Mwisho wa Azra Malama

Mwisho wa Azra Malama

Shunie

JF-Expert Member
Joined
Aug 14, 2016
Posts
157,400
Reaction score
465,165
Mtunzi Boniphance Ngumije sehemu ya 01

“Babu…” sauti ya mtoto ilisikia.
“Naam mjukuu wangu.” Ilijibu sauti nzito ya mtu mzee.

Kisha wanaonekana watu wawili wakiwa wameketi kwenye gogo la mti wakiwa wamejianika pembeni ya moto uliyokokwa na kuwapa mwanga usiku huo.

Mtu mmoja alikuwa ni mwanaume mzee, mweusi na mrefu, mwenye nywele nyingi na alikuwa amejitanda mashuka ya kimasai mwilini mwake yenye rangi ya bluu na nyekundu huku chini mguuni akiwa amekanyagia viatu vilivyotokana na mpira wa tairi la gari.

Mbele ya mwanaume huyo mzee alikuwa ameketi kijana mdogo mwenye miaka kumi na moja, mwembamba aliyekuwa amejitanda pia shuka la kimasai lenye rangi nyekundu yenye weusi kwa mbali.

Wawili hawa walikuwa kwenye mazungumzo na kijana yule aliendelea;
“Azra Malama ndiye nani?” Alimuuliza babu yake.
“Umemsikia wapi?” Babu yake alijibu kwa swali.

“Jina lake linatajwa kila mahali!”
“Azra Malama alikuwa Mfalme wa Swadege ya Rwadege.” Hatimaye babu yule alimjibu mjukuu wake.

“Imekuwaje mpaka akafa na kwa nini anazungumziwa kila mahali?”
“Kuhusu yeye mpaka kifo chake ni historia ndefu mjukuu wangu.”
“Naomba unisimulie.”

Yule mzee alimtazama mjukuu wake na kutabasamu, kisha akaokota kuni na kutupa kwenye moto mbele yake, akajitanda shuka lake la kimasai vizuri na kumtupia macho tena mjukuu wake.

Ukimya ulitawala wa sekunde chache, kisha yule mzee aliamua kuuvunja ukimya huo kwa kuanza kumsimulia mjukuu wake kile ambacho alikuwa anahitaji kusikia.

“Kama nilivyokwambia Azra Malama alikuwa ni Mfalme wa Swadege ya Rwadege, kisiwa ambacho kipo Afrika Mashariki na kimezungukwa na visiwa vya Zanzbar, kusini na Madagaska, kaskazini.

Mwishoni mwa karne ya 19, katika kisiwa hiki kabla ya Azra Malama kuwa mfalme, vipande vya ganda la dunia viliachana na kusababisha volkeno kali iliyoibuka juu ya ardhi ikiwa na gesi, majivu yenye joto kali pamoja na tetemeko la ardhi vilivyopelekea maafa makubwa sana.

Watu wote walikufa kisiwani hapo, mimea ikakauka na hakukuwa na kiumbe hai kilichosalia. Likabaki kuwa eneo tupu lililotelekezwa.







Screenshot_20181027-172928.jpeg
 
Sehemu ya 02

Miaka zaidi ya 400 ilikatika bila kuwa na mtu yeyote aliyeishi kwenye eneo hili, baadaye wakulima waliyokuwa wakitafuta eneo lenye rutuba kutoka maeneo ya jirani taratibu walianza kuvamia Swadege ya Rwadege.

Hapo walikuta udongo ni wa mfinyanzi wenye rangi nyekundu na una rutuba ya ajabu. Walipopanda mazao hata yale yaliyohitaji muda mrefu kukua, yalichipua ndani ya siku moja tu, jambo la kushangaza zaidi ni uwezo wa mazao hayo.
Yalikuwa na nguvu za ajabu.

Kila aliyekula alipatwa na nguvu hizo na kuwa mtu mwenye kasi, busara ya hali ya juu, kutenda maajabu, kufikiri vitu zaidi ya uwezo wa kawaida na siku zote walionekana vijana hata walipozeeka. Pia mazao hayo yalitumika kutibu wagonjwa na kufanya maendeleo makubwa kisiwani hapo.

Watu wa Swadege ya Rwadege wakawa tofauti na binadamu wengine.

Kisiwa hicho kikawa tofauti na sehemu nyingine duniani na maendeleo yaliyopatikana ya kiteknolojia yalikuwa mbele hata ya Marekani ya mwaka 2080, Swadege ya Rwadege ikawa paradiso ya dunia,” Babu yule alisimulia.

“Ningekuwepo wakati huo ningeishi huko,” kijana yule alizungumza kwa shahuku.
“Unafikiri ilikuwa rahisi! Watu wengi walitamani kwenda kuishi Swadege lakini haikuwezekana.

Baada ya maendeleo na watu wa Swadege kufahamu kwamba walikuwa na nguvu za ajabu hawakuruhusu binadamu mwingine kuwaingilia wala kuchukua mazao yao, kila aliyejaribu kuingia aliuawa.

“Mbaya zaidi Swadege ilikuwa haina kiongozi aliyejulikana, suala ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa kwa mataifa makubwa duniani kama Urusi, Marekani na Izrael yaliyotamani kuingia kisiwani hapo na kuchukua mimea iliyosadikika kuwa ya uhai ili kuweza kuboresha mifumo yao ya kiteknolojia.

“Mataifa hayo yalitegemea kujenga uhusiano wa kiutawala na kiongozi wa kisiwa hicho ili baadaye kuweza kuingia na kufanya kila walilokusudia. Lakini bahati mbaya hakukuwa na kiongozi aliyefahamika.

“Hata hivyo, kwa upande wa Marekani hawakupenda kushindwa. Hawa ni sawa na mbwa anayesaka mfupa, hakomi kutafuta mpaka pale anapopata.

Kwa kuwa azima yao ilikuwa ni kwa namna yoyote ile kuingia Swadege, waliamua kumtafuta mtu anayeitwa Azra Malama, waliyeamini angewasaidia kuingia na kutawala kisha kuchukua kila walichotamani.”

ITAENDELEA...
 
Sehemu ya 03

Baada ya babu yule kusimulia kuhusu Swadege ya Rwadege na namna Marekani ilivyanza kusuka mipango ya kumtumia Azra Malama alimtazama mjukuu wake;

“Unasinzia?” alimuuliza.
“Hapana babu ninakusikiliza,” Mjukuu yule alijibu huku akijiweka sawa juu ya gogo.

Kisha aliuliza; “Wali
mtafuta wapi huyo Azra Malama?”
Babu yake alizidi kumsimulia kwamba, jopo lililoundwa nchini Marekani kwa sababu maalumu ya kutafuta namna ya kuingia kwenye kisiwa hicho la watu nane, lilikutana jijini Washington, Novemba 7, 1990, saa 10 jioni kwenye jengo refu la Bill Clinton, kujadili juu ya mbinu mpya za kuingia Swadege ya Rwadege.

“Hawa watu ni wa ajabu sana,” alisema Jaden Smith miongoni mwa wajumbe kwenye jopo hilo aliyekuwa mtaalamu kwenye masuala ya uhusiano wa kimataifa.

“Hakuna jamii duniani, iwe ya wadudu, ndege, wanyama au binadamu ambayo inaishi kiholela bila ya kuwa na kiongozi anayekubalika na kusikilizwa na watu wote au baadhi yao. Hawa wenyewe wanawezaje kuishi bila ya kuwa na kiongozi?”

Smith aliuliza. Lakini kwenye jopo lile hakuna aliyeweza kumjibu. Wenzake walikuwa wakimtazama tu kwa kumkodolea macho.

“Kuna wazo nimepata,” Steve, mjumbe mwingine alizungumza baada ya kuona wenzake wapo kimya.

“Ninafikiri tumtumie yule kijana Azra Malama, ana uwezo wa kutusaidia kukitawala kisiwa hicho!” Aliongeza.

“Azra Malama! Ndiye nani?” Tasha, mjumbe mwingine aliuliza.
“Ha! Ha! Haaa!” Steve alidakia kwa kicheko. “Humfahamu Azra Malama?” aliuliza.

“Ndiyo simfahamu.” Tasha alilisisitiza.
“Huyu ni mtu mweusi hatari sana. Amefungwa kwenye Gereza la Guantanamo yapata miaka saba sasa.

Hadi anafungwa alipatikana na makosa kwenye mashitaka ya kuua, kuteka nyara, kunywa damu za watu, kula nyama za watu na hakuna unyama ambao hajawahi kuufanya duniani.

“Kisa cha yeye kufika Marekani, mababu zake waliletwa kama watumwa kutoka Swadege ya Rwadege kabla ya volkeno kulipuka.

Wakazaa hapa Marekani watoto, ndiyo hawa kizazi cha Azra ambao baadaye wote wakawa Wamarekani kwani baada ya volkeno kulipuka hakuna aliyerudi tena huko kwa miaka mingi.
 
Sehemu ya 04

“Sababu hasa Azra Malama kufanya mauaji na unyama wa kila aina ni baada ya wazazi wake kuuawa kipindi cha ubaguzi wa rangi, lakini ubaya nao una hatima yake, mwishowe aliishia kwenye vyombo vya sheria na sasa ananyolea ndevu gerezani!” Steve aliweka kituo.

“Nimewahi kumsikia Azra pia, ninafikiri anatufaa.” Lucas Tone alichangia. “Kesi yake iliyompeleka gerezani ninaikumbuka vizuri kwa sababu ilikuwa gumzo NewYork, nzima.”

“Ilikuwaje?” Tasha aliuliza.
Lucas Tone alianza kusimulia namna kesi hiyo ilivyoanza, kuwa gumzo kubwa na mpaka mwisho Azra Malama alipotiwa mbaroni.

“Nakumbuka ni miaka kama saba hivi iliyopita na ilikuwa mwezi Novemba. Kundi la wazamiaji kutoka Mji wa Ohio walikwenda kufanya mazoezi kwenye mto uliopo jirani na mji huo.

“Wakiwa huko wanaendelea na mazoezi mmoja wa wazamiaji alikwenda kina kirefu, takribani mita 24, akionyesha umahiri wake wa kupiga mbizi na ndipo alipohisi harufu kali chini ya maji, aliposogea zaidi aligundua kulikuwa na mfuko wa plastiki mkubwa ambao ulikuwa na mabaki ya miili ya binadamu!

“Mzamiaji huyo na wenziye ilibidi wasitishe mazoezi yao na kutoa taarifa polisi, jioni ya siku hiyohiyo, kikosi cha polisi idara ya uzamiaji kilifika kwenye mto huo na kufanikiwa kutoa mfuko ule.

“Walipofungua ule mfuko waligundua kulikuwa na miili ya watu wawili, mwanamke mwenye umri wa miaka chini ya 40 na mtoto wa kike mwenye miaka chini ya 13 na wote walikuwa wamepigwa risasi maeneo ya kichwani. Baada ya uchunguzi wa miili ile walibaini pia ilikaa kwenye maji kwa miaka mitano na walifungwa na vitu vizito ili wasiweze kuelea,” alisimulia Tone.

Tone aliendelea kwamba baada ya polisi kumaliza uchunguzi wao waliripoti tukio hilo kwenye vyombo vya habari na jopo la wapelelezi walianza kazi yao.

Kwa kuanza wapelelezi hao walirudi kwenye mafaili ya miaka mitano nyuma na kuchunguza juu ya watu walioripotiwa kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha.

Haikuwa kazi kubwa kwani waliweza kuwapata mama na mtoto walioripotiwa kupotea mnamo May 20, 1979, mama aliitwa Judith Lewis na mtoto alikuwa Lilian Lewis, wakazi wa Palidon.

ITAENDELEA…
 
Sehemu ya 05

“Askali wa upelelezi walikwenda nyumbani kwa mama huyo kutokana na maelezo yaliyotolewa wakati huo polisi na waliweza kufanikiwa kukuta watu wakiishi nyumbani pale.

Waliwahoji juu ya kupotea kwa wawili hao, mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Linda ambaye alikuwa ni mama wa Judith ndiye aliyetoa maelezo.

“Alisema wakati huo nyumbani hapo marehemu alikuwa anaishi na mwanaye Lilian pamoja na mumewe ambaye alikuwa ni baharia. Kabla ya tukio la kupigwa risasi na miili yao kutoweka, miezi michache iliyopita huyo baharia alipokwenda kwenye safari zake hakuweza kurejea.

“Kwa kuwa ilikuwa kawaida aliposafiri kukaa hata mwezi mmoja mwanzoni hakuna aliyepata wasiwasi, lakini jambo la kushangaza miezi miwili, mitatu hadi minne ilikatika.

“Ndipo mkewe alipoamua kutoa taarifa polisi, kwa ndugu na jamaa ili kupata msaada kufahamu mumewe alikuwa wapi, lakini hakuweza kupatikana, akawa amepotea hivyo.

“Miezi miwili tu baada ya kutoa taarifa polisi na kushindikana kupatikana kwa mumewe, Linda aliendelea kusimulia kuwa, mwanamke naye na mtoto walitoweka katika mazingira ya kutatanisha siku moja walipokuwa wametoka kanisani.

“Polisi waliuliza juu ya siku hiyo ilivyokuwa na mtu wa mwisho kuwaona alikuwa ni nani, Linda aliwaambia alikuwa ni jirani ambaye naye alikwisha fariki.

Ukweli ni kwamba kesi hii ilionekana kuwa na ugumu wa kuifuatilia. Kwanza miaka mingi ilikuwa imekwisha pita, lakini mtu sahihi ambaye angeweza kusaidia uchunguzi alikuwa amekwisha fariki.

“Lakini polisi hawakukata tamaa, waliamua kuelekezea umakini wao kwenye uchunguzi wa kesi hiyo kuona kama wangeweza kufanikiwa kumpata muuaji.

“Ndipo walipoamua kwenda nyumbani kwa jirani yule aliyedaiwa kumuona marehemu saa chache kabla ya kutoweka. Walipofika nyumbani hapo walikutana na binti wa marehemu aitwaye Stellah, mwenye umri wa miaka 18.
 
Sehemu ya 06

“Walifanya mahojiano na binti huyo, alidai ni kweli alikuwa na taarifa za kupotea kwa Judith na mwanaye Lilian kwani wakati wanatoweka yeye alikuwa na umri wa miaka 13.

Zaidi Stellah alisimulia kwamba mama yake ndiye mtu wa mwisho kuzungumza na Judith siku hiyo ya tukio na kwa mujibu wake aliwahi kusimulia kwamba siku hiyo baada ya kutoka kanisani Judith, aliyekuwa jirani na rafiki yake alipita nyumbani pale kumsabahi.
“Baada ya mazungumzo aliondoka.

Lakini mida ya jioni siku hiyo aliyopotea aliona gari aina ya Landrover ikiwa imeegesha uwanjani kwa Judith na ilikuwa ni gari ya kampuni moja la utalii liitwalo Impala.

“Hayo ndiyo yalikuwa maelezo ya Stellah. Baada ya kupata maelezo hayo polisi walianza kuchunguza juu ya kampuni hiyo.

Baada ya uchunguzi waligundua lilikuwa ni kampuni ya utalii ambayo ilihusiana pia na kukodisha magari iliyokuwa Chicago.
“Maafisa wa upelelezo walifunga safari mpaka Chicago kwenye masikani ya kampuni hiyo.

Walipofika walieleza nia yao juu ya upelelezi na kuomba kitabu cha kumbukumbu cha miaka mitano iliyopita, wakachunguza wiki moja mpaka siku ya tukio kuona kama watapata mtu aliyekodi gari,” anaendelea kusimulia Tone.

“Ikawaje?” Tasha aliuliza kwa shahuku.
“Ilikuwa rahisi. Mtu pekee aliyeshukiwa kati ya waliyokodi magari alikuwa ni kijana mmoja aitwaye Wens Lyan, muongoza safari za watalii wa kujitegemea (tour guide).

Rekodi zake zilieleza kwamba baada ya kukodi gari hilo aliliendesha zaidi ya kilometa 3000, zilizotosha kufika mpaka Ohio na kurudi. Lakini zaidi, gari hilo alilirudisha siku moja baada ya tukio.

“Maafisa wale wa upelelezi kabla ya kumtafuta huyo kijana waliendelea kuchunguza katika mji huo kama siku moja kabla ya tukio alifanya manunuzi yoyote, walifanikiwa kupata rekodi zake katika supamaketi moja aliponunua vyakula vya mifugo lakini kwenye vituo vya kuwekea mafuta vyote hakukuwa na rekodi zake.

“Taarifa nyingine ambazo ziliwachanganya ni kwamba katika jioni hiyohiyo ambapo tukio hilo lilitokea kulikuwa na rekodi kwamba Wens, akitoka supemaketi alipata ajali baada ya kumgonga mtembea kwa miguu tena alikuwa anatumia gari nyingine aina ya Prado.
 
Sehemu ya 07

“Suala hilo lilileta picha nyingine kwa wapelelezi. Kwa sababu kama alifanya manunuzi jioni na kupata ajali siku ya tukio hakukuwa na namna kwamba aliweza kusafiri kilometa 1500 kwa saa tano kwenda kutekeleza tukio na kurudi Chicago.

Labda kama alilikodi gari hilo na kumpa mtu mwingine. Hilo lilionekana wazi kutokana na jali aliyopata akiwa na gari lingine.

“Lakini uamuzi wa mwisho uliofikiwa ni kwamba atafutwe Wens, ili wasikie atakachozungumza.

Hilo lilifanyika lakini baada ya kupata mawasiliano yake na kuwasiliana naye alisema kwamba hayupo Marekani, wakati huo alikuwa India amepeleka watalii kwenye milima ya Himmalaya.

“Alisubiriwa kwa muda wa mwezi mmoja mpaka aliporudi. Ndipo alipohojiwa. Wens baada ya kubanwa alikiri kwamba ni kweli yeye ndiye alikodi gari, lakini alikodi kwa ajili ya mteja wake aitwaye Azra Malama,” alisimulia Tone.
“Huyo Azra Malama ulimfahamu vipi?” aliulizwa.

“Ni mteja wangu wa muda mrefu. Mara kwa mara amekuwa akinitumia kama dalali wake kumkodia magari kwa ajili ya safari zake za hapa na pale.” Alijibu Wens.

Tone anaendelea kusimulia kwamba, taarifa za Azra Malama zilikuwa chafu na zinatisha baada ya kuzifuatilia. Kwa maelezo aliyoyatoa Wens, haikuwa na shaka kwamba ndiye aliyetenda tukio hilo ingawa swali lilibaki ni kwa nini alifanya hivyo?

Tone aliendelea kusimulia kwamba wapelelezi wale walimfungulia Azra Malama kesi mahakamani ya kushukiwa kuhusika na mauaji hayo na waliomba kibali mahakamani cha kukamatwa kwake.

Alikamatwa na mara baada tu ya taarifa kutoka kwenye vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwake akishukiwa na mauaji ya Judith na binti yake Lilian, alijitokeza mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Lucy Wolker, ambaye alitoa ushahidi uliosababisha Azra afungwe kifungo cha maisha jela.

“Lucy alidai kwamba aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Azra lakini baadaye, baada ya kugundua alikuwa ni mnyanyasaji wa kijinsia, asiyempa uhuru wa kuzungumza aliachana naye na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na baharia aitwaye Lewis, mume wa marehemu Judith.
 
Sehemu ya 08

“Mwanamama huyo aliendelea kusimulia kwamba akiwa kwenye uhusiano baadaye Azra aligundua na kutokana na wivu wa kimapenzi alimtishia huyo mwanaume Lewis kuwa angemkomesha kwa kumfanyia kitu kibaya.

Wiki moja tu baada ya vitisho hivyo Lewis alipotea katika mazingira ya kutatanisha na miezi miwili familia yake nayo ilitoweka mpaka hapo ilipogunduliwa mtoni.

“Lucy alisimulia kwamba kutokana na matukio hayo aliogopa na kuamua kukimbilia Afrika, nchini Ghana alikokuwa anaishi ndugu yake mmoja kwa sababu alifahamu baada ya hao kutoweka ilikuwa ni zamu yake.

Alirudi Marekani baada ya kusikia habari za kukamatwa kwa Azra Malama kwenye vyombo vya habari!”

Kwa mujibu wa Tone, wakili aliyekuwa anamtetea Azra alishindwa kumnusuru kijana huyo mnyama kwenye kifungo cha maisha, ndipo alipotupwa kwenye Gereza la Guantanamo.

Baada ya simulizi hiyo ya Tone, wote walishusha pumzi. Hakuna aliyekataa kwamba Azra hakuwa mtu hatari na kama isingekuwa umakini wa polisi kwenye kesi hiyo iliyokuwa inamkabili, huenda angekuwa bado mtaani anaumiza watu wengi kwa matukio makubwa zaidi.

Hata hivyo, wote kwa pamoja walikubaliana kufanya mpango wa kumtoa Azra Malama gerezani na kumpeleka Afrika, huko Swadege ya Rwadege kwa ajili ya kazi moja tu, kukitawala kisiwa hicho ili Marekani ipate mimea ya uhai na kujiimarisha zaidi kwenye suala zima la teknolojia.
Guantanamo Bay, Cuba
Saa 2…asubuhi

Anaonekana paka mdogo mwenye rangi ya dhahabu na madoa ya kijivu huku usoni akiwa na michirizi ya rangi nyeusi kama ya chui, akikimbia taratibu kwenye korido la gereza la Guantanamo. Paka huyo alikuwa na kimo cha sentiment nne na urefu wa sentimeta nane.

Akiendelea kukatiza huku akikimbia kwa mwendo usiyo wa kasi mara anafika sehemu na kukwama kwenye kiatu kikubwa, kilichovaliwa na kijana mweusi, mrefu, mwenye misuli mingi, aliyenyoa kipara kichwani kwake huku kidevuni ndevu zake zimezunguka kwa alama ya 0.
Baada ya paka kukwama miguuni mwake kijana huyo aliinama taratibu na kumbeba.

ITAENDELEA…
 
Sehemu ya 09

Hata hivyo alipombeba tu, wakati anainuka na kutupa macho yake mbele alikutana ana kwa ana na macho ya mzee wa Kizungu, mwembamba, mwenye nywele nyingi na ndevu zilizozunguka uso mzima, mzee huyu alikuwa amevaa pia sare za wafungwa wa gereza hilo kama alizokuwa amevaa huyo kijana, lakini yeye kwa juu alivalia jaketi jeusi. “Oh! Asante,” Yule mzee alizungumza akiwa anatabasamu na kunyoosha mikono kumpokea paka.

“Ni wako?” Yule kijana alimuuliza.
“Ndiyo,” alijibu.
“Karibu,” alimpa paka mikononi.
Yule mzee alimpokea paka wake na kumpakata kwa mkono wake wa kulia.
“Unaitwa nani?”

Kijana aliulizwa.
“Azra Malama.” alijibu huku anakunja mikono yake kwa mtindo wa swala.
“Oh!” mzee aliguna.

“Ni lazima utakuwa unatoka Queens, New York!”
Azra alionekana kuishangaa kauli ya mzee huyo kisha akamtazama kwa makini.
“Umefahamu vipi?”

Alimuuliza.
Yule mzee alijibu kwa tabasamu laini kisha alisogea mbele zaidi mpaka alipokuwa amesimama Azra, akampigapiga begani akiwa bado anatabasamu, akaanza kupiga hatua na kundoka mahali hapo.

Azra aligeuza shingo na kumtazama huyo mzee wakati anaondoka lakini mpaka anaishilia bado akilini alijiuliza mzee huyo alifahamu vipi kwamba anatoka Queens, New York, Marekani na alikuwa anamfahamu kwa kiasi gani, ila hakuweza kupata majibu!

Siku hiyo ilipita, siku iliyofuata wafungwa wa gereza hilo walikuwa kwenye Kilima cha Dibt, ambako uchimbaji ulikuwa unaendelea ili kutengeneza njia ya treni zipitazo chini ya ardhi. Kilima hicho kilikuwa kina miamba migumu, kwa hiyo wafungwa walikuwa wanapiga kazi kwelikweli.

Miongoni mwa wafungwa hao alikuwa ni Azra Malama. Alikuwa kifua wazi na jasho lilikuwa linamchuruzika kuliko kawaida, akizidi kurusha sururu juu na kupiga ardhini mara kuna mtu alisimama mbele yake.

Azra aliachana na kile alichokuwa anakifanya akasimama ili kumtambua mtu huyo, aligundua ni yule mzee aliyeonana naye siku iliyopita kule gerezani, alikuwa ametua chini ndoo ya maji, mkono wa kulia alikuwa ameshika kikombe kikubwa cha plastiki na mkono wa kushoto alikuwa ameshika paka wake.
“Maji?” Yule mzee alimuuliza.
“Ndiyo.” Azra alijibu.
 
Sehemu ya 10

Bila kuzungumza neno mzee aliinama na kuchota maji kisha akampa Azra, aliyeyabugia haraka na kuomba aongezwe, aliongezwa na kuyabugia tena kisha akamrudishia yule mzee kikombe.

Baada ya kushika kikombe yule mzee aliinama na kubeba ndoo yake ili aondoke, lakini Azra alimzuia.

“Subiri,” alimwambia. Yule mzee alitua ndoo chini.
“Hujaniambia paka wako anaendeleaje?” alimuuliza.

“Oh!” Yule mzee alisema akimtazama paka wake. Kisha akainua uso na kumjibu Azra; “Yupo salama.”

“Suala lingine, jana nilikutajia jina langu lakini wewe hukunitajia jina lolote, si lako wala la paka wako?” Azra alimwambia yule mzee tena.

Mzee alitabasamu kisha akajibu;
“Paka wangu kipenzi anaitwa Hope.”
“Wewe?”

“Naitwa Steven Kessy.”
“Steven kessy?” Azra aliuliza kana kwamba alikuwa anadadisi jambo.
“Ndiyo, unanifahamu?” mzee Kessy alimuuliza.

“Hapana. Sijawahi kukusikia ndiyo maana bado ninajiuliza umefahamu vipi mahali natoka.”

Mzee Kessy alitabasamu. Kisha alimwambia Azra aendelee na kazi na yeye akapiga hatua kwenda kugawa maji kwa wafungwa wengine.

Azra alimshindikiza kwa macho akiwa bado mwenye maswali mengi juu ya mzee huyo, aliyeonekana kuwa kivutio cha wafungwa wengi kwani kila alikokuwa anapita alikuwa akiitwa Kessy mtu mbaya!.

Hata hivyo baada ya kumaliza kipiga kazi nzito kwenye kilima hicho, majira ya jioni muda ambao wafungwa walitakiwa kupata chakula na kupumzika kidogo kabla ya kuingia kulala, Azra alitafuta mahali alipokaa mzee Kessy ili aweze kukaa pamoja naye. Alimuona na kumfuata.

“Naweza kukaa hapa?’ Azra akiwa amesimama mbele ya mzee Kessy, mkononi akiwa ameshika chakula alimuuliza.

“Kwa nini leo, siku nyingine huwa unakula na rafiki gani?” mzee Kessy alimjibu Azra kwa swali.

“Sina rafiki gerezani hapa, labda kwa sasa nimepata wawili, wewe na paka wako Hope.”

“Mkh!” mzee Kessy aliguna.
“Sasa nikae?” Azra aliuliza tena.
“Karibu.”

Azra Malama aliketi pamoja na mzee Kessy kisha akaweka chakula chake mezani. Ukimya wa muda ulitawala wakimeza mlo wao wa siku hiyo, Azra ndiye aliyeamua kuuvunja ukimya huo.
“Sijawahi kukuona kwenye gereza hili, wewe ni mfungwa mpya?” alimuuliza.
 
Sehemu ya 10

“Hapana, nilikuwa jengo lingine, nimehamishiwa huku siku chache zilizopita baada ya mabadiliko yangu ya kitabia.”

Azra alimuelewa mzee Kessy alikuwa anamaanisha nini. Katika gereza hilo la Guandanamo wafungwa waligawanyishwa kwenye majengo mawili.

Wale watukutu zaidi waliwekwa kwenye jengo lao lililojulikana kwa jina la gereza la kifo. Huko ilikuwa ni kufa na kupona. Ili uishi ulitakiwa kuwa mbabe au uwe rafiki wa mtu au wa kundi linaloogopwa na wafungwa wengine.

Kwenye jengo hilo wafungwa waliuana wenyewe kwa wenyewe na wale waliojaribu kuwaletea ushenzi askari magereza ambao walikuwa wanawalinda walitafunwa wazimawazima mfano wa chui wanavyomrarua swala msituni na askari hao wasiotaka masihala.

Pamoja na hivyo kwa wafungwa ambao walikuwa wanaonekana ni wastaarabu, wasioshiriki kwenye ugonvi mara kwa mara walikuwa wakiamishwa kwenye jengo hilo na kupelekwa kwenye jengo la wastaarabu walipokuwa kina Azra Malama.

Huku walipata nafasi ya kujisomea vitabu tofauto na viongozi mbalimbali wa dini waliwatembelea kuwafundisha neno la Mungu na kuwapa nafasi wale waliojutia matendo yao kutubu dhambi zao na kumrudia muumba wao! “Kwa hiyo…” alizungumza na kushusha pumzi. “Bado hutaki kuniambia unanifahamu kwa namna gani?”

Mzee Kessy aliinua uso na kukiacha kijiko kwenye bakuri la mchuzi, kisha akamuuliza Azra;
“Kwa nini unafuatilia sana juu ya mimi kukufahamu, unawasiwasi au unajificha usifahamike?”

“Hapana, wewe ni mtu wa kwanza kunifahamu gerezani hapa ndiyo maana ninatamani kufahamu ni vipi umeweza kunifahamu.”

“Ninatoka ulipotoka.” Mzee Kessy alimjibu Azra kwa uhakika.
“Queens?”
“Jirani, Manhattan.”
“Oh!”
“Ndiyo.”

“Vipi kuhusu kunifahamu?”
“Sikufahamu wewe, ninafahamu jina lako. Lilikuwa maarufu mahakamani na nimeshiriki kesi zako nyingi.”
“Umeshiriki?’

“Ndiyo. Mimi ni jaji nimefanya kazi kwenye mahakama nyingi New York.”
Baada ya maneno hayo Azra alibaki kimya akimtolea macho mzee Kessy.
“Vipi mbona kimya hujaridhishwa na majibu yangu?” mzee Kessy alimuuliza.

“Nimeridhika. Kikubwa ninashangaa kuona mtu mwenye dhamana ya kupeleka binadamu kutesekea magerezani yupo na wauaji, pamoja na wahalifu mbalimbali kwenye eneo hilo lisilostahili hata
 
Sehemu ya 11

“Hakuna mtu aliye juu ya sheria.”
“Lakini wanasheria na majaji mpo kwenye sheria.”

“Kumbuka hata bingwa wa dunia wa kuogelea anaweza kufa kwa kuzama majini, au mshindi wa mashindano ya olimpiki ya magari anaweza kufa kwa ajali ya gari.”

“Nini umefanya ambacho kimekufikisha hapa jaji?” Azra aliuliza.
“Vipi kuhusu wewe?” Mzee Kessy alijibu kwa swali.

“Unafahamu,” Azra alijibu.
“Kuua!”
“Hilo ni neno jepesi, sema mauaji ya kutisha itakuwa sahihi zaidi.”
“Mkh!”

“Ndiyo. Haya nieleze kuhusu wewe.”
“Niliua pia, mauaji ya kinyama.”
“Jaji!”
“Niamini.”
“Ulimuua nani?”
Swali la Azra, lilikuwa ni sawa na kumkumbusha msichana mzuri tukio la kubakwa lililowahi kumtokea maishani mwake.

Ghafla mzee wa watu alipoteza hali yake ya uchangamfu akakusanya mikono pamoja utadhani mtu aliyekuwa anasali kisha akamkodolea macho Azra.
Ukimya kwa mara nyingine ukatawala.

Lakini ukiwa haujafikia kuwa ukimya wa kupitiliza mzee Kessy taratibu alivua kidani shongoni mwake kilichofungwa na kinachoonekana mfano wa kompasi kisha akakifungua na kukitazama kwa sekunde kadhaa, kisha alimpatia mkononi Azra.

Baada ya kukitia mkononi Azra alikimbiza macho haraka kwenye kidani hicho, kilikuwa na pande mbili ambazo zote zilikuwa na picha.

Upande mmoja ilikuwa ni picha ya mwanamke wa Kizungu mwenye umri wa miaka kama arobaini hivi, upande mwingine kulikuwa na binti mdogo mwenye sura na ngozi ya kuvutia, umri wake usingezidi miaka kumi na sita.
“Ni familia yako?” Azra aliinua uso na kumuuliza mzee Kessy.

“Ndiyo. Ni mke wangu na mtoto, hao ndiyo niliwaua.”
“Mungu wangu.”

“Ni kweli Azra, moyo wangu unaniuma sana, binti mdogo asiye na hatia Candice, nilikuwa ninampenda mno. Moyo wake upumzike penye amani,” mzee Kessy alizungumza kwa simanzi.

Azra aliinamisha kichwa tena kutazama zile picha mbili kwenye kidani alichoshika mkononi, macho yake yaliganda hasa kwenye picha ya yule binti.

“Jaji…”aliita Azra. “Kwa nini uliamua kuiteketeza familia yako?”
“Ni stori ndefu mdogo wangu.”
“Nisimulie tafadhali.”
 
Sehemu ya 12

Mze Kessy alivuta pumzi ndefu ndani na kuitoa nje, kisha alimchukua paka wake Hope mezani alipokuwa, kama kawaida yake alimpakata kwenye mkono wake wa kulia na mkono wa kushoto ukawa unachezea manyoya kichwani kwa paka huyo.

“Jaji tafadhali nisimulie kilichotokea,” Azra alimsisitiza. Mzee huyo hakuwa na namna zaidi ya kuanza kumsimulia;

“Toka nikiwa mdogo nilipenda sana masuala ya sheria na niliota siku moja kuishi mahakamani nikiwatetea wanyonge au kuwapeleka wahalifu jela. Ili kutimiza ndoto zangu baba yangu alinisisitiza kusoma kwa bidii, jambo nililofanya.

“Hatimaye nilimaliza elimu ya msingi, ngazi za sekondari pamoja na chuo. Mungu mkubwa nikafanikiwa kuwa jaji tena maarufu kutokana na busara ya kuamua kesi nyingi, nikawa jaji mwenye mafanikio makubwa katika umri wa miaka 34!

“Sasa nikiwa ninaheshima kwenye jamii, nikila chakula nilichopenda, nikivaa suti kutoka Italia, viata na saa za ghalama ya juu kutoka Japan, nikiishi kwenye nyumba ninayopenda na kuendesha magari yaliyouburudisha moyo wangu, jambo moja likawa linanikosesha furaha nalo lilikuwa ni kukosa mtoto,” anasimulia mzee Kessy na kuendelea kuwa;

“Hadi wakati huo nilikuwa nina miaka minne kwenye ndoa pamoja na mke wangu Amanda, tulikwisha zunguka mahosipitalini na kwenye nyumba za ibada mbalimbali lakini jitihada zetu hazikuweza kuzaa matunda, kwa hiyo ilifika hatua tukaamua kumuachia Mungu atende miujiza yake.”

Mzee Kessy aliendelea kumsimulia Azra kwamba, jambo la kushangaza baada ya miaka kumi mingine wakiwa ndani ya ndoa mkewe aliweza kupata ujauzito na kujifungua mtoto wa kike.

“Sikufichi Azra nilifurahi mno. Kwangu nilichukulia ni sawa na miujiza na kwamba Mungu aliamua kujibu maombi ya mja wake.

Binti huyo wa kike akawa amegeuka faraja kwenye maisha yangu. Nilimpenda na nilimpa jina la mama yangu Candice na hata malezi yake nilimlea mfano wa binti aliyezaliwa kwenye familia ya kifalme.

“Furaha ikawa imeongezeka, lakini Candice akiwa na miaka 16, tabia za mke wangu zilianza kubadilika. Akawa mtu wa kusafiri sana akidai kwamba alikuwa anasafiri kikazi na mambo mengine mengi ambayo sikuwa ninayaelewa.
 
SEHEMU YA 13

“Nikaamua kufuatilia nyendo zake, hapo ndipo nilipogundua kwamba alikuwa na uhusiano wa mtu mwingine. Roho iliniuma mno Azra. Nilijiuliza maswali mengi ni kwa nini mke wangu aliamua kunifanyia hivyo tena kwenye umri wetu wa uzeeni lakini sikuweza kupata majibu.

“Ikabidi nimbane na kumuuliza kwa nini aliamua kufanya hivyo, hakuzungumza lolote, nilipomtishia kumpa talaka hakutishika aliniambia alikuwa anaisubiri kwa hamu, zaidi aliniambia kwamba Candice hakuwa mtoto wangu bali alikuwa ni mtoto wa mwanaume huyo aliyekuwa naye kwenye uhusiano.”

Alipofika hapo mzee Kessy ni kama moyo wake uliingiwa na ubaridi, alikaa kimya kwa sekunde kadhaa kisha akainamisha kichwa chake na machozi yalianza kumbubujika.
“Pole sana jaji Kessy.”
“Asante…”

Alijibu na kufuta machozi. Kisha aliinua uso na kuendelea kusimulia;
“Mwanzoni nilifikiri ni masihara na kwamba zilikuwa ni hasira tu za mke wangu, lakini alizidi kusisitiza mara kwa mara kwamba baba wa binti huyo alikuwa anamtaka mwanaye, hapo ndipo nilipoamua kuchukua uamuzi wa kupima vinasaba, nilihisi kufa pale nilipopewa majibu, Candice kweli hakuwa mwanangu wa damu.

“Jambo hili liliniumiza mno moyoni kwa maana Candice alikuwa ni kipenzi changu, msongo wa mawazo ulinikumba na taratibu nikaanza kupoteza uelekeo kwenye kila kitu nilichokuwa ninakifanya kwenye maisha yangu.

Hakuna ambacho kikawa kinaniridhisha tena maishani, usiku nikilala niliota ndoto za vifo, mchana nikitembea ni kama nilikuwa ninapiga hatua kwenda kaburini na hata kivuli changu nilikiona ni sawa na mtu aliyekuwa ananisindikiza kwa kunisukuma niingie kaburini ili watu wanifukie.
Mzee huyo alizidi kumsimulia Azra kwamba;

“Mpaka kufika hatua hiyo siku zikawa hazisongi tena mbele na giza nene lilitanda kwenye maisha yangu, nikapoteza kabisa matumaini ya kuishi.

“Ustahimilivu katika kila kilichokuwa kinaendelea ulinishinda baada ya mwanamke huyo kuzidi kunidharau na kudai talaka pamoja na kumpeleka mtoto kwa baba yake, hapo ndipo nilipofikia maamuzi magumu mno ya kuwachinja mtu na mama yake kisha nikaenda kujikabidhi kwenye mikono ya polisi na kuwaeleza nilichofanya.”
 
SEHEMU YA 14

“Mh!” Azra aliguna baada ya mzee Kessy kumaliza kumsimulia.
“Ndiyo hivyo.

Hayo yalikwisha tokea na kwa sasa sina uwezo wa kwenda kubadilisha jambo lolote ambalo nimekwisha lifanya, kwa sasa ninaishi kwa kumtegemea Mungu zaidi.
“Huyu paka mdogo unayemuona ndiye tumaini langu jipya ndiyo maana ninamuita Hope.

Mara zote nikiwa peke yangu, utanikuta ninamchezea manyonya maeneo ya shingoni kwake, nikifanya hivyo mawazo hupaa na kujikuta ninawaza juu ya mustakabali wa maisha ya baadaye nje ya gereza.”

“Jaji, upo nje ya akili yako, kwa kesi ya mauaji unawezaje kutoka gerezani?”
“Hapana wala sijachanganyikiwa. Kwa mujibu wa sheria ni kweli kesi ya mauaji ni kifungo cha maisha.

Lakini kwa upande wangu nimekuwa nikizungumza mara kwa mara na Mungu kupitia mawazo yangu na kwenye sala, huniambia kwamba hajamalizana na mimi na ipo siku nitatoka gerezani kwenda kutoa ushuhuda huu kwa wanadamu.”

Mazungumzo ya wawili hawa yalikuwa yamenoga, lakini bahati mbaya wakati haukuwa rafiki kwao, kwani muda wa kula na kupumzika waliokuwa wamepewa wafungwa ulikuwa umemalizika. Kengele ya kuwajulisha muda umemalizika iligonga, mzee Kessy na Azra waliagana na kuahidiana kwamba wangeonana na kuzungumza zaidi siku iliyofuata.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa ukaribu wao gerezani. *** Ukaribu kati ya Azra Malama na mzee Kessy ulizidi kukomaa maradufu. Kila mara wakiwa gerezani humo walikuwa pamoja wakizungumza mambo mengi kuhusu mapito yao ya nyuma na namna wanavyoweza kuishi kwa matumaini.

Siku na miezi vilikatika, hatimaye miaka, na hii ilikuwa ni asubuhi nyingine kwenye majira ya joto, mshale wa saa ulisoma kwenye nane na wafungwa kwenye gereza hilo la Guantanamo, walikuwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida ambapo siku hiyo walikuwa wakisomba mchanga, mawe na kokoto kusaidia ujenzi uliyokuwa unaendelea gerezani hapo.
“Kiukweli tunafanya kazi kama punda,hulioni hili..?”

Azra alimwambia mzee Kessy akibwaga kiroba cha kokoto alichokuwa amebeba begani. Kiufupi alikuwa amechoka kwa kazi siku hiyo. “Mfungwa hana haki.” Mzee Kessy alimjibu.

“NYIE KWENDA!” Ilisikika sauti ya mamlaka kutoka nyuma yao.
 
SEHEMU YA 15

Wote waligeuza shingo pamoja, walimuona askari magereza akiwasogelea huku ameshika mnyororo uliomfunga mbwa mkubwa mwenye manyoya mengi, aliyetoa ulimi nje utafikiri mtu aliyetweta kwenye mbio ndefu na alikuwa anaongoza mbele akinusa ardhini.

Na ubabe wote aliokuwa nao Azra mbele ya mbwa huyo asingethubutu kuonyesha kiburi cha aina yoyote kwani angegeuzwa kitoweo mara moja.

Bila kuzungumza Azra aliinama na kujitwika kiroba chake lakini alivyokifikisha tu begani mara nyuma ya yule askari mwenye mbwa alitokea askari mwingine, alipomfikia yule askari mwenye mbwa alimnong’oneza jambo.

Yule askari mwenye mbwa alionekana akitikisa kichwa akiashiria kuna kitu alikuwa anakubaliana nacho. Kisha akamwambia Azra ambaye alikuwa ameanza kupiga hatua na mzee Kessy kwamba arudishe tena kiroba chake chini na kumfuata yule askari asiye na mbwa.

Azra alibwaga kiroba chini kwa ghadhabu kiasi kwamba askari na wafungwa waliyokuwepo mahali pale walimtupia macho, kisha akaanza kumfuata yule askari kama alivyopewa maelekezo mpaka kwenye moja ya ofisi za gereza hilo.
Baada ya kufungua mlango na kuingia kwenye ofisi hiyo Azra alishangaa kuona Wazungu wanne wakiwa wameketi kwenye viti.

Akamtupia macho yule askari aliyeongozana naye kwenye chumba hicho cha ofisi kana kwamba anamuuliza ‘hawa ni kina nani?’, lakini akiwa hajazungumza neno lolote Mzungu mmoja alisimama na kuanza kutembea kwenye ofisi hiyo.
“Azra Malama…” Mzungu huyo aliita huku anatabasamu.

“Mtu mweusi, mwenye nguvu na jasiri ambaye nguvu zake zinapotelea kwenye ujenzi wa majengo ya magereza, inasikitisha!” Mzungu huyo aitwaye Tone, aliiendelea kubwabwaja.

Azra bado alikuwa ni kama amepigwa butwaa akishangaa kilichokuwa kinaendelea maana kati ya watu wale hakuna hata mmoja aliyekuwa anamfahamu.

“Keti kaka.” Tone alimwambia tena huku akimuonesha mahali pa kukaa.
“Wakoroni…” Azra alisema na kutembeza macho kwa Wazungu hao waliyokuwa mbele yake. “Mnatafuta nini kwangu.” Aliuliza.
“Tumekuja kukupa uhuru,” Tone alimjibu haraka.

“Wakati mwingine kupewa uhuru kunamaanisha kunyang’anywa hata uhuru kidogo ulionao,” Azra alijibu tena huku mikono yake anaikunjia chini ya kifua kwa mtindo wa ‘swala.’
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom