Mtwara: Jinsi Askari Polisi akiwemo Mkuu wa Kituo na Upelelezi walivyoshiriki Mauaji ya Mfanyabiashara wa Madini

Polis ni majAmbaz yeny kibal cha kikaz'_ in voice of langa kileo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino John Mgonja ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara namna mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis Hamis, alivyouawa.

Pia, amewataja washtakiwa waliokuwepo eneo la tukio na yule anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo ya mfanyabiashara huyo aliyekuwa mkazi wa Nachingwea mkoani Lindi.

ACP Mgonja alitoa maelezo hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara. Yeye ni shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka kati ya mashahidi 72 wanaotarajiwa kuitwa na upande wa mashtaka katika kesi hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Gilbert Sostenes Kalanje na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Charles Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Nicholaus Kisinza, Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Shirazi Mkupa na Koplo Salim Mbalu.

Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa waliyemchoma sindano ya sumu katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Hata hivyo, wakati polisi hao wakiwa mahabusu kabla ya kupandishwa kizimbani, mtuhumiwa mwenzao, Grayson Mahembe alidaiwa kujinyonga hadi kufa Januari 22, 2022 akiwa mahabusu.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu aliieleza mahakama kuwa Mussa aliuawa na SP Kalanje Kwa kumziba kwa tambala mdomoni na puani, muda mfupi baada ya Dk Msuya (mshtakiwa wa Tano) kumdunga sindano ya usingizi.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa alipata taarifa za tukio hilo baada ya kuwahoji baadhi ya askari waliokuwa zamu katika kituo cha Polisi Mitengo, pamoja na Dk Msuya mwenyewe na ofisa wa polisi, Grayson (marehemu kwa sasa) ambao walisimulia tukio hilo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, siku ya tukio Januari 5, 2022, mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje alimpigia simu Dk Msuya akamtaka waonane na Dk Msuya ambaye al8ikaribisha ofisini kwake katika zahanati ya Polisi na wakazungumza.

Alidai kuwa SP Kalanje alimueleza Dk Msuya kuwa wana mtuhumiwa wao wa wizi wa pikipiki ambaye amekuwa akifanya matukio ya wizi huo maeneo mbali katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na amekuwa akiwasumbua hivyo wanataka wammalize.

Hivyo alidai kuwa SP Kalanje alimuuliza Dk Msuya kama anaweza kufanya namna ya kupata sindao ya sumu ili wamdunge, lakini Dk Msuya alimjibu kuwa tangu aajiriwe na kuapa kuwa daktari hajawahi kumdunga mtu sindano ya sumu.

Shahidi huyo amedai kuwa badala yake. Dk Msuya alimshauri SP Kalanje wamdunge sindano ya usingi , akizinduka ataanza kueleza matukio yote ya wizi aliyoyafanya, ushauri ambao Kalanje alikubaliana nao.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, licha ya SP Kalanje kutaka waende kutekeleza mpango huo wakati huohuo, lakini Dk Msuya alimueleza kuwa wakati huo bado alikuwa na wagonjwa wengine akiwahudumua na akashauri wafanye baadaye.

Saa 8:30 mchana, Kalanje alifika ofisini kwa Dk Msuya kwa ajili ya kutekeleza mpango huo kama walivyokuwa wamekubaliana, hivyo alimuuliza kama alikuwa tayari akamjibu kuwa alikuwa tayari.

Lakini Dk Msuya alimuuliza SP Kalanje mahali alikokuwa huyo mtuhumiwa wao, akamjibu kuwa alikuwa katika kituo cha Polisi Mitengo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, Dk Msuya alisema yeye anaelewa kituo cha Mitengo kina wahalifu sugu hivyo akajua na huyo amehifadhiwa kwa wahalifu sugu, akakubali akaingia kwenye gari na akakaa kiti cha mbele huku gari likiendeshwa na SP Kalanje.

Wakati gari inaondoka pale zahanati, Dk Msuya alihisi kama viti vya nyuma vina watu.

Hivyo aligeuka kutazama akawatambua watu wawili, ambao ni ASP Onyango na A/Insp Grayson waliokuwa wamekaa viti vya pembeni kulia na kushoto na katikati kulikuwa na mtu mwingine ambaye hakuweza kumtambua.

Waliendelea na safari hadi kituo cha Polisi Mitengo na SP Kalanje alishuka akaenda kuzungumza na mkuu wa kituo hicho, Paulo Kiula.

Dk Msuya na askari wale wawili pamoja na yule mtu ambaye hakumtambua nao walishuka wakamfuata SP Kalanje na mkuu wa kituo walipokuwa wanaelekea ndani ya jengo la kituo hicho.

Dk Msuya alimuomba OCS Kiula amuonyeshe Kalanje ofisi moja ambayo aliingia Kalanje, Onyango, Grayson na yule kijana na yeye akabaki nje.

Lakini baada ya dakika tatu hivi, naye alingia ndani ya hiyo ofisi na alimkuta yule kijana amevuliwa shati yuko kifua wazi na mikono yake ikiwa imefungwa kwa kamba kwa nyuma akiwa amelala kwenye sakafu huku akilia.

SP Kalanje alimwambia Dk Msuya amdunge sindano ya usingizi mkono wa kulia yule kijana.

Na baadaye kidogo, Dk Msuya anasema alimsikia Kalanje akisema huyo anawachelewesha, akachukua tambala akamziba yule kijana pua na mdomo.

Anasema baada ya Dk Msuya kuona vile aliamua kutoka nje akawaacha Karanje na wale wenzake na yule kijana akiwa amelala chini.

Lakini baada ya muda mfupi, Kalanje alimuita Dk Msuya akamuuliza, "tayari?" huku akimuonyesha yule kijana pale chini.

Dk Msuya alimuangalia kama hapumui lakini hakumpima ila alielewa lile swali la SP Kalanje kwamba lilikuwa linamaanisha kama amekufa na yeye alijibu kuwa tayari.

Hivyo wote walitoka mle chumbani na kumuacha yule kijana akiwa amelala pale chini.

SP Kalanje alikwenda kwa OCS akachukua kufuli likiwa na funguo akafunga mlango kisha wakaondoka wote akiwa na huo ufunguo, wakapanda gari na kuondoka.

Kamanda huyo wa polisi ambaye ni shahidi, aliieleza Mahakama kuwa baada ya maelezo hayo ya mdomo kutoka kwa Dk Msuya, alielekeza yaandikwe maelezo kama alivyosimulia na maelezo yake yawekwe kwenye jalada la uchunguzi.

“Wakati huo tulimchukulia Dk Msuya kama mtoa taarifa,” alidai Kamanda Mgonja.

Alidai wakati yote hayo yakifanyika, alijiuliza hayo mauaji ni ya huyo kijana Mussa ambaye ndugu zake walikuwa wanamtafuta au kuna mwingine?

"Hivyo nikaagiza atafutwe mjomba wa Mussa Hamis anayeitwa Salum Mombo aje ofini kwangu, alikuja nikamtaka anitafutie picha za Mussa kusudi ili niangalie yule mtu ambaye askari wanasema walimuona akiingia pale Mitengo ndiyo huyu kijana Mussa Hamis au ni mwingine,” alieleza.

Shahidi huyo alieleza kuwa mjomba huyo akiwa ofini kwake alipiga simu Nachingwea kwa baba wa kufikia wa Mussa akamtaka atafute picha zake azitume kwenye gari.

"Kesho yake Januari 22, 2022 zililetwa picha nikazitazama nikamkabidhi ASP Esau ili waendelee na utaratibu wa upelelezi,” alieleza ACP Mgonja.

Alidai kulikuwa na mauaji Januari 21,2022 niliagiza apatikane Grayson ambaye alikuwa mahabusu Tandahimba, kwanza kati ya watu wote waliotajwa yeye alikuwa ametajwa maeneo mengi.

Alieleza kuwa baada ya Grayson kuletwa aliongeza timu ya wapelelezi akiwajumuisha askari watano wa timu ya Task Force waliokuwa wanashughulikia magaidi wakingozwa na SP Simba, hivyo ikawa timu ya wapelelezi 10 akiwemo yeye mwenyewe.

"Tulifikiri kwa pamoja tukakubaliana tumlete Dk Msuya ili asimulie mbele ya Grayson nini kiliendelea pale Mitengo kama alivyonisimulia mimi.”

"Kwa kuwa Msuya alishuhudia kila kitu kilichofanyika pale Mitengo na Grayson akiwepo, kwa hiyo sisi kama makachero tuliona Grayson akisikia, basi mahojiano yetu naye yatakuwa rahisi."

Shahidi huyo alihitimisha Kwa kueleza kuwa katika mahojiano ya mdomo waliyoyafanya na Dk Msuya mbele ya Grayson, alisimulia kama alivyokuwa amemsimulia yeye na walipomuuliza Grayson, alikubali kuwa alivyosimulia Dk Msuya ndivyo walivyofanya.

“Hivyo mimi kama RCO picha iliyoniijia kichwani ni kwamba, haya sasa ni mauaji na kama ni mauaji hakuna mauaji ambayo hayana mwili au mtu aliyeuawa, hivyo nikamtaka Grayson atuonyeshe huyo ambaye wamemuua yuko wapi."

Hata hivyo wakati shahidi huyo anataka kueleza kile Grayson alichosema, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu aliweka pingamizi akisema kwa kuwa Grayson si mshtakiwa wala shahidi, hawezi kutoa maelezo yake kwa sababu hawatapata fursa ya kumhoji kuhusu ukweli wake.

Pingamizi hilo liliibua mvutano wa hoja na upande wa mashtaka na Jaji Kakolaki baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo Kwa ajili ya kuandika uamuzi wake.

SEHEMU YA PILI

KESI YA POLISI WANAODAIWA KUMUUA MUUZA MADINI: RPC alivyochambua uhusika wa washtakiwa​


Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa Saba wa Polisi mkoani Mtwara; Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino Mgonja amehitimisha ushahidi wake huku akichambua jinsi baadhi ya washtakiwa wanavyohusika katika tuhuma hizo.

ACP Mgonja ametoa uchambuzi huo wakati akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi na maswali ya ufafanuzi kutoka kwa mwendesha mashtaka, kuhusiana na maswali hayo ya dodoso, akihitimisha ushahidi wake juzi jioni baada ya kusimama kizimbani kwa siku tatu.

Wakati wa tukio la mauaji hayo ACP Mgonja alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara na kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Ilala jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi (Insp) John Yesse Msuya, aliyekuwa Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa maksudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Maswali ya dodoso na maswali ya ufafanuzi na jinsi shahidi huyo alivyoyajibu na kufafanua uhusika wa washtakiwa hao yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili Majura Magafu anayewakilisha mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje

Wakili: Wakati Kiula (OCS) anamkabidhi SP Kalanje funguo alimsainisha?

Shahidi: Hakumsainisha.

Wakili: Huyo Paul (Kiula) OCS alikwambia kuna mahali aliweka kumbukumbu kwamba hawa maafisa walifika hapo kituoni?

Shahidi: Hilo hakuniambia.

Wakili: Sasa Gilbert (SP Kalanje) anasema siku hiyo ya tarehe 5 hakufika katika kituo hicho, mbali na ushahidi wako wa maneno una ushahidi wa document (nyaraka) kuthibitisha hayo kwamba walikwenda hapo?

Shahidi: Ushahidi wa document (nyaraka) sina lakini aliyesema yupo na atakuja kueleza.

Wakili: Ulisema baada ya wewe pia kwenda na timu yako mkaona mbavu tano mliziacha palepale kwa nini hamkuzichukua?

Shahidi: Hatukuzichukua kwa sababu tulitaka zije zichukukuliwe na wataalamu maana sisi si wataalamu.

Wakili: Kwani ninyi mngezichukua zingebadilika?

Wakili: Na kwa sababu ya kosa mlilolifanya ndio maana kesho yake mkakuta zimeongezeka na kuwa nane na hamjui nyingine zilitoka wapi.

Shahidi: Hatukufanya kosa maana tuliowaacha askari wa ulinzi.

Wakili: Kuna kanuni ya kikachero kwamba trust nobody (usimwamini mtu yeyote).

Shahidi: Mimi niliwaamini.

Wakili: Sasa mimi nakwambia hamkupata mbavu pale.

Shahidi: Wewe unasema.

Wakili: Hivyo vitu mlivyovipata eneo la tukio (mifupa eneo ulikodaiwa kutupwa mwili wa Mussa) mliviingiza kwenye (kitabu cha kumbukumbu za vielelezo) regista?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Hiyo regista umeileta hapa mahakamani?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Sasa regista hujaleta, unataka mahakama ikuamini kwa mdomo tu kuwa mlipata masalia ya mbavu pale?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ulipokea ripoti ngapi (za uchunguzi wa vielelezo vile, masalia) kutoka kwa Mkemia?

Shahidi: Moja tu.

Wakili: Siyo mbili?

Shahidi: Mbili za kwako.

Wakili: Moja tu, sasa akija hapa mwingine akasema mbili sisi tutashangaa. Unajua kwa nini nakuuliza hivyo? Ni kutokana na yaliyomo kwenye haya makabrasha.

Shahidi: Sikiliza ushahidi wangu, usinilishe matangopori mzee.

Majibu ya ufafanuzi

Wakili wa Serikali: Wakili wa mshtakiwa wa kwanza, Majura Magafu, alikuuliza kama kabla ya kumpeleka Grayson kwenye jopo uliwahi kumhoji kuhusu hizi tuhuma, ukajibu kuwa ni kweli mara ya mwanzo alikataa ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kuwa mwanzoni tulipomhoji alikana akijua kuwa ukweli hautajulikana, lakini baada ya kumuunganisha na Dk Msuya alikiri akatupeleka eneo la tukio na akaandika maelezo ya nyongeza.

Maswali ya wakili Fredrick Odada anayemtetea mshtakiwa wa Pili, ASP Onyango

Wakili: Shahidi, ni kweli au si kweli kwamba licha ya kumtaja mshtakiwa wa pili mara nyingi lakini katika ushahidi wako kwa mujibu wa taarifa uliyopewa na Dk Msuya hakuna sehemu yoyote inayomuonesha kuhusu kifo cha Mussa Hamis Hamis?

Shahidi: Siyo kweli, amehusika maeneo mengi.

Alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Marungu kufafanua jibu la swali hilo ACP Mgonja alieleza:

Shahidi: Nilisema amehusika maeneo mengi nikiwa na maana kwanza alijua harakati zote na akabariki mtuhumiwa yule awekwe mahabusu kwa RB ambayo si ya kweli.

Aliruhusu askari kutoka nje ya mkoa huku akijua hana mamlaka hayo maana hakuwa na kibali cha RPC, huku akijua kosa lililoko katika movement order hiyo kuwatoa nje ya mkoa ni tofauti na kwenye RB.

RB iliandikwa kuvunja nyumba na kuiba yeye akaandika wizi wa pikipiki kuliwafanya watu wa Nachingwea (maafisa wa Polisi) waamini kuwa safari ile ni halali.

Alishiriki kumtoa Mussa Hamis kwa Dk Msuya mpaka Mitengo,

Alitajwa pia na Koplo Jagali kuonekana usiku wa Januari 5, 2022 (siku ya mauaji) wakati walipokwenda kumchukua huyo waliyesema alikuwa mgonjwa wao. Kwa hiyo kusema kuwa ushiriki wake haupo si sahihi.

Maswali ya wakili Emmanuel Msengezi anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Kisinza

Wakili: Kuna tukio gani ambalo watu wa Intelijensia na ofisi yako walikuwa wanafuatilia Newala kati ya Januari 2 mpaka 5, 2022?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Nilitaka nikukimbushe tukio la ajali lililokuwa limetokea Kijiji cha Migumbe Wilaya ya Newala na dereva akakimbia.

Shahidi: Nimesema sikumbuki.

Wakili: Hukumbuki au umechagua kutokukumbuka?

Wakili: Eneo la Newala liko Mtwara?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Kwa hiyo hukumbuki ajali iliyotokea eneo lako ikaua watu 14?

Shahidi: Sikumbuki mbona unaniuliza vitu ambavyo sijavisema na sivikumbuki?

Wakili: Hata hukumbuki ofisa aliyekuwa analishughulikia?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Kwa hiyo nikikwambia tarehe hiyo Nico alikuwa busy kumtafuta dereva wa lori hilo lililosababisha ajali na akakimbia utakuwa hukumbuki?

Shahidi: Wewe wasema, mimi sikumbuki.

Wakili: Katika maelezo yako au ya ofisa yeyote uliyemteua kupeleleza shauri hili hakuna mahali ambako unamtaja Nico kuwepo kituo cha Polisi Mitengo au Mtwara siku ya Januari 5, 2022 kuhusiana na tukio la mauaji ya Mussa, ni kweli?

Shahidi: Yumo alikuwa na information (taarifa) na katika tukio la kukamatwa na kupekuliwa na kuchukuliwa kwa Sh2.3 milioni za Mussa Hamis Oktoba 20, 2021,

Alikuwa anajua mahojiano na uwekwaji mahabusu kwa Mussa kwa MTR /RB/ 1330/2021 ya uwongo ya kuvunja nyumba usiku na kuiba.

Alikuwa anajua movement (mizunguko) ya vijana wake kutoka Mtwara kwenda Nachingwea bila vibali. Alikuwa anajua kilichopatikana kule yaani kilichochukuliwa kule maana vijana hao walimwambia.

Mheshimiwa Jaji kwa kujua huko matukio yote hayo anajua pia tukio lililoendelea pale Mitengo (mauaji).

Wakili: Nje na maneno yako kuna ushahidi wowote uliouleta hapa mahakamani kwa kuonesha Nico alikuwa anajua ya kilichojiri Januari 5, 2022?

Shahidi: Hakuna ushahidi.

Majibu ya maswali ya ufafanuzi

Wakili wa Serikali: Uliulizwa na Wakili wa mshtakiwa wa tatu kuhusu upekuzi uliofanyika Sadina Hotel ukasema hukuwa na shida nao na shida kwako ilikuwa ni common intention, ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kwamba kitendo cha kufika kituoni na kumuweka yule kijana (Mussa) mahabusu kwa kosa lingine hakukuwa halali maana walikuwa wanamtuhumu wizi wa pikipiki na ndilo walikuwa wanatembea nalo mpaka mwisho.

Wakili: Pia Ulipoulizwa na Wakili huyo kuhusu taratibu za kukabidhiana mali zilizokamatwa Ruponda hazikufanyika ukajibu kuwa hazikufanyika maana hao walikuwa na yao, ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kuwa askari hao Marco Mbuta ni askari wa siku nyingi anajua taratibu za kukabidhi vielelezo kwa yeye na wenzake kutokufuata taratibu na kukubali kwenda kwenye kikao na OC-CID, na kukubali kuviacha mezani kama alivyosema OC- CID, hawakuwa na lengo zuri.

Maswali ya Wakili Alex Msalenge, anayemtetea mshtakiwa wa nne, Marco Mbuta Chikingizo

Wakili: Shahidi haina ubishi baada ya malalamiko ya Mussa kutoka NPS (Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuchukuliwa pesa na vitu vyake na Polisi, washtakiwa) na baadaye malalamiko ya shahidi wa kwanza wa mashtaka, (mama wa marehemu, Hawa Bakari) bila shaka akili yako kiupelelezi ilitakakujua nani aliyeenda (kumpekua marehemu) Nachingwea?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Na haina ubishi taarifa ya nani aliyeenda Nachingwea uliipata kwa (askari wa Nachingwea) Inspector Singano?

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Na majina hayo ni Marco (Chikingizo), Shirazi na Koplo Salim?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Na haina ubishi uliwaita wote waweze kuhojiwa Januari 8, 2022?

Shahidi: Sahihi

Wakili: Hawakupinga kuwa walikwenda Nachingwea kufanya upekuzi na wakarudi na mali?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Haina ubishi Marco alikuonesha kuwa walikwenda kwa movement order (kibaki askari kutoka nje ya mkoa wake) iliyosainiwa na OCS wa kituo cha Mtwara (mshtakiwa wa pili) ASP Onyango?

Shahidi: Ndio, ambaye hana mamlaka hayo.

Wakili: Na haina ubishi walikwambai kuwa vile vitu walivikabidhi kwa viongozi wao SP Kalanje, ASP Onyango na Kisinza?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Na kimsingi ushahidi wako hao wakubwa watatu waliodaiwa kukabidhiwa hivyo vitu baada ya wewe kuwahoji walikana kukabidhiwa?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ni sahihi katika ushahidi wako mshtakiwa wa nne alikuongezea kitu kwamba Mussa Hamis (alipofika kituo cha Mitengo alipoitwa kufuata vitu vyake) alipokewa na Grayson Januari 5, 2022 kwa ushahidi wa audio aliyorekodi kwa simu yake?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ni sahihi ulisema Marco baada ya kupata taarifa kwa Singano kwamba kule Nachingwea kuna malalamiko Marco aliongea na bosi wake SP Kalanje lakini majibu aliyoyapata yakampa wasiwasi?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Sasa labda kwa kuwa uliongea naye kwa nini alianza kupata wasiwasi mpaka akaanza kurekodi (majadiliano hayo)?

Shahidi: Alisema alianza kupata wasiwasi sababu aliambiwa vile vitu walivyokamata kule Nachingwea aviache pale mezani.

Pili, alimwambia kuwa kule Singano anasema Mussa Hamis anadai vitu vyake lakini yeye Kalanje akamwambia alikupigia simu mwambie aje kwangu ili nimkamate nimpeleke mahakamani.

Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi wasiwasi alioupata Marco hawakuwa pamoja na bosi wake?

Shahidi: Mh! walikuwa pamoja kwenye upotevu wa mali.

Wakili: Kwa ushahidi ulioutoa hapa kifo cha Mussa kitokea Januari 5, 2023 ndani ya Wilaya ya Mtwara ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Haibishaniwi tarehe hiyo Marco alikuwa katika kituo chake kipya alikohamishiwa Tandahimba?

Shahidi: Sikumbuki.

Majibu ya ufafanuzi wa baadhi ya maswali ya dodoso.

Wakili wa Serikali: Shahidi, uliulizwa na Wakili wa mshtakiwa wa nne, Alex Msalenge kuhusu movement order (kibali cha asakari kutoka nje ya mkoa kikazi) iliyosainiwa na mshtakiwa wa nne (ASP Onyango) kwenda Kijiji cha Ruponda (Newala kumpekua Mussa kwake) ukajibu kuwa ndiyo ambaye hana mamlaka, ulimaanisha nini?

Shahidi: Kwamba movement order ile ilitolewa kwenda nje ya mkoa bila idhini ya Kamanda wa Mkoa ambaye kwa mujibu wa PGO namba 2 ndiye mwenye mamlaka ya kuitoa na bila kibali cha RPC maana yake OCS Onyango anakuwa hana mamlaka ya kuruhuau askari kwenda nje ya mkoa.

Wakili: Pia alikuuliza kwa ushahidi ulioutoa ni mauaji tu na si wa upotevu wa mali (vitu vilivyochukukiwa Ruponda) ukajibu kuwa si kweli, ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilikuwa namaanisha kwamba mauaji ya Mussa Hamis yametokea baada ya kudhulumiwa mali zake. Ili asiendelee kufuatilia mali zake ndio ikabidi auawe, hivyo kusema kwamba ushahidi wangu mimi ni wa mauaji tu hapana.

Wakili: Pia wakili alikuuliza kuwa wakati unahamishiwa hapa Mtwara Desemba hukuwahi kuonana na Marco (mshtakiwa wa nne) wala kufanya naye kazi kwa kuwa alikuwa amehamishiwa Tandahimba ukajibu kuwa ni kweli hukuwahi kuonana naye lakini ukasema kuwa Mtwara si ni hapo tu? Ulimaanisha nini?

Shahidi: Nilimaanisha kwamba Marco kufanya kazi Tandahimba hakuwezi kumzuia kuja Mtwara na kufanya ubovu.

Maswali ya Wakili Robert Dadaya wa mshtakiwa wa tano, Dk. Msuya

Wakili: katika uchunguzi wako Msuya hajawahi kufika kijiji cha Majengo Kata ya Hiari (mahali mwili wa marehemu ulikotupwa) aidha mchana au usiku, ni kweli?

Shahidi: Ni kweli

Wakili: Afande Mgonja nilikusikia ukiongea sana common intention (Nia ya pamoja), sasa tuweke mambo sawa, wakati SP Kalanje na wenzake wanamfuata (Dk Msuya) pale (kazini kwake) hakuwa anajua kwamba kuna mpango wa kummaliza mtu, ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba usiku wa Januari 5, 2022 Dk Msuya hakuwahi kwenda tena katika kituo cha Mitengo?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ulisema wataalamu walichukua funza kwa ajili ya uchunguzi wa sampuli ya sumu ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Ripoti ya uchunguzi sumu (kwenye wale funza) uliipata?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ni kweli kwamba ripoti ile inasema kwamba hapakuwa na sumu kwenye ile sampuli ya funza?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Ni kweli Dk Msuya hakuwa miongoni mwa askari waliomkamata na kuwapekua watuhumiwa katika Hoteli ya Sadina wala kwenye timu ya makachero waliokwenda (nyumbani kwa Mussa) Nachingwea?

Shahidi: Ni kweli, hakwenda.

Baada ya maswali hayo ya kusawazisha upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake kwa shahidi huyo.

Simulizi ya kusisimua

Awali katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu, ACP Mgonja alitoa simulizi ya kusisimua akielezea jinsi mfanyabiashara huyo alivyouawa, akibainisha matukio ya kabla, wakati na baada ya mauaji hayo.

Alibainisha kuwa alipata taarifa na maelezo hayo kwa asakari wa kituo cha Mitengo waliokuwa zamu, na watuhumiwa waliowahoji katika upelelezi wake na timu yake, akiwemo mshtakiwa wa tano, Dk Msuya na Mkaguzi msaidizi Grayson Gatian Mahembe, aliyejinyonga akiwa mahabusu.

Kutokana na maelezo hayo, ACP Mgonja alidai kuwa siku ya tukio, Januari 5, 2022, mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje alimuomba Dk Msuya awasaidie kumuua Mussa kwa kumdunga sindano ya sumu kama alikuwa nayo.

ACP Mgonja alidai kuwa SP Kalanje alimweleza Dk Msuya kuwa huyo ni mtuhumiwa wao wizi wa pikipiki, mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Nachingwea Lindi, kwa kuwa alikuwa akiwasumbua na alikuwa amekataa kutoa maelezo.

Hata hivyo, Dk Msuya alimshauri badala ya sindano ya sumu ambavyo hajawahi kumdunga mtu tangu alipoajiriwa na kuapa kuwa daktari, ni vema wamdunge sindano ya dawa ya usingizi aliyokuwa nayo kidogo ili akizinduka ataje matukio yote ya wizi aliyokuwa akiyafanya.

Alidai kuwa walikubaliana na ushauri wake na Dk Msuya akamdunga Mussa sindano ya dawa ya usingizi aina ya Ketamine CC (sentimita za ujazo) moja, lakini SP Kalanje alisema kuwa huyo alikuwa anawachelewesha, hivyo akachukua tambala akamziba mdomo na pua.

Hata hivyo, alidai kuwa baadaye kidogo SP Kalanje alimuita Dk Msuya ambaye alikuwa ametoka nje ya chumba walimokuwa akamuuliza kama alikuwa tayari (ameshafariki?) na Dk Msuya akajibu kuwa tayari, wakatoka nje na kufunga mlango wakaondoka, SP Kalanje akiwa na funguo za chumba walimomuacha waliyemuita mtuhumiwa wao (Mussa).

Katika sehemu iliyopita ya ushahidi wake, ACP Mgonja alieza jinsi ambavyo mmoja wa watuhumiwa alivyowapeleka mahali ambako alidai kuwa ndiko walikotupa mwili wa marehemu Mussa.

Alieleza kuwa mahali hapo wakiwa na timu ya wataalamu wa uchunguzi walipata mifupa ya mbavu nane na mifupa miwili ya mguu na suruali kisha akamuita mama wa marehemu, kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli kwenda kizifanyia uchunguzi pamoja na mifupa hiyo.

ACP Mgonja aliieleza kuwa Januari 24, mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari alifika ofisini kwake.

Alimueleza kuwa kuna mifupa waliyoipata ambayo wanahisi kuwa ni ya mwanaye Mussa wanayemtafuta na akamuomba achukuliwe sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba ili kupata uthibitisho kama ndiye mtoto wake, naye akaridhia kuwa yuko tayari ili ajue ukweli kama mwanaye yuko hai bado au la.

Hivyo ACP Mgonja aliandika barua kwa Ofisi ya Mkemia Mtwara kuomba uchunguzi ufanyike na ulinganifu wa mabaki ya mifupa ya binadamu waliyoyapata eneo la tukio, kisha vielelezo hivyo (mifupa na funza na sampuli ya mate ya mama huyo) vikapelekwa kwa Mkemia kufanyiwa uchunguzi

Februari Mosi 2022, walipata matokeo ya uchunguzi huo ambayo yalieleza kuwa ile mifupa na vinasaba vilivyotolewa kwa mama vimeoana. Hata hivyo vielelezo hivyo vilibaki ofisi ya Mkemia.

ACP Mgonja alimuita mjomba wa marehemu Mussa; Salum Ng'ombo akamjulisha matokeo ya uchunguzi huo kwamba kwa hiyo sasa wanaamini Mussa ameuawa na akamuomba amjulishe mama wa marehemu.

Baada ya hapo walikamilisha upelelezi na Januari 25, 2022 watuhumiwa walifikishwa mahakamani (na kusomewa shtaka linalowakabili).

SEHEMU YA TATU

KESI YA POLISI WANAODAIWA KUMUUA MUUZA MADINI: Shahidi adai mtuhumiwa alitoa sharti kuonyeshwa mwili ulikotupwa

Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa polisi mkoani Mtwara, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kuwa mmoja wa watuhumiwa alivyokwenda kuonyesha walikoutupa mwili alitoa sharti moja.

Shahidi huyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Yustino Mgonja amebainisha sharti alilolitoa mtuhumiwa huyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Grayson Mahembe kuwa alichagua timu ya wapelelezi ambao alieleza yuko tayari kwenda kuwaonyesha huku akimkataa yeye na timu yake.

Pia, Mgonja ameeleza timu ya wapelelezi hao aliowakubali walipofika mahali hapo ilikuta mbavu nne tu, lakini baadaye yeye alipokwenda na timu yake na wataalamu baada ya kukagua zaidi walipata mbavu nane na mifupa miwili ya mguu wa kulia.

Mgonja wakati wa mauaji hayo shahidi huyo alikuwa Mkuu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara (RCO), kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, jijini Dar es Salaam.

Ametoa maelezo hayo leo Novemba 17, 2023 katika mwendelezo wa ushahidi wake wenye simulizi ya jinsi mfanyabiashara huyo alivyouawa, akibainisha matukio ya kabla, wakati na baada ya mauaji hayo, kwa maelezo aliyoyapata kwa mashuhuda na watuhumiwa katika upelelezi na timu yake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya namba 15/ 2023 ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Nicholaus Stanslaus Kisinza, A/Insp Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi (Insp) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, A/Insp Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wa polisi wanakabiliwa na shtaka la mauaji wakidaiwa kumuua Mussa kwa kumchoma sindano ya usingizi na kisha kumziba mdomo na pua kwa tambala katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Kesi ya maofisa hao saba wa polisi mkoani Mtwara inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika mwendelezo wa ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu, shahidi huyo alidai kuwa Mussa aliuawa na SP Kalanje kwa kumziba kwa tambala mdomoni na puani.

Kwa mujibu wa ACP Mgonja, SP Kalanje alichukua hatua hiyo muda mfupi baada ya Dk. Msuya (mshtakiwa wa tano) kumdunga sindano ya usingizi mfanyabiashara huyo.

Sindano hiyo alidai aliipendekeza Dk Msuya ambayo alidai ingemfanya aeleze matukio yote ya uhalifu aliyokuwa ameshayafanya baada ya kuzinduka, badala ya kumdunga sindano ya sumu aliyokuwa ameipendekeza SP Kalanje kwa madai wanataka wampoteze kabisa.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa alipata taarifa za tukio hilo baada ya kuwahoji baadhi ya askari waliokuwa zamu katika kituo cha Polisi Mitengo, Dk Msuya mwenyewe na A/Insp Grayson (marehemu) ambao walisimulia tukio hilo.

Wakati wa tukio hilo, ACP Mgonja alikuwa RCO Mkoa wa Mtwara na kiongozi wa timu ya wapelelezi watano wa polis na timu ya askari wa kikosi maalumu ya kukabiliana na ugaidi kilichoongozwa na SP Simba aliyoiomba iungane nao kuanzia wakati wa kumhoji mtuhumiwa Grayson.

Kwa mujibu wa ACP Mgonja walikubaliana kuwa kabla ya kumhoji Grayson, walimleta Dk Msuya asimulie mbele yake Grayson nini kiliendelea pale Mitengo kama alivyokuwa amemsimulia yeye.

Dk Msuya alisimulia hivyo na walipomuuliza Grayson akakubali kuwa alivyosimulia Dk Msuya ndivyo walivyofanya.

Hivyo, alimtaka Grayson awaoneshe huyo waliomuua yuko wapi, ndipo akatoa sharti kwamba yuko tayari kuwaonyesha wale askari wa kikosi kazi chini ya SP Simba na si wapelelezi wa timu ya awali aliyoiongoza yeye ACP Mgonja, sharti ambalo walikubaliana nalo.

Hata hivyo, ACP Mgonja alimwelekeza SP Simba kwamba endapo wataonyesha na kuthibitisha, basi awajulishe nao waende kushuhudia na kuthibitisha na wakaondoka kwenda eneo la tukio siku hiyohiyo Januari 21, 2022 yapata muda wa saa tano usiku.

Akiwa katika kituo cha Polisi Mtwara na timu yake baada ya dakika kama 50, ACP Mgonja alipokea simu kutoka kwa SP Simba akimjulisha kuwa wamefika eneo la tukio ni jirani na kiwanda cha Sementi cha Dangote kuna mtu mkubwa mahali panaitwa Majengo Kata ya Hiari.

ACP Mgonja alitaka kujua wameona nini na SP Simba akajibu kuwa kwanza wamekutana harufu kali sana kama ya uozo na kwamba baada ya kumulika na tochi eneo hilo waliona mabaki kama ya mbavu nne.

Hivyo, ACP Mgonja na timu yake nao walikwenda eneo la tukio kwa mwongozo wa SP Simba, ambako pia alisikia harufu ya uozo lakini baada ya kuhesabu zile mbavu alipata tano.

Alielekeza eneo lile tuzungushie utepe na pia akaelekeza askari wawili wenye bunduki Ditektivu Koplo (DC) Denis na Ditektivu Sajenti (DS) Diamond wakilinda mpaka asubuhi watakapokwenda na wataalamu kuchunguza mabaki hayo.

Pia alielekeza Insp Abubakar aandike maelezo ya nyongeza ya Grayson kwenye maelezo yake ya awali katika jalada la uchunguzi.

Pia ACP Mgonja alimuelekeza DC Denis kwamba baada ya Grayson kumaliza kuandika maelezo yake amuweke mahabusu naye akafanya hivyo pale Mitengo chumba cha pekee yake na akawajulisha tena RPC na DCI

Januari 22, 2022, ACP Mgonja aliamka na jukumu la kutafuta timu ya wataalamu kwa ajili ya kwenda eneo la tukio walikoona zile mbavu na kufanya uchunguzi kuzibaini kama ni za binadamu na kuthibitisha walichokuwa wanakitafuta yaani mwili wa Mussa.

Hivyo alimtafuta daktari wa Hospitali ya Mkoa, Mkemia, kutoka ofisi ya Mkemia Mkoa wa Mtwara, mwakilishi wa Ofisi ya Mwendesha mashtaka Mkoa wa Mtwara, Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo na Mtendaji wa kata ya Hiari.

Pia aliandaa askari wa kitengo cha wanne wa kikosi cha uchunguzi wa sayansi jinai wakiongozwa na Inspekta Apobokile.

Taarifa za kujinyonga Grayson

Wakati akiendelea kukusanya timu ya wataalamu hao, muda wa saa nne asubuhi alipokea simu ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mtwara (OCD), Mrakibu wa Polisi Mwandamizi (SSP) Nguvila akimjulisha kuwa kwenye kituo cha Mitengo A/Insp. Grayson amejinyonga akiwa mahabusu.

Yeye, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara (RPC) na timu yake ya wapelelezi na ya Forensic na walipofika kituoni Mitengo walishuhudia kweli Grayson amejinyonga akiwa amening'inia kwenye kamba aliyokuwa ameifunga kwenye dirisha.

RPC alielekeza lifunguliwe jalada la kifo cha mashaka cha Grayson na likafunguliwa, kisha akamuelekeza naendelee kukusanya timu ya wataalamu kwenda eneo tukio walikoonyshwa kuwa ndiko ulikotupwa mwili wa Mussa.

Baada ya kuwapata wataalamu wote walielekea eneo la tukio hilo ambako walifika saa 5:30 wakawakuta mwenyekiti wa Koji cha Majengo na Mtendaji wa kata ya Hiari wakiwa wameshafika pamoja na askari waliowaacha kulilinda eneo hilo ambalo pia lilikuwa kama walivyoliacha.

Baada ya kuwapatia maelezo ya kile walichokuwa wamekiona usiku, wataamu hao daktari, Mkemia na watu wa kitengo cha uchunguzi wa sayansi jinai waliingia kwenye lile eneo wakusanye vitu walivyokuwa wanavipata.

Wao waliona mbavu nyingine tatu pamoja na zile tano za awali zikawa tano. Pia sehamu nyingine waliona mifupa miwili ya miguu na sehemu nyingine pia kulikuwa na kama uozo na kulikuwa na funza wakaweka alama na kupiga picha.

Daktari alieleza kwa ufupi palepale kwamba kwa utaalamu wake zile mbavu ni mbavu za binadamu.

Baada ya kupiga picha na kuchora ramani, mkemia na Apobokile walikusanya vile vielelezo. Pale walichukua mbavu nane na mifupa miwili ambayo daktaria alisema ni ya mguu wa kulia, suruali na funza.

ACP na timu yake walifanya kazi yao ya kikachero kwa maana ya kuandika maelezo ya mashuhuda na wote waliokuwepo pale.

Mabaki hayo yalichukukiwa na Mkemia na Apobokile wakavipeleka ofisini kwa ACP Mgonja, ili aandike barua kuvikabidhi kwa mkemia kwa mujibu wa utaratibu, baada ya kuviwekea lakiri.

"Kwa unyeti wake kwamba ni viungo vya binadamu ambavyo vikitoa majibu vitaunganisha kesi yetu, niliona bora vikae ofisini kwangu, hivyo nilikuwa navitunza mimi kwenye kasiki", alieleza ACP Mgonja na kuongeza:

"Vitu hivyo vilikaa ofisini kwangu toka Jumamosi ya Januari 22 mpaka Jumanne Januari 24, 2022. Siku hiyohiyo (Januari 22) mwili wa Grayson ulisafirishwa kwenda kwao (Tabata- Segerea, Dar es Salaam kwa mazishi)

Januari 23 ACP Mgonja alimpigia mjomba wa marehemu, Salum Ng'ombo amtafute mama wa marehemu, Hawa Bakari ili aende azungumze naye akikubali aende kuchukuliwa sampuli (mpanguso wa mate) akafanyiwe vipimo vya vinasaba (DNA).

Pia aliwajulisha RPC na DCI kuwa kwa ushahidi ambao wameukusanya, unawahusisha askari wao, hivyo akaomba kibali cha kuwakamata na kuwahusisha mauaji hayo.

Januari 24 idhini ikatoka kufungua jalada la mauaji ambapo walifungua jalada la mauaji kumbukumbu namba MTR/IR/154/2022 na akaelekezwa watuhumiwa wote wahojjwe kuhusiana na mauaji ya mfanyabiashara huyo.

SEHEMU YA NNE
Inspekta asimulia walivyofukua fedha ardhini nyumbani kwa marehemu

Shahidi wa nne katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa Polisi mkoani Mtwara, ameieleza mahakama namna baadhi ya washtakiwa walivyofika kituo Cha Polisi Nachingwea na kisha kijijini kwao marehemu Musa na yaliyojiri huko.

Shahidi huyo, askari kutoka Kituo cha Polisi Nachingwea, PF20449, Mkaguzi (Inspekta) wa Polisi, Jacob Bernard Singano, ameeleza yaliyojiri kabla, wakati na baada ya kufika na kufanya ukaguzi nyumbani kwao Mussa. Ametoa ushahidi huo akiwa anaongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu.

Pamoja na mambo mengine, ameieleza mahakama jinsi alivyoambatana na baadhi ya washtakiwa hao kwenda kufanya ukaguzi nyumbani kwa kina Mussa katika Kijiji chaa Ruponda wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi, ambako walipata pesa za Kitanzania na za kigeni (Dola za Marekani) zilizokuwa zimefukiwa ardhini.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi.

Kulingana na wa ushahidi huó, walifika uamuzi huo ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizokuwa wamezichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwao, wakimtuhumu kuziiba na pia wizi wa pikipiki.

Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.



Simulizi ya kamili ya shahidi

Kwa mujibu wa maelezo yake, Oktoba 21, 2021 mchana akiwa kazini kwake kituo cha Polisi Nachingwea, alifika A/Insp Mbuta akiongozana na A/Insp Shirazi (mshtakiwa wa sita) na Koplo Salim (mshtakiwa wa saba) kutoka Mtwara.

Mbuta alieleza kuwa ndani ya gari yao waliambatana na mtuhumiwa aitwaye Mussa Hamis.

Alimweleza Singano kuwa wamefika hapo kwanza kuripoti na pia kupata msaada wa kwenda kwa mtuhumiwa kuwaonesha fedha alizokuwa ameziiba Dar es Salaam.

Mbuta aliionesha movement order (hati ya kibali cha kutoka nje ya mkoa kikazi) iliyokuwa na tuhuma za wizi wa pikipiki Mtwara, kumbukumbu ya uhalifu MTR/IR/1330/2021.

Singano alimuuliza Mbuta namna walivyoweza kumkamata mtuhumiwa, naye akajibu kuwa walikuwa wawili lakini wakati ukamataji mwingine aitwaye Said alikimbia.

Singano alimpeleka Mbuta kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), SP Kavalambi, Mbuta akamueleza OCD huyo kuwa katika mahojiano naye mtuhumiwa inaonesha sehemu ya fedha hizo alizoziiba ziko kwao Ruponda.

Pia Mbuta alimueleza OCD kuwa mtuhumiwa alikuwa tayari ameshazitumia kwa kununua vitu mbalimbali na kwamba wakati wa ukamataji, mwenzake Said alikimbia na hivyo wana wasiwasi kuwa Said anaweza kwenda kuzihamisha hizo fedha.

OCD Kavalambi baada ya kuangalia ile hati alimweleza Mbuta kuwa wana changamoto ya usafiri kwani magari yao yote mawili yalikuwa nje ya kituo yakifanya kazi nyingine.

Mbuta alisema kuwa wataitumia gari yao walivyokuwa nayo, na akamuuliza Singano umbali wa kufika Ruponda, Singano akamjibu kuwa ni kilometa 15 - 20 na Mbuta akasema kuwa gari yake inaweza kumudu.

OCD Kavalambi alimuamuru Singano aambatane nao ili kusimamia upekuzi huo na Singano akaomba askari wengine wawili wa kuambatana nao kwa usalama zaidi na OCD akakubaliana naye. Akawachukua Koplo Mussa na PC Daniel ambao walichukua silaha.

Kisha Singano alikwenda kuangalia gari waliokuwa nalo kina Mbuta aina ya Vitz rangi nyeusi alipochungulia ndani akawaona wale askari wawili wenzake na Mbuta, Shirazy na Salim na mtu mwingine, hivyo akaona ilikuwa imejaa.

Hivyo alimuuliza Mbuta kama kuna ulazima wa watu wote hao kwenda huko na Mbuta akajibu kuwa ulazima upo na wakakubalina wengine wapande pikipiki.

Kisha Singano aliwaambia askari wake Koplo Mussa na PC Daniel waingie kwenye ile gari na wale askari wawili waliotoka Mtwara (Shirazi na Salim wachukue pikipiki, nao wakafanya hivyo wakaondoka.

Singano aliwatafuta kwenye simu viongozi wa Ruponda wa kata na kijiji akampata Mtendaji wa kata aitwaye Editha Ibrahim akamtaka asiondoke ili ashirikiano nao na kushuhudia kazi ya upekuzi.

Walipofika nyumbani kwao Mussa, kijijini Ruponda, Kitongoji cha Magomeni, Mbuta alimtaarifu baba yake Mussa, Bakari Said M Mnali kuwa kijana wake wamemkamata Mtwara ana tuhuma za wizi wa pesa.

Pia Mbuta alimweleza baba yake Mussa kuwa hivyo wamefika naye hapo ili awaonesha sehemu ya pesa hizo na baadhi ya vitu alivyokwishanunua na kwamba pia ana tuhuma za wizi wa pikipiki.

Baba yake Mussa alijibu kuwa hao ni vijana wana mambo mengi, na yeye hawezi kujua lakini kwa kuwa wanaye basi angewaonyesha.

Waliingia ndani Mussa akawaongoza hadi chumba cha tatu na cha mwisho mkono wa kushoto, ambako aliwaonesha baadhi ya vitu hivyo alivyokuwa ameshavinunua yaani solar panel, inventor pamoja na betri.

Pia Mussa akaelekeza wachimbe chini na Koplo Salim akachimba lakini hakuona kitu na hata Mussa mwenyewe alipochimba hakuona kitu, akasema hizo pesa aliziweka hapo.

Alimuuliza baba yake kuwa nani kazichukua lakini baba yake akajibu kwamba jana yake aliipigwa simu na Saidi akamuelekeza mahali hapo azichukue kwa sababu mlikuwa mmekamatwa huko na Polisi na Polisi wanakwenda.

Hivyo baba yake Mussa alieleza kuwa alizitoa na kwenda kuzificha, huku akiwataka waende awaoneshe alikokuwa amezificha.

Wote walitoka nje na baba yake Mussa aliwaonesha na Singano akamtaka afukue mwenyewe naye akafanya hivyo hadi akafika mfuniko wa rangi ya bluu uliokuwa umefunika kopo jeupe la kuhifadhiwa dawa aina ya panadol.

Singano alilitoa kopo hilo akalifungua na ndani kulikuwa na pesa za Kitanzania noti za 26 za Sh5,000 zenye thamani ya Sh130,000.

Pia kulikuwa na Dola za Marekani, noti 119 za Dola 100 thamani yake ikiwa Dola 11,900; noti 32 za Dola 50 yaani jumla Dola 1,600.

Vilevile kulikuwa na noti moja ya Dola 20; noti tatu za Dola 10 sawa na Dola 30 na noti moja ya Dola tano sawa na Dola Tano na noti tatu za Dola Moja sawa na Dola Tatu.

Hivyo jumla ya pesa za kigeni zilikuwa Dola za Marekani 13,558, ambazo Mbuta aliziweka kwenye hati ya ukamataji mali pamoja na solar panel, inventor na betri na wahusika wote wakasaini, kisha wakaondoka na vitu hivyo.

Singano alitoa maelekezo wale mashahidi walioshuhudia waandikwe maelezo akiwemo Editha, Ibrahim, ambaye ni mtendaji Kata ya Ruponda.

Kisha Mussa Mussa akaelekeza kwa Said ambaye alikuwa ameeleza kuwa anaweza kuchukua baadhi ya pesa, lakini walipokwenda kwake hapakuwa na mtu na nyumba ilikuwa imefungwa.

Lakini pembeni kulikuwa na watoto wakicheza akiwemo mmoja ambaye walielezwa kuwa ni mdogo wake Said.

Singano alipomuuliza mahali alikokuwa Said akajibu kuwa hayupo na kwamba aliondoka siku nne zilizopita akiambatana na Mussa. Hivyo Koplo Salim aliandika maelezo ya mtoto huyo aitwaye Omari.

Waliondoka kwenda kituoni na Mussa pamoja na baba yake.

Wakiwa njiani kuelekea kituo cha Polisi Nachingwea walikutana na mama mmoja akiendesha baiskeli na mzee Said Bakari Mnali akamwambia dereva, Mbuta asimamishe gari, kwan huyo alikuwa ndiye mama yake Saidi.

Mbuta alisimamisha gari, Singano akashuka na kumuita yule mama naye akasimama akajitambulisha kwake na kisha akamuuliza kama ana mtoto anaitwa Saidi naye akakubali.

Mama huyo aitwaye Somoe Omari Kalunde alisema kuwa Said aliondoka nyumbani siku nne au tano lakini alimpa maagizo akanunue vifaa vya ujenzi na kwamba ndio alikuwa anatoka mjini kununua.

Singano alimtaka waende naye kituo cha Polisi kutoa maelezo zaidi naye yule mama akakubali na kuacha baiskeli yake nyumba jirani kwa ndugu yake wakaondoka naye hadi kituo cha Polisi Nachingwea.

Alipohojiwa kituoni mama yake Said alieleza kuwa Said alikuwa ameondoka na Mussa na kwamba wakati anaondoka alimpatia pesa kama Sh2 milioni za kununua vifaa vya ujenzi na kwamba mbali na vifaa vile alivyokuwa amenunua, bado kuna pesa nyingine amezihifadhi kwenye begi.

Hivyo Singano alimtaarifu OCD na kwamba wanataka kurudi kuchukua hizo pesa kwa mama huyo na OCD akaelekeza wachukue gari la Polisi kwa kuwa lilisharudi na pia amchukue askari mmoja wa kike.

Hivyo Singano alimchukua WP Amaria na Koplo Heri, dereva, pamoja na timu yote ya awali wakarudi tena huko Ruponda.

Mara hii Singano alimpigia Mtendaji hakumpata, lakini walipofika nyumbani kwao Mussa walimpata kiongozi wa Serikali ya Mtaa aitwaye Said Juwani Said wakaenda naye pamoja na mdogo wake Mussa Hamis aitwaye Maulid Hamis.

Yule mama aliwakabidhi pesa noti 210 za Sh5,000 kila moja sawa na Sh1.05 milioni, Mbuta akaijaza kwenye kumbukumbu, wakasaini Mbuta, Juwani na Somoe kisha askari wale wakaondoka kurudi kituoni wakafika Oktoba 22 Alfajiri.

Kina Mbuta waliondoka na Mussa peke yake wakawaacha baba yake Mussa na Mama yake Saidi, kwa sababu gari ilikuwa ndogo na Singano akawasisitiza warudi haraka kuwachukua, lakini hawakurudi kuwachukua.

Chanzo: Mwananchi
 
Hii kesi inaendelea au?
Nilitaka kujua,hivi polisi hawanaga mahakama zao za jeshi la polisi
 
Acha UJINGA, nimelitumikia Jeshi la Polisi Tanzania kwa miaka 9 na kwa level zote Junior Officer na Senior Officer(Inspector), hivyo nina uhakika wa Asilimia 100 kwa ninachokisema

Yaaan senior officer ndio Inspector? Naanza kupata waswas kama unalijua jeshi weye
 
Kesi hizi huwa mwanzo zinajulikana,Ila mwisho huwa haujulikani.Hakuna updates.
 
Taarifa ina maelezo marefu sana sana, nimeshindwa kuendelea, ahsanteni mlioniwakilisha kuisoma

Duh, askari hao, aibu sana, hawakutegemewa siku moja kupigwa pingu.....haki itendeke
 
Back
Top Bottom