Mzimu unaotabasamu

Madame S

JF-Expert Member
Mar 4, 2015
17,172
34,277
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-01

Mchungaji wa kimataifa wa Kanisa la Revelation lililopo jijini New York nchini Marekani, Gideon Matimya alishtuka kutoka usingizini mara baada ya kusikia mlio wa simu ya mezani iliyokuwa ikiita kwa fujo sebuleni. Alishangaa, kitu cha kwanza kabla ya kuteremka kutoka kitandani ni kumwangalia mkewe, Lucy ambaye naye alishtuka kutoka usingizi na kumwangalia mumewe huyo.
Haikuwa kawaida kwa simu hiyo kuita, ulipita mwezi mzima hawakuwa wameitumia, ilikuwa mbovu na hawakuwa na muda wa kuitengeneza kwa kuwa walikuwa wakitumia simu za mikononi. Kitendo cha simu hiyo kuanza kuita, walishangaa, kitu cha kwanza kabisa ambacho walijiuliza ni siku ambayo waliitengeneza simu hiyo.
Mchungaji Gideon akateremka kutoka kitandani, akatoka chumbani na kuanza kuteremka ngazi. Lucy hakubaki chumbani mule, naye akateremka na kumfuata mkewe huku wote wawili wakionekana kuwa na hofu nzito. Hatua zao zilikuwa za taratibu, walikuwa wakitembea huku wakionekana kuhofia kitu fulani, macho yao hayakutulia chumbani, walikuwa wakiangalia huku na kule kwani walihisi kwamba mbali na wao ndani ya nyumba hiyo, pia kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa akiwatazama.
“Ngriii...ngriii..ngriii...” simu ilindelea kuita mfululizo.
Usingizi wote waliokuwa nao ukakatika, macho yakawa makavu na woga kujaa mioyoni mwao. Walipoifikia simu ile, Mchungaji Gideon akauchukua mkonga wake na kuupeleka sikioni huku akitetemeka kwani alihisi kabisa simu ile haikuwa ya kawaida, ilikuwa ni simu ya hatari, simu iliyotoka kwa mtu hatari.
“Halo...” aliita kwa sauti ndogo iliyosikika kama mtu aliyekuwa na hofu moyoni mwake.
“Halo!” sauti ya upande wa pili ikasikika.
“To whom Am I speaking?” (nazungumza na nani?) aliuliza kwa sauti ya taratibu sana.
“The Smilling Ghost you created.” (mzimu unaotabasamu ulioutengeneza) sauti ya upande wa pili ilijibu.
Mchungaji Gideon akanyamaza, akazidi kutetemeka huku akimwangalia mke wake. Jibu la mtu huyo aliyepiga simu lilimtisha. Hakumjua mpigaji, hakukumbuka kama aliwahi kumtengeneza mtu na kuwa kiumbe kibaya. Katika maisha yake alimwamini Mungu, alimwabudu usiku na mchana na kujitolea katika maisha yake kwamba atamuabudu kwa moyo wake wote mpaka kifo chake.
Aliwawahubiria watu kuhusu kumjua Mungu, aliwaombea na wengine kuokoka na mwisho wa siku kuwabatiza kwa maji mengi. Mtu aliyekuwa amepiga simu alikuwa nani? Na alikuwa akihitaji nini kutoka kwake? Kila alichokuwa akijiuliza, alikosa jibu.
“Unahitaji nini?” aliuliza, kipindi hiki kidogo akatoa sauti iliyokuwa na ujasiri.
“Nilitaka nikwambie kitu kimoja tu kwamba nipo hai, nimeishi maisha ya tabu mpaka kuwa hapa, niliteseka, nililia usiku na mchana, niliumia kwa ajili yako. Jua kwamba sikufa, nipo hai, ninapumua kama unavyopumua,” alisema mtu aliyesikika upande wa pili maneno ambayo yalimchanganya kabisa Mchungaji Gideon.
“Wewe ni nani?”
“Mzimu Unaotabasamu. Mzimu unaotafutwa kila kona katika dunia hii,” alijibu mwanaume huyo.
Hapo ndipo Mchungaji Gideon akamfahamu mtu huyo. Alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa kwa nguvu kubwa duniani kote huku maofisa wa Kijasusi wa CIA wakiwa mstari wa mbele kabisa. Katika orodha ya watu mia moja waliokuwa wakitafutwa kwa udi na uvumba wa kwanza kabisa alikuwa mwanaume huyo. Hakujulikana, hakukuwa na mtu aliyejua sura yake ilifananaje lakini ndiye mtu aliyekuwa akiua watu wengi kila siku duniani.
Alijulikana kama The Smilling Ghost kwa maana ya Mzimu Unaotabasamu, na kwa kuwa hakuwa akijulikana jina lake, hata kwenye orodha hiyo ya CIA waliliandika jina hivyohivyo japokuwa hawakujua mwanaume huyo alifananaje na hakukuwa na mtu aliyejua sababu iliyompelekea kufanya mauaji katika siku ya Jumapili.
“Leo ni Jumapili, huu ni usiku wa kuamkia Jumapili, ina maana unataka kuniua?” aliuliza Mchungaji Gideon huku akianza kuingiwa na hofu kwa mara nyingine.
“Hapana. Nimekupigia simu kukwambia kwamba leo ndiyo siku maalumu ya Mzimu Unaotabasamu kukamatwa. Nahisi baada ya kukamatwa, hakutokuwa tena na mauaji kwa Jumapili ya leo,” alisema mwanaume huyo maneno yaliyozidi kumchanganya zaidi Mchungaji Gideon.
“Unamaanisha nini?”
“Umeangalia stoo?”
“Hapana! Kuna nini?”
“Umeangalia bafuni?” aliendelea kuuliza.
“Hapana. Kuna nini?”
“Hata hukujiuliza kwa nini mbwa wako leo habweki?” aliuliza mwanaume huyo.
Swali hilo lilimfanya Mchungaji Gideon kujiuliza kuhusu mbwa huyo. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea, kila siku usiku mbwa wake aliyempa jina la Bobby alikuwa akibweka mno kuhakikisha nyumba yake inakuwa salama mbali na kamera ndogo za CCTV alizokuwa amezifunga ndani ya nyumba yake.
Siku hiyo alikuwa kimya kabisa, alishangaa, alijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu lakini alikuwa na uhakika kwamba mwanaume aliyekuwa akizungumza naye alifahamu kila kitu. Baada ya kujiuliza kuhusu mbwa huyo, akajiuliza kuhusu huko stoo na bafuni alipokuwa ameambiwa, alihisi kulikuwa na kitu, alihisi kabisa kwamba mwanaume alikuwa amefanya jambo.
“Unataka nini?” aliuliza kwa ukali kidogo.
“Polisi wanaingia hapo dakika chache zijazo. Hakutokuwa na kitu chochote watakachokijua zaidi ya kufahamu kwamba wewe ndiye Mzimu waliyekuwa wakimtafuta kwa miaka kumi na tano, dunia itajua kwamba wewe ndiye mwanaume aliyekuwa akiua kila Jumapili, itajua kwamba wewe ndiye uliyemuua waziri mkuu wa Uingereza, mwanamitindo, Amanda Posh, Mwanamuziki Michael Turner, kwa kifupi, dunia nzima itajua kwamba wewe ndiyo mimi,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.
“Halo..halo..halo..” aliita Mchungaji Gideon lakini simu ilikuwa imekatwa.
Mwili mzima ulikuwa ukitoka jasho, hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima kwenda bafuni na chooni kuona ni kitu gani kilikuwa kimetokea huko. Yeye na mkewe, kwa kasi ya ajabu wakaanza kuelekea bafuni, walipoufikia mlango na kuufungua, hawakuamini walichokiona, maiti ya mwanamke ilikuwa sakafuni, ilichomwa visu vinne kifuani, damu zilikuwa zikitoka huku kwenye paji la uso kukiwa na alama ya msalaba, yalikuwa ni aina ya mauaji yaleyale aliyokuwa akiua mtu huyo aliyekuwa akitafutwa.
Mkewe akaanza kupiga kelele kwa woga, hakuamini alichokuwa akikiona, moyo wake ulikufa ganzi na mwili kumtetemeka. Mchungaji Gideon akachanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka maiti ile kuletwa ndani ya nyumba yake.
Akatoka na kueleka stoo, alipoufikia mlango na kuufungua, akakutana na maiti nyingine ya mtoto iliyokuwa sakafuni. Nayo ilichomwa visu viwili kifuani na kwenye paji la uso kulikuwa na alama ya msalaba, ilikuwa ni aina ya mauaji yaleyale aliyokuwa akiyafanya Mzimu.
“Mungu wangu! Kwa nini mimi?” alijiuliza na kutoka ndani.
Akaelekea katika banda la mbwa, alichokikuta huko ni maiti ya mbwa wake ikiwa chini. Aliuawa kwa kuchomwa visu mfululizo.
Machozi yakaanza kumtoka, hakuamini. Hata kabla hajafikiria ni kitu gani kilikuwa kimetokea, akaanza kusikia mlio ving’ora vya polisi wakija kule ilipokuwa nyumba yake, akazidi kuogopa.
Haraka sana akarudi ndani ya nyumba yake, akamkuta mkewe akiendelea kulia, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Wakati akimchukua mkewe kwa ajili ya kumpeleka chumbani, polisi nao wakapiga teke geti kubwa na kuingia ndani huku wakiwa na bunduki mikononi mwao, tena wengine walikuwa wale polisi waliokuwa na silaha nzito ambao walikuja na gari lao lililoandikwa kwa maandishi makubwa yaliyosomeka S.W.A.T.
Hawakuingia kistaarabu, wakavunja mlango wa sebuleni na kuingia ndani. Walipofika, wakamkuta Mchungaji Gideon akiwa na mkewe, walikuwa wamekumbatiana chini huku wote wakilia kama watu waliokuwa wamefiwa.
“Mpo chini ya ulinzi! Nyanyueni mikono juu,” alisema polisi mmoja huku wakiwanyoonyeshea bunduki, wakatii na kufanya hivyo.
Kabla ya kufungwa pingu, polisi wale wakaanza kuangalia ndani ya nyumba hiyo, tena moja kwa moja wakaelekea stoo na bafuni na kuzikuta maiti hizo, yaani walikuwa kama watu ambao walijua maiti zilipokuwa. Wakawafunga pingu na kutoka nao ndani ya nyumba ile.
“Hatukuua! Hatukumuua mtu yeyote! Mimi ni mchungaji, mnanijua, mimi ni mpaka mafuta wa Bwana, sikumuua mtu yeyote yule,” alijitetea Mchungaji Gideon huku akiwaangalia polisi hao.
“Tumekutafuta sana. Kumbe mchungaji anayeaminika duniani, mpaka mafuta wa Bwana, anayewahubiria watu Neno la Mungu ndiye Mzimu Unaotabasamu tunayemtafuta! Mungu wangu! Kweli dunia imekwisha,” alisema polisi mmoja huku akionekana kushangaa.
Hakukuwa na mtu aliyemsikiliza, wakawachukua na kuwapeleka katika kituo cha polisi hapo kilichokuwa Manhattan jijini New York na kuwatuliza huko huku wakitakiwa kusubiri mpaka asubuhi itakapofika na mambo mengine ya kimahakama kuendelea.
Kukamatwa kwake haikuwa siri hata kidogo, usiku huohuo taarifa zikaanza kupelekwa sehemu mbalimbali kwamba hatimaye Mzimu Unaotabasamu alikuwa amekamatwa. Watu wengi walishtuka na kushangaa baada ya kupewa taarifa kwamba Mzimu wenyewe alikuwa mchungaji Gideon aliyekuwa na kanisa kubwa lililokuwa na washirika zaidi ya milioni moja duniani kote.
Ilipofika majira ya saa 10:15 alfajiri, Mchungaji Gideon akatolewa kutoka katika chumba alichokuwemo na kupelekwa katika chumba kingine kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano. Muda wote alikuwa akilia huku akisisitiza kwamba hakuwa muuaji bali kulikuwa na mtu aliyekuwa ameua na kuzipeleka maiti katika nyumba yake.
Hilo halikusikilizwa. Alipofikishwa ndani ya chumba cha mahojiano, akakalishwa kwenye kiti na kuanza kuhojiwa. Muda wote alikuwa akilia, aliikunja mikono yake kama mtu aliyekuwa akisali, mara kwa mara alikuwa akifanya ishara ya msalaba lakini yote hayo yalionekana kama unafiki machoni mwa polisi waliokuwa ndani ya chumba hicho.
Wakaanza kumuuliza maswali kadhaa. Kila swali alilokuwa akiulizwa, Mchungaji Gideon aliwaambia kwamba hakuwa ameua na hakumfahamu mtu aliyekuwa amezileta maiti zile nyumbani kwake kwani alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Mzimu Unaotabasamu na kuzipeleka maiti zile nyumbani kwake lakini si yeye aliyekuwa amefanya mauaji hayo.
“Fungua hiyo bahasha,” alisema mwanaume aliyekuwa akimuhoji huku akimpa bahasha kubwa ya kaki na kumwambia afungue.
Haraka sana akaifungua. Humo akakutana na picha mbili zikimuonyesha yeye akiwa amesimama nje ya nyumba moja huku mkononi akiwa ameshika kisu kilichokuwa na damu, na ndani ya nyumba hiyo kulikutwa maiti mbili za wanawake ambazo zilichomwa visu vifuani na kuwekewa alama ya msalaba katika paji la uso la kila mmoja.
“Huyu ni nani?” aliuliza polisi yule swali ambalo Mchungaji Gideon alishindwa kabisa kulijibu kwani kila alipokuwa akiiangalia sura ile, alikuwa yeye ila hakukumbuka kama kulikuwa na siku aliwahi kwenda kufanya mauaji yoyote yale.
“Huyu ni nani?” aliuliza polisi kwa sauti ya juu. Badala ya kujibu, Mchugaji Gideon akaanza kulia kwa sauti kama mtoto mdogo huku akisisitiza kwamba hakuua.
 
