Toka Magufuli atoe kauli nimekuwa kimya kumjibu nikiendelea na majukumu mengine jimboni na ya kitaifa. Magufuli hakujibu hoja, na badala yake ametoa kauli zisizokuwa na ukweli wowote dhidi yangu, kauli potofu zikiachwa zitaonekana milele kuwa sahahi. Kwa hiyo nimeamua kesho nizungumze na wanahabari kuweka msimamo wangu wazi ili kuweka rekodi muafaka: Mosi, nitajibu hoja kwa hoja, kwa masuala yote aliyoyasema dhidi yangu. Pili, nitaweka bayana kwanini nimeunga mkono kwa GN ihairishwe kutekelezwa, hoja za msingi zijibiwe na mabadiliko muhimu yafanyike.
JJ
Mheshimiwa Mnyika, wakati tunasubiri ufafanuzi wako, naomba nikupe ushauri wa bure wakati unajiandaa kujibu hoja za Magufuli. Katika majibu yako kwa Magufuli, hoja zako zitapimwa katika mazingira yafuatayo:
Moja, kwamba, kwa Mh. Mnyika, ni haki kwa watanzania wanaoishi maeneo ya vivuko vingine huko mikoani (kama vile pangani), kuongezewa nauli mara kwa mara katika kipindi cha miaka 15 yani (1996 – 201l), lakini sio haki kwa wakazi wa Dar-es-salaam, ingawa wakazi wa mikoani, kiuchumi, wana hali mbaya zaidi ya wale wa DSM.
Mbili, msimamo wako kwamba nauli ibakie kuwa sh. 100, unatokana na hoja yako kwamba tatizo ni usimamizi wa mapato ya kivuko. Na huu ndio utakuwa ni uelewa wa mwananchi wa maeneo kama pangani ambae atakuwa anakusikiliza kama Katibu wa siasa na uenezi wa chama cha siasa anachokiunga mkono, ili kubaini kwanini vivuko vyao nauli zinapanda kila mwaka, wakati wenzao wa Dar-es-salaam, nauli zilibakia kuwa sh. 100 kwa miaka 15.
Tatu, kwa hali ilivyo sasa, nauli ya sh. 200 ni kubwa mno kwa mkazi wa kawaida DSM ukifananisha na nauli y ash. 100 ya awali, lakini kwa kule maeneo kama Pangani, ni sawa tu kwani wao wanaweza kumudu. Hapa wasikilizaji watatilia maanani kwamba Mh. Mnyika ni mtunga sheria na pia ni msimamizi wa utekelezaji wa sheria hizo, ambazo zinatakiwa kuzingatia fairness, equity and justice kwa watanzania wote.
Nne, katika kipindi cha miaka 15 (yani 1996 – 2011), wakati nauli ya Ferry Kigamboni imebakia kuwa shillingi mia, nauli ya daladala (katika kipindi hicho hicho) imeongezeka mara tatu. Lakini kwako binafsi, hili sio tatizo kubwa kama lile la ongezeko la sh. 100 ferry ya kigamboni.
Tano, wasikilizaji watakuwa wanakupima huku wakijaribu kubaini iwapo Magufuli yupo sahihi kwamba unapambana na vita visivyokuwa na maana zaidi ya vita nyingine kubwa zaidi iliyokuwa mbele yenu kama wawakilishi wa wananchi. Wasikilizaji watazingatia masuala yafuatayo kubaini nani yupo sahihi:
a) Katika kipindi hicho cha miaka 15 ambapo nauli ilibakia kuwa sha 100 kwa DSM, huku mikoani ikibadilika mara kadhaa, Bei ya mafuta ya diesel inayotumika kuendeshea ferry imeongozeka mara nne (kati ya mwaka 1996 – 2011). Mwaka 1996, lita moja ya diesel ilikuwa ni sh. 500, leo hii bei ya lita ni sh. 2,000.
b) Halafu haraka haraka watakumbuka takwimu za mfumuko wa bei (kutoka NBS) kama ifuatavyo:
Inflation Figures 2010 - 2011(%)
| Item(s) | 12 month change (2010-2011) |
| 1.Food and non – alcoholic | 22.5% |
| 2.Housing, water, electricity and other fuel | 21.7% |
| 3.Furnishing, housing equipment and routine maintenance of the house | 14.2% |
| 4.Restaurant and Hotels | 11.5% |
| 5.Transport | 10.8% |
Source: NBS
Watazamaji watabaini kwamba, tatizo kubwa la wakazi wa DSM lipo katika bei ya chakula, kodi ya nyumba, mafuta ya taa, umeme na maji. Hapo watagundua kwamba, ingawa inawezekana Mh Mnyika ana hoja, lakini kumbe Magufuli yupo sahihi kwamba anapigana vita visivyo muhimu sana (yani ongezeko la nauli ferry kwa sh. 100), kwani mbali ya nauli ya ferry, hata nauli za mabasi ya kwenda mikoani na daladala za mijini, pamoja na ukweli kwamba zimekuwa zinaongezeka mara kwa mara, lakini hilo sio tatizo kubwa ukifananisha na kupanda kwa gharama za umeme, mafuta, chakula, chakula na kodi ya nyumba.
Watazamaji wengi wataanza kunyanyuka kutoka katika viti vyao baada ya kubaini kwamba kumbe kweli Mh. Mnyika anapigana the "wrong war", unless ni the "right war" kwa sababu za siasa;
Wakazi wengi wa DSM wenye umri wa kukumbuka maisha yalivyokuwa mwaka 1996, tofauti na sasahivi wataendelea kufikiria yafuatayo:
Mwaka 1996, bei ya kilo moja ya sembe ilikuwa ni sh.100. Leo hii (miaka 15 baadae), kilo hiyo hiyo moja ya Sembe ni Sh. 1,000, huku nauli ya ferry ikiongezeka kwa sh mia tu katika kipindi hicho hicho.
Mwaka 1996, kilo moja ya mchele ilikuwa sh. 300. Leo hii kilo hiyo hiyo ni sh. 2,000, huku nauli ya ferry ikiongezeka kwa sh. 100 tu katika kipindi hicho hicho.
Mwaka 1996, kilo moja ya Sukari ilikuwa ni sh. 200, Leo hii kilo hiyo hiyo moja ni zaidi ya Sh.2,000, huku nauli ya ferry ikiongezeka kwa sh. 100 tu katika kipindi hicho.
Wakazi wengi watabaini kwamba, kumbe sakata hili la nauli ya ferry ilitakiwa lichukue sura iliyo kinyume na hali ya sasa kwa maana ya kwamba – kumbe ilitakiwa Mheshimiwa Mnyika na wenzake kina Zungu, Ndugulile, Mtemvu na wengineo, kuwaongoza na kuwahimiza wapiga kura wao wampe pongezi nyingi sana Magufuli kwa sababu, pamoja na kupanda sana kwa gharama za maisha katika kipindi cha miaka 15 (yani 1996 – 2011), bado nauli ya ferry imebakia bei karibia na bure, tofauti na ongezeko la huko mikoani. Wakazi wengi zaidi watajipanga sasa kuwatumeni nyinyi wawakilishi wao kwenda bungeni mwezi Juni kupambana na
Uchumi Uchwara wa Mkullo, na kumbana aje na mikakati itakayopelekea serikali kuja na bajeti itakayosaidia kuwapunguzia wapiga kura wenu, na wananchi kwa ujumla, ugumu ya maisha kwenye maeneo nje kabisa ya shilingi mia moja ya Feri.
Mwisho, wakazi hao wataomba sana kupitia imani zao mbali mbali kwamba, mjadala wa sasa uliojaa siasa kuliko mantiki, usipelekee hali ambayo kivuko cha ferry kitaacha kuwa chini ya usimamizi wa serikali, na badala yake soko huria, kwani wakazi hao kwa urahisi sana wataelewa kwamba iwapo hilo litatokea, basi ongezko la nauli ya kivuko cha ferry litaanza kukimbizana sambamba na bei ya kilo ya unga wa sembe, kama sio kilo ya sukari, mchele, au lita moja ya mafuta ya taa.