*CHUMBUKO LA KUWAOMBEA MAREHEMU KWA WAKATOLIKI*
Kitabu cha wamakabayo ni moja ya vitabu katika agano la kale vinavyoelezea kuwaombea marehemu. Sisi wakatoliki tumekuja kupata urithi wa kuwaombea marehemu kutokana na historia ambayo iliwahi tokea katika kitabu cha wamakabayo *(2Makabayo12:39-45)* kwamba Yuda Makabayo akiwa kiongozi wa wayahudi wakati ule aliongoza kikosi cha wanajeshi wake katika mapambano mnamo mwaka 163BC. Wakati vita ilipoisha, Yuda Makabayo alitoa amri kwa vikosi vyake kuzika wale wanajeshi waliouawa wakati wa mapambano, lakini wakati hao wanajeshi wanajiandaa kuwazika wenzao waliokufa katika mapigano, walipata tambua kuwa walikuwa wamevalia mashanga viunoni waliyoyachukua kutoka katika hekalu la wapagani, wakiamini kuwa yangelikuwa kinga yao dhidi ya maadui. Na ni kwa jinsi hii, tayari sheria ya torati ilishavunjwa na huo uvaaji wa mashanga kutoka katika hekalu la wapagani, hivyo Yuda Makabayo na vikosi vyake waliamua kusali ili kuwaombea wenzao kwa Mungu ili wasamehewe hizo dhambi zao za kuvaa mashanga yaliyochukuliwa kutoka hekalu la kipagani. Na huu ndoo umekuwa mwanzo na msingi katika Biblia na hasa katika imani yetu sisi wakatoliki kuwaombea marehemu.
Pia ukienda katika agano jipya pia utapata kusikiliza mluzi ule ule uliopigwa katika kitabu cha wamakabayo juu ya kuwaombea wafu. Mfano halisi ni katika moja ya barua za mtume Paulo alivyokuwa anamwombea mtu mmoja aliyeitwa, Onesiforo, (2Timotheo1:18), *"Bwana na ampe kuona Rehema machoni pa Bwana siku ile. Na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso, wewe unajua sana."*
Na kadiri ya utafiti ni kwamba hata kwenye makaburi ya zamani huko Roma(catacombs)waumini hapo zamani walikuwa pia wamejiwekea utaratibu wa kusali kwenye hayo makaburi wakiwaombea wenzao waliotangulia mbele ya haki.
Hivyo ndugu zangu tulifanyalo sisi wakatoliki lina mwanzo na msingi wake katika maandiko matakatifu na pia katika mapokeo ya Kanisa.