ERIC SHIGONG
MZIMU UNAOTABASAMU-02

Kila mtu alishangaa, hakukuwa na mtu aliyeamini kama yule mchungaji waliyempenda, aliyekuwa akitenda miujiza huku akiwa na wafuasi zaidi ya milioni moja nyuma yake ndiye alikuwa muuaji aliyekuwa akitafutwa kila kona duniani.
Wengi waliweka vikao kulijadili suala hilo, wengine wakakimbilia katika mitandao ya kijamii na kuandika hisia zao juu ya taarifa hiyo. Washirika wake walichanganyikiwa, walimjua mchungaji wao, alikuwa mtu mkimya, aliyempenda Mungu huku muda wote uso wake ukionekana kuwa na huruma kupita kawaida.
Kile kilichokuwa kimetangazwa hakikuaminika. Wengi walihisi kwamba mchungaji huyo alisingiziwa lakini pia kulikuwa na wengine waliosema kwamba alikuwa muuaji kwani haikuwa mara ya kwanza kwa mchungaji kufanya mauaji, hata miaka ya nyuma kulikuwa na wachungaji wengi waliofanya mauaji kwa kutumia kivuli cha uchungaji.
Washirika wake zaidi ya laki sita nchini Marekani wakaingia mitaani huku wakiwa na mabango na kuishinikiza serikali imuachie mchungaji huyo kwa kuwa si mtu aliyekuwa amefanya mauaji. Walishika mabango makubwa yaliyobeba ujumbe mzito kwamba polisi walikuwa wamemtengenezea kesi hiyo mchungaji wao kwa lengo la kumpoteza kwa kuwa tu huduma yake iliwafikia watu wengi kwa kipindi hicho.
“Police are antichrist. He is not the one who did this,” (polisi ni wapinga Kristo. Si yeye aliyefanya hili) lilisomeka bango moja lililokuwa limeshikwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na mwili mkubwa mithiri ya mtu aliyekuwa akipigana katika mchezo wa sumo.
Maandamano hayo yalikuwa yakifanyika hapo Upper Manhattan lakini baada ya muda yakaanza kutapakaa sehemu nyingine nyingi kama Lower Manhattan, Brooklyn, Washington, Boston, Nevada, Texas na sehemu nyingine nyingi, kote huko watu walikuwa wakiandamana kuhakikisha polisi wanamuachia mchungaji huyo na mkewe ambao hawakuonekana kuwa ndiyo muuaji aliyekuwa akitafutwa.
“Mchungaji Gideon hawezi kuwa Mzimu! Nahisi kuna mtu atakuwa amefanya mipango ili kumpoteza mchungaji huyu,” alisema mwanaume mmoja, alionekana kuwa na hasira mno.
“Kweli kabisa. Hivi kweli mtu anaweza kuwa muuaji halafu akasimame madhabahuni, huyo Mungu atakuwa anamwangalia tu! Hapana! Huyu si muuaji,” alisema mwanaume mwingine.
Kila mtu alimuogopa muuaji aliyejipa jina la Mzimu Unaotabasamu. Alikuwa mtu hatari ambaye kwa kipini cha miaka kumi na tano polisi walikuwa wamehangaika kumtafuta. Alikuwa ni kama muuaji aliyetumia uchawi kwani kuna kipindi polisi waliambiwa kwamba alikuwa sehemu fulani lakini cha ajabu, baada ya dakika chache kwenda huko, hawakufanikiwa kumpata.
Aliwasumbua polisi, aliua watu wengi wakiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza, Bwana Andrew Williamson, mwanamitindo, Amanda Posh, Mwanamuziki Michael Turner na wengine wengi. Hakukuwa mtu aliyekuwa akijua sababu ya watu hao kuuawa kinyama kwani hakuwa amejulikana na hakukuwa na taarifa zozote kujua historia ya muuaji huyo aliyekuwa akisumbua mno kwa kipindi hicho.
Shirika la ujasusi nchini Marekani, CIA lilihangaika dunia nzima kumtafuta mwanaume huyo aliyekuwa akiua kwa kutumia kisu chake na kuziwekea alama ya msalaba maiti zote alizokuwa akizimaliza. Watu waliogopa, viongozi waliishi kwa hofu, matajiri wakaongeza ulinzi kwa kuhisi kwamba mua wowote ule nao wangeweza kuuawa kama walivyouawa watu wengine.
Nchini Marekani, FBI hawakutulia, kila siku walikuwa wakikesha kuhakikisha ulinzi ukidumishwa kila kona lakini cha ajabu kabisa, mkurugenzi wa shirika hilo la kipelelezi nchini Marekani, Bwana Sean Powell naye aliuawa na mwanaume huyo hali iliyowafanya wengi kuhisi kwamba muuaji alikuwa ndani ya shirika hilo.
Kwa miaka mingi walimtafuta bila mafanikio. Ingekuwa ni rahisi sana kujua hata sura yake ili wajue ni kwa jinsi gani wangeweza kumpata au hata kupata alama za vidole vyake, ilikuwa vigumu kupata kitu chochote kile kwani hata alipokuwa akiua, kila sehemu ambayo aliigusa kwa vidole vyake aliifuta kwa kitambaa na wakati mwingine alivalia glovusi kuficha alama za vidole ambazo zingemfanya kugundulika.
Kwa jinsi alivyokuwa akitafutwa kila kona huku akiwa hajulikani hata sura yake, wengi wakamfanisha na muuaji aliyevuma sana jijini California nchini Marekani miaka ya 1960 na 1970 aliyejulikana kwa jina la Zodiac ambaye mpaka leo hii dunia haikufahamu muuaji huyo alifananaje mbali na kumtafuta kila siku sehemu mbalimbali.
Wakati washirika wake wakiendelea kuandamana kuhakikisha kwamba anaachiwa na polisi alipokuwa ameshikiliwa, Mchungaji Gideon alikuwa na majonzi. Moyo wake ulikuwa na huzuni tele, hakuamini kile alichokuwa akikipitia muda huo.
Kama kulia, alilia sana, hakujua maana ya Mungu kumpitisha kwenye jaribu kubwa kama hilo. Kwa kipindi kirefu alimtumikia Mungu, alifuata njia zote alizotakiwa kuzifuata, alimuomba kwa kipindi kirefu na kumtumikia kwa moyo wote, kwa kile kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kuwa kama jaribu moja kubwa ambalo hakuwahi kukutana nalo maisha yake yote.
Hakuona kama angeweza kutoka, kitendo cha kuonyeshewa picha yake akiwa amesimama nje ya mlango huku akiwa ameshika kisu kilichokuwa na damu kilimaanisha kwamba huo ulikuwa ushahidi tosha kwamba yeye alikuwa muuaji. Alilia usiku kucha, hakujua ni kwa namna gani Mungu angeweza kumtoa pale alipokuwa kwani kwa ushahidi huo wa picha tu ulionyesha kwamba yeye ndiye alikuwa huyo mzimu.
“That wasn’t me! That wasn’t me,” (yule si mimi! Yule si mimi) alipiga kelele Mchungaji Gideon huku akilia, moyo wake ulimuuma mno, hapohapo akapiga magoti na kuanza kumuomba Mungu huku akilia.
Mahabusu wote waliokuwa ndani ya sero ile walibaki wakimshangaa huku wengine wakianza kumuonea huruma. Hakukuwa na aliyeamini kama mchungaji huyo ndiye alikuwa muuaji ametafutwa kwa miaka mingi pasipo kugundulika.
Katika kipindi alichoingizwa ndani ya sero hiyo kwa mara ya kwanza, mahabusu wote walimuogopa baada ya kusikia kwamba mchungaji huyo alikuwa Mzimu Unaotabasamu, wakajitenga pembeni kabisa kwani walijua hakuwa mtu wa kawaida lakini baada ya kumuona akisistiza kwamba hakuwa mzimu kama ilivyokuwa ikitangazwa duniani kote, wakamsogelea na kuanza kumfariji.
Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutaka kuzungumza na wakili wake, Bwana Johnson Perr alikuwa kwenye kesi nzito ambayo aliamini kwamba asingeweza kupona, haraka sana wakili akatafutwa na kuanza kuzungumza naye kituoni. Alimwambia ukweli kwamba hakuwa ameua bali huyo muuaji alitaka kumuingiza matatani pasipo kujua chanzo cha kufanya hivyo.
“Ila nilisikia kwamba kuna picha zinakuonyesha ukiwa umeshika kisu!” alisema Perr huku akimwangalia Mchungaji Gideon.
“Ni kweli! Ni mimi lakini nashangaa, sikuwahi kufanya jambo kama hilo hata siku moja,” alisema mchungaji huyo.
“Una uhakika?”
“Ndiyo! Siwezi kukuficha kitu. Mimi ni mtumishi wa Mungu, nimekuwa nikimtumikia Mungu kwa miaka yote hii, sikuwahi kufanya mauaji tangu nilipoingia katika huduma hii! Perr, sikuwahi kufanya mauaji,” alisema mchungaji huku akilia kama mtoto.
Walizungumza mambo mengi na muda wote mchungaji huyo alisisitiza kwamba hakuwa amefanya mauaji hayo. Mpaka anaondoka kituoni hapo bado msimamo wa mchunguaji ulikuwa uleule.
Perr akatoka kituoni na kuelekea nje alipopaki gari lake, akaingia, akaliwasha na kuondoka mahali hapo. Njiani alikuwa akimfikiria mteja wake huyo, hakujua ni jambo gani alitakiwa kufanya, yeye mwenyewe alikuwa na uhakika kwamba hakuwa ameua lakini kilichokuwa kikimshangaza ni juu ya hizo picha zilizomuonyesha mchungaji huyo akiwa na kisu chenye damu mkononi mwake.
Hakurudi nyumbani kwake, akapitia mpaka ofisini kwake ambapo alifanya kazi zake nyingine kwa saa kadhaa na kurudi nyumbani kwake. Alipofika, akafunguliwa geti na mlinzi aliyekuwa amemuweka na kuingia ndani, akaliegesha gari lake na kuelekea mpaka ndani kabisa ya nyumba yake.
Alipofika huko, kitu cha kwanza kabisa ambacho alikiona kutokuwa sawa ni bahasha aliyokutana nayo juu ya meza yake. Kwanza akaangalia huku na kule, mazingira ambayo aliyaacha, yalikuwa vilevile, mabadiliko yaliyokuwepo ni uwepo wa bahasha ile tu.
Alihisi kulikuwa na kitu. Akaichukua na kuifungua. Humo akakutana na karatasi moja ambayo kwa juu iliandikwa ‘Remind him’ iliyomaanisha ‘mkumbushe’ na kwa chini kulikuwa na maneno yaliyosomeka ‘John’s story was amazing. 01059623059T’ ambayo yalimaanisha ‘Stori ya John ilistaajabisha. 01059623059T’.
Hakujua ujumbe huo ulimaanisha nini lakini alijua dhahiri kwamba haukuwa ujumbe wake, inawezekana kabisa ulikuwa ujumbe wa Mchungaji Gideon. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kutoka nje ambapo akamfuata mlinzi na kumuuliza kuhusu bahasha ile.
Alichomjibu ni kwamba kuna mwanaume alifika hapo na gari kubwa la takataka, alikuwa mkusanya uchafu ambaye aliingia mpaka kule kulipokuwa na mifuko ya takataka na kuikusanya, hakuwa amemfuatilia ila alishtukia akiondoka na mifuko ya takataka na kumwambia habari kuhusu Mchungaji Gideon kwamba inawezekana alikuwa akionewa kwamba alikuwa muuaji au alikuwa mwenyewe.
“Tulizungumza sana kuhusu Mchungaji Gideon. Baadaye akasema kwamba kuna kitu ungekiona, mpelekee mchungaji,” alisema mlinzi.
Mpaka kufikia hapo, kwa maelezo yale alikuwa na uhakika kwamba huyo mtu alimaanisha bahasha ile. Hakutaka kuchelewa, siku iliyofuata Perr akarudi kituoni na kumuonyeshea Mchungaji Gideon karatasi ile, alipoisoma, hakukumbuka kitu chochote kile.
“Sijui kitu chochote kile,” alisema mchungaji, hata kwa sura yake tu alionyesha kwamba hakujua chochote.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Kama ungekuwa unafahamu kuhusu hili, ninatumaini kabisa muuaji tungemjua. Hebu jaribu kukumbuka kuhusu hili, ukifanikiwa, tutakuwa tumemjua muuaji. Hakikisha hulali pasipo kuijua hii stori ya John na hizi namba. Jitahidi sana,” alisema Perr huku akimwangalia mchungaji huyo.
“Sawa. Nitajitahidi.”
“Hakikisha kesho nikija ushakumbuka.”
“Sawa. Nitajitahidi,” alisema Mchungaji Gideon na Perr kuoondoka huku akimuachia mchungaji karatasi ile kwa ajili ya kuyafikiria maneno yale usiku kucha
IMG_20181019_222826.jpg
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-03

Mchungaji Gideon alikuwa sero, bado alikuwa na mawazo, alimfikiria mkewe kule alipokuwa, alitamani hata kuona akiwa pamoja naye akimfariji hata kabla hawajafikishwa mahakamani.
Mkononi mwake aliishikilia karatasi iliyokuwa na namba zilizoandikwa, aliziangalia, alijiuliza mara kadhaa juu ya namba zile, zilikuwa na maana gani na kwa nini aliandikiwa yeye? Mbali na namba hizo pia kulikuwa na stori kuhusu John, hakujua muandikaji alimaanisha lakini moyo wake ulimwambia kwamba kulikuwa na maana kubwa sana katika namba hizo.
Mpaka siku nyingine inaingia bado hakupata majibu. Alichokifanya ni kuzungumza na polisi na kuwaambia kuhusu kilichotokea hasa namba zile alizokuwa ameachiwa, kama alivyoulizwa na mwanasheria Perr, nao polisi wakamuuliza kama alijua maana ya namba hizo.
“Sikumbuki chochote kile,” alijibu.
Polisi wakaziandika namba zile pembeni na kumtafuta mpelelezi wao, Jason Warner kwa ajili ya kuzitafakari kwani walihisi kwamba angeweza kugundua kitu chochote kile kwa kuwa alikuwa akifanya kazi kubwa mno kwa kutumia akili yake.
Jason alikuwa miongoni mwa wapelelezi waliokuwa na uwezo mkubwa katika shirika la kipelelezi la FBI. Alikuwa mtu wa kusoma hisia, kila matukio makubwa yalipokuwa yakitokea, hata kama hakukuwa na watu mahali hapo, alipokuwa akisimama kwa dakika kadhaa huku akiwa kimya kabisa, alikuwa na uwezo wa kukwambia kwamba hapo kulikuwa na watu wangapi, walisimama vipi na walishika nini.
Ulikuwa ni uwezo wa ajabu, yeye ndiye aliyekuwa akitumika katika matukio makubwa. Japokuwa alikuwa na umri wa miaka hamsini lakini bado alikuwa na nguvu kubwa. Alipoletewa karatasi iliyokuwa imeandikwa maneno na namba zile, akaanza kuziangalia.
Hakutaka kuzungumza, akaelekea katika ofisi yake na kutulia humo. Aliziangalia zile namba, zilimchanganya, hakujua zilimaanisha nini na kwa nini mtu huyo aliziandika. Kila mtu kituoni hapo alikuwa akimsikiliza yeye, wote waliamini kwamba mwanaume huyo asingeshindwa kuzitambua namba zile, kila mmoja alimwamini.
“01059623059T. What does this mean?” (01059623059T. Hii ina maana gani?) alijiuliza huku akiziangalia namba zile.
Hakutaka kutoka ndani ya chumba kile, akatulia, baada ya saa nne, akatoka chumbani mule, polisi wote wakamsogelea kwani walijua kabisa kwa muda aliokuwa amekaa ndani ya chumba kile, tayari alijua maana ya namba zile.
Uso wake tu ulionyesha tabasamu pana, tabasamu lililomfanya kila mmoja kuona kwamba tayari Jason alijua maana ya namba zile. Akaelekea katika kiti kimoja kilichokuwa nyuma ya meza kubwa na kukaa, polisi wote wakamsogelea kwani walihisi kuwa kitendo cha kuifahamu namba ile basi wangeweza kumgundua Mzimu Unaotabasamu aliyewasumbua kwa kipindi kirefu mno.
“This is the date!” (hii ni tarehe) alisema Jason huku akimwangalia kila mmoja.
“A date?”(tarehe?) aliuliza polisi mmoja huku akionekana kushtuka.
“Yes! 01059623059T is 01/05/1996,” (Ndiyo! 01059623059T ni 01/05/1996) alijibu Jason maneno yaliyomfanya kila mmoja kushtuka.
“What about 23059T?” (na vipi kuhusu 23059T?) aliuliza mwingine.
“It’s time in twenty four hours format! It is 11pm in twelve hours format,” (ni muda katika mtindo wa saa ishirini na nne! Ni saa tano usiku kwa mtindo wa saa kumi na mbili) alijibu, kila mmoja akastaajabu.
“What about 9T?” (Vipi kuhusu 9T?)
“It’s is the modern short form of night. Many social network users use 9T as night just like have the G9T which means Goodnight,” (hicho ni kifupisho cha kisasa cha neno usiku. Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanatumia 9T kama usiku, kwa mfano G9T inayomaanisha usiku mwema) alisema Jason.
Kila mmoja alistaajabu, hakuamini kama mwanaume huyo angeweza kujua kile kilichokuwa kimeandikwa katika karatasi hiyo. Kila mmoja akajua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea siku hiyo usiku na inawezekana kabisa kwamba Mchungaji Gideon alikuwa akifahamu hilo.
“Kuna kitu kilitokea siku hiyo saa tano usiku. Huyu mtu amekiandika ili mchungaji akikumbuke kitu hicho. Ni kitu gani? Hatujui, ni lazima aulizwe,” alisema Jason.
Hawakutaka kuchelewa, hapohapo wakamfuata Mchungaji Gideon na kumuuliza kilichokuwa kimetokea siku hiyo. Alitulia, kichwa chake kikaanza kukumbuka, ilikuwa vigumu mno, ilikuwa ni miaka ishirini na moja iliyopita, hakuweza kukumbuka kitu chochote kile.
“Sikumbuki! Labda mtoto wangu atakuwa akikumbuka hilo!” alisema mchungaji na hivyo kufanya harakati za kumtafuta mtoto wake.
****
Kijana Davis Matimya alikuwa nchini Ujerumani akiendelea kusoma Masomo ya Biashara katika Chuo cha Munich kilichokuwa nchini humo. Kwa kumwangalia, isingekuwa vigumu kugundua kwamba alikuwa kijana mpole mno, alikuwa mkimya huku muda mwingi akiutumia katika kusoma mambo mbalimbali hasa kuhusu wafanyabiashara wengi waliokuwa wamefanikiwa.
Taarifa za baba yake kukamatwa alizipata akiwa chuoni hapo, alishtuka baada ya kusikia kwamba kulikuwa na maiti mbili zilizokuwa zimekutwa ndani ya nyumba yake. Moyo wake ulimuuma, alijua kabisa kulikuwa na kitu, alimfahamu mzee wake, alikuwa mcha Mungu, katika maisha yake aliamua kumtumikia Mungu mpaka kifo chake.
Alijua kulikuwa na mchezo uliokuwa umechezwa hivyo kuanza kufanya harakati za kusafiri kuelekea nchini Marekani, akazungumze na baba yake hata kabla hajapandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka.
Mpaka siku tatu zinakatika bado hakufanikiwa kupata kibali lakini baada ya siku moja mbele, akapigiwa simu na watu ambao walijitambulisha kama maofisa wa CIA ambao walimtaka kuondoka naye kuelekea nchini Marekani kwa kuwa kulikuwa na kitu.
Akajua kwamba mtu aliyekuwa akimuhitaji alikuwa baba yake, haraka sana akaonana nao na kuondoka kwa ndege binafsi mpaka jijini New York nchini Marekani. Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa baba yake, hakujua ni kitu gani alikuwa ameitiwa na wanausalama hao.
Ndege ilipofika New York, akachukuliwa na kupelekwa katika hoteli aliyokuwa ametakiwa kukaa na siku iliyofuata kuelekea katika kituo cha polisi na kuulizwa kuhusu yale maneno yaliyokuwa yameandikwa katika karatasi ile.
“Tarehe hiyo? Naikumbuka vizuri sana!” alisema Davis.
“Kuna kitu gani kilitokea hasa kwenye usiku wa majira ya saa tano?”
Kabla ya kujibu kitu chochote kile, Davis akainamisha kichwa chake chini na kutulia, alipoyainua macho yake, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, alionekana kukumbuka kitu kilichouumiza mno moyo wake.
“Kifo cha ndugu yangu!”
“Ndugu yako?”
“Ndiyo! Tulizaliwa mapacha, kaka yangu aliitwa David. Alikufa usiku huo, tena muda kama huo,” alisema Davis huku akiendelea kububujikwa na machozi.
“Alikufa? Kifo gani?”
“Alitekwa na watu wasiojulikana, baada ya siku mbili akakutwa ameuawa kinyama katika ufukwe wa Coco,” alisema Davis, akanyamaza na kuendelea kulia, moyo wake ulimuuma mno kwani hakutegemea kama kila kitu kilichokuwa kimetokea kingemuhusisha ndugu yake huyo aliyekuwa akimpenda mno.
“Pole sana! Na kuhusu hii stori ya John?”
“Sifahamu kitu chochote kile.”
“Tuambie ukweli! Baba yako yupo kwenye hatari, kutuambia ukweli ndiyo nafasi pekee ya kumtoa kutoka katika mdomo wa kifo. Tuambie ukweli!” alisema Jason huku akimwangalia Davis.
“Kama ningejua ukweli, ningewaambia! Sijui chochote kile. Kifo cha David kilituchanganya sana, alikufa kwenye maumivu makali, alitobolewa macho, akatolewa pua na masikio na hata mashavuni alitobolewa kwa chuma chenye ncha kali. Mwili wake ulitisha, kilichotufanya tujue kwamba ni yeye ni nguo alizovaa tu. Hebu jifikirie, unampoteza mama, mwezi mmoja baadaye unampoteza ndugu yako, unahisi utakuwa na maumivu makali kiasi gani?” alihoji Davis na kuendelea kulia.
Kwa hicho alichokuwa amekisema, kidogo kikawapa mwanga wa kile kilichokuwa kimetokea, wakamfuata Mchungaji Gideon na kumuuliza baadhi ya maswali, walipomkumbusha, akakumbuka kila kitu kwamba kweli siku hiyo ilikuwa ni kifo cha mtoto wake, pacha aliyeitwa David ambaye alitekwa na watu wasiojulikana na kesho yake mwili wake kukutwa ufukweni ukiwa umeharibiwa vibaya.
“Na ni nani aliyemteka, ulijua chochote?”
“Hapana! Sikujua chochote kile, polisi walipeleleza sana lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na majibu. Tuliumia sana,” alisema Mchungaji Gideon na kuanza kulia.
“Pole sana. Tulisikia kwamba mkeo alikufa mwezi mmoja uliopita hata kabla ya mtoto wako?”
“Ndiyo! Aliamua kujiua. Aliacha barua iliyosema sababu ya kufanya hivyo ni kuchoka na maisha aliyokuwa akiishi,” alisema Mchungaji Gideon.
“Maisha gani?”
“Sikuyajua, aliyafanya kuwa siri sana. Alikuwa amebadilika, akawa mlevi, wakati mwingine hakuwa akilala nyumbani, aliondoka kwenda baa na kurudi asubuhi,” alisema Gideon.
“Kipindi hicho ulikuwa mchungaji?”
“Hapana! Sikuwa nimeokoka! Miaka kumi baadaye ndipo nikaokoka na kumtumikia Mungu mpaka leo hii,” alisema Gideon na kuendelea kulia.
Kila mmoja akamuonea huruma, historia yake iliwasikitisha wote. Moja kwa moja wakahisi kwamba historia ya nyuma ndiyo iliyomfanya mchungaji huyo kuwa mahali hapo, na kama kulikuwa na mtu alimuwekea maiti zile ndani ya nyumba yake, basi mtu huyo alikuwepo katika tukio hilo la tarehe hiyo lililokuwa limefanyika.
“Na huyo mkeo ulikuwa naye kwenye uhusiano kwa kipindi hicho?” aliuliza Jason.
“Nani? Lucy?”
“Ndiyo!”
“Ndiyo tulikuwa tumeanza uhusiano baada ya kifo cha mke wangu. Inaniuma sana, mke wangu alikunywa sumu, kwa nini? Lilian, kwa nini ulijiua mpenzi wangu? Tatizo lilikuwa nini? Kwa nini ulifanya hivyo mpenzi?” aliuliza Mchungaji Gideon huku akilia kama mtoto mdogo.
“Pole sana. Naomba utupe muda, tunaamini kwamba tutajua kila kitu kilichokuwa kimetokea. Cha kwanza tutawatuma watu wetu waende Tanzania, huko, watakwenda katika kituo cha polisi na kuchukua faili la kifo cha mtoto na mke wako, nadhani tukianzia hapo, mwisho wa siku tutamjua mtu aliyefanya mauaji ya mtoto wako na hata kujua sababu ya mkeo kunywa sumu! Pia, tutaweza kumfahamu huyu Mzimu Unayetabasamu,” alisema Jason.
“Nitashukuru sana!”
“Sawa,” alisema Jason na kuondoka ndani ya chumba hicho cha mahojiano, alichokitaka ni kuwatuma watu waelekee nchini Tanzania kwa lengo la kuchukua mafaili hayo na kuyapitia wajue ni kitu gani walitakiwa kufanya.
***
Mkurugenzi wa FBI, Bwana Donald Power akawasiliana na Mkuu wa CIA, Bwana Luke na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Alikwishapelekewa taarifa hiyo, ilikuwa kwenye meza yake lakini suala la utambuzi wa herufi na namba hakuwanalo kabisa.
Kwake likaonekana kuwa jipya, aliamini kwamba kwa kupata maelezo kidogo kuhusu namba zile basi ingekuwa rahisi kwake kuwatuma vijana wake kuelekea nchini Tanzania na kuhakikisha wanapata ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea na hatimaye huo Mzimu Unaotabasamu kujulikana.
“Lengo kubwa la kukupigia ni kwamba tunahitaji utusaidie kuwapeleka baadhi ya vijana wako nchini Tanzania, sisi huku kama FBI tutashughulika na suala zima la upelelezi nchini humu kujua hasa muuaji ni nani kama si mchungaji,” alisema Power.
“Haina shida. Na vipi kama tutatumia interpol?”
“Sidhani kama watakuwa makini katika kulichunguza suala hili. Kumbuka kwamba tunamtafuta muuaji anayetusumbua kwa mwaka wa kumi na tano sasa, kama hatutotumia nguvu zetu kubwa, tutashindwa kumkamata. Kama tukitumia intepol, inamaanisha kwamba tutawatumia na polisi wa Tanzania. Sasa itakuwaje kama kutakuwa na polisi anashirikiana na muuaji kwa namna moja au nyingine? Hakika tutashindwa,” alisema Power.
Walizungumza mambo mengi kuhusu muuaji huyo na mwisho wa siku kukubaliana kwamba ni lazima maofisa watatu wa CIA watumwe kuelekea nchini Tanzania kwa ajili ya kubaini kitu kilichokuwa kimetokea usiku wa tarehe 1/05/1996. Huko, walitakiwa kufika mpaka katika kituo kikuu cha polisi ambapo wangeambiwa ni wapi walitakiwa kwenda na huko kuanza kufuatilia hatua kwa hatua kile kilichokuwa kimesababisha mtoto wa Mchungaji Gideon kuuawa kinyama.
“Tunakwenda na kuahidi kuja na ripoti nzuri,” alisema ofisa mmoja wa CIA aliyeitwa Fredrick Turnbull na hivyo kuanza safari.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-04

