Kwanza, sijasema Mungu hayupo kwa sababu anatesa watu. Akitesa watu atakuwa yupo, si hayupo.
Nasema Mungu hayupo kwa sababu dhana ya Mungu kuwapo inajipinga yenyewe. Mara unaambiwa Mungu ana upendo mkuu, mara unaona vitoto vichanga masikini vinakufa kwa utapiamlo.
Watu wametunga dhana ya Mungu.
Wakampa Mungu tabia za watu. Ndiyo maana unasikia Mungu anatoa mtihani, Mungu anakasirika, Mungu anaghairi mambo aliyopanga na kuleta mafuriko duniani.
Mungu anakasirikaje wakati anajua kila kitu kitakavyokuwa? Anaghairi nini wakati anajua kila kitu kitakavyokuwa?
Anatoa mtihani ili iweje wakati yeye anajua yote yatakavyokuwa?
Mtihani ni sehemu ya maisha ya dunia ya watu wasio na nguvu zote, uwezo wote wala upendo wote. Kupimana ili kujua nani anajua zaidi. Na hata katika dunia hii, kuna baadhi ya jamii zinaondokana kwenye mifumo ya mitihani.
Sasa Mungu mjuzi wa yote, mwenye uwezo wote na upendo wote, kwanza kwa nini aweke mitihani mibaya sana inayoweza kuumiza watu wake anaowapenda?
Hivi, kuna baba mwenye akili zake timamu, anayewapenda watoto wake, anayesema leo najenga nyumba, naitegeshea mabomu ndani yake, ili wanangu wapate kujua kukwepa mabomu, wakati anaweza kujenga nyumba ambayo haina mabomu?
Hivi, msichana wa miaka 10 anayejiuza mjini Manila Philippines ili apate kula tu, anapewa mtihani wa maisha hayo na Mungu mwenye mapenzi?
Wale Wahutu na Watusti waliochinjana kama kuku, yani Mungu hata kama tunasema anatoa mitihani, alishindwa kuwapa mtihani mzuri ambao hauna mauaji ya kinyama?
Kwa nini Mungu anayejua kila kitu na kuweza kila kitu na mwenye upendo wote ahitaji kuwepo na mtihani, hususan kama mtihani wenyewe unaumiza sana viumbe wke anaowapenda?
Usiongelee mtihani kama kitu ambacho hakiepukiki katika dunia hii tunayoiona, ongelea mtihani kutoka perspective ya Mungu muweza yote, mjuzi wa yote na mwenye upendo wote.