SEHEMU YA 78
WASWADEGE walipiga shangwe ya nguvu baada ya kuhakikisha Azra Malama, amepoteza maisha.
Zoezi hilo lilipomalizika , Shebo ambaye aliyaongoza kwa ushujaa mkubwa mapambano hayo dhidi ya Azra Malama, akatangaza watu wote warudi majumbwani kwa ajili ya msiba wa kitaifa ambao walikuwa wamepata, kutokana na watu wengi kufariki kisiwani hapo.
Hicho ndicho kilichofuatwa. Watu wakarudi nyumbani kwa ajili ya msiba.
***
Mimah hakuwa na raha hata kidogo, muda mwingi aliutumia akilia na kusononeka kutokana na kifo cha rafiki yake Jemima, kilichomuua mno moyoni mwake.
Mbali na kusikitika, Mimah ndiye aliuchukua mwili wa mwanadada huyo Malkia wa Swadege ya Rwadege kwa ajili ya kuuzika, aliuchukua akisaidiana na Shebo.
Wawili hao walifanya msiba na kwenda kuuzika mwili huo kwenye makaburi ya halaiki ambapo marehemu wote waliofariki kwenye vita hiyo, walizikwa.
Hiyo ndiyo ikawa safari ya mwisho ya Jemima duniani.
Wakati wa mazishi yake alipigiwa mizinga ya heshima, na wanajeshi wa Swadege, tena zaidi ya mara moja, kuonyesha namna walivyouheshimu na kuuthamini mchango wake kwenye zoezi zima la kumuua Azra Malama..
Mazishi ya halaiki yalipomalizika, zilitolewa siku chache kwa ajili ya kumalizia maombolezo. Baada ya siku hizo kupita pia, Waswadege ya Rwadege wakaendelea na maisha yao. ***
“Ni lazima dunia ifike mahali ikubaliane na sisi,” Mzee Makimbi alikuwa akimwambia Shebo. “Tuna aina ya maisha yetu na hatuwezi kuishi kama mtu yeyote atakavyo.
“Maisha yetu ni amani, furaha na kusherehekea zawadi mbalimbali ambazo Mungu ametujalia. Ikiwa dunia inataka tuwasaidie. Tutawasaidia! Lakini si kulazimisha tuishi kama watakavyo wao tena kwa kututawala.”
Mzee Makimbi alipumzika na kumeza mate.
“Nakutuma, nenda katangaze juu ya msimamo wetu na ueleze wazi tunahitaji kuachwa tuishi kwa namna tutakavyo sisi!
Shebo hakuweka pingamizi lolote lile.
Alikubaliana na mzee huyo na maandalizi ya shujaa huyo kwenda kuzungumza kwenye kikao cha Umaja wa Mataifa, ambacho walikuwa wamealikwa huko Uingereza, yalianza.
Shebo alipanga kuwawakilisha vyema Waswedege!