Nianze kwa kuweka hapa habari ya Mwandishi wa Gazeti la "Familia" kuhusu hili tukio na kama kuna masuala mahususi yatahitajika nitaongezea:
Tanzania sasa kupata katiba Mpya
- Kongamano la pili lapitisha mpango mkakati
- Timu ya wataalam yaundwa
- Vyama vya siasa kuchangishana fedha
Umma wa Watanzania umeanza mchakato wa kuunda katiba mpya na kudai tume huru ya uchaguzi. Hilo limejidhihirisha hivi karibuni baada ya mpangomkakati kuwasilishwa mbele ya kongangamano la wawakilishi wa vyama vyote vya siasa visivyoshika dola, asasi za kiraia, wawakilishi wa makundi ya wazee, vijana na wanawake, taasisi za kidini na wanahabari, lililofanyika siku ya Jumanne tarehe 24 Mwezi Machi mwaka huu katika hoteli ya Peackock jijini Dar es salaam. Katika kongamano hilo lililokusanya watu wa kada mbalimbali toka Tanzania bara na visiwani kamati ya kudumu ya watu 20 iliundwa, ikiwajumuisha Maalim Seif Shariff Hamad ( Mwenyekiti wa kamati), Mh. Zitto Kabwe, Bw. Anthony Komu, Bw. Benedicto Mtungirehi, Bi. Ndelakindo Kessy, Bi Riziki Shahari Ngwali na Prof. Abdallah Jumbe Safari miongoni mwa wengine.
Aidha Dr. Sengondo Mvungi alikabidhiwa na kongamano jukumu la kuongoza jopo la wataalam katika mchakato mzima wa kuandika katiba mpya na kudai tume huru ya uchaguzi.
Akifungua kongamano hilo mgeni rasmi Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) aliainisha kuwa kongamano hilo, lisilofungwa na imani wala itikadi ya chama, ni la kuandika na kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi na kusema, Uchaguzi wa Tunduru umethibitisha kwa mara nyingine tena haja ya kudai katiba mpya. Aliendelea kueleza kuwa matumizi ya dola yaliyojitokeza katika uchaguzi wa Tunduru umethibisha kwa kiwango gani wateuliwa wa Rais wanavyoweza kupoteza uhuru wao wa kuongoza na kutoa haki kwa Watanzania wote linapokuja suala la uchaguzi huru ambamo chama cha Rais kinashiriki pamoja na vyama vingine vya kizalendo.
Prof. Lipumba aliendelea kusema kuwa ni udhalimu mkubwa kuutumia umaskini wa Watanzania kuuendeleza umaskini wenyewe kwa kununua hati zao za kupigia kura na hivyo kuwanyima haki ya kufanya mabadiliko ili kujiletea ustawi wa maisha yao.
Akikumbushia maneno ya Baba wa Taifa Prof. Lipumba alisema, Baba wa Taifa aliwahi kutoa kauli ambayo Mheshimiwa Mbatia hupenda kuirudia, ikiwa wakoloni hawatotupa uhuru tutamwomba Mwenyezi Mungu, lakini kama Mwenyezi Mungu hatatusikia katika hili basi tutamwomba shetani. Lakini aliendelea, Hatutaki kufikia kumwomba shetani kutusikia katika hili.
Katika kongamano hilo mpango mkakati wa kuandika na kudai katiba mpya pamoja na tume huru uliwasilishwa na kamati maalum iliyoundwa na Mwenyekiti wa kongamano la kwanza lililofanyika katika hoteli hiyohiyo Januari 29 na 30 mwaka huu, Maalim Seif Shariff Hamad kwa mamlaka aliyokabidhiwa na azimio namba tisa la kongamano hilo. Kamati hiyo iliundwa na Stephen Chonya (National Productivity Institute) ambae alikuwa ni Mwenyekiti, Julius Miselya ( Taasisi ya Ford), Yahya Hamad (Zanzibar Law Society), Elias Michael (Rugazia Advocates), John Mnyika (CHADEMA) na Hussein Mmasi (CUF) ambae alikuwa katibu wa kamati hiyo.
Mkakati huo uliopitishwa na kongamano la pili lililokuwa na wenyeviti wawili, Mhe Augustine Lyatonga Mrema mwenyekiti wa Taifa TLP na Prof. Lipumba, na unaokadiriwa kutumia kiasi cha fedha kisichopungua bilioni 2.68 shilingi za kitanzania, unatarajiwa kuhusisha wilaya 126 za Tanzania bara na wilaya 10 za Tanzania visiwani, tarafa 140 na kata 2553. Katika hatua hizo za awali, mchakato huo umewezeshwa kifedha toka ruzuku za Chama cha Wananchi, imefahamika.
Akiwasilisha kwa kina mkakati huo Bw. John Myika ambae ni mkurugenzi wa vijana wa CHADEMA alisema, Suala la kudai katiba mpya ni kama vita na ushindi ni lazima.
