Kesi ya polisi wanaodaiwa kumuua muuza madini: Shahidi adai washtakiwa walitumia gari la OCD

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Gari la Polisi lililodaiwa kutumiwa na washtakiwa wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis kwenda katika kituo cha Polisi Mitengo Mtwara na kisha kuondoka na mtu aliyebebwa kwenye machela limetajwa kuwa lilikuwa ni la Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Mtwara.

Hayo yamebainishwa na shahidi wa sita wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, Sajenti Mwaya Salimin Mwaya wakati akijibu maswali ya dodoso aliyoulizwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, Wakili Majura Magafu, leo Jumanne, Novemba 21, 2023.

Hata hivyo, hatua ya washtakiwa hao kutumia gari hilo kuliibua utata namna ambavyo washtakiwa hao walipata gari hilo, baada ya shahidi huyo ambaye siku hiyo ndio alikuwa msimamizi wa chuma cha mashtaka ambako funguo za magari yote hutunzwa kueleza kuwa haijulikani nani aliwapa funguo hizo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara, ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi, Mkaguzi John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi.

Kulingana na wa ushahidi huo, walifikia uamuzi huo ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizokuwa wamezichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwake wakimtuhumu kuziiba pamoja na pikipiki.

Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Awali gari hilo limetajwa na shahidi wa tano Sajenti Jagati Samson, kuwa washtakiwa walikwenda nalo katika kituo cha Polisi Mitengo (Mikindani) Januari 5, 2022.

Kituo cha Mitengo ndiko Mussa Hamis anakodaiwa kuuawa na washtakiwa hao, kisha mwili wake wakaenda kuutupa Majengo Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha saruji cha Dangote.

Sajenti Jagati amedai kuwa siku hiyo alikuwa zamu ya ulinzi kituoni hapo na wenzake na kwamba muda wa saa sita kuelekea saa saba gari hilo liliingia kituoni hapo.

Amebainisha kuwa lilikuwa likiendeshwa na mshtakiwa wa kwanza SP Kalanje, akiambatana na mshtakiwa wa pili ASP Onyango, Grayson Mahembe (aliyejinyonga) na mtu mwingine aliyekuwa amefunika uso.

Amedai kuwa walishuka, huku Grayson na yule aliyefunika uso wakiwa na machela, ASP Onyango akamwambia kuwa wamekwenda kumchukua mgonjwa wao na wote wanne wakaingia ndani ya kituo hicho, huku yeye akiwachungulia hadi wakaingia kwenye chumba kimoja kinachotumika kama stoo.

Amesema baada ya dakika 15 walitoka wakiwa wamebeba mtu kwenye machela wakamuingiza ndani ya gari hilo harakaharaka wakaondoka uelekeo wa Mtwara mjini lakini dakika 10 baadaye aliliona gari hilo likitoka uelekeo wa Mtwara likiendeshwa kuelekea uelekeo wa Lindi.

Hata hivyo, alipoulizwa na Wakili Magafu namba za usajili wa gari hilo, Sajenti Jagati alijibu kuwa hakumbuki.

Kwa upande wake shahidi wa Sajenti Mwaya ambaye ni mtunza vielelezo katika kituo Kikuu cha Polisi Mtwara ameieleza Mahakama hiyo leo Novemba 21, kuwa siku hiyo aliwaona washtakiwa hao wawili, SP Kalanje, ASP Onyango na A/Insp. Grayson wakiondoka kituoni hapo wakiwa na machela.

Akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, Kassim Nassri amedai kuwa siku hiyo Januari 5, 2022 alikuwa zamu ya usiku akiwa msimamizi wa chumba cha mashtaka (CRO).

Amedai kuwa saa 5:00 usiku SP Kalanje, ASP Onyango na Grayson walifika kituoni hapo wakitofautiana muda mfupi.

Shahidi huyo ameeleza kuwa baada ya dakika kama 15 aliteremka SP Kalanje akampitia ASP Onyango wakatoka nje wakaenda mbele ya kituo kwenye maegesho ya magari.

"Baadaye kidogo Grayson alitokea nyuma ya kituo akapita CRO akiwa amebeba machela akaelekea kwa kina SP Kalanje na ASP Onyango walikokuwa kwenye magari.

"Grayson aliingia kwenye gari ya Polisi namba PT1918 upande wa nyuma pamoja na ile machela. OCS Onyango naye aliingia akakaa mbele pembeni mwa dereva na OC-CID Kalanje akaendesha hilo gari.

Baada maelezo hayo ndipo Wakili Magafu akamuuliza maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake huo, ndipo Sajenti Mwaya akabainisha kuwa gari hilo walilolitumia siku hiyo washtakiwa ni la OCD pamoja na utata wa namna ambavyo washtakiwa hao walivyolipata.

Mahojiano baina yao (maswali na majibu) yalikuwa hivi:

Wakili Magafu: Shahidi ukitaka kujua siku fulani tarehe fulani mwezi fulani askari fulani alikuwa zamu unatakiwa kuangalia kwenye nini?

Shahidi: Unatakiwa kuangalia kwenye OB

Wakili: Occurrence Book, sawa. Askari anapopangwa zamu ni kitu gani unatakiwa kukitazama kujua askari huyo alikuwa zamu siku hiyo mbali na OB? Au unajua kitu kinaitwa duty roster

Shahidi: Naifahamu.

Wakili: Huwa inaandaliwa na nani?

Shahidi: Inaandaliwa na Meja.

Wakili: Huwa inaandaliwa ya muda gani?

Shahidi: Ya mwezi mzima.

Wakili: Hebu tusaidie umekuja na hiyo roster ili tuone kwamba kipindi hicho cha Januari 5 ulikuwa kazini?

Shahidi: Sijaja nayo.

Wakili: Na OB umekuja nayo?

Shahidi: Sijaja nayo.

Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi kwamba hakuna ushahidi wa maandishi kuwa wewe siku hiyo ya tukio ulikuwa ni In charge wa CRO?

Shahidi: Sasa hivi sina ushahidi wa maandishi.

Wakili: Onyango alikuwa ni OCS, na ofisi yake ilikuwa jirani na ya CRO, Kalanje alikuwa OC-CID na ofisi yake ilikuwa juu ghorofani na A/Insp. Grayson naye ofisi za wapelelezi ziko juu ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Kwa hiyo hawa watu watatu ili wakutane lazima walioko ghorofani wateremke chini au OCS awafuate hawa wawili walioko juu?

Shahidi: Hawawezi.

Wakili: Kwa nini? kwani wa kwa jengo hilo lilivyo wa chini hawezi kuwafuata wa juu?

Shahidi: Anaweza lakini mimi nazungumzia nilichokiona.

Wakili: Uliwahi kushiriki mazungumzo yao hawa watu watatu?

Shahidi: Sikuwahi kushiriki mazungumzo yao.

Wakili: Kwa hiyo hujui waliongea nini walipokutana?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Kwani wewe unavyojua kwa uzoefu wako vitendea kazi vingine vya ofisi ukiondo silaha vinakuwa chini ya nani?

Shahidi: Vitendea kazi vingine kama vipi?

Wakili: Kama machela.

Shahidi: Mtunza stoo.

Wakili: Hapo kituoni kwenu nani alikuwa mtunza stoo?

Shahidi: Sasa hivi simkumbuki alikuwa nani.

Wakili: Kabla ya kwenda kuchukua hicho kifaa cha kufanyia kazi unakwenda moja kwa moja stoo au unaanzia kwa nani?

Shahidi: Unaanza kwa mtunza stoo

Wakili: Mtunza stoo anatakiwa afanye nini kabla ya kukukabidhi hicho kifaa?

Shahidi: Hakuna cha kufanya zaidi ya kukusajili.

Wakili: Hicho kitabu kinaitwaje kwa mujibu w PGO (Mwongozo wa Utendaji Kazi wa Jeshi la Polisi)? Maana vitabu vyote viko kwenye PGO 70.

Shahidi: Sikifahamu kwa sababu mimi si mtunza stoo.

Wakili: Kabla ya kuja leo kutoa ushahidi uliwahi kuwasiliana na mtunza stoo ili kujua kama kweli Grayson alichukua hiyo machela?

Shahidi: Sijawahi.

Wakili: Sasa mimi nakwambia kuwa Grayson hajawahi kuchukua hiyo machela maana huna ushahidi wa maandishi, wewe unasemaje?

Shahidi: Hilo naiachia Mahakama.

Wakili: Anaiachia Mahakama mheshimiwa (Jaji) maana hana jibu. Unaiachia mahakama ikusaidie kutoa jibu?

Shahidi: Kwa sababu nimeshasema alichukua kwa hiyo yenyewe ndio itaona.

Wakili: Lakini huna maandishi, ni kweli?

Shahidi: Ndio sina maandishi.

Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba OCD huwa ana gari lake na dereva wake?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Dereva wa OCD anaitwa nani?

Shahidi: Koplo Justine

Wakili: Kawaida dereva wa OCD huwa anaendesha gari gani?

Shahidi: PT1918 (ambalo aliitaja awali kuwa ndilo washtakiwa SP Kalanje na ASP Onyango waliondoka nalo na machela)

Wakili: Siku hiyo Januari 5, 2022 OCD na dereva wake waliokuwepo?

Shahidi: Hawakuwepo

Shahidi: Utakubaliana mimi kwamba ili gari ya OCD iende kwenye shughuli nyingine ni lazima yeye mwenyewe ndio atoe kibali aridhie?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: OC-CID naye kwa ushahidi wako huwa ana gari yake?

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Nani dereva wake wa kila siku?

Shahidi: Koplo Said.

Wakili: Siku hiyo alikuwa wapi?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Hiyo gari ya OC-CID ni namba ngapi?

Shahidi: PT1420

Wakili: Hawa maofisa watatu wewe siku hiyo uliwaona waliingia gari gani?

Shahidi: PT1918

Wakili: Ambayo ni ya nani?

Shahidi: Ni ya OCD.

Wakili: Kwani kwa kawaida funguo za magari hayo yote huwa anatunza nani?

Shahidi: Zinatunzwa CRO

Wakili: Kwa hiyo mtu yeyote anaweza kuja CRO na kuchukua gari (funguo)?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Anakabidhiwa nani?

Shahidi: Dereva.

Wakili: Kuna sehemu anaweka rekodi?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Inaandikwa kwenye kitabu gani?

Shahidi: OB.

Wakili: Siku hiyo hizo funguo alikabidhiwa nani?

Shahidi: Haijaandikwa.

Wakili: Kama kitabu kiko kimya maana yake kuna mawili, ama siku hiyo gari haijatoka au aliyechukua funguo alipewa kinyume na utaratibu, ni kweli au si kweli?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Kwa siku hiyo nani alikuwa anawajibika pale CRO kuwakabidhi madereva funguo?

Shahidi: Aliyetakiwa ni CRO.

Wakili: Ambaye alikuwa nani siku hiyo na muda huo?

Shahidi: Nilikuwa ni mimi.

Wakili: Uliwahi kuwauliza wenzako uliokuwa unasaidiana nao nani alitoa funguo za gari ya OCD akamkabidhi OC-CID SP Kalanje?

Shahidi: Niliwahi kuuliza lakini wakaniambia kwamba hakuna aliyetoa funguo.

Wakili: Uliwahi kumuuliza huyu dereva wa OCD kama aliwahi kuchukua funguo na kumkabidhi OC-CID?

Shahidi: Dereva hakuwepo.

Wakili: Ni utaratibu gani hutumika wakati wa kurejesha funguo?

Shahidi: Mtu anaporejesha hukabidhi CRO anaandika kwenye OB.

Wakili: Kati ya hao maofisa wawili OCS (ASP Onyango) na OC-CID (SP Kalanje) uliwahi kuona mmojawapo anakwenda CRO kukabidhiwa hizo funguo?

Shahidi: Sikuwaona.

Wakili: Uliwahi kuona kati ya hao wawili mmojawapo akaja kurejesha hizo funguo?

Shahidi: Sikuona.

Wakili: Na mpaka leo hii uliposimama hapo kizimbani hakuna sehemu inayoonyesha kuwa OC-CID alikabidhiwa hiyo gari akaondoka nayo?

Shahidi: Hakuna sehemu inaonyesha hivyo.

Wakili: Sasa kwa kuwa hujaonyesha ushahidi wa maandishi kuwa tarehe hiyo ulikuwa kazini, utakubaliana na mimi kuwa wewe tarehe hiyo hukuwa kazini?

Shahidi: Si kweli.

Wakili: Lakini huna ushahidi wa maandishi, ni kweli?

Shahidi: Ushahidi wa maandishi sina.

Wakili: Na vile vile huna ushahidi wa maandishi kuonyesha siku hiyo Grayson alichukua machela?

Shahidi: Sina ushahidi wa maandishi.

Wakili: Vile vile huna ushahidi wa maandishi kuwa siku hiyo aidha Grayson, OCS au OC-CID alikuja CRO akachukua funguo za hilo gari?

Shahidi: Ushahidi wa maandishi sina.

Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba hizi regista zimewekwa kwenye vituo vya Polisi kwa ajili ya kutunza kumbukumbu?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba hizi kumbukumbu zimewekwa ili kuwashughulikia watendaji ambao hawafuati taratibu zilizowekwa?

Shahidi: Hilo sina hakika.

Wakili Fredrick Ododa kwa mshtakiwa wa pili, ASP Onyango.

Wakili Ododa: Shahidi ni kweli kuna kitabu kinaitwa Station Diary ambacho kinarekodi matukio mbalimbali kituo cha Polisi Mtwara?

Shahidi: Kipo.

Wakili: Ni kweli kwa ushahidi na maelezo yako hujatoa hicho kitabu hapa mahakamani kama sehemu ya ushahidi wako?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Moja ya wajibu wako kama CRO ni kurekodi mkuu wako wa kituo anapotoka na kurudi?

Shahidi: Siyo kweli.

Wakili: Kwa mujibu wa ushahidi wako hujaeleza kuhusiana na kutoa taarifa kwa Polisi yeyote kuhusu tukio hilo lililotokea siku hiyo kituoni hapo.

Shahidi: Siyo kweli.

Kesi hiyo itaendelea kesho kwa mashahidi wengine wa Jamhuri

Chanzo: Mwananchi
 
utashangaa wanashinda kesi hii ama wanapewa tu adhabu ya kuua bila kukusudia
Screenshot_20231122-084436.jpg
 
sasa kama incharge wa CRO kila kitu anasema HAJUI kaenda Mahakamani kutoa ushahidi gani??ndio matatizo ya Askari kufanya kazi bila kufuata maelekezo ya PGO wakati PGO ndio Dira
 
utashangaa wanashinda kesi hii ama wanapewa tu adhabu ya kuua bila kukusudiaView attachment 2821378
Hawa Polisi wauaji wanapoteza muda tu wa Mahakama. Kama Jeshi la Polisi lingekuwa serious ma endapo kama kweli linawachukia Polisi Wahalifu wanaolichafua Jeshi lao, basi haobAskari Polisi wote hawa waliohusika na tukio la kumuua huyu Mfanyabiashara ingekuwa tayari wamepewa adhabu kama hii ya hawa kwenye video hapa chini.
 

Attachments

  • 5573680-34448019a8aba77133acd881c124fa56.mp4
    16.6 MB
Majura magafu kwenye ubora wake

Kila kitu polisi hajui ,upelelezi hua wanafanyaje au umefanywa kwa kulindana

Eti!

Inakuwaje vielelezo viachwe visifikishwe mahamani ,kama OB na vingine kama hivyo
 
Back
Top Bottom