Dar es Salaam, 1996

Hali ya hewa ilibadilika, jua kali lililokuwa likiwaka katika jiji la Dar es Salaam likafunikwa na mawingu mazito yaliyoonyesha kwamba muda wowote ule mvua kubwa ingeweza kunyesha.
Watu waliokuwa njiani kurudi majumbani mwao, wakaanza kutembea harakaharaka ili hata kama mvua kubwa ingenyesha basi wawe tayari wamefika majumbani mwao. Kwa wanawake waliokuwa wakiishi katika mitaa ya uswahilini, wakatoa ndoo za maji na kuziweka nje kwa lengo la kukinga maji ya mvua kubwa ambayo kila mtu alitegemea kwamba ingenyesha muda mchache ujao.
Ndani ya jumba moja kubwa na la kifahari lililokuwa Mikocheni B, mwanaume mmoja mwenye miaka arobaini na sita alikuwa katika sebule yake ndani ya jumba hilo akiangalia televisheni. Pembeni yake kulikuwa na meza ndogo ambayo juu yake kulikuwa na glasi ya juisi ya machungwa aliyokuwa akinywa.
Kwa kumwangalia, alionekana kuwa mtu mwenye furaha, muda wote tabasamu pana lilionekana usoni mwake. Hakuonekana kuwa na tatizo lolote, alikuwa na afya tele na muda mwingi macho yake yalikuwa yakiangalia saa yake.
Alikuwa na maisha mazuri, alikuwa na kila kitu, aliishi ndani ya jumba kubwa la kifahari, katika uwanja wa jumba hilo kulikuwa na magari zaidi ya matatu ya kifahari, katika suala zima la usafiri alikuwa na uamuzi wa kuchukua gari lolote lile, kama ni Range Rover SUV, Hammer au V8 zilizokuwa zimepaki mbele ya jumba lake hilo.
Mwanaume huyo aliitwa Gideon. Hapo kabla hakuwa katika maisha hayo, hakuwa na pesa, hakuwa na magari na hata kula yake ilikuwa ni kwa bahati sana. Alikulia maisha ya kimasikini, aliishi uswahili Tandika kwa miaka yote kabla ya kukutana na msichana mrembo, Lilian aliyekuwa na maisha mazuri.
Lilian akatokea kumpenda Gideon ambaye kipindi hicho alikuwa fundi mtangeneza makochi katika Mtaa wa Chang’ombe. Wawili hao walikutana mahali hapo na kupendana. Kwa kuwa Gideon alikuwa na maisha magumu, Lilian akaanza kuyabadilisha maisha ya mwanaume huyo, akampa kiasi kikubwa cha pesa na kumfungulia biashara kubwa ambayo ilianza kumuingizia pesa.
Gideon akabadilika, hakuwa yule aliyekuwa kipindi cha nyuma, muonekano wake ukabadilika, akapendeza na kuonekana mtu wa thamani ya juu kuliko kipindi cha nyuma.
Lilian alichanganyikiwa, hakutaka kujificha kwa Gideon, kila siku alimfuata kwa gari mahali hapo na kuondoka naye. Uhusiano wao wa kimapenzi uliendelea mpaka pale Lilian alipopata ujauzito na hatimaye kuanza kuishi pamoja katika jumba lake lililokuwa Mikocheni B katika Mtaa wa Mbuni.
Yule Gideon aliyechoka hakuwa huyu, thamani yake ikapanda, akayabadilisha maisha yake, kutoka katika kazi ya uchongaji makochi mpaka kuwa mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa akizisimamia biashara za mpenzi wake ambaye alishindwa kufanya lolote kutokana na ujauzito aliokuwanao.
Miezi ikaendelea kukatika mpaka pale Lilian alipojifugua mapacha wa kiume, wa kwanza akapewa jina la David na wa pili Davis. Kuzaliwa kwa watoto hao kukaongeza upendo ndani ya nyumba, kila mmoja akazidisha mapenzi kwa mwenzake, wakapendana kwa nguvu zote kiasi kwamba kila mmoja akahisi kabisa wangeweza kuishi katika upendo huo mkubwa maisha yao yote.
“Ni watoto wazuri, ni jambo la kumshuru sana Mungu kupata watoto wazuri kama hawa mke wangu,” Gideon alimwambia Lilian huku akiwaangalia watoto wake.
Walikuwa na sura nzuri, walichukua sura ya mama yao na baadhi ya vitu walichukua kwa baba yao. Kila mtu aliyekuwa akiwaangalia watoto hao, aliwapenda, walikuwa na afya njema huku kila mtu aliyekuwa akiwaangalia alitamani kuwa na watoto kama hao.
Gideon alijitoa kufanya kazi. Kumbukumbu ya maisha aliyopitia hata kabla hajakutana na Lilian yalikuwa yakijirudia kichwani mwake. Aliumia, alishashinda sana na njaa, alichoka kimaishi kupita kawaida. Hakutaka kurudi kule alipotoka na ndiyo maana aliamua kupambana usiku na mchana kuhakikisha biashara alizokuwanazo na Lilian zinakwenda vizuri kila siku.
Baada ya watoto kufikisha mwaka mmoja, wawili hao wakaamua kufunga ndoa kanisani na kuwa mume na mke. Kila mmoja alifurahi, thamani ya maisha yao ikazidi kupanda, kila walipokuwa wakiziangalia pete walizokuwa wamevalishana ziliwapa nguvu za kuendelea kupendana zaidi ya walivyokuwa wakipendana kipindi hicho.
Kila siku asubuhi Gideon alikuwa akiamka asubuhi na mapema, mara baada ya kujiandaa ilikuwa ni lazima kumbusu Lilian na watoto wake na kuelekea kazini. Hakutaka kuwa mbali na watoto wake, aliwapenda, muda wote alitamani sana kuwa pamoja nao, aliwapa kila kitu, kila alipokuwa akitoka ilikuwa ni lazima kurudi na zawadi kwa ajili ya watoto wake hao.
“Nitahitaji wasome sana, wasome mpaka wanyewe waseme imetosha,” alisema Gideon huku akimwangalia Lilian.
“Kweli kabisa. Urithi pekee ambao wazazi tunatakiwa kuwapa watoto ni elimu tu ambayo itawaongoza maisha yao yote hata kama hawatokuwa na kitu mikononi,” alisema Lilian.
Walipofikisha miaka mitatu wakawaandikisha katika Shule ya Chekechea ya Golden iliyokuwa hapohapo Mikocheni B. Ilikuwa shule ya gharama, watoto wengi waliokuwa wakisoma mahali hapo walikuwa ni wale ambao wazazi wao walikuwa na pesa nyingi au viongozi mbalimbali wa serikali.
Hapo ndipo waliposoma mpaka walipofikisha umri wa miaka saba na hivyo kuanza masomo katika Shule ya Msingi ya St. Louis iliyokuwa Msasani jijini Dar es Salaam.
“Unataka kuwa nani Davis?” aliuliza Gideon huku akimwangalia mtoto wake.
“Nataka kuwa daktari, ninataka niwatibu watu magonjwa wanayougua kila siku katika hospitali yangu,” alijibu Davis huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Na wewe David?”
“Nataka niwe mchungaji kama Regnard Bonkke. Nihubiri neno la Mungu duniani kote,” alijibu David huku akimwangalia baba yake.
Hizo ndizo zilikuwa ndoto zao. Kila siku wazazi wao waliwahimiza kusoma, waliwaambia kwamba pasipo kusoma sana basi wasingeweza kufikia malengo waliyokuwa wamejiwekea. Kwa David na mdogo wake hawakutaka kupuuza, kila siku ilikuwa ni lazima kusoma huku kila mmoja akiwa na uhakika wa kutimiza ile ndoto aliyokuwa amejiwekea.
Wakati watoto wao walipoingia darasa la saba huku wakiwa na miaka kumi na nne ndipo Lilian akaanza kujisikia hali ya tofauti mwilini mwake. Kila siku alisikia maumivu makali, wakati mwingine alikuwa akisikia kizunguzungu na hata kuzimia. Hali hiyo ilimtisha mno, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea hivyo kuelekea hospitalini na mumewe.
Huko, waliambiwa kwamba Lilian alikuwa na ugonjwa kansa ya damu iliyokuwa ikimtesa mno kipindi hicho. Aliogopa, aliufahamu ugonjwa huo, ulikuwa hatari na uliokuwa ukipoteza maisha ya watu kila siku.
“Nina kansa ya damu?” aliuliza Lilian huku akiwa haamini majibu aliyopewa na daktari yule.
“Ndiyo mke wangu! Ila hii haimaanishi kwamba utakufa,” alisema Gideon huku akimwangalia mke wake.
“Nina kansa ya damu mume wangu! Nina kansa ya damu, nitakufa mume wangu,” alisema Lilian na kuanza kulia.
Mume wake ndiye alikuwa mfariji pekee aliyekuwa naye katika maisha yake. Gideon akamkumbatia mke wake na kumpoza moyo kwamba hakutakiwa kulia kwani kwa Mungu hakukuwa na kitu kilichokuwa kikishindikana, kama watu wengine walikuwa wakitibiwa na kupona, vipi kuhusu yeye?
Maisha yake yakabadilika, muda mwingi Lilian akawa na huzuni, kila alipoyaangalia maisha yake ya mbele ni kifo tu ndicho alichokiona. Hali ya kuwa na mawazo mengi ikaudhoofisha mwili wake, akapoteza hamu ya kula na hatimaye kuanza kuonyesha dalili mbaya, kutoka damu masikioni na wakati mwingine kutoka puani.
“This is my end! I am going to die,” (Huu ni mwisho wangu! Ninakufa) alisema Lilian huku akimwangalia mume wake.
“You will surely die but not from this desease,” (Ndiyo utakufa lakini si kwa ugonjwa huu) alisema Gideon na kumkumbatia mke wake aliyeonekana kukata tamaa.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-05

Gideon hakuwa na furaha, kila alipomwangalia mke wake, Lilian moyo wake ulimuuma mno. Hakuamini kama alikuwa akipitia hatua hiyo katika maisha yake. Mke wake mpendwa, alikuwa kwenye mateso makubwa, kansa ya damu ilimtesa na kumlaza kitandani muda mwingi.
Kila siku walikuwa wakienda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa lengo la kupata tiba lakini kote huko hawakufanikiwa kwa kuwa tiba yenyewe haikuwa imesambazwa kwa wingi kutokana na kuwa na wagonjwa wachache wa kansa ya damu nchini Tanzania hasa kwa kipindi hicho.
Hakutaka kukata tamaa, kila alipozungumza na mke wake, alimwambia wazi kwamba hakuwa akienda kufa, kwa muujiza wa Mungu ilikuwa ni lazima apone na kurudi katika hali ya kawaida.
Walikwenda katika hospitali mbalimbali kwa ajili ya kupata tiba lakini cha ajabu huko hawakupata msaada wowote ule hivyo kuanza kwenda katika makanisa kuombewa lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale. Maombi hayakusaidia kwa kuwa tu Lilian hakuamini, alikata tamaa na kuhisi kwamba muda wowote ule angefariki dunia.
“Mume wangu ninakufa,” alisema Lilian.
“Huwezi kufa!”
“Ninakufa mume wangu!” alisema Lilian.
Aliamini hivyo, siku zikakatika, hali yake iliendelea kuwa mbaya, msaada mkubwa aliokuwanao kwa kipindi hicho alikuwa mume wake tu. Ndugu zake wachache walifika nyumbani hapo mara kumuona lakini asilimia kubwa ya ndugu hao hawakwenda hata kumuona.
Gideon hakutaka kuona akimpoteza mke wake, alichokifanya ni kuanza kumtafutia hospitali nyingine nchini Afrika Kusini, alipozipata, akampeleka huko kwani aliamini kwamba kulikuwa na matibabu makubwa lakini napo huko hakukuweza kupona, aliendelea kuwa vilevile, alidhoofika kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Walihangaika kwa muda wa miezi sita lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale, Gideon mwenyewe akakata tamaa, akaona kwamba kweli huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mke wake. Hakwenda kazini, kila kitu kwa wakati huo ni kama kilikuwa kimesimama, asingeweza kufanya kitu chochote kile kwa kuwa hakujua hatima ya mke wake ingekuwaje.
“Mume wangu! Mwisho wangu haumaanishi ndiyo mwisho wa kila kitu. Tuna biashara, endelea kuzisimamia. Unakumbuka ulipotoka, hakuna sababu ya kurudi kule na wakati unaweza kupambana. Endelea kupambana, mwisho wa maisha yangu haimaanishi kwamba ndiyo mwisho wa kila kitu,” alisema Lilian huku akimwangalia mume wake.
“Sitaki kuona ukiteseka.”
“Najua! Ila hutakiwi kuacha kila kitu kwa ajili yangu. Ninatamani uendeleze mali tulizokuwanazo, endelea kupambana mume wangu,” alisema Lilian kwa sauti ya chini kabisa.
Hilo ndilo lililofanyika, Gideon akarudi tena katika biashara zao na kuendelea kuzifanya kama kawaida. Hakuwa na furaha lakini alitakiwa kuendelea kuzisimamia biashara hizo kwa kuwa tu kifo ameandaliwa kila mtu.
Baada ya miezi miwili ndipo akakutana na msichana mmoja mrembo wa sura, mfanyabiashara aliyehitaji kushirikiana naye, msichana huyo aliitwa kwa jina la Lucy.
Alikuwa na figa matata, mrefu huku kiunoni akiwa hipsi kubwa ambazo kwa vijana wa sasa wangeziita kwa jina la bastola. Alijua kuringa, alijua kutembea, sura yake ya kitoto iliwachanganya wanaume wengi, kila mtu aliyekuwa akimwangalia, alimtamani sana msichana huyo.
Alikutana na Gideon katika kipindi ambacho msichana huyo alihitaji kusambaza kumpyuta mashuleni kutoka nchini Marekani. Hakujua wapi pa kuanzia lakini kwa kuwa Gideon alikuwa akifahamu mambo mengi, akaona kuwa angekuwa msaada wake mkubwa kama tu wangeshirikiana kufanya jambo hilo.
“Ila nasikia mwaka 2000 ndiyo mwisho wa dunia,” alisema Gideon huku akimwangalia Lucy, huo ulikuwa mwaka 1996.
“Hahah! Na wewe unaamini hilo?” aliuliza Lilian huku akimwangalia Gideon.
“Wanasema wanasayansi kwamba ndiyo mwisho wa dunia!” alijitetea Gideon.
“Hutakiwi kuamini upuuzi huo. Tufanye kazi, tupambane mpaka tuhakikishe biashara inakua, ninahitaji sana unisaidie katika hili. Kuna mzigo wa kompyuta laki moja zinakuja, pia kuna simu za mezani nazo zinakuja, naomba unisaidie katika hili,” alisema Lucy huku akimwangalia Gideon aliyeonekana kama kuchanganyikiwa kwani dili alilokuwa akipewa na msichana huyo, kwa kipindi hicho lilikuwa kubwa.
“Haina shida.”
“Nashukuru! Tukifanikiwa katika hili, nasikia pia kutaanzishwa simu za mikononi, natumaini kama tukiingia katika biashara hilo itakuwa na faida sana. Tusubiri kwanza tuone kama serikali itaongea chochote katika hilo,” alisema Lucy.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa ukaribu na msichana huyo. Kila siku ilikuwa ni lazima kuonana na kuzungumza mambo mengi kuhusu biashara walizokuwa wakizifanya. Hakutaka jambo hilo liwe siri, akamshirikisha mke wake katika suala hilo na hivyo kuukubalia ukaribu huo kwa kuamini kwamba ungezifanya biashara zao kukua kila siku.
Ukaribu huo ukaanza kuibua vitu vingine mioyoni mwao, wakaanza kusikia kitu cha tofauti kabisa. Kila alipokuwa akikaa na mkewe, Gideon hakujisikia furaha kama ilivyokuwa akikaa na Lucy. Aliuona moyo wake kuanza kuuona umuhimu wa Lucy kuliko hata wa mkewe huyo. Kila siku ilikuwa ni lazima kuzungumza kwenye simu, alikuwa bize na simu, mkewe hakuwa na wasiwasi, aliamini kwamba kila kitu kilichokuwa kikizungumziwa kilikuwa ni biashara tu.
Gideon alipokuwa na mkewe na Lucy kupiga simu, mazungumzo yalikuwa ni biashara tu, mipango gani ilitakiwa kufanywa ili biashara zikue lakini alipokuwa mbali na mkewe, mazungumzo yalikuwa mengine kabisa, hawakuzungumzia biashara bali walizungumzia vitu vingine kabisa.
Walikuwa wakisifiana, Gideon alitumia mwanya huohuo kumwambia jinsi alivyokuwa ameumbika, alivyokuwa na tabasamu pana, hipsi kubwa na hata mwendo wa maringo aliokuwa akitembea. Kwa Lucy, moyo wake uliridhika, alipenda sifa, alijiona kuwa kama malaika, alijiona kuwa mwanamke mzuri kuliko wanawake wote katika dunia hii.
“Mungu anajua sana kuumba,” alisema Gideon huku simu ikiwa sikioni mwake, hakutaka kutumia simu ya chumbani, aliamua kutoka na kwenda kutumia simu ya sebuleni ili apate nafasi ya kuzungumza kimahaba na msichana huyo.
“Mmh! Kwa nini unasema hivyo?”
“Najaribu kutafakari. Sisi wengine Mungu alituumba huko akiwa anafanya kazi nyingine, yaani alikuwa akiniumba mimi huku akitengeneza mito na kuongeza maji baharini, ila kwako, yaani aliacha kazi zote na kuanza kukuumba wewe. Unanidatisha kinoma,” alisema Gideon kwenye simu. Alikuwa akitumia nguvu nyingi kumsifia mwanamke ambaye hakujua hata stori ya maisha yake ilikuwaje.
“Jamaniiiiiii! Unanifanya nijisikie aibu mwenzako,” alisema Lucy.
“Kweli tena!” alisema Gideon.
Wakati akizungumza hayo, kwa mwendo wa kujikongoja Lilian akatoka chumbani na kuelekea sebuleni, haraka sana Gideon akabadilisha mazungumzo na kuanza kuzungumzia biashara ikiwa ni kumzuga mkewe asijue kilichokuwa kikiendelea.
“Kwa hiyo kompyuta ngapi zitaingia mwezi ujao?” aliuliza Gideon, Lucy alijua hali hiyo inapobadilika huwa na kitu gani nyuma yake.
“Elfu hamsini!” alisema msichana huyo.
“Ooh! Safi sana! Ngoja nishughulikie mambo ya shule na vyuo ili tujue zitafikia wapi na wapi,” alisema Gideon.
“Basi haina shida.”
Huo ulikuwa uhusiano wa siri, hakukuwa na mtu yeyote aliyegundua zaidi yao wenyewe. Gideon hakutaka kuonyesha mabadiliko kwa mkewe, alimpenda vilevile, alimthamini na kufariji katika kila hatua kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kwake kugundua kwamba mume wake alianza kutembea nje ya ndoa.
Watoto wao waliokuwa na miaka kumi na nne walifanya vizuri darasani, walisoma kwa bidii na kufauru mitihani yao kiasi kwamba wakafanya vizuri na kujiunga kidato cha kwanza katika Shule ya St. Alexandria iliyokuwa Msasani jijini dar es Salaam.
Mapenzi yao kwa watoto wao hayakupungua, kwao, hao walikuwa kila kitu. Mpaka kufikia miaka hiyo, tayari tabia zao zilijulikana, kwa David alikuwa kijana mpole, mkimya ambaye mpaka kuongea kwake ilikuwa ni kwa tabu sana lakini kwa Davis alikuwa mtoto mzungumzaji mno, hata alipokuwa akiongea na wazazi wake, alikuwa na uwezo wa kuongea zaidi ya maneno mia mbili ndani ya sekunde thelathini tu.
Mapenzi ya watoto yaligawanyika, Davis alimpenda sana baba yake, alipenda kukaa naye kila alipokuwa lakini kwa David, mapenzi yake yalikuwa makubwa kwa mama yake, hata alipokuwa akirudi nyumbani mtu wa kwanza kabisa kuongea naye alikuwa mama yake, alimpenda na kila alipomuona jinsi alivyokuwa akiteseka, moyo wake ulimuuma kupita kawaida.
Gideon alifanya mambo yake kwa tahadhali sana, mara nyingi alikutana na Lucy na kufanya mapenzi. Hiyo ndiyo nafasi pekee aliyokuwa akiitumia msichana huyo kumchanganya Gideon. Alijua kucheza na mwili wake, alimfanyia vituko kitandani ambavyo alijua kabisa Lilian hakuwahi kumfanyia.
Hilo ndilo lililomchanganya sana Gideon, hakuambiwa lolote, kwake, Lilian akaanza kuonekana si chochote, penzi lake la dhati kwa kipindi hicho lilihama kwa mke wake na kuhamia kwa mchepuko.
“Nataka tuzungumze,” alisema Lucy huku akimwangalia Gideon, walikuwa kitandani katika Hoteli ya Sheraton jijini Dar.
“Unataka tuzungumze nini mpenzi?”
“Nataka kuishi na wewe, tujenge familia yetu,” alisema Lilian.
“Kuishi na mimi?”
“Ndiyo!”
“Na mke wangu itakuwaje?” aliuliza Gideon.
“Mke wako! Ile maiti inayotembea ndiyo inataka kukuzuia wewe kuishi na mimi?” aliuliza Lucy huku akimwangalia Gideon.
“Pleaseee!” (tafadhali!)
“Ile ni maiti inayotembea. Niambie, unataka kuendelea kuishi na maiti yako au mimi?” aliuliza Lucy.
“Wewe mpenzi!”
“Basi muue!”
“Nimuue?”
“Ndiyo!”
“Nimuue Lilian?”
“Ndiyo! Kwani ugumu upo wapi? Ukimuua ndiyo tutapata nafasi ya kuishi kwa raha na maisha yetu lakini ukimuacha, hatutoweza kuishi kwa raha. Kama upo tayari, muue na kama haupo tayari niambie nikaendelee na maisha yangu,” alisema Lucy huku akijidai kujipeleka pembeni.
“Subiri kwanza mpenzi! Mbona umekasirika hivyo!”
“Sikuelewi! Utaua kwa ajili yangu au hutoua?” aliuliza.
“Subi....”
“Nijibu! Utaua au?”
“Kwa ajili yako, nitamuua! Kwanza pale kwenyewe ni mfu tayari,” alisema Gideon, alichanganyikiwa kwa penzi la Lucy, hakutaka kuona akimkosa msichana huyo kisa mkewe ambaye aliamini kuwa muda wowote ule angekufa!
“Lini?”
“Subiri kwanza! Si ndiyo najifikiria! Ikiwezekana haraka sana! Nitamuua lakini unatakiwa kusubiri!” alisema Gideon.
“Nakupa wiki moja. Usipokamilisha hili, mimi na wewe ndiyo mwisho,” alisema Lucy, akasimama na kuanza kuvaa nguo zake, alipomaliza, akamsogelea Gideon, akambusu mdomoni na kuondoka mahali hapo huku akimwacha mwanaume huyo akiwa na mawazo tele, amuue mkewe au asimuue, ila kila alipokumbuka kwamba alikuwa mgonjwa, hakuwa na jinsi, akakubaliana na moyo wake kwamba lazima amuue ili alilinde penzi lake na mtoto mzuri Lucy.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-06

Gideon alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alimwangalia Lucy, maneno aliyoyazungumza yalipenya masikioni mwake, alikuwa na mtihani mzito, kumuua mke wake lilikuwa jambo gumu ambalo kwa uwezo kawaida wa kufikiri, aliona kuwa gumu ila kwa mapenzi aliyokuwanayo kwa msichana huyo, kuna wakati aliona kuwa jambo jepesi mno.
Lucy akaondoka huku akimwacha katika lindi la mawazo, alikumbuka namna mke wake alivyokuwa akiteseka, mwili wake ulikongoroka, hakuwa na nguvu za kutosha, alitia huruma na kansa ya damu ilikuwa ikimmaliza taratibu. Aliumia moyoni mwake, alijiahidi kwamba kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima kumlinda mke wake, kuhangaika mpaka kuhakikisha kwamba anapona lakini wakati akilifikiria hilo, tayari kulikuwa na mwanamke aliyemwambia kwamba ili kuendelea naye ilikuwa ni lazima kumuua Lilian.
Hakutaka kukaa sana hotelini, akaondoka zake kurudi nyumbani. Njiani, kichwa chake kilimuuma, alikuwa na mawazo tele, alimfikiria mke wake muda wote, hakuona kama kulikuwa na sababu ya kufanya kile alichokitaka Lucy akifanye, alikumbuka kwamba kanisani alimuahidi kuwa angekuwa naye hatua kwa hatua mpaka siku ambayo angeingia kaburini.
“Siwezi kumuua mke wangu!” alisema huku machozi yakianza kujikusanya machoni mwake.
Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani kwake, geti likafunguliwa na kuingia ndani. Alipofika sebuleni tu na macho yake kutua kwa mke wake mpendwa aliyelala kwenye kochi, machozi yale yakaanza kutiririka mashavuni mwake, alipokumbuka maneno ya Lucy kwamba alitakiwa kumuua mwanamke huyo, alihisi kabisa kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.
Akamsogelea na kumkumbatia kwa nguvu. Hakuwahi kumkumbatia mke wake kwa nguvu namna hiyo, siku hiyo alimkumbatia kwa hisia kali kiasi kwamba Lucy akawa anashangaa.
“Why are you crying baby?” (kwa nini unalia mpenzi?) aliuliza Lilian huku akimwangalia mume wake aliyekuwa akitiririkwa na machozi mashavuni mwake.
“I am sorry!” (samahani!) alisema Gideon.
“You have done nothing to me! What is going on?” (hujanifanya kitu chochote kile! Nini kinaendelea?) aliuliza Lilian huku akimwangalia mume wake.
Kwa kile alichokuwa amemwambia Lucy kwamba angemuua mke wake ndicho kilichomfanya kuanza kumuomba msamaha. Hakumwambia mke wake ukweli, alimdanganya kwamba alimuomba msamaha kwa kuwa tu alimuacha peke yake na kuchelewa kurudi.
Kwa Lilian hakukuwa na tatizo lolote lile, akamwambia mume wake kwamba hakutakiwa kujali sana, kitu cha msingi kabisa kilikuwa ni kuhakikisha kwamba biashara zinakwenda vizuri. Walibaki sebuleni hapo wakizungumza mambo mengi mpaka muda wa kwenda kulala ulipofika.
Kitandani, hakuwa na usingizi kabisa, japokuwa alikuwa na mkewe lakini mawazo yake yalikuwa kwa Lucy. Aliyakumbuka maneno yake kwamba amuue mkewe vinginevyo ndiyo ingekuwa mwisho wa kuwa pamoja. Aliumia, hakutaka kumpoteza Lucy wala Lilian lakini pia sababu maisha aliyokuwa ametokea mpaka hapo alipofikia, Lilian alikuwa amechangia sana mpaka kuwa hapo.
“Haiwezekani!” alijikuta akisema kwa sauti.
“Haiwezekani nini?” aliuliza Lilian, alishtuka baada ya kumsikia mume wake.
“Kukuacha tena! Ninaumia sana, wewe ni mtu muhimu sana kwangu! Siwezi kukuacha tena,” alisema Gideon, aliunganishia stori lakini muunganiko wake aliokuwa ameusema si ule ambao alimaanisha kile alichokuwa amekiwaza kabla.
Kichwa chake kilimuuma, alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Kumuua mke wake ulikuwa ni mtihani mzito ambao hakuwahi kufikiria kwamba kuna siku angetakiwa kufanya jambo kama hilo. Kila alipomwangalia, alimuonea huruma na wakati mwingine kuisikia sauti moyoni mwake ikimwambia kwamba kama kweli alikuwa akimpenda Lucy basi ni lazima amuue mke wake.
Mbali na huruma hiyo pia akaanza kuwangalia watoto wake, walikuwa wakielea ujanani, wangeishi vipi kama siku moja wangegundua kwamba yeye ndiye aliyemuua mama yao waliyekuwa wakimpenda sana? Hakika mbele yake kulikuwa na mtihani mgumu sana.
“Baba! Mbona unakuwa na mawazo sana?” aliuliza David, kila alipokuwa akimwangalia baba yake, akahisi kuna kitu.
“Hakuna! Nipo sawa tu!”
“Kweli?”
“Ndiyo! Huwa ninakumbuka kuhusu stori aliyonisimulia baba yangu siku moja,” alisema Gideon.
“Stori gani?”
“Kuhusu mwanaume aliyeitwa John. Siku zote ukitenda ubaya, malipo yake yapo hapahapa duniani,” alisema Gideon huku akiwaangalia watoto wake.
Walimzoea baba yao, mara kwa mara alikuwa akiwaambia mifano mingi ya watu mara tu anapohitaji watende wema au jambo moja kwa ajili ya kumfurahisha Mungu. Siku hiyo walijua kwamba baba yao alikuwa na kitu cha kuwaambia kuhusu huyo John, hivyo wakakaa na kuanza kumsikiliza.
“Kuna siku Hakimu John alimuona Juma akimuua Hosea porini kwa kumpiga na shoka kisha kukimbia. Baada ya siku tatu, kesi ikafika mezani kwake kwamba mtu aliyemuua Hosea alikamatwa na kufikishwa mahakamani, ila alipomwangalia, hakuwa Juma ambaye alimuona, alikuwa Dickson,” alisema Gideon huku akiwaangalia watoto wake.
“Mmh! Akafanyaje sasa?” aliguna Davis na kuuliza.
“Alimfahamu muuaji ila hakuwa na namna ya kumsaidia. Kila alipoangalia faili, lilionyesha kabisa kwamba muuaji alikuwa Dickson, ila alikuwa na uhakika kwamba hakuwa huyo. Akasimamisha kesi, akaenda katika chumba kidogo, akalia sana, ila mwisho wa siku akahitaji kuzungumza na Dickson,” alisema Gideon.
“Alifungwa?” akadakia David.
“Alipokwenda, John akamwambia kwamba anajua kuwa hakuua, ila kwa nini ushahidi wote unaonyesha kwamba aliua? Dickson alichokisema ni kwamba hakuua, alisingiziwa kesi hiyo japokuwa ushahidi wote unaonyesha kwamba aliua,” alisema Gideon na kujiweka vizuri.
“Dickson aliendelea kujitetea lakini mwisho kabisa John akamuuliza kama aliwahi kuua! Dickson akalia sana lakini akamjibu kuwa aliwahi kuua japokuwa hakuwahi kukamatwa na hakuna mtu aliyejua kama aliua,” alisema Gideon.
“Mmh!”
“Kusema hivyo tu! John akamwambia kwamba basi ile hukumu ya siku hiyo si ya kifo cha Hosea, bali Mungu alitaka kumuhukumu kwa kifo cha kipindi cha nyuma alichokuwa amekifanya,” alisema Gideon.
“Dad! This is amazing story!” (Baba! Hii stori inastaajabisha) alisema David huku akimwangalia baba yake.
“Ndiyo! Unapofanya ubaya leo, Mungu atakuletea malipo yake kwa staili nyingine kabisa. Leo unapoua, Mungu hakuhukumu leo, anaweza kukuhukumu siku nyingine. Unapoiba leo, si kwamba Mungu atakuhukumu leo, anaweza kukuhukumu utakapokuwa mzee. Tunachotakiwa ni kutenda wema katika maisha yetu yote,” alisema Gideon, alipomaliza kusimulia hivyo tu, akaanza kulia.
Hakukuwa na mtu aliyejua kile kilichokuwa kikiendelea. Walishangaa, mke wake akaanza kumbembeleza akimtaka kunyamaza. Alichokifanya Gideon ni kusimama na kuelekea chumbani kwake. Huko, akajilaza kitandani, alikuwa akiendelea kulia tu.
Wakati akiwa kwenye majonzi, akasikia simu ya mezani sebuleni ikiita, ikapokelewa na David ambaye alisikia sauti ya mwanamke ikihitaji kuzungumza na baba yake. Akamuita, Gideon akaelekea sebuleni, akachukua mkonga wa simu na kuupeleka sikioni.
“Umekwishamuua?” lilikuwa swali la kwanza la Lucy aliyesikika kutoka upande wa pili.
“Mbona unauliza kibabe jamani?”
“Sasa unataka nikubembeleze? Nitambembelezaje mtu asiyenisikiliza? Hunijali, unataka nikubembelezeje?” aliuliza Lucy.
“Si hivyo!”
“Kumbe?”
“Naomba unipe muda kwanza,” alisema Gideon.
“Sawa. Najua hunipendi. Najua unanichukia, najua hunisikilizi, sawa, si hunipendi, sawa, niache na maisha yangu,” alisema Lucy na kilio kuanza kusikika, mbaya zaidi, hapohapo simu ikawekwa pembeni.
Mapigo ya moyo wa Gideon yakaanza kudunda kwa nguvu, hakuamini kile alichokisikia, akaanza kuita, simu haikuwa ikiita kuonyesha kwamba ilikatwa na mkonga kuwekwa pembeni.
Alichanganyikiwa, hakutaka kumpoteza Lucy, alikuwa tayari kupoteza kila kitu katika maisha yake lakini si msichana huyo. Hakutaka kubaki nyumbani, haraka sana akatoka nje huku kila mtu akimshangaa.
“Mume wangu! Kuna nini?” aliuliza Lilian huku akimwangalia mumewe.
“Nakuja!”
“Unasemaje?” aliuliza Lilian, hakuwa amesikia vizuri.
“Nakujaaaa..” alisema Gideon kwa sauti ya juu iliyokuwa na ukali.
Lilian hakuamini alichokisikia, hakuwahi kumsikia mume wake akimwambia kwa ukali kama siku hiyo, akahisi kulikuwa na tatizo. Watoto wake, David na Davis nao walikuwa wakishangaa, wakamuona baba yao akielekea nje, haraka sana David akaelekea dirishani na kumchungulia baba yake ambaye akafungua mlango wa gari, akaingia na kuondoka zake.
Njiani, Gideon alichanganyikiwa, ilikuwa ni lazima kuzungumza na Lucy, alimkwaza hivyo alitaka kumuomba msamaha. Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani kwa msichana huyo, kitu cha kwanza akapiga magoti na kumuomba msamaha kiasi kwamba mpaka machozi yakaanza kumtiririka.
“Nisamehe mpenzi kwa kuchelewa kufanya hivyo,” alisema Gideon huku akilia.
“Nimesema niache! Niache huko wewe si hutaki kuuridhisha moyo wangu! Niache,” alisema Lucy huku akilia.
“Nisamehe mpenzi. Nakuahidi kwamba leo nitaua! Nakuahidi kwamba nitammaliza leo hii hii!” alisema Gideon.
“Sitaki tena! Niache!”
“Mpenzi! Haki ya Mungu leo namuua! Nakwambia ukweli leo simuachi. Nipe muda, mpaka kesho asubuhi utasikia kashakufa,” alisema Gideon, kila alipomwangalia Lucy, nguvu ya kufanya mauaji ilizidi kumkamata.
Ilikuwa ni vigumu kuamini kile kilichokuwa kikiendelea. Mwanaume aliyekuwa na nguvu, msimamo thabiti leo alimpigia magoti mpenzi wake na kumuomba ampe muda wa kumuua mke wake. Lucy akazidi kiburi moyoni mwake, akazidi kumkatalia Gideon asiende kumuua mke wake kwa kuwa hakutaka kumjali lakini mwanaume huyo alihitaji muda, na siku hiyo usiku angemuua kama alivyokuwa amemwambia.
“Na usipomuua?” aliuliza Lucy.
“Niache! Nisipomuua! Niache tu. Nakusisitizia kwamba ni lazima nimuue,” alisema Gideon, Lucy akakubaliana naye, akamwambia aondoke lakini ajue kwamba mpaka inafika asubuhi huku ikiwa bado hajamuua Lilian basi ndiyo utakuwua mwisho wa kuwa wapenzi.
“Nakuahidi! Usiku wa leo namuua! Namuua, niamini, ni lazima nimuue,” alisema Gideon, Lucy akamruhusu kuondoka.
Kichwa cha Gideon kikaanza kufikiria kitu kimoja tu, kumuua mke wake aliyemwambia kila siku kwamba alikuwa akimpenda.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-07

Hakukuwa na kipindi ambacho Gideon alikuwa na wakati mgumu kama kipindi hicho. Moyo wake ulikuwa na mawazo tele, kile kilichokuwa kikiendelea maishani mwake kilimsumbua kupita kawaida.
Alimpenda sana mkewe, Lilian, alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile kwa ajili yake lakini kwa kitendo cha msichana Lucy kuingilia kilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na ugumu wa kutunza ahadi aliyomwambia siku ya harusi yake kwamba angeishi naye bega kwa bega mpaka vifo vyao.
Hakutaka kuona Lilian akifariki dunia lakini kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa Lucy, wakati mwingine aliona kwamba huo ndiyo wakati wa kufanya ukatili huo, alitakiwa kufumba macho lakini mwisho wa siku kuhakikisha anamuua kwa mkono wake kuufurahisha mchepuko wake.
Alipofika nyumbani, akamkuta Lilian akiwa sebuleni akimsubiri. Siku zote mwanamke huyo alikuwa mtu wa kumsubiri mume wake, haikujalisha alikuwa katika maumivu makubwa kiasi gani, wakati mumewe akiwa nje ya nyumba hiyo, ilikuwa ni lazima amsubiri na hata kama angelala, ni bora kulala sebuleni kuliko kwenda kulala chumbani na wakati mume wake hakuwa amerudi.
Gideon akaanza kumsogelea mke wake, alipomfikia, akakaa katika kochi lile alilokaa mke wake na kuanza kuzungumza naye. Alimuonyeshea tabasamu, alikenua na kuzungumza naye kwa kirefu, alimsisitizia kwamba alimpenda japokuwa alikuwa akipitia katika kipindi kigumu kama hicho.
Lilian akafarijika na kumshukuru Mungu mno kwa kumpatia mwanaume mvumilivu, aliyekuwa akimsaidia kwa hali na mali kama ilivyokuwa kwa Gideon pasipo kujua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa akitamani kumuua ili kumfurahisha mwanamke wa pembeni.
“Ninakupenda mume wangu,” alisema Gideon.
“Nakupenda pia!”
Gideon akamwambia mke wake kwamba usiku huo alitaka kumtoa mtoko wa usiku waende katika mgahawa mmoja na kula chakula. Hilo halikuwa tatizo kwa Lilian, alikubaliana naye na hivyo kujiandaa.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi kwa Gideon kukamilisha kile alichokihitaji. Akaelekea jikoni na kuchukua kisu, akakiweka kiunoni na kuondoka nyumbani hapo.
“Nitamuua hukohuko!” alisema Gideon.
Njiani, ndani ya gari walikuwa wakizungumza mambo mengi, katika kila sentensi kumi alizoongea Gideon ilikuwa ni lazima kumwambia mke wake jinsi gani alimpenda. Alitaka mwanamke huyo amuamini kwa kila kitu, alimuondoa hofu ili asiogope kwa kitu chochote kile ambacho kingekwenda kutokea huko walipokuwa wakienda.
Kichwani mwake ni sauti ya Lucy tu ndiyo iliyokuwa ikisikika. Aliisikia vilivyo ikimwambia kwamba kama kweli alitaka kuishi naye basi ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba anamuua mwanamke huyo ili wapate nafasi ya kuyafurahia maisha yao milele.
Wakafika katika Mgahawa wa Jumanj uliokuwa Masaki jijini Dar es Salaam na kukaa katika meza moja na kuagiza chakula. Muda wote Gideon alikuwa akijipapasa kiunoni kuhakikisha kama kisu chake kilikuwepo.
Lilian alikuwa na furaha, kila alipomwangalia mume wake, alizidi kumpenda, kitendo cha kumtoa mtoko wa usiku kilionyesha ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alimpenda na kumthamini japokuwa alikuwa katika hali ya ugonjwa mkubwa aliokuwa nayo. Baada ya kumaliza, wakaondoka, wakaingia ndani ya gari na safari ya kuelekea ufukweni kuanza.
“Twende ufukweni?” aliuliza Lilian huku akimwangalia mume wake.
“Ndiyo! Tukapigwe na upepo kisha turudi nyumbani,” alisema Gideon huku akiachia tabasamu kumficha ukweli wa kile walichotaka kwenda kukifanya ufukweni.
“Mmh!”
“Usijali mke wangu! Upo kwenye mikono salama ya mwanaume wa shoka,” alisema Gideon na kutabasamu.
Lilian hakuwa na hisia zozote mbaya, kwa kuwa alikuwa na mume wake aliamini kwamba safari hiyo ilikuwa ni ya amani kabisa. Hawakuchukua muda mrefu wakafika ufukweni, ilikuwa ni usiku, hakukuwa na watu wengi, wachache waliokuwepo walikuwa katika baa kubwa iliyojengwa ufukweni hapo.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya kumuua mke wake kwa kumchoma kisu. Akamvuta kimahaba kwenye kiti kile alichokuwepo na kumkumbatia kimahaba huku akimsisitizia kwamba angekuwa naye bega kwa bega mpaka vifo vyao.
“Hii ndiyo nafasi,” alijisemea Gideon.
Hakutaka kuchelewa, akaupeleka mkono wake kiuoni, akachomolea shati lake na kutoa kisu alichokiweka kiunoni mwake. Alitaka kumchoka mke wake huku wakiwa wamekumbatiana kwani ndiyo ilikuwa nafasi pekee aliyokuwa nayo ambayo alitakiwa kumfurahisha Lucy.
“Moja...mbili...ta...” alihesabu lakini hata kabla hajamaliza tu, ghafla akashtuka kusikia kioo cha gari kikigongwa, haraka sana akakirudisha kisu kiunoni mwake na kushusha kioo.
“Vipi?”
“Ebwana haruhusiwa mtu kupaki hapa!” alisikika mwanaume mmoja, alikuwa mlinzi maeneo hayo.
“Haruhusiwi mtu?”
“Ndiyo! Liondoe gari lako hapa,” alisema mlinzi huyo huku akiwa na kirungu mkononi mwake, hapohapo mlinzi mwingine akaja.
“Vipi mbona wamepaki hapa?” aliuliza huyo mwingine aliyefika mahali hapo.
“Nimewaambia sehemu hii hairuhusiwi na inatakiwa waondoke haraka sana,” alisema mlinzi wa kwanza kufika hapo.
Gideon hakutaka kubisha wala kuongea kitu chochote kile, akawasha gari hilo na kuondoka mahali hapo. Alichanganyikiwa, usiku huo ndiyo ulikuwa wa mwisho aliopewa na Lucy na ilimaanisha kwamba kama asingefanikiwa kumuua basi huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuwa naye.
Kichwa chake kilimuuma, hakuzungumza chochote na mkewe, alifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya kwani ilikuwa ni lazima kuhakikisha Lilian anakufa haraka sana hata kabla asubuhi haijafika.
Wakati wakiwa njiani wakirudi nyumbani, Gideon akalisimamisha gari lake pembeni ya barabara. Lilian akashtuka, mahali gari liliposimama hakukuwa na mtu yeyote, kila kona kulikuwa na giza huku ukimya mkubwa ukiwa umetawala.
“Kuna nini? Mbona umesimamisha gari?” aliuliza Lilian huku akimwangalia mume wake.
Gideon hakujibu kitu, akazima taa, akateremka na kwenda katika upande aliokaa Lilian, akaufungua mlango na kuanza kumwangalia mke wake. Hapo ndipo Lilian alipogundua kwamba Gideon alibadilika, hakuwa yule aliyekuwa akimfahamu, sura ya upendo, kwa wakati huo alikuwa kama mtu mwingine kabisa, mwenye roho mbaya ambaye hakuonekana kuwa na masihara yoyote yale.
“Mume wangu...” aliita Lilian huku akimwangalia Gideon aliyebadilika ghafla.
Hakutaka kuchelewa, hakukuwa na mtu mahali popote pale, walikuwa wao tu, kwa kutumia nguvu zake, akamvuta Lilian na kumuweka mbele yake nje ya gari lile na kuanza kumkaba huku akiwa nyuma mithili ya mwizi aliyekuwa akimkaba mtu kwa lengo kumuibia pesa zake.
“Aagghh...” Lilian akaanza kuguna kwa maumivu makali, alitamani kupiga kelele lakini kila alipojitahidi kufanya hivyo, sauti haikutoka, mishipa ya damu ikazuiliwa kusafirisha damu kwenda kichwani, akabaki akianza kukakamaa tu, alitamani kujiondoa mikononi mwake lakini alishindwa.
Gideon hakutaka kuacha, aliendelea kumkaba zaidi na zaidi, pumzi zikaanza kukata, kila alipotaka kuomba msaada kwa kupiga kelele alishindwa kabisa na mwisho wa siku macho yake kuanza kuwa mazito, ndani ya dakika chache tu, akayafumba macho yake, kasi ya udundaji wa mapigo yake ya moyo yakapungua na mwisho wa siku moyo kusimama na kufariki dunia.
“Ahsante Mungu!”
Hakutaka kuchelewa, haraka sana akamrudisha ndani ya gari, kabla ya kuliondoa mahali hapo. Haraka sana akaanza kuelekea katika Hospitali ya St. Monica iliyokuwa Upanga kwa lengo la kujifanya kuangalia tatizo lilikuwa nini.
Akaliwasha gari lake na kuondoka mahali hapo. Mwili wa mkewe ulikuwa katika kiti cha pembeni, hakuumia, moyoni mwake alijiona kufanya jambo la kawaida ambalo alihitaji kupongezwa kwa nguvu kubwa kwani japokuwa ulikuwa mtihani mzito lakini alifanikiwa kwa asilimia mia moja.
Hakuchukua muda mrefu akafika Upanga, akaishusha maiti ya mkewe na kuwaita manesi ambao walikwenda na machela na kuilaza na kuanza kuisukuma kuelekea ndani ya hospitali hiyo. Ili kuonekana kwamba aliumia, machozi yalikuwa yakimtoka huku muda mwingi akimuita mke wake.
“Mke wangu amka! Mke wangu usiniache...amka mke wangu...” alisema Gideon huku akijifanya kulia kama mtoto machozi yaliyoonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa ameumia.
Mke wake akaingizwa ndani ya chumba kimoja kwa lengo la kupewa huduma. Pale nje alipobaki, bado Gideon alikuwa akilia kwa uchungu, kila mtu aliyekuwa akimwangalia alimuonea huruma huku wengine wakimbembeleza anyamaze kwani alionekana kuumia mno.
“Nyamaza kaka! Piga moyo konde,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa pembeni.
“Mke wangu! Mke wangu amekufa...nitaishi vipi bila mke wangu! Dokta ninamtaka mke wangu,” alisema Gideon huku akianza kuupiga mlango wa chumba alichoingizwa mke wake.
Kama ni maigizo, Gideon alijua kuigiza, alikuwa akilia kama mtoto mdogo huku akionekana kuumia mno kwa kifo cha mke wake. Hakukuwa na mtu aliyejua ukweli wa kilichokuwa kimetokea. Mule chumbani, Dk. Gibson alimwangalia Lilian an kugundua kwamba mwanamke huyo alikuwa amefariki dunia.
“Pole sana Gideon,” alisema Dk. Gibson huku akimwangalia Gideon.
“Niambie ukweli! Mke wangu amekufa?”
“Pole sana Gideon!”
“Niambie ukweli dokta...mke wangu amekufa?” aliuliza Gideon huku akimwangalia daktari.
“Ndiyo! Amekufa!” alijibu daktari kwa sauti ya chini.
Kilio cha Gideon kikaongezeka zaidi, alitaka kumthibitishia daktari kwamba alikuwa ameumia mno. Katika kila neno alilokuwa akilizungumza mahali hapo alisema kwamba kansa aliyokuwa akiugua mke wake ndiyo iliyoondoa uhai wake.
Usiku huo hakutaka kuondoka hospitalini hapo, ilikuwa ni lazima kufanya kila liwezekanalo daktari asiangalie kifo kilichomuua mke wake kwani angegundua kwamba alikabwa hivyo kufanya harakaharaka kushinikiza maiti ipelekwe mochwari na yeye kufanya mipango ya mazishi.
Akawapigia simu ndugu zake na kuwaambia kilichotokea, kila mmoja alihuzunuka, watoto wake, David na Davis walilia sana, hawakuamini kama kweli huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mama yao. Waliichukia kansa, waliahidi kusoma kwa bidii na mwisho wa siku kuwasaidia watu waliokuwa wakiteseka kwa magonjwa ya kansa ambayo yalikuwa yakiua watu kwa nguvu mno.
Taarifa zilipomfikia Lucy, hakuamini, kwanza akatabasamu, akainuka kitandani na kurukaruka kwa furaha. Hatimaye kitu alichokitaka kilifanikiwa. Ili kuishi kwa furaha na mwanaume huyo, Gideon hakutakiwa kuishia kumuua mke wake tu bali alitakiwa kufanya kazi nyingine, kumwambia Gideon kuwaua watoto wake mapacha, David na Davis ambao aliona kama wangekuwa kikwazo chake hapo baadaye.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-08