Mpango mkakati huo umeainisha sababu 25 zakudai katiba mpya. Zifuatazo ni sababu hizo:
Uundaji wa katiba iliyopo haukuwashirikisha wananchi. Rasimu ya katiba iliyopo ilipendekezwa na kuasisiwa na kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) Mchakato wote wa kupata katiba hii ulifanywa kwa muda wa mwezi mmoja tu. Hivyo, hakukuwa na muda wa kukusanya maoni ya wananchi. Ndio maana katiba hii sasa ina uhalali wa kisheria tu lakini haikubaliki kwa watu.
Ndani ya katiba iliyopo ibara ya 8 inayotamka kuwa mamlaka ya umma yamo mikononi mwa wananchi yamewekwa kama pambo tu. Mtu hawezi kwenda kuyadai mahakamani. Ndio maana hivi sasa wananchi hawana sauti wala mamlaka kwa viongozi waliowachagua wenyewe. Kwa mfano, hata mbunge akiwasaliti wananchi wake hawawezi kumuondoa madarakani. Lakini mbunge huyohuyo akikisaliti chama basi kinamuondoa madarakani mara moja.
Katiba iliyopo inautata mkubwa kuhusu suala la Muungano. Kwa kuwa katiba hii ni ya muungano, ifafanue wazi mambo yanayohusu Muungano. Hakuna haja ya katiba ya Zanzibar kuwemo ndani ya katiba ya Jamhuri. Kwa mfano, katika katiba haijulikani tunaungana nini? Kwani Ingawa ibara ya kwanza ya katiba inatamka kuwa Jamhuri ya Muungano ni nchi moja, ukiangalia orodha ya mambo ya muuungano; ardhi sio suala la muungano. Sasa hiyo nchi moja iko vipi kama Zanzibar wana ardhi yao.
Katiba yetu haina kabisa suala la umiliki wa ardhi, Ingawa ardhi ndio msingi wa maisha na suala la uchumi. Dosari hii ndio imekuwa chanzo cha watu kunyanganywa ardhi zao bila huruma au kusikilizwa. Mfano, wananchi kufukuzwa kwenye maeneo yao ili kupisha migodi au mashamba yao kuuzwa kwa wawekezaji wengine.
Katiba iliyopo sasa haina kabisa suala la uraia. Wananchi wote tumekuwa kama wakimbizi ndani ya nchi yetu. Hata suala la uzalendo wa dhati limefifia miongoni mwa wa Watanzania. Wasomi na wasiosoma mathalan, wamekuwa na mawazo ya kwenda kuishi Ulaya.
Katika katiba hii, haki ya kupiga kura ambayo ndio msingi na kielelezo cha mamlaka ya umma katika uongozi wa nchi, sio sehemu ya haki za msingi za binadamu ( imewekwa ibara ya tano ambapo sio sehemu ya haki za bianadamu). Hivyo hata mtu akinyimwa kupiga kura hawezi kudai mahakamani. Ndio maana nyakati za uchaguzi watu wamekuwa wakipanga mistari, karatasi za kupigia kura zikiisha, hawawezi kwenda mahakamani kudai haki yake ya kupiga kura.
Ingawa katiba ndio sheria mama, hakuna kifungu cha wazi ndani ya katiba kinachotamka hivyo. Iwekwe wazi ndani ya katiba kuwa ndio inayoshika hatamu. Hakuna mtu yeyote, sheria yoyote au chombo chochote kitakachokuwa juu ya katiba kwa sababu imekuwa ni kawaida kwa watawala na Bunge kutunga sheria zinazo pingana na katiba ilimradi tu zinakidhi haja zao.
Katiba inaweka madaraka makubwa sana tena ya mwisho kwa Rais. Ni hatari sana kuweka hatma ya nchi mikononi mwa mtu mmoja na sio Bunge ambalo ndilo wawakilishi wa wananchi. Cha ajabu, Rais anaweza kuvunja Bunge kama litakataa kupitisha bajeti yake.
Rais ndie anamamlaka ya kuteua na kufukuza wajumbe wa tume ya uchaguzi. Hali hii inaifanya tume kutokuwa huru. Kila wakati inajitahidi kumpendezesha Rais (Chama Tawala) ambaye ndio bosi wao.
Katiba Ingawa inaanzisha mfumo wa vyama vingi, haifafanui wajibu na haki za vyama vingi. Kwa mfano, haitamki kama kiongozi wa upinzani ni kiongozi wa Kitaifa kama alivyo spika.
Katiba hii haitambui wala kuzilinda haki nyingi za msingi. Kwa mfano, haki za elimu, vijana , walemavu, wazee, familia, hifadhi ya wakimbizi, vyombo vya habari, kuandamana, kiuchumi, biashara, taaluma, kutendewa haki na watawala, huduma ya afya, chakula bora, hifadhi ya mazingira, utamaduni, nk.
Katiba hairuhusu wagombea binafsi kwenye nafasi mabalimbali za uongozi wa nchi. Hivi sasa mtu akitaka kushiriki uongozi wa nchi lazima awe mwanachama wa chama cha siasa. Hali hii inawanyima nafasi ya uongozi Watanzania walio wengi ambao si wanachama wa vyama vya siasa. Hata Mahakama kuu imepitisha uamuzi kuwa ruksa mgombea binafsi (Kesi ya Mhe. Mtikila).
