Mzimu unaotabasamu

Mzimu unaotabasamu

MZIMU UNAOTABASAMU-22

Bilionea Msuya alikuwa kimya chumbani kwake, moyo wake ulikuwa umetulia, maumivu ya kuuawa kwa familia yake yalikwisha zamani sana. Alikuwa akiendelea na maisha yake kama kawaida. Muda mwingi alikuwa bize na biashara zake kwani aligundua kwamba kuendelea na biashara ya madawa ya kulevya kungemfanya kukamatwa na mwisho wa siku kufungwa gerezani.
Aliyapenda maisha yake, hakutaka kuendelea na biashara ile, aliachana nayo na kufanya mambo yake mengine kabisa. Hakutaka kabisa kutenda dhambi, alihitaji kumtumikia Mungu katika maisha yake kwani kwa jinsi umri ulivyokuwa ukizidi kusonga na ndipo mwili wake ulipoanza kukosa nguvu.
Kila siku akawa mtu wa kanisani, hakutaka kuacha kumuabudu Mungu. Akawa mshirika mzuri kabisa ambaye alishiriki kila ibada kanisani, si Jumapili tu bali hata ibada za katikati ya siku zote hizo alikuwa akishiriki.
Maisha yake yalibadilika kabisa. Akawasamehe watu wote waliokuwa wamemkosea lakini mtu ambaye alikuwa mgumu kusameheka moyoni mwake alikuwa bilionea Armando. Mwanaume huyo alimuumiza mno, alimrudisha nyuma kutoka kuwa na familia mpaka kumuacha akiwa hana kitu mikononi mwake.
Alitamani kusafiri kuelekea nchini Ujerumani kwa lengo la kumuua mwanaume huyo lakini yeye mwenyewe aliogopa. Maisha yake hayakuwa ya furaha kwa kuwa tu Armando alikuwa akiendelea kuishi.
Wamarekani waliendelea kumtafuta mzee huyo kila kona, kazi yake Msuya ilikuwa ni kumuomba Mungu ili siku mwanaume huyo akamatwe na kuhukumiwa kifo. Sala yake haikujibu, kila siku alikuwa mtu wa hasira japokuwa kila alipokuwa kanisani ilikuwa ni vigumu kujua kile kilichokuwa moyoni mwake.
Usiku huo akiwa nyumbani kwake ndipo akasikia simu yake ya mkononi ikianza kuita. Kwanza akashtuka, huwa ni vigumu kupokea simu kwa wakati kama huo. Watu wote ambao walikuwa na namba zake, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwaonya kwamba hakutaka kupigiwa simu usiku.
Kwa muda huo, aliamini kabisa mtu aliyekuwa akipiga simu alikuwa mgeni, mtu ambaye hakuufahamu utaratibu aliokuwa amejiwekea. Akateremka kutoka kitandani na kuanza kuelekea mahali simu ile ilipokuwa, alipoifikia, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuangalia kioo cha simu ile, namba ilikuwa ngeni kabisa, hakutaka kujali, akaipokea na kuipeleka sikioni.
“Halo!” aliita.
“Halo! Bwana Yesu asifiwe,” alisikika mwanaume mmoja kutoka upande wa pili.
Sauti yake ilikuwa ni ya mchungaji wake wa kanisa la Uinjilisti aliyeitwa Carthbert. Alishangaa, haikuwa kawaida kumpigia simu usiku huo, alihisi kulikuwa na jambo ambalo mchungaji huyo alitaka kumwambia.
Vitu vingi vikawa vinapita kichwani mwake. Alikuwa akifikiria mambo mengi hata kabla hajapata jibu ya kile kilichompelekea mchungaji huyo kumpigia simu usiku namna hiyo.
“Amen mchungaji! Mbona usiku tena?” aliuliza mzee Msuya kwa sauti ya upole kabisa.
“Kuna jambo nataka nizungumze nawe,” alisikika mchungaji.
“Jambo gani mtumishi wa Mungu?”
“Naweza kuonana nawe?”
“Sasa hivi?”
“Ndiyo mtumishi!”
“Usiku huu?”
“Kama itawezekana! Utanisamehe kama nitakuwa ninakusumbua,” alisema mchungaji huyo.
“Wapi?”
“Nyumbani kwangu! Nakuomba mtumishi manake sina wa kumshirikisha jambo hili kubwa,” alisema mchungaji huyo.
“Nakuja!”
Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea huko, moyo wake ulikuwa mzito kukubaliana na jambo hilo. Wakati mwingine alihisi kwamba kulikuwa na kitu, lisingekuwa jambo jepesi kwa mchungaji huyo kumpigia simu kwa namba ngeni na wakati alikuwa na simu yake ambayo kila wiki alikuwa akimjazia muda wa maongezi.