Muda wote aliokuwa chumbani Lucy alikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli Gideon alichukua uamuzi wa kumuua mkewe kisa yeye. Alijisifu kwa kufanikiwa kuushika moyo wa mwanaume huyo vilivyo, kila alipofikiria namna alivyomchombeza kwa maneno mengi ya mahaba wawapo chumbani mpaka kufanya lile alilotaka alifanye, hakika alijiona shujaa.
Yeye alikuwa miongoni mwa watu waliokwenda nyumbani kwa Gideon kushiriki mazishi ya Lilian, alipokuwa mahali hapo, uso wake ulionyesha majonzi makubwa na wakati mwingine machozi yakimtoka. Alijifanya kuhuzinika hata zaidi ya ndugu wa marehemu waliokuwa mahali hapo.
Alichokifanya ni kumfuata Gideon na kuanza kumfariji, ilikuwa ni vigumu kwa mtu mwingine kugundua kwamba wauaji waliokuwa wamemmaliza Lilian walikuwa hao wawili. Walionekana kuwa na huzuni mno huku kila mmoja akijua kwamba kilichomuua mwanamke huyo kilikuwa ni ugonjwa wa kansa, hakukuwa na taarifa kama mwanamke huyo alikuwa amekufa kwa kukabwa na mume wake.
“Kansa ni ugonjwa hatari, nasikia marehemu alikuwa akiteseka sana,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa msibani hapo.
“Ndiyo! Huu ugonjwa si wa kuupuuzia, wakati mwingine tunatakiwa kuogopa hata zaidi ya tunavyoogopa Ugonjwa wa Ukimwi,” alisema mwanaume mwingine.
Watu wengine waliweka makundi msibani hapo, kila mmoja aliyemzungumzia Lilian, alimzungumzia jinsi alivyoteseka kipindi kirefu kwa ugonjwa wa kansa ya damu.
Watoto wake aliowaacha, David na Davis walikuwa wakilia, hawakuamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mama yao, kama walivyoamini watu wengine nao pia walijua kuwa ugonjwa wa kansa ya damu ndiyo uliokuwa umemuua mama yao. Hawakuhisi kabisa kama baba yao ndiye aliyekuwa amemuua mama yao kwa lengo la kuishi na mwanamke mwingine.
Walibembelezwa na watu wengine, wakafarijiwa mpaka walipokwenda makaburini na Lilian kuzikwa huko. Hapo ndipo Gideon akajisikia amani, akaona kwamba alikuwa amemaliza kila kitu kwani kama ni kumzika mkewe, alifanya hivyo huku akiwa amejitahidi kuwazuia madaktari kuangalia ni kitu gani hasa kilikuwa kifo cha mke wake huyo.
Maisha mapya yakaanza, mapenzi yake kwa Lucy yaliongezeka, kila siku walikuwa wakikutana na kukaa pamoja hotelini, wakati mwingine hakuwa akilala nyumbani, alilala hotelini na mwanamke huyo. Hakutaka kumpeleka nyumbani kwake, kitu cha kwanza kilikuwa ni kusubiri mpaka miezi mitatu ipite ndiyo amchukue mwanamke huyo na kwenda naye nyumbani kwake.
Aliwafariji watoto wake, siku nyingine aliwatoa mtoko na kwenda nao sehemu. Alijua kwamba yeye ndiye mtu pekee aliyekuwa amebaki katika maisha yao, alijitahidi kuwarudishia furaha waliyokuwanayo kabla kwa kuwaambia kwamba kila kitu kingekwenda sawa kama tu wangeamini kuwa Mungu wa Mbinguni angewafanya kusahau kila kitu kilichotokea. Iliwachukua muda mpaka waliporudi katika hali ya kawaida kuendelea na maisha yao.
“Kuna kitu nataka kuzungumza nayi,” alisema Gideon, alikuwa akiwaambia watoto wake ambao walikaa na kumsikiliza, walitaka kujua ni kitu gani walitaka kuwaambia.
“Hakuna shida.”
“Ninataka kuoa mwanamke mwingine. Siwezi kuishi bila kuwa na mtu mwingine, sina furaha, kila kitu ninachokiangalia chumbani kinanikumbusha mama yenu,” alisema Gideon huku akijifanya kuingiwa na huzuni ya ghafla.
“Kuoa mwanamke mwingine?” aliuliza Davis aliyekuwa muongeaji sana.
“Ndiyo! Mnanishauri vipi?” aliuliza, alitaka kuwashirikisha katika kila jambo.
“Sioni kama ni tatizo,” alisema Davis.
“Na wewe David?”
“Hakuna tatizo japo lingekuwa suala muhimu kama tungemfahamu mwanamke huyo,” alisema David huku akimwangalia baba yake.
Hilo halikuwa tatizo kabisa, siku iliyofuata Gideon akamleta Lucy nyumbani hapo na kuwaambia watoto wake kwamba huyo ndiye alikuwa mwanamke aliyetaka kuishi naye. Kila mmoja alishangaa, hawakuamini kuona mwanamke yuleyule ambaye alikuwa akishirikiana na baba yake ndiye ambaye alitakiwa kuwa mama yao wa kambo.
Hawakuuliza swali, wakakubaliana na baba yao na hivyo kuanza kufanya mikakati ya harusi huku tayari ikiwa imepita miezi mitatu tangu Lilian auawe kinyama na mume wake huyo. Hilo likafanikiwa na baada ya mwezi mmoja harusi kubwa na ya kifahari ikafanyika jijini Dar es Salaam na kuwa miongoni mwa harusi zilizohudhuriwa na watu wengi mashuhuri.
Alichokuwa akikihitaji Lucy alikipata, mbele yake kulikuwa na kazi moja tu aliyokuwa ameibakiza, kuhakikisha watoto mapacha, David na Davis wanakufa kwa gharama yoyote ile. Hakutaka kumtumia muuaji kutoka nje, alijua kabisa kwamba kama angemtumia Gideon lingekuwa jambo jepesi sana kukamilisha mpango huo.
Hakutaka kuwa na haraka, kitu ambacho alikuwa makini nacho kwa muda huo ni kutokushika mimba. Alijua tarehe zake, alijua ni siku gani kwake zilikuwa za hatari, alijitahidi kujikinga kwa kila kitu asishike mimba mpaka pale ambapo angekubaliana na Gideon kwamba watoto hao walitakiwa kufa haraka sana.
Ndoa ilipofikisha miezi sita ndipo akaanza kumwambia lengo lake, alianza kama utanj vile, alijifanya kulalamika kwamba hakuwa na furaha ndani ya nyumba, maisha yake yalikuwa mabaya mno na kuna wakati alitamani kujiua kwani alijiona kutokuwa na thamani yoyote ile.
Kazi kubwa ya Gideon ikawa ni kumtia moyo pasipo kujua mwanamke huyo alikuwa na maana gani nyuma ya pazia. Mwezi mmoja baadaye ndipo Lucy akamwambia ukweli kwamba Gideon alitakiwa kufanya kitu kimoja tu ili awe na furaha, vinginevyo asingeweza kuwa na furaha maisha yake yote.
“Unataka nifanye nini mpenzi?” aliuliza Gideon huku akimwangalia mke wake.
“Ninataka furaha! Ninataka niishi mimi na wewe, sipo tayari kuona nalea watoto wa mwanamke mwingine,” alisema Lucy maneno yaliyomshtua Gideon.
“Unamaanisha nini?”
“Sitaki kuwaona watoto wako ndani ya nyumba yangu,” alisema Lucy huku akimwangalia mume wake, ili kuonyesha kwamba aliumia mno kuwaona watu hao ndani ya nyuma hiyo, akaanza kulia.
“Usilie mpenzi! Nitahakikisha nawapeleka shule za bording wakasome huko,” alisema Gideon.
“Sitaki kuwaona kabisa, ukiwapeleka shule, kuna siku watarudi, yaani sitaki kuwaona kabisa,” alisema Lucy.
“Unamaanisha nini?”
“Wafanye kama ulivyofanya kwa mkeo ili niwe na furaha, sitaki kuwaona,” alisema Lucy na kuanza kulia.
Gideon alishtuka mno, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, alimwangalia vizuri mke wake, uso wake ulionyesha kumaanisha kile alichokuwa akikizungumza. Kwake, kuwaua watoto wake lilikuwa suala jingine ambalo aliona kabisa lisingewezekana kabisa.
Akamuuliza Lucy mara mbilimbili juu ya kile alichokuwa amekisema, alisisitiza kwamba ni lazima awaue watoto wake vinginevyo angeondoka ndani ya nyumba hiyo. Huo ulikuwa mtihani mgumu, hakukubali, aligombana na Lucy na wakati mwingine kumkaripia lakini hakuwa radhi kuona akiwaua watoto wake kama alivyofanya kwa mke wake.
Nyumba ni kama iliwaka moto, kuna kipindi hawakuwa wakiongea, kila Gideon aliporudi nyumbani, kitandani Lucy aligeukia upande mwingine na kujikausha tu. Gideon alikuwa akimbembeleza lakini mwanamke huyo hakutaka kukubali, msimamo wake ulikuwa uleule kwamba kama mume wake alitaka amani irudi ndani ya nyumba basi ilikuwa ni lazima kuhakikisha anawaua watoto wake.
“Ila Mungu hapendi,” alisema Gideon.
“Ulipomuua mke wako alipenda?”
“Nisikilize Lucy!”
“Gideon! Waue hawa nguchiro, ukikataa kufanya hivyo nitakwenda kueleza polisi jinsi ulivyomuua mke wako,” alisema Lucy huku akimwangalia Gideon kwa hasira.
“Yamekuwa hayo tena!”
“Hivi unanionaje? Mimi ni mtu mwenye misimamo, sasa kama unabisha, subiri mpaka Jumamosi uone kama sijakwenda kutoa taarifa polisi, si hutaki, sasa utaona,” alisema Lucy na kugeukia upande wa ukutani kitandani.
Gideon alichanganyikiwa, alijiona kuwa kwenye wakati mgumu, alimpenda sana Lucy lakini pia aliwapenda mno watoto wake. Kitendo cha kuambiwa na mwanamke huyo kwamba asipowamaliza basi angekwenda kuripoti polisi kwamba alimuua mke wake kilizidi kumtisha.
“Lakini Lucy! Unajua nakupenda sana mke wangu! Kwa nini unanifanyia hivi?” aliuliza Gideon huku naye akianza kulia. Lucy hakujibu, akanyamaza, alipoona Gideon analalamika sana, akatoa bonge moja la msonyo.
“Nyooooooo...” alisonya mwanamke huyo na kujifunika shuka.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-09