Katiba haifafanui mambo mengi ya msingi kama vile vita dhidi ya rushwa, umiliki wa uchumu na mwelekeo wa sera za nchi. Sehemu ya maelezo yaliyopo kwenye ibara ya tisa ni pambo tu kwani hayahojiwi mahakamani.
Haki ya elimu haimo kwenye kwenye katiba. Kilichoandikwa ni kwamba, kila mtu ana haki ya kujielimisha. Tena nayo si sehemu ya haki za msingi za binadamu.
Kuna mkanganyiko mkubwa kwenye katiba baina ya mamlaka ya serikali za mitaa na serikali kuu. Kwa mfano, katiba haifafanui nafasi ya wakuu wa mikoa na wilaya katika katiba. Aidha, haikuweka wazi kati ya viongozi hao, madiwani na wabunge yupi ana nguvu. Imekuwa kawaida wakuu wa mikoa na wilaya kuwanyanyasa madiwani ambao ndio waliochaguiwa kwa kura na wananchi. Hata hivyo wakurugenzi wa wilaya wanaingiliwa na wakuu wa wilaya ambapo wote wameteuliwa na Rais.
Bunge haliruhusiwi kupendekeza na kupitisha muswada wowote unaoweza kuigharimu fedha serikali. Miswada ya aina hii, ni lazima ianzie serikalini. Hali hii imelifanya Bunge la Jamhuri ya muungano, kuwa kama muhuri tu wa serikali bila mamlaka yoyote katika usimamizi wa mambo ya wananchi.
Rais anaweza kulivunja Bunge wakati wowote kama akikataa kusaini Muswada lililopitisha au likikataa bajeti ya serikali.
Rais anateua viongozi wa juu wa nchi bila kushauriana na mtu yeyote. Na anaweza kuwafuta kazi apendavyo. Baadhi ya madaraka ya Rais yanaweza kupewa vyombo vingine vya dola; Kwa mfano, kuteua wakuu wa mikoa, mabalozi, makamanda wa vikosi vya ulinzi na usalama, Jaji Mkuu, mwanasheria mkuu, mkurugenzi wa mashitaka, nk. Wanaweza kuteuliwa na Rais na kuidhinishwa na kamati zinazohusika za Bunge.
Katiba hii haiweki mahakama ya katiba. Ingawa mahakama kuu imepewa mamlaka ya kusikiliza mambo ya kikatiba. Kuna utata. Katiba ni suala la muungano, wakati mahakama kuu sio suala la muungano. Hivyo maamuzi yake hayana nguvu Zanzibar.
Serikali imeshaunda tume mbalimbali. Zote zimeshauri wazi kuwa katiba hii haifai. Mfano tume ya jaji nyanyalali, tume ya jaji kisanga nk. Hivyo katiba mpya inahitajika.
Katiba hii haina kifungu cha mamlaka ya kulinda wananchi wasionewe na serikali au vitendo vya watala ( Public Protector). Hivi sasa wananchi wanapigwa au kukamatwa na polisi na kubambikiziwa kesi halafu mtu akilalamika, polisi walewale ndio wanachunguza. Wananchi wengi wamekuwa wanayimwa haki.
Katiba imeweka namna ya taifa kulipa deni la nchi, lakini haifafanui namna ya kushughulikia madeni ya serikali ndani ya nchi. Aidha, hakuna kifungu kinacholazimisha serikali kuwalipa fidia wananchi inapodhihirika serikali haikuwatendea haki. Hali hii imesababisha watu wengi kutolipwa na serikali Ingawa mahakama imeamua walipwe. Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa watu inaopenda yenyewe kama hisani.
Hakuna kifungu cha wazi kuelezea namna ya kurekebisha katiba. Kifungu kilichopo kinaruhusu katiba kurekebishwa tu kama sheria nyingine. Hivyo, kama Bunge linaweza kurekebisha katiba yote.
Hivi sasa kunamchakato wakuharakisha ushirikiano wa kisiasa (Shirikisho) kwa nchi za Afrika ya Mashariki, itakuwa vigumu kwa Tanzania kuingia kama katiba mpya haijatungwa; kwa sababu katiba iliyopo inamapungufu mengi sana.
Katiba hii haina kifungu cha tafsiri/ ufafanuzi kinachojitosheleza. Ibara ya 152 inayotoa ufufanuzi haitoshi kabisa. Kuna mambo mengi hayaelezwi maana yake. Kwa mfano hakuna tafsiri ya neno maslahi ya umma. Hii imesababisha watu wengi kunyimwa haki kwa madai ya maslahi ya umma kumbe ni maslahi ya viongozi wachache wenye maslahi binafsi.
Akifunga Mkutano huo Mhe James Mbatia mwenyekiti wa Taifa wa NCCR Mageuzi alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuwa na Uzalendo wa kweli kwa nchi yao.