MZIMU UNAOTABASAMU-21
Kila mtu alibaki akimwangalia baba mwenye nyumba, walitaka kusikia mengi kutoka kwake kwa kuamini kwamba ingeweza kuwasaidia katika upelelezi wao. Mzee huyo alibaki akifikiria mambo mengi, uwepo wa watu hao kutaka kuwaona wapangaji waliokuwa wamepanga katika nyumba hiyo ulimkumbusha mbali.
“Ni kwamba kuna vijana wanne walikuwa wamepanga hapa,” alisema baba mwenye nyumba.
“Kipi kinakufanya kuwa na wasiwasi?”
“Ni kwamba sikuwa nikiwaelewa, nyumba yangu waliifanya kama jumba fulani la vituko. Mara leo anakuja kulala huyu, kesho humuoni, anakuja mwingine, yaani hawakuwa wakieleweka kabisa,” alisema baba mwenye nyumba huku akiwaangalia watu walioku mbele yake.
“Hao vijana wapo wapi sasa hivi?”
“Wamehama. Ilikuwa ghafla sana, yaani wapange nyumba kwa kodi ya mwaka mzima halafu wakae mwezi moja waondoke, ni kitu kigumu sana, si ndiyo?” alisema baba mwenye nyuma na kuuliza swali dogo.
“Ndiyo!”
“Basi wao walifanya hivyo sasa.”
Kila mmoja akaanza kupatwa wasiwasi na vijana hao waliokuwa wamepanga ndani ya nyumba hiyo na kuhisi kwamba inawezekana watu hao wakawa wamehusika katika upotevu wa pesa zile kule benki.
“Una picha zao?”
“Jamani! Sasa niwe na picha zao za nini? Mimi niliangalia pesa tu, hayo mambo ya picha mitandaoni,” alisema mzee huyo.
Akahitaji majina ya vijana hao, hakuwa na majina yao bali alimtambua mtu mmoja ambaye ndiye aliyekuwa amelipa pesa na kusema kwamba angekaa na wenzake hao, mwanaume huyo aliitwa Mike Okwara.
Haraka sana wakakimbilia katika mitandao ya kijamii na kuanza kutafuta picha za mtu aliyekuwa na jina hilo. Waliamini kwamba kwa kijana kama huyo hasa kwa kipindi hicho ambacho mitandao ya kijamii ilikuwa imeshika kasi ilikuwa ni lazima awepo kwenye mitandao hiyo.
Huko, wakakutana na kina Mike Okwara zaidi ya mia moja lakini hawakuonekana kuwa na hofu kwani mzee waliyekuwa naye walikuwa na uhakika kwamba alikuwa akimfahamu vizuri kabisa. Mwanaume huyo akapewa picha za watu hao waliokuwa kwenye mtandao wa Kijamii wa Facebook na kuanza kuangalia picha zao.
Aliangalia picha za watu wengi lakini hakuweza kumuona mtu aliyezoea kumuona ila baada ya kuangalia kwa picha zaidi na zaidi hatimaye akamuona mtu aliyefanana na Mike aliyekuwa akimfahamu kabisa.
“Huyu hapa!” alisema baba mwenye nyumba.
Wakamwangalia kijana huyo, wakaridhika naye, walichokifanya ni kwenda katika ‘information’ zake, wakagundua kwamba alikuwa akisoma katika Chuo cha Yaba Technology kilichokuwa hapohapo jijini Lagos. Hapo wakapata uhakika kwamba Mike alikuwa amehusika katika wizi huo kwani hata chuo alichokuwa akisoma kilikuwa ni cha mambo ya kompyuta, hilo likawafanya kuwa na uhakika zaidi.
Hawakutaka kuchelewa, haraka sana wakaondoka na kuelekea huko, walitaka kufahamu mahali vijana hao walipokuwa. Huko chuo wakaelekea katika ofisi ya mkuu wa chuo na kuanza kumuulizia kijana huyo. Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, akawaambia kuhusu kijana huyo kwamba alimfahamu lakini kitu kilichokuwa kikimtatiza ni mahali alipokuwa kipindi hicho.
“Sijamuona wiki nzima,” alisema mkuu wa chuo.
“Ila tunasikia alikuwa na marafiki zake walipanga nyumba sehemu fulani!” alisema Thierry.
“Ooh! Inawezekana! Ila nafahamu alikuwa na urafiki na watu wengine wanne,” alisema mkuu wa chuo.
“Ni wakina nani?”
Mkuu wa chuo hakuwa na hofu, akawaambia kuhusu watu waliokuwa na urafiki mkubwa na Mike. Hakuishia hapo, kwa kuwa watu hao walitaka kuona hata picha zao, akawaonyeshea katika tovuti ya chuo.
Picha zao zote zilikuwa zikionekana isipokuwa picha ya mtu mmoja tu. Jina lake lilikuwa likionekana vizuri, aliitwa David Armando lakini kwenye suala la picha, hakukuwa na picha yoyote ile.
Hilo liliwachanganya, si wao tu bali hata mkuu wa chuo. Kila mwanafunzi aliyekuwa chuoni hapo kulikuwa na picha yake. Hakujua sababu iliyoifanya picha ya David kutokuonekana katika tovuti ya chuo. Hilo likawapa majibu mepesi kwamba mwanaume huyo alikuwa ameifuta picha yake katika tovuti hiyo kwa kuwa alijua kabisa kuna jambo lingetokea hapo baadaye.
“Tuwatafuteni hawa kwanza, ila kabla ya yote hebu twendeni kwa wale mabosi kule kituoni tukawaulize kuhusu watu hawa,” alisema Thierry.
Hawakuwa na muda wa kupoteza, haraka sana wakaondoka mahali hapo na kwenda kituoni, walipofika huko, wakaonana na wale mabosi wa benki na kuwaonyeshea picha zile walizokuwa wamezipata katika mitandao ya kijamii. Bwana Daniel alipoiona picha ya Tim, akashtuka, alimfahamu kijana huyo vilivyo.
“Ninamfahamu kijana huyu,” alisema Daniel huku akionekana kushtuka.
Hakuwa na jinsi, akawaelezea kila kitu kuhusu kijana huyo kwamba alikuwa mtu aliyemletea wanawake wazuri na kutembea nao. Alikuwa na urafiki naye wa karibu sana lakini hakuwahi kumwambia kitu chochote kile kuhusu pleti aliyokuwa nayo.
“Sasa alijuaje kuhusu hiyo pleti?”
“Sijajua! Sikuwahi kumwambia. Urafiki wetu uliisha ghafla sana, sikumuona tena,” alisema Bwana Daniel huku akiwaangalia polisi.
“Huyu ndiye aliyechukua namba kwenye pleti yako, alichukuaje? Hatujui ila tukimpata itakuwa vizuri zaidi,” alisema Thierry.
Picha za watu wote walizoonyeshewa walizifahamu isipokuwa picha zote na hata Bi Pamela alipoonyeshewa picha ya Mike, alimkumbuka, mtu huyo alijifanya kuwa mchungaji kutoka nchini Ghana. Aliposema hivyo tu, polisi wakafuatilia zaidi na kugundua kwamba kweli mwanaume aliyekuwa amebandikwa picha zake kama mhubiri mashuhuri duniani alikuwa yeye na ule mkutano uliotakiwa kufanyika haukufanyika, uliahirishwa ghafla sana.
Wakawa na uhakika wa kuwapata watu hao ila tatizo lilikuwa moja tu, David hakujulikana mahali alipokuwa. Hilo ndilo lililowachanganya, kama wangefanya kazi ya kuwakamata hao wanne akiwemo msichana Mercy ambaye walihisi kamba alishirikiana nao, ilikuwaje kwa huyo David?
“Ninamfahamu hata nikimuona, ni mpenzi wangu,” alisema Cecilia.
“Ooppss! Sasa tutaipataje picha yake? Wewe hna?”
“Sina! Sikuwahi kumpiga picha, alikuwa akinikwepakwepa tu kufanya hivyo, sikujua sababu, ila leo ndiyo nimejua kwa nini alikuwa akinikwepakwepa,” alisema Cecilia.
Hakuamini kilichokuwa kikiendelea, alimwamini sana David lakini mwisho wa siku mwanaume huyo aliondoka mikononi mwake na kumfanyia jambo lililomfanya kuwa kituoni muda huo. Pamoja na mabaya aliyokuwa ameyafanya, alishindwa kumchukia David, alimpenda kutoka moyoni mwake, hata kama mwanaume huyo alikuwa akiigiza kumpenda lakini bado moyoni mwake alikuwa na nafasi kubwa mno.
Polisi na wapelelezi wakaondoka, wakazichapisha picha zile na kuanza kuwatafuta watu hao. Kitu cha kwanza wakaenda uhamiaji, huko wakashangaa kuona watu wanne wakiwa wamepiga pasipoti kwa siku tatu tofauti na walipoangalia majina, walishangaa kuona ni watu walewale, ila kilichowashangaza, David hakuwepo.
“Huyu David yupo wapi? Mbona anataka kutusumbua huyu?” aliuliza polisi mmoja.
“Nakumbuka yule mwanamke alisema kwamba huyu jamaa ni Mkenya, inawezekana alikwenda kwao,” alisema polisi mmoja.
Mawasiliano baina ya interpol yakafanyika katika ya Nigeria na Kenya. Taarifa walizozipata ni kwamba kijana huyo aliondoka nchini humo miaka mingi iliyopita na kuelekea nchini Nigeria na bahati mbaya ni kwamba hakuwa amerudi mpaka kipindi icho.
“Huyu mtu atatusumbua sana. Hebu tumalizeni kazi na hao wengine. Kwa kuwa uhamiaji wanajua nchi walizokwenda, twendeni huko,” alisema Thierry ambaye alionekana kufanya kazi kubwa kuliko hata Wasauzi waliokuwa wameitwa kwa lengo la kuwatafuta watu hao.
***
Maisha ya David nchini Ujerumani yalikuwa mazuri, alikuwa akipiga stori na Bwana Armando kama rafiki yake wa kipindi kirefu mno. Walikuwa wakizungumza mambo mengi, mzee huyo alikuwa na kazi kubwa aliyotaka kumpa ambayo aliamini kwamba kulikuwa na watu wengi waliyoishindwa.
Hakutaka kumficha, alimgusia hilo tangu kipindi cha nyuma, muda huo alimwambia kwamba alitaka kumpa kazi kubwa ya kumuua kila mtu aliyeonekana kuwa adui katika maisha yake. David akashtuka, hakuamini kusikia kile alichoambiwa, hakuwa ametarajia kwamba mzee huyo alimfanyia kila kitu alichokuwa akikihitaji kumbe dhumuni lake lilikuwa ni kuhakikisha anafanya mauaji.
Hakukubali, alimkatalia mzee huyo, alimwambia kwamba asingeweza kuua kwa kuwa hakuwahi kuua. Hilo Bwana Armando alitegemea kulisikia lakini akamwambia kwamba kila kitu kingefanyika kwa umakini na kamwe asingeweza kugundulika.
Bado David alikuwa akikataa, kwake, kuua lisingekuwa jambo jepesi hata kidogo. Mzee huyo akampa muda na kumwambia ajifikirie na ndani ya siku tatu angehitaji kupata jibu kutoka kwake.
Katika kipindi cha kusubiria majibu hakutaka kumuona akipata tabu, alimfanyia kila kitu alichohitaji, alimpatia kiasi kikubwa cha pesa, mapenzi ya mzee huyo yakawa kwa David, alimchukulia kama mtoto wake wa kumzaa kiasi kwamba mpaka watu wengine wakaonekana kushangaa.
Baada ya siku tatu kumalizika mzee huyo akamkumbushia kuhusu suala lake. Kutokana na kufanyiwa mambo mengi mazuri, David hakuwa na jinsi, hakutaka kumkasirisha mzee huyo hivyo kukubaliana naye kishingo upande kwamba alikuwa tayari kuua.
Hilo likamfanya mzee Armando kufurahi zaidi. Mtu wa kwanza kabis aaliyetamani kuona akiondoka katika dunia hii alikuwa bilionea Msuya wa nchini Tanzania. Bado alikumbuka mzigo wake aliotapeliwa, alikuwa na hasira naye, hakutaka kumuona akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii, ilikuwa ni lazima kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba anauawa haraka iwezekanavyo.
Baada ya siku mbili, David akatumwa nchini Tanzania kwa lengo la kukamilisha mpango huo. Kabla ya kwenda huko, akawekewa sura ya bandia kutoka kwa mtaalamu wa upasuaji, Mchina, Young Lee, sura ambayo alikuwa na uwezo wa kuivua na kuiaa tena.
Haikuishia hapo, akatengenezewa pasipoti nyingine iliyokuwa na jina la Michael Casper raia wa nchini Ujerumani, akapigwa picha na sura yake ya bandia na kisha kuanza safari ya kuelekea nchini Tanzania kwa kupitia Nigeria.
Mipango yake ilikuwa ni kwenda moja kwa moja mpaka Tanzania lakini baada ya kusikia kwamba viongozi wa benki kuu nchini Nigeria walikuwa wamekamatwa kwa kesi ya kushiriki katika wizi wa pesa katika benki hiyo, akaona ni bora apitie huko ili kumjulisha Cecilia kwamba alikuwa pamoja na yeye.
***
Saa 12:46 ndege ya Shirika la Ndege la Emirates ilikuwa ikitua katika Uwanja wa Kimataifa wa Murtala Muhammed uliokuwa Ikeja, Lagos nchini Nigeria. Hali ya hewa ilikuwa ni ya nyuzijoto 33°C, joto kali ambalo ilikuwa ni sawa na jijini Dar es Salaam.
Baada ya ndege kusimama, abiria wakaanza kuteremka na kwenda katika jengo la uwanjani hapo kwa ajili ya kukaguliwa mizigo yao na kuondoka mahali hapo. Wale waliokuwa na makoti ndani ya ndege wakayavua kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, kila mmoja alihisi joto kali mwilini mwake.
David alikuwa miongoni mwa abiria walioteremka kutoka ndani ya ndege hiyo. Mwendo wake ulikuwa ni wa taratibu, hakuyatuliza macho yake, alikuwa akiangalia huku na kule, tabasamu pana lilionekana usoni mwake kiasi kwamba kama mtu yeyote angemwangalia, ilikuwa ni vigumu kugundua kama mtu huyo alikuwa na woga moyoni mwake.
Walipoingia ndani ya jengo hilo na kukamilisha taratibu zote za kukaguliwa, akachukua begi lake, akatoka uwanja wa ndege, akachukua teksi na kuanza kumpeleka katika Hoteli ya Leopard iliyokuwa hapohapo jijini Lagoa.
Mawazo yake yalikuwa kwa msichana Cecilia. Alikuwa msichana mrembo ambaye hakutaka kabisa kuona akimkosa, alimpenda kwa moyo wake wa dhati na hata kitendo cha kuteremka nchini Nigeria ilikuwa ni kutaka kumuonyeshea msichana huyo kwamba bado alikuwa akimpenda japokuwa naye alichangia kumuingiza katika matatizo.
Teksi haikuchukua dakika nyingi ikafika katika hoteli hiyo, harakaharaka akateremka na kuanza kuelekea katika hoteli hiyo ambapo akachukua chumba na kwenda kupumzika. Alifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea kupitia televisheni iliyokuwa chumbani.
Aliona jinsi polisi walivyokuwa wakihangaika kuwatafuta, kila kona nchini humo gumzo lilikuwa ni kuibwa kwa pesa katika benki kuu nchini humo. Kila mtu aliyekuwa akihojiwa alisema lake huku wengine wakidiriki hata kusema kwamba serikali ilicheza mchezo, iliamua kujiibia ili kuwatimua kazi viongozi wa benki hiyo.
Hakutaka kujali. Ilipofika saa mbili asubuhi, akatoka kwenda mitaani, akanunua maua mazuri yaliyokuwa na rangi nyekundu ambayo hutumika kuonyesha upendo mkubwa kwa mtu mwingine na kwenda nayo katika ofisi ya Cecilia kwa lengo la kumuachia.
Hakukuwa na mtu aliyemtambua kama alikuwa yeye. Alikuwa na sura ya bandia, kila mtu aliyekuwa akimuona alijua kwamba alikuwa mgeni. Alipitia vizuizi vyote vya ulinzi na kufika katika ofisi ya msichana huyo. Akakutana na sekretari ambaye akazungumza naye na kumwambia kwamba aliagizwa kuleta yale maua katika ofisi hiyo.
“Nani kakutuma?” aliuliza sekretari huku akimwangalia David.
“Jamaa mmoja anaitwa David. Amesema kwamba nimletee mpenzi wake,” alisema David huku akiwa amesimama kiheshima kabisa.
“Sawa.”
“Una kalamu?”
“Hii hapa,” alisema sekretari na kugawia David kalamu ambapo akaanza kuandika ujumbe. Alipomaliza, akamgawia sekratari.
Sekretari akayachukua maua yale na kuelekea ndani ambapo akayaweka juu ya meza. Sura yake haikuacha kuonyesha mshangao, alijua jinsi wawili hao walivyokuwa wakipendana, je, ingekuwa ni rahisi kiasi gani mpaka muda huo David asijue kilichokuwa kikiendelea na wakati taarifa ilikuwa ikitangazwa kila kona barani Afrika? Akahisi kulikuwa na tatizo, hakutaka kujali sana.
David akaondoka, hakutaka kubaki nchini Nigeria, usiku wa siku hiyohiyo akaondoka kuelekea nchini Tanzania kwa lengo la kuifanya kazi aliyokuwa amepewa na mzee Armand ya kumuua bilionea Msuya aliyekuwa amemtapeli mzigo wake wa madawa ya kulevya.
Alichukua saa kumi akafika nchini Tanzania, akaondoka na kwenda katika Hoteli ya Johanesburg na kutulia hapo. Kichwa chake kikaanza kuifikiria kazi kubwa aliyokuwanayo hapo mbele, alijua fika kabisa kwamba bilionea huyo alikuwa na ulinzi mkubwa, hakujua ni kwa jinsi gani angemfikia lakini alihakikisha kutumia kila ujanja kumfikia mwanaume huyo na kuifanya kazi aliyopewa.