“Is there any report from Tanzania?” (kuna ripoti yoyote kutoka nchini Tanzania) lilikuwa swali moja kutoka kwa Mzee Armando Kurtiz.
“Yes sir! Our three men had been shot and gone,” (ndiyo kuu! Watu wetu walipigwa risasi na kufa) alisema mwanaume mmoja.
Mzee Armando akanyamaza, akawaangalia vijana wake, uso wake ulijaa ndita, alikasirika baada ya kupewa taarifa kwamba vijana wake aliokuwa amewatuma kwenda nchini Tanzania walikuwa wamepigwa risasi na kufa.
Huyo alikuwa muuzaji namba moja wa madawa ya kulevya duniani. Alikuwa mzee mwenye pesa nyingi aliyejilimbikizia pesa zake na kutanua kadiri alivyoweza. Aliishika Serikali ya Ujerumani, alifanya kitu chochote kile alichotaka na kumfanya kuwa mtu mwenye heshima kubwa nchini humo.
Kila mtu alijua kwamba alikuwa muuzaji wa madawa ya kulevya namba moja lakini hakukuwa na mtu aliyemsumbua hata kidogo. Alisambaza madawa hayo kila kona na kila mtu aliyesimama mbele yake kwa ajili ya kumzuia, alimuua pasipo kipingamizi chochote kile.
Aliwamaliza mawaziri wengi, ndani ya polisi alikuwa na watu wengi aliokuwa akishirikiana nao, kila mipango ya kukamatwa kwake ilipokuwa ikisukwa, alipewa taarifa na kuwamaliza watu wote waliojifanya kimbembele.
Wapelelezi wengi waliokuwa wakitumwa kwa ajili ya kumkamata au hata kumuua, aliwaua yeye hata kabla ya kufikiwa. Kila mtu alimlalamikia, serikali ya Ujerumani ikagombana na serikali za nchi nyingine kwa ajili ya Mzee Armando aliyekuwa mwiba mkali kwa Wamarekani ambao walikesha huku wakimtafuta, walituma majasusi wao kutoka CIA lakini mwisho wa siku waliuawa wao.
Mtu aliyekuwa akimchanganya kichwa kipindi hicho alikuwa Mzee Msuya, Mchaga aliyekuwa akifanya biashara hiyo kwa kupokea madawa ya kulevya kutoka nchini Ujerumani ambayo yalichukuliwa kutoka katika Jiji la Karach nchini Kuwait na kuyapeleka huko.
Mtu huyo alikuwa na biashara kubwa, alijua kucheza na wafanyabiashara wenzake, alijua kuwatapeli. Siku alipopewa mzigo mkubwa wa madawa ya kulevya kutoka kwa Mzee Armando, moyo wake ukafikiria kumtapeli tu.
Hayo yalikuwa kama matusi kwa Armando, alichokifanya ni kuwatuma vijana wake kwenda kule ili kumuua Mzee Msuya lakini kitu cha ajabu hata kabla hawajamfikia, wakauawa wao kitu kilichomchanganya sana mzee huyo.
“Natuma watu wengine kwenda huko. CIA wananitafuta usiku na mchana, wananiogopa, kama naogopwa na watu hao, kwa nini Msuya asiniogope? Kwa nini nisimmalize? Kurt, tuma vijana wengine wanne waende huko, utanipa taarifa,” alisema Mzee Armando huku akionekana kuwa na hasira kali.
“Sawa bosi. Nitakupa majibu baada ya kuwatuma kwenda huko,” alisema Kurt na kuondoka nyumbani hapo.
***
Moyo wa Gideon ulikuwa na presha kubwa, alijiona kuwa na mtihani mkubwa mbele yake, kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kuwamaliza watoto wake kilimchanganya mno.
Mapenzi ya msichana Lucy yalimchanganya, alimpenda mno na alikuwa tayari kupoteza kitu chochote lakini si msichana huyo aliyekuwa akiuendesha moyo wake kupita kawaida.
Jukumu alilompa lilikuwa kubwa, mbali na mapenzi aliyokuwa nayo kwa msichana huyo lakini pia aliwapenda watoto wake mapacha. Walikuwa watoto wazuri ambao kila siku walimuhitaji, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya lakini kwa kuwa Lucy aling’ang’ania sana awamalize watoto wake hakuwa na pingamizi lolote zaidi ya kukubaliana naye kuwamaliza watoto wake.
Akaanza kusuka mipango, kuwaua halikuwa jambo la kawaida, ilikuwa ni lazima ajipange ili awamalize huku kukiwa hakuna mtu yeyote atakayejua kama kweli yeye ndiye aliyewaua watoto hao kwa mkono wake.
Alichokifikiria ni kuwapeleka msituni ambapo huko angewapiga risasi halafu na yeye mwenyewe angejipiga ya mguu kuonyesha kwamba kuna mtu aliwateka, akawapeleka msituni na baadaye kuwaua watoto wake na yeye kupigwa risasi ya mguu kama ishara ya kumuonya kutokana na upinzani mkubwa aliokuwanao sokoni.
“Hii itafaa sana. Nitasema kwamba hizi biashara ninazozifanya zina maadui wengi, wameamua kuwaua watoto wangu na kunipiga risasi kama ishara ya kunionya kwa kile nilichokuwa nikikifanya sokoni,” aliwaza Gideon.
Hakutaka kubaki kimya, akaanza kuzungumza na Lucy na kumwambia jinsi ambavyo alitakiwa kufanya mauaji hayo, ni kwamba angewachukua na kuelekea nao porini ambapo huko angewamaliza kama alivyommaliza mama yao.
“Una uhakika utawamaliza?” aliuliza Lucy.
“Ndiyo mke wangu! Nitawamaliza. Kama nilimuua mama yao, nitashindwa vipi kuwaua watoto hawa, tena wawili tu, hawawezi kunitisha,” alisema Gideon huku akimwangalia mke wake.
Huo ulikuwa usiku, wakati wakizungumza hayo, hawakujua kama David alikuwa nje ya mlango wa chumba chao. Alitoka chooni, alikuwa akielekea chumbani kwake, alipopita karibu na mlango wa chumba cha wazazi wake, akawasikia wakizungumza tena kwa sauti ya kawaida kwa kuamini kuwa kwa usiku huo kila mmoja alikuwa amelala.
Alitamani kuondoka na kutokusikiliza mazungumzo hayo lakini moyo wake ulikuwa mgumu kufanya hivyo, akasimama, akalala chini na kuliweka sikio lake karibu na uwazi wa mlango kwa chini na kuanza kusikiliza kila kitu kilichokuwa kikizungumwa.
Alisikia kila kitu, hapo ndipo akagundua kwamba mama yao hakufa kwa kansa kama walivyokuwa wakihisi bali baba yao aliamua kumuua kwa mkono wake. Hilo lilimtisha lakini jambo lililomtisha zaidi ni kwamba kulikuwa na watu wawili waliotakiwa kufa, mipango ya kuwamaliza ilikuwa ikisukwa. Hakujua ni wakina nani lakini baada ya kusikia kwamba kama baba yao alimuua mama yao, angeshindwa vipi kuwaua na wao, akajua kwamba watu waliokuwa wakizungumzwa alikuwa yeye na ndugu yake.
“Una uhakika utawamaliza?” alisikia Lucy akiuliza.
“Ndiyo mke wangu! Nitawamaliza. Kama nilimuua mama yao, nitashindwa vipi kuwaua watoto hawa, tena wawili tu, hawawezi kunitisha,” aliisikia sauti ya baba yake.
Hakutaka kubaki mlangoni hapo, akakimbilia mpaka chumbani, akakaa kitandani na kuanza kulia. Hakuamini kama kweli kifo cha mama yao hakikuwa ni ugonjwa wa kansa kama kila mtu alivyokuwa akijua bali baba yao aliamua kumuua kwa kuwa alitaka kuishi na mwanamke huyo.
Hilo lilikuwa jambo kubwa sana kuligundua, akatamani kumwamsha Davis na kumwambia kilichokuwa kikiendelea kwamba nao walikuwa katika mpango kabambe wa kuuawa na baba yao ambaye kila siku walimwamini kwamba alikuwa mtu mzuri aliyekuwa akiwalea katika malezi mema kabisa.
“Baba alimuua mama! Baba anataka kutuua na sisi!” alijisemea huku akionekana kuchanganyikiwa, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kumchukia baba yake, hakumpenda, kila alipokuwa akimuona, hasira ilimkaba kooni na kutamani kushika kisu na kumuua. Chuki yake haikuishia kwa baba yake tu bali hata kwa Lucy ambaye alitakiwa kumuheshimu kama mama yake wa kumzaa.
Kila alipoiona sura ya mwanamke huyo alitamani kumfuata na kumchoma kisu cha tumbo. Aliamini kwamba mapenzi ya baba yake kwa mwanamke huyo ndiyo yalikuwa chanzo cha kila kitu na ndiyo maana mama yao alipokufa baba yao hakuchukua muda mrefu kumuoa Lucy na kumleta ndani ya nyumba hiyo.
Akaanza kuishi kwa hofu kwa kuona muda wowote ule wangeuawa kinyama na baba yao ambaye hakutaka kujali kuhusu wao, kitu pekee alichokijali ni kuona akimfurahisha mwanamke aliyekuwa akiishi naye tu.
Wakati David akiendelea kuishi kwa hofu upande wa pili Gideon alikuwa akijipanga, roho yake ilibadilika, hakuwa na huruma hata kidogo, kuhusu kumwaga damu kwake lilikuwa jambo la kawaida sana ambalo muda wowote ule angeweza kulifanya pasipo gharama yoyote ile.
Siku ziliendelea kwenda mbele, aliambiwa kwamba mpaka Jumamosi kila kitu kilitakiwa kuwa tayari, watoto hao walitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo. Akajipanga, ilipofika siku ya Ijumaa, akawaita watoto wake na kuwaambia kwamba kuna sehemu alitaka kwenda nao jioni ya siku hiyo.
“Wapi?” aliuliza David, alionekana kuwa na hofu.
“Sehemu fulani! Msijali, tutakwenda na kurudi salama kabisa,” alisema Gideon huku akiwaangalia kwa sura iliyoonyesha tabasamu pana.
Wakati yeye akipanga kwenda na watoto hao kwa lengo la kuwamaliza, upande wa nyuma Lucy alijipanga kivyake. Alijua dhahiri Gideon asingeweza kukamilisha kile alichokihitaji, hivyo alichoamua ni kujiongeza.
Akawasiliana na watu wawili, walikuwa marafiki zake waliokuwa na kundi kubwa la kihuni, alichokitaka ni kuwapa kazi ya kuwamaliza watoto hao ambao wangekwenda na baba yao msituni ambapo huko ndipo alipotakiwa kufanya mauaji hayo.
“Msitu gani?” aliuliza jamaa kwenye simu.
“Bila shaka ni Msitu wa Pande! Hakikisheni mnakuja karibu na nyumba yangu na kusubiri, akiondoka nao, na nyie anzeni kufuatilia gari hilo, wakifika msituni, wamalizeni watoto. Mume wangu msimguse. Narudia tena! Mume wangu msimguse,” alisema Lucy kwa msisitizo.
“Sawa madame!”
Hilo likafanyika haraka sana. Lucy akaongea na mumewe na kumwambia ratiba nzima hivyo muda wa kuondoka ulipofika, tayari vijana wale walifika na gari lao nyumbani hapo, Gideon alipoondoka nao tu, wakaanza kulifuatilia gari hilo.
Gideon hakujua kama alikuwa akifuatiliwa, alikuwa akizungumza na watoto wake ndani ya gari, alijaribu kuzungumza nao kwa furaha tele ili kuwaondoa hofu lakini kwa David hakuonekana kuwa na furaha kabisa kwani alijua kile kilichokuwa kikienda kutokea mbele ya safari.
Walikwenda mpaka walipofika katika Msitu wa Pande, akaliingiza gari, kiunoni mwake alihakikisha kama bastola yake ilikuwepo kwani ndiyo ambayo angeitumia kuwaulia watoto wake.
“Tumefika,” alisema Gideon, akazima gari, akaufungua mlango na kuteremka huku akiwataka watoto wake nao wateremke.
“Hapa msituni?” aliuliza Davis.
“Nimesema teremkeniiiiii...” alisema Gideon kwa sauti ya ukali na ya juu sana, wote wakaanza kutetemeka, wakaanza kuteremka kutoka garini.
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-10

Mzee Armando akawatuma vijana wake kuelekea nchini Tanzania, moyo wake ulikuwa na hasira mno, hakuamini kama Msuya, mwanaume aliyekuwa akifanya naye biashara ya madawa ya kulevya alimtapeli madawa yake na mbaya zaidi akawamaliza vijana aliokuwa amewatuma.
Akawatuma wengine kuelekea huko, moyo wake ulikuwa na hasira sana, baada ya vijana hao kuelekea nchini Tanzania, akaanza kuwasiliana nao kwenye simu na baada ya wiki moja akapigiwa simu na kijana mmoja na kumwambia kwamba wenzake walikuwa wameuawa, yule Msuya waliyekuwa wakimtafuta ili wammalize, aliwamaliza vijana wake wawili na kumuacha mmoja kwa lengo la kumpeleka taarifa.
“Unasemaje?” aliuliza Armando.
“Wenzangu wote wameuawa, wameniacha kwa lengo la kukupa taarifa ya kile kilichotokea. Huyu mtu ana ulinzi mkubwa sana,” alisema kijana aliyekuwa akizungumza naye kwenye simu.
“Wenzako wameuawa?”
“Ndiyo bosi! Wameniacha mimi tu,” alisema kijana huyo.
Akili yake ikaruka, hakuamini kilichokuwa kimetokea, kitendo cha vijana wake kuuawa kilimaanisha kwamba Mzee Msuya alikuwa mwanaume mwingine mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kitu chochote kile. Hakutaka kuona akiendelea kuwamaliza vijana wake, kwa kuwa yeye ndiye alikuwa na mtu mwenye mzigo ule, akaamua kuwaambia vijana wake kwamba alitakiwa kwenda Tanzania kupambana na huyo Msuya.
“Vipi kuhusu CIA?” aliuliza kijana mmoja.
“Sijali! Nimempa mzigo wa gharama kubwa mno, pasipo kumkabili, inamaana kwamba kila kitu kitakuwa kimepotea, ni lazima niende huko. Mpigie simu Theofil,” alisema mzee huyo na haraka sana simu kupigwa mpaka nchini Tanzania kwa kijana anayeitwa Theofil ambaye ndiye alikuwa akishughulika na baadhi ya wateja wake waliokuwa huko isipokuwa Mzee Msuya aliyekuwa akichukua mzigo mkubwa.
Simu ikapigwa, akaanza kuzungumza na kijana huyo, alimwambia lengo lake la kuondoka Ujerumani na kuelekea nchini Tanzania huku lengo kubwa likiwa ni kumuua Msuya ambaye alionekana kuwa mtu hatari.
CIA walikuwa wakimtafuta kila kona, walijua mahali alipokuwa akiishi lakini hakukuwa na mtu aliyediriki hata kuisogelea nyumba yake kwa kuwa kulikuwa na ulinzi mkali, ila mbali na ulinzi huo, asilimia tisini ya polisi nchini Ujerumani walikuwa upande wake hivyo kila mipango iliyokuwa ikipangwa kwa ajili ya kummaliza, aliipata haraka sana.
Akaiita familia yake na kuiambia kile kilichokuwa kikiendelea kwamba ni lazima aelekee nchini Tanzania kwa lengo la kupambana na Msuya kwani kwa kile alichokuwa amemfanyia, hakika alistahili kifo, hakutakiwa kubaki hai kwani kwake mzigo aliokuwa amempa mzee huyo kwa lengo la kumuuzia ulikuwa na thamani zaidi ya uhai wa mtu.
“Na CIA?” aliuliza mke wake.
“Nitapambana nao.”
“Utapambana nao?”
“Ndiyo! Naomba niende huko. Jericho, mwangalie ndugu yako, kwa lolote litakalotokea, pambana kumuokoa,” alisema Armando akimwambia mtoto wake wa kwanza aliyekuwa na miaka ishirini, Jericho.
“Haina shida. Natasha atakuwa salama,” alisema Jericho.
Hakuwa na muda wa kupoteza, haraka sana akaondoka kuelekea uwanja wa ndege ambapo akapanda ndege na kuanza safari ya kuelekea Tanzania, moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kumpata Msuya aliyejiona kuwa mjanja hata zaidi yake.
Njiani hakuacha kuzungumza na Theofil aliyemwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari, kumpata Msuya mwenyewe lilikuwa jambo gumu lakini kuipata familia yake lilikuwa jambo jepesi mno.
“Basi tuanze na hao! Nitataka kumuonyeshea kwamba mzigo aliokuwanao una gharama kuliko hata roho ya mtu,” alisema Armando.
“Sawa. Haina shida, nitafanya hivyo.”
“Sawa,” alisema Mzee Armando pasipo kujua kwamba upande wa pili, majasusi wa CIA kutoka nchini Marekani walipata taarifa kwamba mzee huyo alikuwa akielekea Tanzania, hivyo nao wakaanza kufuatilia ili kama ikiwezekana, wamkamate huko au hata kumuua kama tu angeleta ubishi.
***
Wakati Armando akiwa njiani kuelekea nchini Tanzania, tayari maofisa wa kijasusi wa CIA waliokuwa nchini Kenya walipigiwa simu kutoka nchini Marekani na kuambiwa kile kilichokuwa kikiendelea. Mwanaume aliyekuwa akitafutwa duniani kote kutokana na kujihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya alikuwa njiani kuelekea nchini Tanzania, hivyo ilikuwa ni lazima kumfuata na kumkamata huko.
Maofisa hao walipopigiwa simu, hawakutaka kuchelewa, haraka sana wakaondoka nchini humo walimokuwa wakifuatilia masuala ya kisiasa na kuanza kuelekea Tanzania. Njiani, kila mmoja alionekana kuwa na presha kubwa, Armando aliisumbua dunia, aliwasumbua kwa kipindi kirefu na kila mmoja akaona kuwa huo ndiyo ulikuwa wakati muafaka wa kumkamata na kuitangazia dunia kwamba Marekani haikuwa ikishindwa na kitu chochote kile.
Walichukua saa nne mpaka kufika nchini Tanzania. Hawakutaka kuondoka uwanja wa ndege, waliambiwa kwamba siku hiyo ya Jumamosi mwanaume huyo angeingia kwa ndege ya kukodi hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba wanampata kwa gharama yoyote ile na kama kungekuwa na ugumu wa kumkamata basi hawakuwa na budi kumuua.
“We want him alive, if he resists, kill him,” (tunamtaka akiwa hai, kama akibisha, muueni) alisikika mkurugenzi wa kitendo hicho cha kijasusi cha nchini Marekani.
Maofisa wanne waliendelea kusubiri, hapo uwanja wa ndege walikuwa wamejigawa, watatu walikuwa nje ya uwanja huo huku wakijifanya kumsubiri mwenzao lakini mwingine alikuwa katika ghorofa lililokuwa mbali kidogo na uwanja huo, juu kabisa huku akiwa na bunduki yake ya masafa marefu iitwayo Blaser R93 LRS2 ambayo ilikuwa na uwezo wa kupiga mpaka umbali wa mita mia tatu.
Alikuwa makini, kule ghorofani alipokuwa hakukuwa na mtu aliyemuona, mlango wa kuelekea huko alikuwa ameufunga, hakutaka mtu yeyote kumuingilia kwani alitaka kupata utulivu kabisa na kama ingetokea ubishi wowote wa mwanaume huyo kukamatwa basi angempiga risasi ya kichwa na kummaliza kabisa.
Kule juu alipokuwa alikiona vizuri kiwanja cha ndege, kwa kutumia darubini ndogo iliyokuwa katika bunduki ile aliweza kuona vitu kwa ukaribu kabisa. Baada ya kusubiri huko kwa saa moja, hatimaye ndege iliyombeba Armando ikaanza kutua katika uwanja huo. Iliposimama, mlango ukafunguliwa.
“Chris, he is here..” (Chris, amefika) alisema mdunguaji (sniper) aliyekuwa ghorofani.
“We are waiting for him! If he resists, just shoot him down, right?” (Tunamsubiri! Kama akikataa, mpige risasi, sawa?) alisema Chris.
“No problem,” (hakuna tatizo)
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua kama yule muuza madawa ya kulevya aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba duniani kote alikuwa nchini Tanzania. Ujio wake ulikuwa siri sana na watu wengi, hasa Watanzania hawakuwa wakifahamu hata sura yake alifanana vipi.
Watu wakateremka kutoka ndani ya ndege hiyo na kuanza kutembea kwa mwendo wa taratibu kabisa. Mdunguaji aliyeitwa Peter alikuwa makini kabisa kule ghorofani, aliwaambia wenzake kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Wanaume waliokuwa wameshuka kwenye ndege aliwaona sura zao, walikuwa warefu lakini kuna mmoja alikuwa amevalia suti nyeupe huku kichwani akiwa na kofia kubwa ya Marlboro na kila alipotembea, alikuwa akiangalia chini tu.
“Peter! Umemuona?” aliuliza Chris kule alipokuwa.
“Nawaona wanaume wanne wakitembea, nahisi ni wasaidizi wake. Kuna mwanaume mmoja pia, amevalia kofia kubwa ya Marlboro, nadhani ndiye Armando, amevaa hivyo ili asigundulike na muda wote anaangalia chini,” alisema Peter aliyekuwa ghorofani.
Aliendelea kuwaangalia wanaume wale, walipoanza kuingia ndani ya jengo hilo akawaambia kwamba tayari walikuwa wameingia ndani ya jengo hilo hivyo walitakiwa kumsubiri palepale nje walipokuwa.
“Anakuja!”
Baada ya dakika moja macho yao yakatua kwa wanaume watano waliovalia suti ambao walikuwa wakiingia kule sehemu ya kuchunguzia mizigo ya abiria. Hakutaka kujifanya kwamba ana pesa kwani aliamini kwa kufanya hivyo kungezua maswali mengi kwa watu wengi na hivyo kushtukiwa.
Mwanaume yule akapita na wenzake, walipopita salama na kuelekea nje, wakashangaa wakifuatwa na wanaume watatu waliokuwa na bastola zilizokuwa viunoni mwao.
“Upo chini ya ulinzi,” alisema Chris huku akimwangalia mwanaume aliyevalia kofia, hakutaka kuishia hapo, akatoa bastola na kuishika kiwizi, hakutaka watu wengine waione.
“Chini ya ulinzi! Nimefanya nini?” aliuliza mwanaume huyo huku akiuinua uso wake na kumwangalia Chris aliyefika na wenzake mahali hapo.
Kila mmoja akapigwa na butwaa, mtu waliyekuwa wakimwangalia hakuwa Armando kama walivyoambiwa bali alikuwa mtu mwingine kabisa. Alishangaa, hakujua sababu ya kuwekwa chini ya ulinzi.
Hakukuwa na mtu yeyote ndani ya uwanja huo aliyejua kilichokuwa kikiendelea, walichohisi ni kwamba Wazungu walioingia walipokelewa na wenzao waliowafuata kitu ambacho hakikuwa kweli.
“Usipige risasi. Si yeye,” alisema jamaa mwingine kwa kutumia kiwaya fulani kilichopitishwa mpaka sikioni, alikuwa akizungumza na Peter aliyekuwa ghorofani.
“Siyo yeye?”
“Ndiyo! Ni mtu mwingine. Subiri kwanza!”
Kila mmoja alichanganyikiwa, walijua kabisa ndege ile ilikuwa ni ya Armando, na ndiyo ambayo alikuwa akiitumia mara zote alizokuwa akisafiri kisiri kuelekea sehemu mbalimbali, kitendo cha ndege hiyo kutumiwa na mtu mwingine kwa kudhani kwamba alikuwa Armando kilimfanya kila mmoja kushangaa.
Wakahitaji idadi ya watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo, wakaambiwa kwamba walikuwa tisa, yaani wao watano, dada wawili wa huduma na marubani wawili.
“Na mmekuja kufanya nini?”
“Kutembelea mbuga za wanyama. Kwani kuna tatizo lolote?” aliuliza mwanaume huyo aliyeonekana kuwa bosi.
“Hapana! Sawa. Unaweza kwenda,” alisema Chris na kuwaruhusu watu hao waondoke mahali hapo.
Wakawasiliana na bosi wao aliyekuwa nchini Marekani na kumwambia kilichotokea. Wao wenyewe hawakuamini, waliambiwa kabisa kwamba mwanaume huyo alipanda ndani ya ndege na kuondoka nchini Ujerumani, sasa nini kilitokea mpaka mwanaume huyo kutoonekana uwanjani hapo? Kila walichojiuliza, wakakosa majibu.

Je, nini kitaendelea?
 
ERIC SHIGONGO
MZIMU UNAOTABASAMU-11

Mzee Armando na vijana wenzake walikuwa ndani ya ndege kutoka jijini Berlin nchini Ujerumani kwenda Dar es Salaam nchini Tanzania. Moyo wake ulikuwa na hasira kali dhidi ya Msuya aliyejiona kuwa mjanja kuliko yeye.
Hakutulia, muda mwingi aliwasiliana kwa barua pepe na mtoto wake, Jericho aliyekuwa jijini Berlin. Aliendelea kumsisitizia kwamba ni lazima amchunge sana Natasha kwani ile safari aliyokuwa akielekea haikuwa salama hata kidogo.
Aliwaogopa maofisa wa CIA, alijua dhahiri kwamba ni lazima walikuwa na taarifa kuhusu safari yake hiyo kuelekea nchini Tanzania. Hakuwa na amani, na kwa sababu alitaka kufika salama nchini humo ilikuwa ni lazima afanye kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba anafika salama kabisa.
Wakati ndege ikiwa imefika katika anga ya Kenya, akawauliza wenzake kile alichokuwa akitakiwa kufanya kwani ilikuwa ni lazima maofisa wa CIA kuwa na taarifa juu ya ujio wake wa kuelekea nchini humo.
“Ni lazima ujibadilishe na kuwa rubani,” alishauri jamaa mmoja.
“Mmh! Kivipi?”
“Ndege itakapotua uwanja wa ndege, utatakiwa kubadilishana mavazi na rubani, nina uhakika kwamba kama kweli wapo basi watakuwa bize kuwaangalia watu wengine lakini si marubani, hiyo ndiyo njia nzuri ya kuwaepuka watu hawa,” alisema kijana huyo aliyeitwa kwa jina la Kurt.
Hilo ndilo lililofanyika, baada ya kufika nchini Tanzania, akamwambia rubani mmoja kwamba wabadilishane mavazi. Huo ndiyo ujanja uliofanyika uwanjani ndani ya ndege kwani Chris na wenzake walikuwa bize na rubani yule aliyevaa kibosi pasipo kugundua kwamba hakuwa Armando bali wale marubani wawili waliokuwa wamepita na kuchukua teksi, mmoja ndiye alikuwa Armando waliyekuwa wakimtafuta.
Akaondoka na rubani mwingine, wakaingia ndani ya teksi moja na kuondoka mahali hapo huku wakiwaacha wenzao wakiendelea kuhojiana na maofisa wa CIA waliokuwa wamewasimamisha nje.
Safari yao hiyo ikaishia katika Hoteli ya Africa One iliyokuwa Posta jijini Dar es Salaam ambapo wakachukua vyumba hapo na kutulia huku wakiwa wamekwishawasiliana na wenzao kwamba walitakiwa kuchukua vyumba katika hoteli nyingine kabisa kwani kwa jinsi CIA walivyokuwa, huo usingekuwa mwisho wa kumtafuta kwani walikuwa na uhakika kwamba alikuwa nchini Tanzania.
Mipango yake mikubwa ilikuwa ni kwa Msuya, hakutaka kuona akikamatwa kabla ya kumpa taarifa mwanaume huyo. Kichwa chake kilisumbuka mno na ilikuwa ni lazima kuhakikisha anamuua yeye au hata kuiangamiza familia yake.
Akawasiliana na Theofil na kumwambia kwamba tayari alikuwa nchini Tanzania hivyo alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba familia ya Msuya inatekwa na hivyo kuiangamiza kama onyo kwa watu wengine kwamba hakutakiwa kuchezewa hata mara moja.
“Haina shida. Ngoja niwapange vijana,” alisema Theofil.
Hakukuwa na jambo jingine lililotakiwa kufanywa mahali hapo zaidi ya Theofil kuwapanga vijana wake kwa ajili ya kufanikisha kile walichoambiwa. Walijua kuwa sehemu sahihi ya kuipata familia ya mwanaume huyo ilikuwa ni kanisani ilipokuwa ikienda kusali.
“Kwa hiyo tukaiteke kanisani?” aliuliza Godfrey, mmoja wa vijana waliokuwa wamepewa mchongo mzima na Theofil.
“Pigia mstari!”
“Lakini si anaweza kuwepo mwenyewe?”
“Ndiyo! Na kama mwenyewe akiwepo itakuwa ni hatari zaidi kwani ni lazima tutapambana kwa risasi, hatujui ni nani atapona, cha msingi tumtoe kanisani kabla ya ibada kumalizika,” alisema Theofil.
“Tumtoe kanisani?”
“Ndiyo! Dakika ishirini kabla ya ibada kumalizika ni lazima atoke kanisa,” alisema Theofil.
Huo ndiyo uamuzi uliokuwa umepangwa, kabla ya jambo hilo kufanyika kitu cha kwanza kabisa kilitakiwa ni kufanywa uchunguzi kugundua muda sahihi wa ibada hiyo kumalizika. Wakaelekea katika Kanisa la The Great Cross mahali Msuya na familia yake walipokuwa wakisali na kuangalia ratiba ya siku ya Jumapili.
“Kanisa lina ibada moja tu, inamalizika saa sita kamili mchana. Ni lazima tufike hapa kabla. Ikiwezekana Iddi kesho ingia kanisani, sali, ila macho yako yawe kwa huyu mzee na familia yake,” alisema Theofil.
“Haina noma! Hata ukiniambia nihubiri kwa kesho nipo tayari,” alisema Iddi na wote kuanza kucheka. Mipango ikaanza kusukwa, iwe isiwe ilikuwa ni lazima familia yake ya mke na watoto wawili itekwe na kupelekwa sehemu na kuuawa huko.
***
Ulikuwa ni mpango kabambe uliokuwa umeandaliwa, kila mtu alijua siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa familia ya Bwana Msuya aliyekuwa tapeli mkubwa kwa wafanyabishara wengi wakubwa. Alijua kwamba alikuwa kwenye hatari kubwa hivyo ilikuwa ni lazima kujilinda kwa nguvu zote.
Aliajiri watu kwa ajili ya kumlinda tu, alihakikisha kuwa kila anapokuwa anakuwa salama na hakuna mtu yeyote atakayeweza kumdhuru. Alijiamini, mbali na ubilionea mkubwa aliokuwa nao, mzee huyu alikuwa na udhaifu mmoja mkubwa maishani mwake, nao ulikuwa ni upendo mkubwa aliokuwanao kwa msichana aliyeitwa Juliet.
Hakukuwa na mtu aliyejua kitu ambacho msichana huyo alimpa mzee huyo, aliukamata moyo wake, mapenzi yake mazito yalikuwa kwa msichana huyo. Alimpenda, alimthamini na kila siku alitaka kuwa peke yake kwa msichana huyo mrembo na kila mwanaume aliyemnyemelea, alimuua.
Juliet alipata alichokitaka kutoka kwa bilionea huyo, alinunuliwa magari ya kifahari, alijengewe jumba kubwa na hati ya jumba hilo kuandikwa jina lake. Alimfanyia mambo mengi kiasi kwamba mpaka watu wengine walikuwa wakishangaa na kujiuliza nini kilikuwa kikiendelea chumbani? Je, msichana huyo alikuwa na maajabu gani kiasi kwamba mzee huyo kufa na kuoza kwake?
Mzee Msuya aliipenda sana familia yake lakini kwa Juliet alikuwa mtu mwenye muonekano mwingine kabisa, alikuwa tayari kukosa kitu chochote kile lakini si kutokumuona msichana huyo ambaye alikuwa radhi kumpa kitu chochote kile lakini si kumkosa.
Jina hilo lilipokuja kichwani mwa Theofil akagundua kwamba wanaweza kumtumia Juliet kwa ajili ya kumtoa mzee Msuya kanisani. Hakutaka kuchelewa, haraka sana akaanza kutafuta mahali alipokuwa akiishi msichana huyo.
Wala hakupata tabu, akapafahamu alipokuwa akiishi na kuanza kusuka mipango ya kumteka msichana huyo na kumtaka mzee huyo aondoke kanisani na kazi ianze kufanyika.
Asubuhi ya siku ya Jumapili Theofil na mwenzake aliyeitwa kwa jina la Issa walikuwa nje ya nyumba ya Juliet, walikuwa wakisubiri kupigiwa simu na kuambiwa waanze kufanya kazi yao kwani kwa muda waliokuwa wamefika hapo asubuhi sana walikuwa na uhakika kwamba msichana huyo alikuwa ndani ya nyumba.
Ilipofika majira ya saa nne asubuhi, wakaanza kuusogelea mlango wa kuingia ndani na kuugonga. Mlinzi akaufungua mlango kwa lengo la kuwasikiliza watu hao walichokuwa wakihitaji.
“Samahani. Tumeagizwa na bosi Msuya. Juliet yupo?” aliuliza Theofil huku akimwangalia mlinzi.
“Ndiyo! Nikawaitie?” aliuliza mlinzi huku akiwaangalia watu hao kwa zamu, kwa jinsi walivyokuwa wamevaa mashati na kuchomekea kwa heshima ilionyesha kabisa kwamba hawakuwa watu wabaya na mbaya zaidi akababaika na kutokutaka kuwauliza maswali.
Walipokuwa na uhakika kwamba msichana huyo alikuwa ndani ya jumba hilo, wakatoa bastola zao na kumuweka mlinzi chini ya ulinzi na kumwambia waende naye ndani ya jumba hilo huku mlango ukifungwa.
Mlinzi alibaki akitetemeka, hakujiamini, moyo wake ulikuwa na hofu kubwa, imani ya kuwaamini watu wale ikamgharimu na kujikuta akiwa chini ya ulinzi. Hakuwa na ujanja wowote ule, akachukuliwa na kuelekea sebuleni huku midomo ya bastola ikiwa pembeni yake.
“Kifo hakina taarifa, muda wowote tu unaweza kufa,” alisema Theofil, akaanza kumtisha mlinzi.
“Tunachohitaji ni kuwa na msichana huyo tu. Chumba chake kiko wapi?” aliuliza Theofil kwa sauti ya kibabe.
Mlinzi akasimama na kuanza kuelekea katika mlango wa chumba cha Juliet, alipofika, akaugonga na kumuita msichana huyo aliyekuwa amelala.
Juliet aliposikia hodi hiyo, akaamka kichovu na kuanza kwenda mlangoni ambapo mlinzi alihitaji ufunguliwa na kuzungumza naye. Hilo halikuwa kawaida, mlinzi hakuwahi kuingia ndani na kumgongea asubuhi kama hiyo, moyo wake ukamwambia kwamba inawezekana kulikuwa na tatizo kubwa.
Alipoufungua, macho yake yakakutana na midogo miwili ya bastola, akaamliwa kutulia kwani vinginevyo angegeuzwa jina na kuitwa marehemu.
“Naomba msiniue...nitawapeni kiasi chochote mnachotaka, naomba msiniue,” alisema Juliet huku akitetemeka kwa hofu.
“Inategemea, unaweza kuachwa hai au kuuawa, hilo linategemea na uamuzi wako,” alisema Theofil, wakamchukua msichana huyo na kuelekea naye sebuleni.
Wakamwambia akae kwenye kochi na kutulia, Juliet alikuwa akitetemeka, hakujua kama watu hao walikuwa majambazi au la. Hawakuonekana kuhitaji pesa, walivalia kibosi na hapo sebuleni hawakutaka kumwambia kile kilichokuwa kimewapeleka nyumbani pale.
Walisubiri kwa dakika nyingi tu huku muda mwingi wakiutumia kuangalia saa zao. Ilipofika saa tano na nusu, Theofil akamwambia Juliet kuchukua simu yake kwa kuwa alitaka kuitumia. Msichana huyo akainuka na kuanza kuelekea chumbani huku Issa akimfuatilia kwa nyuma, alipofika, akachukua simu yake na kurudi sebuleni ambapo alitakiwa kumpigia Mzee msuya.
“Nimwambie nini?” aliuliza Juliet huku akitetemeka.
“Mwambie kwamba umevamiwa na watu wenye bastola na umuite nyumbani hapa haraka sana vinginevyo tutakuua,” alisema Theofil.
Hakutaka kupinga, haraka sana akampigia simu Mzee Msuya, simu hiyo ilianza kuita kwa sekunde chache tu na mzee huyo kupokea na kuanza kuongea kwa sauti ya chini.
“Bebi! Nipo kanisani,” alisema mzee huyo.
“Bebi nimevamiwa, kuna watu wanataka kuniua, bebi niokoe, bebi nimevamiwa nyumbani,” alisema Juliet na kuanza kulia.
“Nani kakuteka, bebi upo wapi? Nini kinaendelea?” aliuliza mzee huyo maswali mfululizo huku akionekana kuchanganyikiwa.
Wakati mzee huyo anaongea kwa simu kanisani, Iddi alikuwa akifuatilia kila kitu, kwa muonekano wake tu mzee huyo alionekana kuchanganyikiwa, alizungumza kwa makini huku akiangalia huku na kule. Haikuchukua muda, akasimama na kuanza kuondoka kanisani hapo pasipo kumwambia mkewe kitu chochote kile.
Bi Eva alibaki akishangaa tu, hakujua kilichokuwa kikiendelea kwa mume wake, alipomuona ametoka, haraka sana naye akasimama kwa lengo la kumuuliza kilichokuwa kikiendelea lakini mzee huyo hakuwa radhi kusema chochote kile. Akaingia ndani ya gari, akaliwasha na kuondoka nalo.
Iddi akamtumia meseji Theofil na kumwambia mzee Msuya ameondoka kanisani na alibaki na familia yake hivyo kazi ilikuwa kwao tu kuhakikisha kwamba wanaiteka na kuondoka nayo.
“Ngoja nimcheki Emmanuel, anakuja kuwachukua,” alisema Theofil.
Bi Eva aliduwaa, hata hamu ya kuendelea kukaa ibadani ikamuisha ila ikambidi tu kuendelea kubaki hivyohivyo tu mpaka ibada ilipokwisha. Kwa kuwa mumewe aliondoka kwa gari, akaona njia rahisi ya kurudi nyumbani na watoto wake ni kukodi teksi ambayo ingewapeleka mpaka nyumbani.
Waliposalimiana na washirika wengine na kutoka katika eneo la kanisa, mara gari zuri aina ya Toyota Landcruser likasimama mbele yao, kijana mmoja aliyevaa kitanashati akateremka, alikuwa Emmanuel aliyekuwa ametumwa na Theofil.
“Bwana Yesu asifiwe mama,” alisalimia Emmanuel huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu.
“Amen!”
“Mzee alinipigia simu amesema nije niwachukue, kuna simu alipokea ambayo si nzuri, amewahi bandarini,” alisema Emmanuel kwa sauti ya upole na ya unyenyekevu kabisa.
Bi Eva hakuwa na hofu, kwa jinsi alivyomwangalia yule kijana, alivyovaa na hata kuzungumza nao alionekana kuwa mtu mwema kabisa, akawafungulia mlango, wakaingia ndani na kuondoka mahali hapo.
Haraka sana Iddi akaanza kuwafuatilia, walipofika Kinondoni, gari likasimamishwa, wanaume watatu akiwemo Iddi wakaingia ndani ya gari hilo huku wakiwa na bastola, wakawataka watu hao watulie kama wananyolewa.
“Jamani tumefanya nini?” aliuliza mwanamke huyo.
“Nyamaza. Ukiuliza swali tu, ubongo wako utatapakaa kote humu,” alisema Iddi huku akiwa na bastola mkononi mwake, wote wakabaki kimya.
Alichokifanya Emmanuel ni kumpigia simu Theofil na kumwambia kwamba tayari walikuwa na familia ya mzee huyo.
“Safi sana. Tumekwishaondoka nyumbani kwa yule malaya! Tumewafunga kamba, atajijua mwenyewe akifika huko. Unganisha mpaka maskani kwanza,” alisikika Theofil.
“Haina noma! Dakika chache tu mwamba,” alisema Emmanuel na kuanza kubadilisha gia tu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom