MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO),
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2014/2015
(Kanuni ya 99(9) yaKanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefikisha umri wa nusu karne tangu ilipozaliwa tarehe 26 Aprili, 1964. Kama anavyosema Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda katika hotuba yake ya tarehe 7 Mei, 2014 Kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2014/2015:Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi.Waziri Mkuu ametumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinazoonyesha kwamba asilimia 90.6 ya Watanzania wotewamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Kwa maneno ya Waziri Mkuu,sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo kwa Watanzania wengine wengi, na mimi pia nimezaliwa ndani ya Muungano. Ninaamini kwamba ukweli huu unawahusu pia waheshimiwa wabunge wengi waliomo ndani ya Bunge hili tukufu. Na sisi pia tunaomba kutendewa haki kuhusu Muungano huu. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, haki tunayoomba kutendewa ni moja tu: kuambiwa ukweli juu ya Muungano huu na historia yake, hali yake ya sasa na mwelekeo wake wa baadaye. Haki tunayoomba kutendewa ni kwa watawala kuacha propaganda na uongo juu ya Muungano na kutuambia ukweli wote juu ya Muungano huu.
Bob Marley, aliyekuwa mwanamuziki mpigania uhuru wa watu weusi maarufu kutoka Jamaica, aliwahi kusema katika wimbo wakeGet Up, Stand UP, Stand Up For Your Rights(Amkeni, Simameni, Simameni kwa Haki Zenu) kwamba:You can fool some people some time, but you cannot fool all the people all the time, yaani,unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote! Baada ya nusu karne ya uongo na propaganda kuhusu Muungano huu, Watanzania wa kizazi hiki cha Muungano wanataka ukweli.
Na Watanzania hawa hawataulinda, wala kuuimarisha au kuudumisha Muungano huu endapo wataendelea kudanganywa au kufichwa ukweli juu ya mambo mengi yanayouhusu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, sisi kizazi cha Muungano tunahitaji kutendewa haki: acheni propaganda na uongo kuhusu Muungano huu ndipo muweze kutuambia tuulinde, tuuimarishe na tuudumishe!
SHEREHE ZA MUUNGANO NA WAASISI WA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano ni mahali pazuri pa kuanzia kudai ukweli juu ya Muungano huu. Mtu yeyote anayetembea sasa katika Barabara ya Nyerere kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam; au Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia Morocco hadi katikati ya jiji, ataona kila mlingoti wa taa za barabarani umepambwa kwa picha za Waasisi rasmi wa Muungano, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, wakiwa katika matukio mbali mbali ya siku za mwanzo za Muungano. Picha hizo za Waasisi hao pia zimepambwa karibu kila mahali katika barabara za katikati ya Eneo Kuu la Kibiashara (CBD) la Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, barabara zote kuu za Mji wa Zanzibar, ikiwamo ile inayotoka Mji Mkongwe kupitia Ikulu ya Zanzibar hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, hakuna picha hata moja ya Waasisi wa Muungano katika matukio yanayoonyeshwa kwenye picha zilizoko Dar es Salaam. Badala yake, barabara hizo zimepambwa kwa picha za Marais wa Zanzibar toka Mapinduzi ya mwaka 1964 hadi wa sasa. Ni ndani ya eneo la wageni maarufu (VIP) pekee ndio kuna picha moja ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Hii ni katika wiki ambayo Muungano huu umeadhimisha miaka hamsini tangu kuzaliwa kwake!
Kwa jinsi ambavyo tangu mwaka huu uanze Watanzania tumepigwa propaganda za kila aina juu ya Muungano na TBC na vyombo vingine vya habari vya serikali na vya binafsi, kukosekana kwa dalili yoyote ya sherehe za Muungano kwa upande wa Zanzibar wakati wa kilele cha sherehe hizo kunatilia shaka juu ya uimara wa misingi ya Muungano wenyewe. Hii ndio kusema kwamba pengine kuna ukweli katika hitimisho la Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Tanganyika ndiyo imevaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na pengine ndio maana Muungano huu haujawahi kuungwa mkono Zanzibar kwa kiasi ambacho wanaopenda kutuaminisha vinginevyo wamekuwa wakidai. Aidha, pengine ndio maana hata picha za kuchanganya udongo zinazoonyeshwa na TBC kila kukicha zinamwonyesha Mwalimu Nyerere akichanganya udongo peke yake, wakati Sheikh Karume haonekani kabisa!
Mheshimiwa Spika,
Kuna jambo lingine linalofikirisha sana kuhusu picha hizi za Sherehe za Miaka Hamsini ya Muungano zilizopamba mitaa ya Dar es Salaam. Baadhi ya picha hizo zinawaonyesha watu wengine ambao wamefutwa kabisa katika historia rasmi wanayofundishwa watoto wetu mashuleni na vyuoni. Hivyo, kwa mfano, katika picha maarufu ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano wapo pia, kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa upande wa Zanzibar wanaoonekana kwenye picha hiyo ni Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo. Aidha, kuna picha inayowaonyesha Mwalimu Nyerere, Sheikh Karume na Kassim Hanga wakitabasamu kwa furaha kubwa.
Katika kitabu chakeKwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabiakilichochapishwa mwaka 2010, Harith Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, na baadaye kufanikisha Muungano na Tanganyika wa Aprili 26 ya mwaka huo. Katika kitabu chakeThe Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya Dhoruba, Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe ameeleza kwamba ni Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde ndio waliompelekea Sheikh Karume nakala za Hati ya Makubaliano ya Muungano kabla ya Hati hizo kusainiwa tarehe 22 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni waasisi hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida kwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia rasmi ya Muungano na waasisi wake? Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Bhoke Munanka alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
KatikaKwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa muda wote wa nusu karne ya Muungano huu.
Kuhusu Oscar Kambona, inafahamika kwamba katika miaka ya mwisho ya ukoloni na miaka ya mwanzo ya uhuru, mwasisi huyu wa Muungano alikuwa mtu wa karibu sana wa Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere ndiye alikuwaBest Manwa Kambona wakati wa harusi yake iliyofanyika London, Uingereza mwaka 1960. Inafahamika, hata hivyo, kwamba mwaka 1967 Oscar Kambona.....