomba Mungu anisimamie ndoa yangu ifanyike salama usalimini.
Saa zilisogea hatimae siku ya siku ikafika. Kila kitu kilipangwa kwa mujibu wa ratiba. Sulu naye alikuwa miongoni mwa waliohudhuria ndoa yangu na kuwa tayari kushuhudia kila kitu ndani ya kanisa ingawa yeye hakuwa miongoni mwetu kiimani. Alikuwa rafiki wa kweli ambaye nilishampoteza kizembe kabla Mungu kumrejesha kimuujiza. Watu wengi walimiminika kanisani wakiwa tayari kushuhudia tukio kubwa la ndoa yangu.
Kwaya maalum ilikuwa tayari kwa kutumbuiza. Magari ya kifahari yaliegeshwa nje ya kanisa. Watu walikuwa wengi zaidi ya matarajio yangu. Hakika baba mkwe aliigharamia ndoa ya bintiye zaidi hata zile gharama tulizoandaa upande wetu. Ukumbi wa kifahari ndani ya hoteli ya nyota tatu tayari ulishakodiwa kwaajili ya sherehe maalum baada ya ndoa kanisani.
Saa sita mchana maharusi tuliwasili kanisani tukiwa na wapambe wetu. Hakika tulipendeza mno. Nilipendeza zaidi na zaidi nilivyopendeza kwenye ndoa yangu na Atuganile. watu pekee waliokuwa kanisani ambao walijua kama niliwahi kuoa awali walikuwa ni mimi mwenyewe, Sulu, mama na dada zangu.
Moyoni nilikuwa na furaha sana baada ya kugundua hakuna pingamizi lolote lililoletwa kanisani baada ya tukio la ndoa yangu kutangazwa kwa zaidi ya wki mbili.
Nilijua sasa naenda kukata mzizi wa fitina ya ile ndoa na Atuganile na hii ya sasa ndiyo itakuwa ndoa yangu rasmi.
Baada ya bendi ya kanisa kutumbuiza kwa nyimbo mbalimbali zilizoandaliwa kwa niaba yetu maharusi hatimaye ulifika muda rasmi sasa wa kutuunganisha pamoja mimi na Rose kuwa mwili mmoja.
Mapigo ya moyo yalienda mbio kadiri mtumishi wa Mungu alipokuwa ananukuu vifungu vya biblia juu ya uumbaji na maisha ya watu wawili kuwa mwili mmoja huku akisisitiza kuwa hakuna kitu kitachoweza kututenganisha zaidi ya kifo.
Lakini tukiwa katikati ya ibada ile tukufu kabla hata hatujaanza kuvalishana pete za baraka ghafla sauti kali za ukelele zilisikika na kumstua kila aliyekuwemo kanisani hadi viongozi wa kanisa.
"PINGAMIZIIIII....PINGAMIZIIIIIII...PINGAMIIIIIZIIIIIII"
Macho ya wote yaligeuka upande wa lango kuu la kanisa. Msafara wa watu sita uliingia kwa kishindo wakipiga hatua kama wanajeshi kuelekea madhahabuni tulipokuwa tumepiga magoti tayari kwa kuunganishwa kuwa mwili mmoja mimi na Rose.
Watu hao walikuwa ni Atuganile, mamaake, baba mdogo, mpambe wa Atuganile kule Iringa sambamba na viongozi wa Kanisa akiwemo yule aliyenifungisha ndoa yangu ya kwanza.
Aaaaaaah! nikiwa katikati ya taharuki kuu nilimshuhudia mamaangu aliyekuwa amesimama mstari wa mbele akikata moto na kuanguka kama mzigo.
Eeeeeeh! Mungu kwanini mimi! aaaahh Ndoaaaa Yanguuu! ni zaidi ya maumivu!!!!!!!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom