Movement: Tunataka Katiba Mpya Tanzania

mzeewabusara

Member
Jun 7, 2006
12
24
Wanabodi ninakerwa na jambo hili naomba tujadili. Hivi serikali ni nani? Nilidhani ni wananchi ambao wanawakilishwa na Bunge?

Kutokana na majadiliano yanayoendelea bungeni kuhusu mikataba ambayo serikali haitaki ijadiliwe sisi kama wananchi ambao tumewachagua wabunge hawa tunapenda kuonyesha msimamo wetu kwa kufanya maandamano ya amani na mkutano mkubwa kutoa msimamo wetu. Mikataba yote ipelekwe bungeni. Sisi wananchi ndio tunasema.

Tanzania kweli ni nchi ajabu sana duniani. Ni kama nchi isio na watu wenye uchungu nchi yao. Jamani mawaziri mnasafiri sana nchi za watu na kuona maendeleo yao. Hivi kweli mna vision kuwa kuna siku Tanzania itaendelea? Ni lazima mfike mahali pa kuona wivu wa maendelo ya nchi siyo yenu binafsi tu. Tafadhali mheshimiwa Mbowe tunaomba uandae mkutano huo na kutoa tamko. Aliye karibu na mheshimiwa tafadhali mpelekee salamu. Msisubiri mpaka wakati wa uchaguzi tu.

" KWA MTAJI HUU NDOTO YA KUWALETEA WATANZANIA WOTE MAISHA BORA NA MEMA HAIWEZEKANI KABISA - IT IS NOT POSSIBLE FULLSTOP"

Sauti za wabunge hawa zisipuuzwe

KAMA kweli wabunge ndio wawakilishi wa wananchi, serikali sasa itaondoa pamba masikioni, itawasikiliza na kutekeleza wanachopendekeza.

Kwa siku nyingi sasa, kilio cha wabunge kuhusu mikataba ya madini na mikataba mingine mikubwa, kimezidi kiwango.

Kilio chao kimevuka mipaka ya kawaida. Kimewagusa hata wale ambao hawakuwa na shauku ya kukisikia.

Wabunge wanataka mikataba ipitiwe. Wanataka kujua kilichomo kwenye mikataba hiyo. Serikali haiwakilishi wananchi. Bunge ndicho chombo cha wananchi.

Wabunge wanapojadili jambo lenye manufaa kwa nchi, wanafanya hivyo kwa niaba ya wananchi wao.

Haiwezekani wabunge wapige kelele za kutaka kupitiwa mikataba, lakini serikali iendelee kuwa jeuri.

Awamu ya Tatu ya uongozi wa taifa hili ilitamba kwa kaulimbiu hewa ya uwazi na ukweli. Hapakuwa na uwazi wala ukweli.

Mikataba ilisainiwa. Wageni wakamilikishwa mali za taifa. Mikataba mingi ya kipuuzi kabisa ikasainiwa. Mzigo wa mikataba hiyo sasa unabebwa na walipa kodi wa nchi hii.

Serikali haikuwa wazi. Ilipuuza maoni ya wananchi, na hata ikafikia hatua ya kuwatisha wabunge waliosimama kidete kuhoji uoza fulani fulani.

Inasikitisha, na kwa kweli inakasirisha, kumsikia leo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, akiunga mkono kupitiwa upya kwa mikataba ya madini!

Yeye ndiye aliyekuwa kinara wa kuponda wote waliohoji mikataba hiyo, hata akafikia hatua ya kuwaita waliohoji kuwa ni wavivu wa kufikiri.

Waandishi wa habari walioandika au kuhoji mikataba hiyo, walionekana si wazalendo, na ni watu wasiokuwa na maarifa yoyote.

Serikali ya Awamu ya Tatu ilijaa ujuaji na ubabe. Net Group Solution walipingwa mno. Watanzania wengi walisimama kuipinga kampuni hiyo na hata wakurugenzi wake ambao wengi walikuwa vihiyo.

Lakini kilichofanywa na serikali ni kuwaita FFU wenye bunduki na gesi za kutoa machozi, kuwasindikiza Wazungu hao hadi ofisini.

Kimsingi yamefanyika mambo mengi ya ajabu katika nchi hii. Ndiyo maana tunasema kilio hiki cha wabunge sasa, lazima serikali ikifanyie kazi.

Miktaba ya kipuuzi, kwa mfano ya kuukodisha Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kwa dola 1,000 kwa mwaka, ni laana isiyosameheka mbele ya Mola.

Hivi kweli Tanzania kwa utajiri wake ina sababu ya kuomba misaada mingi kama ilivyo sasa? Je, kwa ukwasi uliopo, kuna sababu ya watu kufa kwa magonjwa kama malaria?

Laana ya Tanzania ni nini? Je, si kweli kwamba laana ya Tanzania ni viongozi jeuri na wasioambilika? Kama kweli sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, basi sauti hii ya wabunge lazima iheshimiwe. Serikali ipeleke mikataba bungeni.

Katiba yenyewe hii hapa:

KATIBA YA JAMHURI WA MUUNGANO WA TANZANIA na mabadiliko ya 2005

Angalia attachments hizi mbili (English and Swahili)​
 

Attachments

  • Katiba_Tanzania_2005.pdf
    111.8 KB · Views: 122
  • Tanzania_Constitution_2005.pdf
    507.5 KB · Views: 75
Mzee wa Busara, kinachoudhi na kunikera ni hiki kimbelembele cha waandishi kushangalia na kupiga vigelegele kwa kitu ambacho hakina kichwa la miguu. Kufuatia habari kuwa tume itaundwa na Rais Kikwete amesimamisha mikataba mipya, je watanzania tuna sababu ya kucheka au kulia? Binafsi nasema, tumezugwa tena ili tunyamazishwe. Mimi nitafurahia tume kupitia hii mikataba endapo tu maswali haya yatajibiwa (nisikilize kwenye mwanakijiji.podomatic.com). Nitayarudia hapa kwa kifupi:

a. Tume hii ya kupitia mikataba ina nguvu gani ya kisheria? Je ina uwezo wa kuita mashahidi (subpoena power) na uwezo wa kutoa kinga (immunity power) kwa mashahidi?

b. Je Mhe. Kikwete, Mhe. Edward Lowassa, na viongozi wengine waliokuwa katika nyadhifa mbalimbali wakati mikataba mbalimbali ikiingiwa wako tayari kuja na kuketi mbele ya tume hii huru na kutoa ushahidi wao chini ya adhabu ya kuongopea tume (under the penalty of perjury)

c. Je wale wote (wanasheria na viongozi wa wizara, idara, nk) ambao walihusika katika majadiliano ya mikataba (negotiations) kati ya serikali na mashirika, au makampuni ya kigeni wataitwa mbele ya tume hii na kujibu swali la kama makampuni ya kigeni yaliwapa "kitu kidogo" au asilimia 10 ili waweke vipengele fulani kwenye mikataba hiyo (kujibu swali hilo nashauri watu hao wapewe kinga!)

d. Je bunge letu liko tayari kupitisha sheria inayokataza mara moja kwa kampuni yoyote ya kigeni au ya ndani inayoingia mikataba na serikali ya tanzania au taasisi zake kutoa aina yoyote ya malipo kwa wawakilishi wa serikali kwenye mazungumzo au familia zao, malipo ambayo yanaweza kupotosha utendaji wa haki au uhuru wao wa kufanya kazi yao?

e. Je serikali iko tayari kuvunja mikataba yote (siyo kuifanyia marekebisho tu) ambayo imekiuka sheria za Tanzania au ambayo iliingiwa kwa njia za kilaghai?

Nikisikia majibu ya maswali hayo ndiyo nitajua kama nicheke au nilie, ama sivyo haya yote ni MAZINGAOMBWE!!!!!!
 
Mwanakijiji Nimekupata mkuu.

Hayo uliyoelekeza ndio lengo kufikia ingawa sidhani kama litafikiwa katika karne hii kwa nchi kama ya Tanzania. Bunge letu limefeli kutoa changamoto ya kweli. Waandishi wa habari nao ndio hivyo tu. Vyama vya siasa navyo vinachechemea tu. Siasa za Tanzania bwana Mwanakijiji ni ngumu sana. Inahitaji commitment na sacrifice ya hali ya juu sana ambayo hadi sasa hajapatikana mtu wa aina hiyo.


Ila kama Mwalimu alivyosema kuwa upinzani wa kweli ni lazima utokee ndani ya CCM. Nami naamini huenda ipo siku baadhi ya wana CCM wataona na kuyakataa maovu haya ambayo yanatia aibu taifa letu.

Tatizo kubwa ambalo watanzania tunalo ni kukosa moyo wa uzalendo, utaifa na mawazo ya kujenga future ya nchi kama Tanzania. Kama tungekuwa na moyo huu si rahisi kuingiza nchi mikataba ya kuua kabisa nchi.

Ndio maana mie nasema kwa mtaji huu maono ya kuwaletea watanzania wote mema hayawezekani. Maana keki yote ya taifa mnakula nyie wachache akina mwanakijiji.
 
Kwa mawazo yangu baada ya kuja JK na kasi zake zote nilidhani ataendelea kwa kasi kutupatia majibu ya maswali aliyo yauliza Mzeemwanakijiji hapo juu kumbe nimekuta na yeye Serikali inakodisha uwanja wa KIA kwa pesa mbuzi , mawaziri wake wanasema mikataba ni siri , wengine wanawazuia wabunge kushusha hoja lakini waandishi haya hawayasemi kabisa na watanzania wanasema Serikali ya awamu ya 4 ni kiboko kwa utendaji kwa nini tunashindwa kuelezwa kiini cha kuvurundwa mikataba?

Nina amani kwamba JK kama hakuhusika nan mikataba angalikuwa kesha ifanyia kazi hadi sasa .Wabunge wamepewa baadhi ya mikataba baada ya kutishia kwenda Mahakamani .Ukweli huu mbona tunauhutaji sana ndugu JK ?Tunataka kujua sisi nani alituingiza huko kubaya na baada ya hapo ndugu JK washitakiwe hata kama ni wanasheria wa sheria huo ndiyo utawala bora na si zaidi ya hapo.
 
Kuna kutofautiana kati yetu wachangiaji, kuhusu maana ya serikali. Hilo lilijitokeza vile vile katika mada ya "Wasiwasi wa Udini". Sam na Mkandara wametoa definition kwamba "serikali ni watu". Kwa maoni yangu, tatizo lililoko hapa ni la msingi kabisa, kwani linahusu maana ya neno "definition" lenyewe. Kuchanganua kinachofanywa na serikali bila kjua serikali ni nini kuna matatizo yake.

Kuna tofauti kati ya definition, description na slogan. "Serikali ni watu" is a slogan, and a political one at that. Ni kama Mzee Aboud Jumbe alivyokuwa anasema "Ujamaa ni utu". Hiyo siyo definition ya Ujamaa, ni slogan tu. Definition inayotolewa kwa lugha ya Kiswahili inabakia kuwa definition hata ukitafsiri kwa Kiingereza. Serikali ni watu translates into governement is people, which is clearly not a definition. Ni slogan, basi.

Kwenye Elimu ya Viumbe, wanasema binadamu ni myama. Ni kweli, lakini hiyo sio definition ya binadamu. Kusema serikali ni watu kuko level moja na kusema binadamu ni myama. To define is to characterize. These are not characterizations.

To define is to put boundaries. A definition of the term government should put boundaries around it in such a way that everything inside the boundaries is government, nothing that is outside is government, and nothing that is government is not inside the boundary.

Kimsingi, serikali yetu ni ya demokrasia. A well known definition of democracy is that it is a government of the people, for the people and by the people. Matatizo yanayotuletea ufanisi mbaya serikalini yanatokana na kukiukwa kwa baadhi ya kanuni hizi.

The government of Tanzania is of the people (true), but it falls short on being by the people and for the people. Ili iwe by the people, inabidi maamuzi yake makuu yote yawe na ridhaa ya wananchi, kwa kupitia wawakilishi wao, yaani Bunge. Serikali "by the people" haiwezi kuwekeana mikataba na watu na makampuni bila kupata kibali cha wananchi, yaani kibali cha Bunge. Mikataba ya IPTL na mikataba yote kati ya Tanzania na makampuni ya nje ya uchimbaji wa madini imewekwa bila ridhaa ya wananchi. Hicho ki kithibitisho tosha kwamba serikali yetu sio by the people.

Ili iwe for the people, serikali ingeweka maslahi ya wananchi mbele ya vitu vingine vyote. Kuwapa watu wa nje ruhusa ya kuchukua dhahabu ya wananchi kwa kuwapa asilimia 3 tu ya thamani yake sio kuweka maslahi ya wananchi mbele. Serikali inayoacha fedha za wananchi kuibiwa kwa mabilioni mengi kila mwaka na kufunika funika uchunguzi kuhusu wezi wenyewe sio for the people.

Ili kuimarisha utendaji serikalini basi, inabidi kuimarisha demokrasia. Mikataba isiwe sheria kabla ya kupitishwa na Bunge. Serikali ipate kwanza ridhaa ya Bunge kabla haijawekeana mkataba na mwekezaji yoyote.

Augustine Moshi
 
Nadhani huu ni muda muafaka wa wapinzani kuanza harakati za kudai mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi.

Haya matatizo ya kashfa za CCM nina amini wanajimaliza wenyewe na sasa ni wakati wa wananchi kupiga kelele wenyewe maana vyombe vyetu vya habari vinalamba miguu ya mnene JK, na kwa kuwa wananchi ndiyo walio wakataa wapinzani kwa kuwanyima kura za hata wabunge wakiwa wanasikiliza wimbo wa Dr. Kikwete wa mafiga matatu sasa wacha wapikwe.

Baada ya muda wa kuburuzwa na kukaangwa naamini sasa wapinzani wakisimama na kusema wanaomba kura wananchi watawapa na kusahau kununuliw kwa pilau, unga , sh.500, pombe za kienyeji, khanga, sukari na ushabiki.

Madhara yake ni makubwa baada ya Uchaguzi na sasa wamesha ona nini maana ya kura. Wapinzani na serikali inahitaji kukaa na kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi ambazo kimsingi zinawabana sana wapinzani. JK anaweza kufanya hayo kwa nia njema kama kweli ana nia ya kuijenga Tanzania na kuwapa maisha bora.

Maisha bora yanaweza kupatikana pia chini ya upinzani mkali hapo ndipo kila chama kilichoo madarakani kitaweza kufanya kazi badala ya sasa ilivyo .

Kwa hiyo kwa maoni yangu haya naomba kutoa hoja .
 
Ndugu naungana na wewe huu ni muda muafaka wa kushinikiza mabadiliko ya katiba,badala ya kufanya maigizo ya uchaguzi mwaka 2010. Upo wasiwasi kwamba,Kwa namna JK alivyo,hatapenda kupunguza kura zake 80%(ambazo uhalali wake unahojika) mwaka 2010,atataka na naamini anatamani kupanda juu zaidi.Sasa badala ya kupoteza mabilioni ya fedha kwa kiini macho ingekuwa vyema vyama vya upinzani vikasisitiza mabadiliko ya katiba sasa.

Kwa taratibu za uchaguzi za sasa,matokeo ya uchaguzi mkuu ujao yanatabirika kirahisi mno.Tujiandae na asilima tisini amabazo hazitakuwa halali kama kawaida. Ni mjadala huu upanuliwe kuhusisha mgawanyo wa rasilimali katika vyama.

Ni hatari kuendelea kutuma ujumbe kwa watu kwamba mabadiliko hayataletwa kwa njia ya kura. Ndio, wapiga kura watapungua,lakini muda utakavyo ongezeka,na hali ikizidi kuwa mbaya,watu wataanza kufikiria njia mbadala ya kuleta mabadiliko.Nasema kila tunapofanya uchaguzi kwa mtindo wa sasa tunapandikiza chuki na uhasama na hali ya kukataa tamaa na demokrasia jambo amblo si zuri kwa mustakabali wa taifa letu.
 
Naona kicha cha topic hii kimeenda shule lakini lazima tuanzia mahali fulani kujadili.

Nadhani hiki ni kilio cha viongozi wengi wa upinzani Katiba Katiba Katiba.

Nakumbuka huko nyuma BWM aliwaambia viongozi wa vyama vya upinzani waseme ni mambo gani ndani ya katiba wanataka yabadilishwe, nadhani walienda kuisoma hiyo katiba na baada ya hapo waliamua kukaa kimya mpaka hii leo. Kwa mfano, rais ndiye anayeteua mwenyekiti wa tume ya uchaguzi lakini anatakiwa ateuliwe kutoka miongoni mwa majaji wa mahakama kuu au mahakama ya rufaa. Na mtu yeyote ambaye ni kiongozi wa chama cha siasa hatakiwi kwenye tume hiyo lakini wakati wa uchaguzi kila chama kinatakiwa kitume mawakala kwa idadi iliyo sawa.

Kwa hiyo kila chama kinakuwa na uwakilishi sawa kwenye uchaguzi. Pamoja na hiyo katiba kuna mambo ya kijamii ambayo yanakuwa vigumu sana kuepukika. Sidhani kama ni zoezi rahisi kumpata mwenyekiti wa tume asiye na mapenzi na chama chochote, kama kuna njia nyingine nzuri ni jukumu la vyama vya upinzani kutueleza ni kivipi wanataka tume ya uchaguzi iwe. Kwa hali ilivyo hivi sasa tunaweza kuamua kila chama kitoe wajumbe wa tume lakini at the end of the day watu wote wakawa wapenzi wa CCM au wakanunuliwa na CCM.

Kwa upande wangu bado naamini siyo katiba inayovifanya hivi vyama vishindwe labda sheria za uchaguzi zilizotungwa na bunge kwa mfano mambo ya takrima, najaribu kuzitafuta ili nizisome. Lakini kama alivyoeleza mtoa hoja muda ni sasa, wanatakiwa watueleze ni kivipi Katiba inawaathiri kwenye uchaguzi na ni nini mapendekezo yao nadhani siyo busara kusubiri karibu na uchaguzi na kuanza kulalamika bila hata kuwa na hoja zinazo support malalamiko yenu.

JJ tunakusubiri utupe maoni yako kwenye hili, na kama kweli lipo ni kivipi mliamua kuingia kwenye uchaguzi ambao Katiba au sheria za uchaguzi zitawafanya mshindwe?
 
Nina hoja mbili kwa kuanzia:
1) Sisi sote ni waathirika wa mfumo mbaya wa siasa zetu. Sasa basi tusiwaambie wapinzani tu wadai katiba. Ni jukumu letu sote. Nchi zote zilizofanikiwa kupata katiba nzuri za nchi zao haikudaiwa na wapinzani pekee. Mfano wa karibu kabisa ni wenzetu wa Kenya. Walioongoza na wanaoendelea kudai mabadiliko ya katiba Kenya ni Viongozi wa dini, Civil Society Orgnisations, Vijana, Vyuo Vikuu halafu ndo wanakuja vyama vya siasa. Tatizo letu ni pale tunapofikiri kuwa tatizo fulani si tatizo mpaka pale litakaponiathiri mimi.

Lazima tubadilike. Kwa kawaida wanasiasa wa kiafrika hawaoni mbali zaidi ya madaraka. Tukiwaachia wapinzani kudai katiba peke yao hawatadai zaidi ya tume huru ya uchaguzi. Naamini tatizo la katiba ni kubwa kuliko tume huru ya uchaguzi. Vyama vya upinzani na wadu tu katika mchakato wa maendeleo ikiwemo siasa na katiba. Sote tunawajibika.

1) hakuna kipya ambacho hakijulikani tunachokitaka katika katiba. Tuongelee kuinishikiza serikali kupeleka mswada bungeni wa ku-adopt mapendekezo yaliyokwishatolewa huko nyuma. Tuna mapendekezo kutoka tume ya Nyalali, Shivji na Jaji Kisanga. Ripoti zote hizi zilianisha kwa kina matatizo ya katiba yetu na mapendekezo ya kufanyika. Huwezi kuniambia leo Mrema atakuja na mapendekezo tofauti na yale yaliyopo kwenye hizo tume zilizoongozwa na watu wenye vichwa vyao.

Narudia tena, matatizo ya kisiasa ikiwemo katiba katika nchi yetu hayawezi kuwa ya wapinzani peke yao. Ni ya kwetu wote nasi sote tunawajibika kuyatatua. Kuwataka kina JJ peke yao walete hoja ni kukwepa wajibu. Sam tupe maoni yako pia.
 
Well said Kitila Mkumbo,

Unajua tatizo la watanzania walishazoea kila kitu kifanywe na mwalimu.

Sasa baba hayupo tunahitaji kujitegemea wenyewe,haya mambo ya kufikiri kuwa fulani yupo atafanya kitu yameisha au mambo ya katiba tuwaachie upinzani hayapo siku hizi, matizo ya watanzania tunahitaji kuyakabili sisi wenyewe.

Na mimi nafikiri changamoto kubwa kabisa kwa sisi watanzania ni kukuza demokrasia,
vijana wengi zaidi tunahitaji kutoka nje na kuanza kuwaelimisha vijana wenzetu umuhimu wa kushiriki katika siasa na hasa kujiunga na vyama hivi na kuvi support kwa kila hali.

Mimi nafikiri CHADEMA ina mtizamo na vision yao ni nzuri kwa siku zijazo.

Vijana tuamke.
 
Ndugu yangu CHINGWANJI mabadiliko ya katiba duniani kote hayafanywi na vyama vya upinzani pekee kama unavyofikiri.

Huwa yanafanywa na nguvu kutoka kwa wananchi, Trade unions, NGO'S Wataalamu wa helimu ya siasa na Uraia na vyama vya upinzani bila kusahau TZ MEDIA. Sasa Tanzania vyama halisi vya upinzani hakuna, NGO'S zipo za kwenye briefcase, Trade Unions ni kama hakuna TZ,MEDIA ndio kabisa mbovu na inanuka.

TZ MEDIA sasa imekumbwa na kimbunga kipya kinaitwa "Tsunami mtandao". Kama tutabakia na mawazo ya kale ya kusubili vyama vya Upinzani kudai Katiba walahi tutaingia kabulini bila katiba mpya. Suala la katiba inabidi wanachi wenyewe tulivalie chunga, vyinginevyo hakuna katiba mpya Tanzania.

CCM wanajua kuruhusu katiba mpya ni kifo cha CCM; sasa nani anakubali ajiue mwenyewe. Hao wapinzani unaowategemea kila kukicha wanarudi kundini (CCM), kutimilisha ile injili iliyoandikwa na Nabii Sumaye 4:18-19. inayosema ukitaka mambo yako yakunyookee lazima ujiunge/ urudi CCM.
 
Kitila Mkumbo

Naona hapa tunazungumzia vitu viwili tofauti. Nadhani wewe unazungumzia matatizo ya Katiba ambayo na mimi kuna mambo mengi ndani ya katiba siyaungi mkono kwa mfano muundo wa muungano na madaraka ya rais. Kama sijamuelewa vizuri mtoa hoja amezungumzia jinsi katiba inavyoathiri usawa kwenye uchaguzi.

Nimeisoma katiba kwenye vipengele vya uchaguzi kwa bahati mbaya sijaona uzito mpaka niseme hizo ndizo sababu zinazosababisha kutokuwepo na usawa kwenye uchaguzi na kuipendelea CCM. Ndiyo kuna mambo kama nchi inafuata mfumo wa ujamaa na kujitegemea kwenye katiba one can say ni sera za CCM kwenye katiba ya muungano, je kikiondolewa hicho kipengele kitaleta usawa kwenye uchaguzi?

By the way, how many people know that? Nadhani kama tunataka kujadili matatizo ya katiba hiyo ni topic nyingine kabisa mambo mengi kwenye katiba yamepitwa na wakati na yanatuathiri kisiasa na kiuchumi.

Anyway, mimi siishi kwa siasa ningependa kusikia wanasiasa wanathirika vipi na katiba kwenye uchaguzi.

Kwa mfano mimi kama mwananchi ambaye siko kwenye chama chochote cha siasa ninaweza kusimama kifua mbele na kusema Katiba hainitendei haki kwa kutoruhusu wagombea binafsi na kunilazimisha nimchague mtu toka chama fulani cha siasa. Pamoja na kunyimwa haki hiyo natambua hata nikipewa nitakuwa najifurahisha roho tu kwani bado nchi haijafikia sehemu mgombea binafsi akashinda kwenye urais labda ubunge.

Je, vyama vya upinzani vinasema nini? Kama tunataka tujadili matatizo ya Katiba nadhani hiyo ni topic nyingine kabisa na hizo tume za wana CCM ulizozitaja zilisema nini kuhusu hayo matatizo yanayozungumzwa na vyama vya upinzani?

Labda tu kama kuna mtu ana data atuwekee ripoti ya hizo tume hapa na sisi tuzisome.
 
jamani I am lost labda ninazungumza nje ya topic. Hebu niwekeeni hivyo vipengele ambavyo kinasababisha uchaguzi usiwe na usawa au tubadilishe topic kuwa "MATATIZO YA KATIBA". Naona wote mnachangia bila kueleza hivyo vipengele za katiba mnavyozungumzia, shusheni data wazee wa kazi.
 
SASA NIMEMAILIZIA MAONI YANGU:

Mimi sijawahi kuisoma sehemu ya katiba ya Tanzania inayohus uchaguzi. Hata hivyo hisia zangu ni kwamba inatoa mwanya mkubwa sana kupendelewa kwa chama kilichoko madarakani, na ndiyo maana CCM wamekuwa wakiwekea ngumu effor za kubadilisha katiba.

Tatizo kubwa sana pale kwetu ni kutokuwepo kwa tofauti kati ya serikali na Chaman tawala. Mara kwa mara viongozi wa CCM wamekuwa wakifanya mabo kama vile ni viongozi wa serikali. Miaka ya nyuma kidogo nilimsikia Bwana Maregesi akitaka DC aje kumpokea bila kujali kuwa DC ni kiongozi wa kiserikali na hatakiwi kuwa mwanasiasa. Kwa hali hiyo utaona kuwa viongozi wote wanaosimamia uchaguzi wameegemea chama tawala. Utaona vyombo vya habari vya serikali vinatumia na chama tawala freely, na viongozi wa serikali wanatumia rasilmali za serikali wakati wa kampeini bila woga wowote, na mbaya zaidi askari polisi wanatumiwa kuwanyanyasa opposition, nakumbuka Mzee Mahundi akitamba kuwa CUF watamtambua. sasa haya yote no mapungufu yatokanayo na Katiba yetu.

Baadhi ya mambo ninayoshauri kubadilsihwa ni kama ifuatavyo:

(1) Rais asiteue mawaziri ma RC, DC na mabalozi kutokana na wabunge.
In fact mad-DC, na ma-RC wasiteuliwe, hawa wachaguliwe na wanachi kusudi kuwafany wawe more accountable kwa wananchi.

(2) Rais asiteuwe wabunge wake wenyewe.

(3) Uteuzi wa Mawaziri majaji, makamanda wa polisi, na makamanda wakuu wa majeshi ukamilishwe na Bunge, Rais atoe pendekezo na bunge ndilo likamilishe uteuzi. Baada ya kupitisha na Bunge, Rais asiwe na madaraka ya kuwafukuza kirahisi bila bila kupata baraka za Bunge.

(4) Bunge liwe na uwezo wa kumvua Rais na viongozi wengine madaraka yao ikithibita kuwa utendaji wao haukufuata maadili ya madaraka hayo.

(5) Kuundwe tume ya utumishi wa serkali inayojitegemea; uteuzi wa tume hiyo ufuate utaratibu sawa na (2) hapo. Tume hii iwe na wajibu wa kuhakikisha kuwa wafanya kazi wa serikali hawaingizi siasa katika shughuli za serikali.

(6) Tume ya uchaguzi iwe huru; iundwe kwa kufuata utaratibu wa (2) hapo juu.

(7) Muundo wa serikali uandikwe kwenye katiba, yaani wizara na idara za serikali zijulikane kikatiba, siyo Rais akurupuke na kuunda baraza la mawaziri 100 ili kuridhisha marafiki zake.

(8) Viongozi wa serikali wasiwe na madaraka ya kutoa vyeo au kufukuza wafanya kazi wa serikali; shughuli hiyo iachiwe tume ya utumishi kwa wafanya kazi wa ngazi ya kati na ngazi ya chini, na bunge liwe na madaraka juu ya wafanykazi wa ngazi za juu kama vile makamishna wa idara na makatibu wakuu wa wizara kwa kushauriana na tume ya utumishi. Viongozi wa serikali wanaweza kupendekeza tu
 
Mzee Kichuguu umesahau kitu kimoja:
6) Waziri wa Serikali za mitaa asichague madiwani watatu kwa kila wilaya.
Huu ni Mswaaaaaaaaaada mpya kwa sasa upo njiani kuelekea Dodoma kupitishwa na Bunge.
 
Kichuguu na sam
Mmegusa mambo mazito na ambayo ni shida kubwa kwenye katiba ya Nchi .Mimi sioni haja ya Nchi ya Vyama vingi kuwa na Wabunge wa upendeleo ama kuteuliwa .Hili linaniumiza kichwa sana .Mbunge wa kuteuliwa na Rais kama Meghji na wenzake watalinda maslahi ya Rais .Mkapa alitumia vibaya nafasi zile kwa kuwahonga ama kuwarubini wapinzani maana akina Lamwai walifanya kazi ya Mkapa na CCM kisa wamepewa Ubunge .

Do we need wabunge wa kuteuliwa na Rais ?Teuzi zingine zote ni haramu na sidhani kama tunamhitaji Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa . Vyeo hivi ni vya kisiasa na vina madhara makubwa na kupelekea matumizi mabaya ya dola nk wakati wa Uchaguzi na hata wakati wa maisha ya kawaida .

Now nilisema Katiba kubadilishwa ili kumnyima Rais kumteua hata Msajili wa Vyama na Mkurugenzi wa Uchaguzi. Sheria za Uchaguzi ni chafu sana na ukizisoma utaona ninacho kisema . Nitajaribu kutafuta vipengele na kuja navyo muda ukiruhusu .

Ndiyo maana nimesema kwamba we need mabadiliko kwa kwa NGO, na vikundi vingine vya harakati vimebanwa na kuishia kujipendekeza na magazeti yanamlamba Dr.Kikwete miguu basi inakuwa kazi kubwa .Tujipange basi tumtafute wakili kama Mtikila twende Mahakamani kuomba haki maana tukisema tuitishe shule ya nguvu kwa wananchi watasema hatuna kibali na hatuna kikundi na tutashitakiwa kama wahaini .
 
Kwa kuongezea,tuondoe nguvu ya waziri mkuu au waziri wa TAMISEMI kufuta serekali za mitaa na kuweka tume. Mara kadha viongozi wamekuwa na tabia ya kutishia mabaraza ya madiwani kwamba wasipofanya kazi watafuta baraza na kuunda tume.Kazi ya kuwajibisha viongozi iwe ni ya wananchi wenyewe na si mtu mmoja.

Tuondoe kipengele kinacho kataza matokeo ya uraisi kupingwa.Hii inawapa watu kiburi kuiba kwa maana kwa sheria za sasa tume ikisha tangaza matokeo ya uraisi mtu hawezi kuyapinga.

Vyama lazima vitangaze vyanzo vya mapato yake.CCM irudishe mali za wananchi kama viwanja ambazo zilichangiwa na wananchi wote pasipo kujali itikadi.

Halufu suala la ushiriki wa NGO kwenye siasa liwe wazi,kwa mfano NGO mmoja kipindi cha nyuma ilifutwa kwa maelezo kwamba inajihusiha na siasa ila cha kushangaza kwenye uchaguzi wa viti maalum wa CCM kulikuwa na nafasi ya washindani toka kwenye NGOS(Jumuiya za kiraia),kulikuwa na wagombea toka NGOs mbamali ambapo mama sita alishinda.
 
Kwa kuongezea,tuondoe nguvu ya waziri mkuu au waziri wa TAMISEMI kufuta serekali za mitaa na kuweka tume. Mara kadha viongozi wamekuwa na tabia ya kutishia mabaraza ya madiwani kwamba wasipofanya kazi watafuta baraza na kuunda tume.Kazi ya kuwajibisha viongozi iwe ni ya wananchi wenyewe na si mtu mmoja.

Tuondoe kipengele kinacho kataza matokeo ya uraisi kupingwa.Hii inawapa watu kiburi kuiba kwa maana kwa sheria za sasa tume ikisha tangaza matokeo ya uraisi mtu hawezi kuyapinga.

Vyama lazima vitangaze vyanzo vya mapato yake.CCM irudishe mali za wananchi kama viwanja ambazo zilichangiwa na wananchi wote pasipo kujali itikadi.

Halufu suala la ushiriki wa NGO kwenye siasa liwe wazi,kwa mfano NGO mmoja kipindi cha nyuma ilifutwa kwa maelezo kwamba inajihusiha na siasa ila cha kushangaza kwenye uchaguzi wa viti maalum wa CCM kulikuwa na nafasi ya washindani toka kwenye NGOS(Jumuiya za kiraia),kulikuwa na wagombea toka NGOs mbamali ambapo mama sita alishinda.
 
Eric Ongara said:
Tuondoe kipengele kinacho kataza matokeo ya uraisi kupingwa.Hii inawapa watu kiburi kuiba kwa maana kwa sheria za sasa tume ikisha tangaza matokeo ya uraisi mtu hawezi kuyapinga..

Halafu tuoengeze transition period; baada ya Uchaguzi, tuwe na muda wa kutosha, kama mwezi mmoja kabla ya Rais kuapishwa ili kutoa mwanya kwa malalamiko yote ya uchaguzi kushughulikiwa kabla ya rais mteule hajaapishwa rasmi. Kwa sasa hivi anaapishwa siku mbili tu baada ya uchaguzi na hivyo kuwanyima nafasi watu wenye malalamiko kuhusu uchaguzi kutoa malamiko hayo.
 

Similar Discussions

18 Reactions
Reply
Back
Top Bottom