Alijiuliza, kuna wakati mawazo mabaya yalikuwa yakimjia na kuhisi kwamba mchungaji alitaka kumuuza kwa watu au kumuua. Mawazo hayo yalipokuwa yakimjia, alikemea na kuyaondoa kabisa kichwani mwake.
“Kuna nini? Mbona usiku halafu namba ngeni?” alijiuliza huku akivaa nguo zake.
Alikuwa akienda kuonana na mchungaji, japokuwa alikuwa na hofu lakini hakufikiria kabisa kuchukua bastola yake na kwenda nayo. Akatoka ndani, akachukua gari lake na kuondoka nyumbani kwake.
Njiani alikuwa na mawazo mengi, bado jambo hilo lilimsumbua sana kichwani mwake. Alichukua dakika ishirini ndipo akafika Bezi Beach alipokuwa akiishi mchungaji huyo, akapiga honi, mlinzi akafungua geti na kuliingiza ndani.
“Mchungaji yupo?” lilikuwa swali la kwanza alilomuuliza mlinzi.
“Yupo?”
“Ana ugeni?” aliuliza huku akitoa tabasamu.
“Hapana! Yupo na familia yake,” alijibu mlinzi.
Hilo kidogo likampa uhakika kwamba hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea kwani kama angeambiwa kuwa alikuwa na ugeni lingemtia hofu zaidi na kujua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Baada ya kulipaki gari lake, akateremka na kuanza kuelekea ndani. Akaingia, sebuleni hakukuwa na mtu, hakutaka kujali, akakaa kwenye kochi na baada ya dakika chache mfanyakazi wa ndani akatokea na kumkaribisha.
“Karibu sana baba,” alimkaribisha dada wa kazi na kusalimiana kwa kupeana mikono.
Mikono ya msichana huyo ilikuwa imelowanishwa. Hayakuwa maji, lilikuwa jasho lililokuwa likimtoka, alipomwangalia usoni, msichana huyo alikuwa akitokwa na kijasho chembamba hali ambayo ikamtia hofu.
“Kuna nini?” aliuliza Msuya huku akimwangalia msichana huyo.
Msichana yule akashindwa kujibu swali hilo, akabaki kimya, hofu ilionekana usoni mwake. Mpaka kufikia hali hiyo tayari Msuya akahisi kabisa kulikuwa na jambo baya lililokuwa likiendelea.
“Kuna n...” aliuliza Msuya lakini hata kabla hajamaliza swali lake, ghafla umeme wa nyumba nzima ukakatwa.
Akashtuka, hakujua kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Huku akianza kujiuliza juu ya kitu kilichokuwa kikiendelea, akahisi kabisa kulikuwa na vishindo vya mtu vilivyokuwa vikija kule alipokuwa.
Akasimama, hata kabla hajachukua uamuzi wowote ule, akashtukia akipigwa na kitu kizito kwenye paji lake la uso, hapohapo akaanza kuyumba, hakuchukua hata sekunde kumi, akaanguka chini, akapoteza fahamu na hakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.
***
David hakutaka kushindwa, alihakikisha anammaliza Bilionea Msuya kama alivyokuwa ameagizwa. Hapo hotelini alipofikia, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mzee Msuya, ilikuwa ni lazima ammalize kwani ndiyo kazi kubwa aliyokuwa amepewa na mzee Armando ambaye alimuheshimu kama baba yake.
Kitu cha kwanza kabisa alichotakiwa kufanya ni kufuatilia mahali bilionea huyo alipokuwa akisali, aliona kuwa njia nyepesi ya kumpata bilionea huyo haikuwa sehemu nyingine zaidi ya kwenye nyumba ya ibada.
Hiyo ndiyo kazi aliyoanza nayo asubuhi ya siku iliyofuata. Akaanza kuwauliza wahudumu wa hoteli hiyo ambayo walimfahamu vema bilionea huyo na kumwambia mahali alipokuwa akisali.
“Hujui anaposali?” aliuliza mhudumu mmoja huku akimwangalia David, kwa jinsi Msuya alivyokuwa maarufu jijini Dar kila mtu alifahamu maisha yake mpaka alipokuwa akiishi.
“Sifahamu ndiyo maana nimeuliza.”
Akaanza kumuelekeza mahali alipokuwa akisali. Alikuwa akisali katika Kanisa la Uinjilisti lilikuwa Mwenge jijini Dar es Salaam. Alipafahamu Mwenge lakini hakujua mahali kanisa hilo lilipokuwa. Alichokifanya ni kuondoka na kuelekea huko, alipofika Bamaga, akauliza, haraka sana akaelekezwa mahali kanisa hilo lilipokuwa.
Akaelekea huko. Akawakuta vijana waliokuwa wakiimba kwaya na kuwauliza mahali alipokuwa akiishi mchungaji wao. Hakukuwa na mtu aliyejua kama mwanaume huyo alimtafuta mchungaji huyo wa lengo baya, wakamuelekeza na yeye kuanza kwenda huko.
“Mikocheni si mbali na hapa,” alijisemea huku akiwa ndani ya teksi na kuelekea Mikocheni.
Akafika mpaka mahali nyumba ya mchungaji huyo ilipokuwa. Ilikuwa nyumba kubwa na ya kifahari, mlangoni kulikuwa na mlinzi mmoja aliyeshika kirungu. Hakutaka kumfuata, huo haukuwa muda wa kuingia ndani ya nyumba hiyo, alitaka kurudi mahali hapo usiku na kufanya kile alichotaka kukifanya.
Akaondoka mahali hapo. Kichwani mwake kukawa na kitu kimoja tu kwamba ili aingie kwa urahisi ndani ya nyumba ile ilikuwa ni lazima aingie kwa mtindo wa kujifanya mchungaji ili aweze kumlaghai mlinzi na hatimaye kufanikiwa kuingia ndani.
Hilo halikuwa tatizo, akajiamini na hivyo kuelekea mtaani ambapo huko akanunua shati jeusi, kibeji cheupe cha kiaskofu kinachokaa shingoni ndani ya shati ili mara mlinzi atakapomwangalia aone kwamba alikuwa mchungaji.
Hakuishia hap, kwa kuwa alitamani kuwa na bastola, akanunua bastola ya bandia nyeusi iliyokuwa na muonekano kama bastola ya kweli, aliamini kwamba kama angeitumia hiyo, mchungaji na familia yake wangeogopa kwa kudhani kwamba ilikuwa bastola ya kweli. Alipokamilisha kila kitu, usiku akaanza kuelekea huko huku akiwa na teksi ya kukodi.
“Kama watu wanaiba baa, benki kwa bastola za bandia, kwa nini na mimi nisitumie? Nahisi hakuna mtu atakayenigundua,” alisemea huku teksi ikiendelea na safari ya kuelekea nyumbani kwa mchungaji.
Saa moja kamili usiku alikuwa nje ya nyumba hiyo. Teksi ilisimama na kuteremka huku akimwambia dereva amsubiri kwani angetoka muda si mrefu, hilo halikuwa tatizo, teksi ikasubiri na yeye kulifuata geti na kuanza kugonga.
Hazikupita sekunde nyingi geti dogo likafunguliwa, macho ya mlinzi yakatua kwa David aliyekuwa ameshika Biblia na uso wake ulijawa tabasamu pana.
“Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu!” alimsalimia mlinzi aliyekuwa akimwangalia, bila kutarajia naye mlinzi akarudisha tabasamu pana.
“Amen mtumishi! Karibu!”
“Ahsante sana. Mchungaji Carthbert yupo?”
“Yupo mchungaji!”
“Nashukuru sana!”
Akaingia ndani, alijipa muonekano wa kichungaji na hata kwa jinsi alivyokuwa akitembea, alitembea kana kwamba alikuwa madhabahuni akihubiri. Alikuwa na heshima zote, muonekano wa kipole ambao ulimfanya mlinzi kutokugundua kwamba mtu huyo hakuwa mchungaji na wala hakuwahi kusomea uchungaji.
Wakafika mpaka kibarazani na kumwambia mlinzi amuitie mchungaji Carthbert, mlinzi akaingia ndani, akamuita mchungaji huyo ambaye kwa haraka sana akatoka.
Macho yake yalipotua kwa David, hakuelewa kile kilichokuwa kikiendelea. Aliambiwa kwamba aliitwa na mchungaji Mshana ambaye alikuwa akimfahamu sana lakini baada ya kutoka nje macho yake yakatua kwa mtu ambaye hakumfahamu kabisa.
Hakutaka kuonyesha mshangao wake, alichokifanya ili kuonekana mtumishi wa Mungu akamkaribisha ndani, David akaingia na kukaa kwenye kochi sebuleni. Akajitambulisha kwamba aliitwa Mchungaji Mshana aliyekuwa na kanisa lake huko Mpanda mkoani Katavi.
“Oh! Kumbe mchungaji Mshana!”
“Ndiyo mtumishi!”
“Za masiku mtumishi!”
Alimsalimia kana kwamba alikwishawahi kuonana naye kabla. Walikaa na kuzungumza sana huku muda mwingi David akiwa anaiangalia saa yake ya mkononi. Mchungaji Carthbert akaiita familia yake na kumtambulisha David kama mchungaji Mshana kutoka katika kanisa la Uinjilisti huko Mpanda.
Kila mtu akafurahi na kukaribishwa. Alichokifanya ni kumwambiamchungaji huyo amwambie mtoto wake akamruhusu dereva teksi aondoke kwani yeye asingeweza kuondoka muda huo, hilo halikuwa tatizo mtoto wake akaenda huko.
Mlinzi hakuwepo getini, alikuwa nyuma ya nyumba akiendelea kufanya mambo yake. Wakati dereva teksi alipoambiwa aondoke, hakujua hilo na hata aliporudi na kuona teksi haipo, akili yake ilimwambia kwamba mchungaji huyo aliondoka.
Wakazungumza sana mpaka majira ya saa tatu. Muda wote wa mazungumzo hayo Mchungaji Carthbert alikuwa akijaribu kukumbuka ni mahali gani aliwahi kumuona mchungaji huyo. Ni kweli alimchangamkia lakini kitu kilichomfanya kutokukumbuka ni mahali alipowahi kumuona mchungaji huyo.
“Ni wapi? Mchungaji Mshana wa Mpanda. Mpanda sehemu gani pale?” alijiuliza kichwani mwake lakini hakupata jibu.
Baada ya familia ile kuondoka, Dakika kumi baadaye David akasimama na kumfuata mchungaji kule alipokaa, alipomkaribia, akapeleka mkono kiunoni na kutoa bastola ile ya bandia kisha kumuonyeshea kisiri.
Mchungaji Carthbert alibaki akishangaa, hakuamini kile kilichotokea. Alipoiangalia bastola ile, ilikuwa ni vigumu sana kugundua kama ilikuwa ya bandia, akaogopa, akaanza kutetemeka huku akijawa hofu. Akamwangalia David usoni, sura ile ya kutabasamu ikapotea na kuingia sura nyingine kabisa, sura ya kikatili ambayo kwa harakaharaka ilitafsiriwa kama mtu aliyekuwa amefanya sana mauaji huko nyuma.
“Kina mambo mawili! Ukipiga kelele au ukileta ubishi wowote ule, nakuua,” alisema David, hata sauti yake ilibadilika.
Mchungaji Carthbert hakuwa na jinsi, alitakiwa kutulia kama alivyokuwa. Kijasho chembamba kikaanza kumtoka huku kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele ndivyo aivyozidi kutetemeka. Akaambiwa anyanyuke, haraka sana akafanya hivyo.
“Iite familia yako na kwenda stoo,” alimwambia mchungaji.
Ili kuika nafsi yake ilikuwa ni lazima kufanya hivyo. Akaiita, ilipokuja, ikashangaa kuona kile kilichokuwa kikiendelea. Akawaambia kwamba walitakiwa kwenda stoo kwani kama wangebisha tu angemwaga damu humo ndani.
“Mkibisha nitawaua kama nilivyoiua familia ya mzee Mkude,” alisema David, japkuwa hawakuwahi kusikia mauaji hayo, kila mmoja akaogopa na kuona kweli kulikuwa na mzee aliyeitwa Mkude ambaye aliuawa na mwanaume huyo aliyesimama mbele yao.
Wakaelekea stoo, akamwambia mchungaji aichukue simu yake na kumpigia bilionea Msuya. Mchungaji huyo hakujua sababu, alishangaa lakini hakuwa na jinsi. Kwa kuwa simu yake ilikuwa mfukoni, haraka sana huku akitetemeka akaitoa na kutafuta jina la bilionea huyo.
“Nifanye nini?” aliuliza.
“Muite! Mshawishi mpaka aje, asipokuja, nawaua wote,” alisema David na kuwafanya watu hao kuzidi kuogopa.
Huku akitetemeka mithili ya mtu aliyekuwa akisikia baridi kali mchungaji akapiga simu na kumuita mwanaume huyo ambaye alimwambia kwamba angefika mahali hapo muda si mrefu.
Baada ya nusu saa, gari likasikika nje, akajua dhahiri kwamba alikuwa mchungaji huyo. Baada ya sekunde kadhaa mlango wa sebuleni ukafunguliwa na kutumwa dada wa kazi kwenda kufungua, aliporudi tu kule stoo, David akaufunga, akachukua kipande cha nondo kilichokuwa jikoni, akaifuata ‘main switch’ na kuzima kisha kuelekea sebuleni kumshambulia mzee huyo.
 
Back
Top Bottom