Ndoa Yangu

Ndoa Yangu

NDOA YANGU (01)
‘Chozi langu litalipwa’
By; KING T CONTROL

Nilipokuwa mdogo kipindi bado nasoma, nakumbuka maneno aliyokuwa anapenda kunambia marehemu baba. Maneno ambayo awali niliyachukulia mepesi sana kwa kuyanukuu pasipo kuujua uzito uliokuwa ndani yake. Endapo ningeyabeba na kumakinika nayo…. Huenda hadithi hii isingekuwepo kwenye maisha yangu.
Baba alisema....
"Utapokuwa mkubwa usije kuoa mwanamke eti kwa sababu unampenda naye anakupenda…! hapana. Bali oa mwanamke ambaye unamuhitaji na ukahakikisha naye anakuhitaji. Hapo mtaishi vizuri na kujenga familia bora. Kua ukikumbuka haya mwanangu ili usije kukosea kuoa kwani utakuwa umeyakosea kabisa maisha."
Maneno haya ya baba yaliishia kuwa ya baba akilini mwangu wala sijawahi kufikiria kama ipo siku yanaweza kuzitesa hisia zangu na kuuchoma moyo wangu kila nikumbukapo puuzio langu.
Hakika hii ni hadithi ya kweli katika maisha yangu. Hadithi ya NDOA YANGU...... Ingawa yanaweza kuwa ni makosa yangu lakini sikustahili malipo haya. Maumivu makali ya moyo yalizishawishi akili zangu zilipe kisasi lakini imani yangu ndiyo iliyonizua ikinikumbusha kuwa yupo mkuu baba mwenye kutoa hukumu siku ya malipo. Siku ambayo sote tutakuwa wadogo zaidi ya chembe ya punje ya haradali. Kama tunaamini kweli Mungu yupo na ndiye mwenye kuhukumu basi naamini kwa ubaya niliotendwa…….. chozi langu litalipwa.
Karibu kwenye mkasa wangu naamini nawe utajifunza mengi.
*******
Naitwa Onesmo, ni mtoto wa mwisho na pekee wa kiume kati ya watoto watano kwenye uzawa wetu. Nilipokuwa mkubwa baada ya kumaliza kidato cha nne baba alifariki kwa ajali ya gari na kutuachia ukiwa. Maisha yalibadilika siku baada ya siku na kuwa magumu. Dada yangu mmoja tu alibahatika kuolewa huku wengine wakizalishwa wakiwa nyumbani. Hali hii iliniumiza sana. Ndoto yangu ilikuwa kuona siku moja tunaishi maisha mazuri na ya fahari. Mama aliniusia mara nyingi sana kuwa nina mzigo mkubwa kwenye familia yetu, hivyo yanipasa niwe na upeo mkubwa kuweza kuwaongoza dada zangu nikiwa ndiye kaka yao wa pekee.
Hali hii ilinifanya niishi kwa kujituma sana kwenye kazi ingawa nilifeli kuendelea na masomo ya elimu ya juu. Siku zote niliamini kufeli shule sio kufeli maisha.
Nilijituma na kujichanganya kwenye kazi mbalimbali. Sikuchagua kazi ilimradi tu iwe ya halali isiyovunja maadili na utu. Na hapo ndipo nilipojijengea marafiki wengi wanaopenda kujishughulisha. Ni kweli kabisa ukiwa mvivu basi utatengeneza marafiki wengi wavivu. Ukiwa tapeli utawapata marafiki wengi matapeli. Halikadharika ukiwa mwizi vivyohivyo kama ukiwa mpenda kukaa vijiweni basi rafikizo watakuwa wa vijiweni tu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu kupenda kujituma na kufanya kazi ilinijengea kutengeneza marafiki wa tabia zangu. Na ndipo baada ya miaka kadhaa nilijiunga na kampuni moja ya umeme kama kibarua kipindi cha kujenga miradi ya umeme vijijini iliyosimamiwa na REA. Jitihada zangu kwenye kazi ngumu za umeme zilinifanikishia kuujua ujuzi wa kazi yenyewe mara baada ya kudumu kwenye miradi zaidi ya miwili mwishowe nikawa najua kila kitu kuhusu ufundi wa kujenga umeme mkubwa. Tabia yangu ya ucheshi na heshima ikawa kivutio cha kupendwa na kila mtu. Na ndipo viongozi wengi wa ‘site’ waliponizoea na kuniita kwenye miradi mbalimbali hadi pale nilipoajiriwa kwenye kampuni moja iliyoitwa Intercity Builders ltd. Sikuamini punde nilipoletewa barua ya kuajiliwa na kampuni hiyo kama fundi daraja la pili tulipomaliza mradi wa Dodoma.
Taratibu hadithi ya maisha yangu ikaanza kuwa nzuri mara baada ya kufika ofisini na kupewa maelekezo yote. Niliiona nyota njema ya ndoto yangu ikiangaza mbele yangu. Mkataba wangu ulikuwa wa miaka miwili sambamba na mshahara wa laki saba. Haikuwa pesa nyingi kwa wenye nazo, lakini kwa mwenzangu na mimi ilikuwa ni zaidi ya tunu ya ndoto. Kiwango cha mshahara ambao sijategemea kama nitakipata nikiwa na umri ule. Miaka ishirini na nne tu! Hakika ilikuwa furaha si kwangu tu bali kwa familia nzima.
“Mwanangu nakupa baraka zote, kafanye kazi utukumbuke baba kuwa makini sana na matumizi ya pesa unaona hali yetu baba. Nakuombea kila la heri baba uende salama.”
Hayo yalikuwa maneno ya mama siku moja kabla ya safari. Usiku ambao tulikesha kuzungumza mambo mengi sana ya kimaisha. Ilikuwa ndio ajira yangu rasmi ya kwanza na kazi ilikuwa jijini Mbeya.
“Usijali mama, nawaahidi sasa ugumu wa maisha tuliyopitia unaenda kuwa kikomo.”
Nilizingatia moyoni na kumuahidi mama huku nikimtoa hofu.
Alfajiri saa kumi na moja mama na dadaangu walinisindikiza hadi Ubungo nilipokutana na mafundi wenzangu wawili tayari kuelekea kazini mkoani Mbeya. Tuliagana na kujumuika na wenzangu huku moyoni nikiwa mwingi wa matumaini. Nilijua fika sitoweza ufanyia mchezo mshahara wa laki saba kwa mwezi. Kila nilipofumba macho niliziona picha za utajiri wangu baada ya miaka miwili ya mkataba. Daaah! Laiti ningelijua juu ya safari ile ndio itakuwa chanzo cha matukio ya kuumiza maisha yangu? Basi nisingelithubutu kukubali kwenda huko wala kusaini mkataba na kampuni ile. Hakika wao ndio walionifanya nipajua Mbeya kwa mara ya kwanza na kunikutanisha na hasidi wa maisha yangu…………
Oooooh! ! NDOA YANGU
Hakika Chozi langu LitalipwaView attachment 903932
01

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 05

"Onesmo usinichekeshe bwana. Ukweli naomba uelewe kuwa katika kitu ambacho hakijawahi kuwa akilini mwangu wala sina mpango wa kukifikiria basi ni mapenzi sijui mchumba au mume! sijawahi kujihusisha wala sitarajii kwasasa nawaza kusoma tu. Elimu ije kutukomboa. Ila nashukuru kwa kumsaidia mamaangu lakini usitumie hiyo kuwa sababu ya kukupenda ama kukubali ushawishi wako. Hapana! kama nia ya msaada wako kwetu ndiyo hiyo basi naomba kuanzia leo usipeleke chochote kwa mama wala usinitafute tena. Kwaheri." Alikata simu Atuganile na kuniacha kinywa wazi.
Nilimpiga lakini simu ilikatwa. Nilipiga tena nikaambiwa kashaondoka. Nilichoka!
Nilijilaumu kwa haraka zangu za kumwambia yale kwa njia ya simu. Lakini pia sikuwa na budi sababu nilijua mradi unaelekea mwishoni na huenda tukaondoka kabla ya kuonana tena na Atu wangu.
Niliumia lakini sikukoma kumpigia simu kwa ile namba lakini jitihada zangu za kuongea nae ziligonga mwamba kila nipigapo. Ikafika hatua hata nilikuwa namboa yule dada mwenye simu.
"Kakaangu ni vyema tukaheshimiana! unanigombanisha na mpenzi wangu kwa simu zako za mara kwa mara. sasa hadi usiku unapiga simu ikiwa unajua kuwa kina Atuganile nakutana nao mchana. Pia kama atahitaji kuzungumza nawe yeye ndie atapiga. Naomba usinipigie tena mpenzi wangu hanielewi sababu yako."
Aliniwakia siku moja yule dada baada ya kumpigia usiku walau kujua kama kina Atu alionana nao siku hiyo na alimpa ujumbe wangu. Sikuwa na budi zaidi ya kuomba radhi na kuwa mpole. Niliacha kumpigia tena yule dada ingawa moyo wangu ulitamani kujua habari za Atuganile. Muda wote masikio yangu yalikuwa makini pindi simu iitapo niliwahi kuangalia namba ya mpigaji nikihisi Atu amenitafuta tena, lakini haikuwa hivyo.
Huo naweza kuthubutu kusema ndio ulikuwa mwanzo na mwisho wa kuzungumza na Atuganile kwa njia ya simu pindi akiwa shule anasoma.
Siku zikaenda, nikajifunza kumsahau Atuganile kama alivyohitaji mwenyewe.
"Mwanamke mzuri si Atu pekeake ndugu yangu kuna wazuri wengi kuliko yeye. Ni ujinga unavyojikondesha kumfikiria mtu ambae hata mwaka haujafika tokea umemjua. Huyo si riziki yako One achana nae utakufa bure na mawazo ya kupenda ujinga."
Hayo yalikuwa maneno ya Sulu yaliyonichochea ujasiri wa kumsahau Atuganile. Kuna muda nilijiuliza inakuwaje nilimpenda kiasi kile? ilikuwa ajabu kwa kweli.
Miezi ikasonga hatimaye ulibaki mwezi mmoja tu wa mradi kumalizika. Nakumbuka ilikuwa mwanzoni mwa mwezi wa kumi na mbili.
Siku hiyo nikiwa tunamalizia kuunga nyaya. Nikiwa nimeamka mwenye afya kabisa na kujumuika na wenzangu kazini kama kawaida. Nakumbuka vizuri ilikuwa katika kijiji kilekile cha Mtakuja ndani ya Ipinda wilaya ya Kyela mkoani Mbeya. Ilikuwa majira ya saa tatu za asubuhi, Ndio kwanza tulikuwa tumefika 'site'.
Tukiwa tunatembea kuelekea tulipofunga transfoma, ndipo nilishangaa kuona kitu cha ajabu kikitokea mbele yangu. Kitu ambacho kilikuwa kama ndoto ayotayo mtu aliye macho.Ndoto ya ajabu na ya kutisha isiyostahili kuitwa ndoto. Ilikuwa ni hali halisi kabisa kwa maono yangu lakini sivyo ndivyo ilivyokuwa inatokea kwa maono ya wenzangu tuliokuwa pamoja.
Nakumbuka kitu cha kwanza chaajabu nilichokiona eneo tulilokuwa tunapita ambapo kulikuwa na shamba dogo la mahindi yaliyostawi ukijani, niliona ghafla mahindi yote yakipoteza hali ya ustawi wake na kuanza kunyauka kana kwamba yamepigwa na jua kali kupita maelezo. Nikiwa natembea tena huku nazungumza na wenzangu nilishangaa na kujaribu kuipotezea hali ile akilini mwangu nikihisi labda mawenge yangu tu. Lakini ajabu kadri nilivyopiga hatua ndivyo yale mahindi yalivyozidi kunyauka na hatimaye yakaanza kutoweka kabisa mithili ya nailoni iyayukayo kwenye moto.
Nilijikuta nasimama kwa staajabiko la mwaka. Wenzangu waliendelea kusonga mbele wakiwa hawana shaka nami. Bumbuwazi lilinipiga zaidi baada ya kuona hata wenzangu nao wakipotea katika uso wa ulimwengu na kujiona nikiwa mwenyewe ndani ya ulimwengi wa ajabu usiokuwa na kitu chochote chenye uhai wala jani bichi. Ilikuwa sehemu ya jangwajangwa. Sehemu iliyoshiba ukame. Sehemu isiyofaa kuwa makazi ya kiumbe yoyote hai.
Nikiwa naanza kuchanganyikiwa kwa kile kinachotokea kwenye mboni zangu, ghafla sekunde zilezile kwa mbali nilishuhudia ardhi ikipasuka na kuibuka kiumbe wa ajabu sana. Kiumbe wa kutisha akija kwa kasi kule niliko mara tu alipoibuka. Alikimbia mwendo wa kishari. Uso wake mbovu wa umafia ulionesha wazi alikuwa amenilenga kuja nifanyia unyambizi. Lilikuwa ni jitu moja kubwa sana kama jitu la kale. Nywele nyingi timutimu zilishona kichwani mwake huku akiwa kavaa manguo makubwa yaliyofanana na ukame wa eneo zima. Ngozi yake ilishiba mpauko wa jangwa kuonesha yeye si kiumbe wa kawaida. Sikujua kama ni shetani ama jitu la kuzimu.
"SUUULUUUUU"
Niliita kwa sauti kuu nikijaribu kuomba msaada kama kuna mtu ananisikia katika ulimwengu wa kawaida lakini sikusikia majibu yoyote wala kuona dalili za kusaidiwa zaidi ya kushuhudi jitu likizidi kunikaribia.
"Nikizubaa nitakufa kizembe!" Nafsi ilitoa sauti iliyoungwa mkono na viungo vyote vyaq mwili. Kwa ujasiri wa hali ya juu punde yule kiumbe aliponikaribia na kunirukia kwa nguvu nilijikuta namkamata shingo juuu kwa juu huku naye akinikamata shingo na tukaanguka chini kama mafurushi.
Alinikaba kooni nami nikamkaba kooni kisawasawa. Kwa nguvu zangu zote. Niligumia maumivu na kuzidisha kumkaba na yeye.
Kumbe kipindi nadondoka kina Sulu waliniona wakiwa kwenye ulimwengu wa kawaida. Wote walishangaa na kunikimbilia. Walikuta nikitetema mwili mzima mithili ya mtetemo wa simu. mtetemoi ulioweza kuusukuma mwili sehemu moja kwenda nyengine. Wao walinishika na kuniita huku kila mmoja akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa sana.
Lakini kwa ulimwengu nilokuwepo mambo yalikuwa mengine. Nilikuwa katika vita nzito na kile kiumbe chaajabu kilichodhamiria kuinyofoa nafsi yangu.
Tumaini la imani ya kushinda halikuniisha nafsini ingawa maumivu ya kukabwa yalikuwa hayavumiliki. Sikumbuki ilikuwaje baadae kwani nilihisi kupoteza fahamu nikiwa kwenye ulimwengu ule wa ajabu. Lakini kwa hali halisi upande wa kina Sulu walichanganyikiwa na kuwaita viongozi waliokuwa eneo la pili la kijiji wakiendelea kukagua kazi ya mradi. Fomeni wetu akiwa na Injinia aliyekuja siku mbili tu za nyuma walifika haraka sambamba na dereva. Wote walishangaa kwa hali waliyoikuta. Nilikuwa bado kwenye mtetemo wa ajabu mithili ya jenereta.
"Mvueni viatu na mkanda! Chinga leta gari haraka daaah! wee Sulu imekuwajeee?"
Alichanganyikiwa fomeni na kuuliza huku akiwa haelewi wala haamini kile akionacho. Ingawa hayo yote nilikuja kuyajua baadae sana kwa kilichokuwa kinatokea, lakini ukweli ulikuwa kwa muda huo sikuwa nasikia wala kuhisi chochote kwenye ulimwengu. Nilikuwa sehemu tofauti kabisa. Hata walivyonihangaikia hata kuniweka kwenye gari ya kazi na kunikimbiza hospitali sikuwa najua wala kuhisi chochote. Nilikuwa nusu mfu nusu mtu.
Kila aliyesikia juu ya tukio lililotokea asubuhi ile kwa fundi umeme alishangaa sana na aliumia zaidi aliposikia kuwa mpatwa tukio lenyewe ni mimi. Kijana niliyesifika utulivu na heshima. Kila mtu aliyenijua na hata asiyenijua alizijua sifa zangu. Hii iliwatoa machozi wengi na kushika tama pindi nikikimbizwa hospitalini ihali bado sijafa.
Nilifikishwa hospitali ya Ipinda ambapo baada ya daktari kunifanyia uchunguzi alionesha wasiwasi mkubwa. Ingawa nilitundikiwa dripu lakini hali yangu ilizidi kukatisha tamaa. Mwishowe niliacha kutetema na macho yakaanza kubadilika kwa kuingia ndani. Hapo ndipo vilio vilipoanza hospitalini palepale. Hata daktari aliyenipokea alionesha dariri zote za kukata tamaa na kumwambia fomeni kuwa hospitali yake ni ndogo, hivyo ni vyema nipelekwe hospitali ya wilaya Kyela kwa kuwa pale hata mochwali haikuwepo.
Kauli ya daktari kuitaja mochwali ndiyo ilipelekea fomeni atoe machozi na kulia kama mtoto. Daaaah! mafundi wenzangu na vibarua nao kila mmoja alijitenga upande wake akilia kivyake. Walinililia na kushangazwa kwanini nakufa ghafla vile! Nini kinaniua? Yaani tena nakufa katika hatua za mwisho kabisa za kula matunda ya mradi? Hii iliwachoma wengi hasa pale ilipofika gari ya wagonjwa na kubebwa nikiwa nimetulia tuli sitingishiki. Pumzi zangu zilikuwa zinatoka kwa mbali sana tena kwa shida. Hospitali nzima na Ipinda yote ilizizima kwa huzuni huku habari ya tukio langu ikisambaa kwa kasi kama umeme hata kufika shuleni kwa kina Atuganile.
Aaaaaagh! ama kweli mtu ujuae anakupenda kwa dhati na asiyechoka kukusaidia kwenye heri! utamringia kipindi akiwa mzima anasema..lakini ukisikia yu mahututi ama amekata kauli...Lazima nafsi itakusuta kwa upande mmoja utahuzunika na kuyakumbuka mazuri yake yatayokuchoma moyo kwa kutomlipa hisani yake hata kumwambia asante hadi ameondoka. Aaaaaaah Atuganile! hakika mshtuko wako ulikuwa na maana kubwa.
5

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom