Mwisho wa Azra Malama

Mwisho wa Azra Malama

SEHEMU YA 79

WAWAKILISHI kutoka mataifa mbalimbali walikua wamekusanyika kwenye Ukumbi wa St. Lois Elizabeth, jijini London, Uingereza.

Katika ukumbi huo kulikuwa na kikao mahususi kilichokuwa kinahusu nchi washiriki wa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa, ambapo kisiwa cha Swadege ya Rwadege kuliomba kushiriki kama mgeni mualikwa, kwa sababu hakikuwa kwenye jumuiya hiyo.

Kilikaribishwa.
Shamlashamla zikashamili, na kikao hicho kilikuwa kinaogozwa na katibu wake James Vero, kutoka nchini Ghana.

Kwenye kikao hicho, mambo mengi yalijadiliwa na wawakilishi hao ambapo baada ya ratiba zote kufanyika alikaribishwa muwakilishi kutoka kisiwani Swadege ya Rwadege, kupanda jukwaani kwa ajili ya kuzungumza ujumbe alio uandaa kwa wana jumuia wa Umoja wa Mataifa.

Kamanda wa Jeshi la Swadege ya Rwadege, Shebo, alisimama.
Alikuwa amevaa mavazi ya asili. Shati lake lilikuwa ni la sufi lililonakishiwa kwa urembo wa ngozi ya simba na vikorombwezo vingine.

Chini alikuwa amevaa pensi iliyotengenezwa kwa ngozi ya chui, pembeni ya kiuno chake alichomeka ala yenye panga.

Shebo taratibu alikatiza katika ya wanajumuiya hao na kwenda kusimama mbele yao kabisa akawa anawatazama wao.

Ukumbi mzima ulikuwa kimya kumsikiliza yeye. Kijana huyo ambaye alionekana kivutio mahali hapo kutokana na mavazi yao, yaliyokuwa yanawawakilisha wana Swadege ya Rwadege, alirekebisha sauti ili azungumze;

“Hii ni simulizi ya kaka zangu na dada zangu, tunaoishi katikati ya maji,” Shebo alianza kuzungumza. Watu wote wakaongeza umakini kumsikiliza.

“Kwa muda mrefu dunia imekuwa ikipambana na sisi ili tu, iharibu aina ya maisha ambayo tumechagua kuishi. Mataifa makubwa na watu mbalimbali wanatamani tuishi kama wao, tuvae kama wao, tutembee kama wao na tutende kama wao.

“Lakini sisi tunaamini kupitia kile Mungu alichotubariki. Katuwekea upendo katikati yetu, katupa vipaji vinavyoongeza ustadi kwenye aina ya maisha tunayoishi na ametupa fahari ambazo zinatusaidia kuboresha miundo mbinu na kutibu wagonjwa.

“Tunajivunia kuwa Waswadege. Tutaishi tutakavyo na si dunia itakavyo. Hii ni kwa ajili ya mtu mmojamoja duniani pia. Ishi wewe na si uishi vile mtu mwingine anahitaji uishi.
 
SEHEMU YA 80

“Unapoishi kama mtu mwingine, jiulize nani ataishi kama wewe? Jibu ni hakuna. Kama sisi Waswadege tulivyotayari kupambania mazao yetu ya uhai na kuyakinga kwa sababu ya kizazi chetu, hata wewe una wajibu wa kupambania kipaji chako kwa ajili ya kizazi chako.

“Kipaji pekee ndiyo kitakufanya uione thamani ya kuishi na wengine waione thamani hiyo kupitia wewe. Maisha ni wewe, na hayawezi kukamilika kwa upande wako bila kuwepo wewe mwenyewe.

“Si Mzungu wala Mwafrika. Ni wewe. Kuwa wewe, ishi wewe. Pambana kwa ajili yako, na Mungu atakubariki!”
Shebo alimaliza.

Ukimbi mzima ulishangilia. Lugha aliyoizungumza ilieleweka kwa kila mjumbe ambaye alikuwa kwenye kikao hicho.

Mbali na ujumbe mzito alioutoa kwa kila aliyekuwa mahali hapo, lakini pia yalikuwa ni matusi kwa Wamerekani ambao walikuwa wanahitaji kuharibu namna yao ya kuishi.

Wamarekani walijiona wenye hatia. Walitambua watu wa Swadege ya Rwadege walihitaji kuishi kwa aina ya maisha waitakayo na kufurahia yale ambayo wamejaaliwa na kubarikiwa.

Sasa kwa nini wabuguziwe. Kwa nini dunia iwalazimishe waishi kama inavyotaka au watu wajaribu kuwaingilia ili kuwatawala ilimradi tu kuwaharibia aina yao ya maisha.

Lilikuwa jambo ambalo si sawa.
Alipopata nafasi ya kupanda jukwaani mjumbe aliyekuwa anaiwakilisha Marekani, aliomba radhi kwa yote ambayo taifa lake lilifanya kwa Swadege ya Rwadege.

“Ukisimamia kile unachokiamini, na kukipambania kufa na kupona, itafika wakati dunia itakuelewa. Sisi Marekani tumewaelewa Swadege ya Rwadege. Tutawaacha Waswadege waishi kama wao. Hiyo ndiyo furaha yao,” alisema mjumbe huyo kutoka Marekani.

Hii ndiyo simulizi ambayo kijana Elemoti, alisimuliwa na babu yake alipokwenda kumtembelea huko umasaini na kumuuliza kuhusu Azra Malama na Swadege ya Rwadege.
Mpaka leo, Waswadege wanaishi kwa raha mustarehe.

Wanaishi katika aina ya maisha waitakayo.
Walijua maana ya maisha.
Wanafurahia maisha!

MWISHO!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom