Mkuki Kwa Nguruwe (Kisa Cha Kweli)

SEHEMU YA 15


Ikapita wiki, kutokana na shughuli za kazi nyingi, nikawa kama nimeshamsahau rafiki yangu huyo, na nikawa na migongano ya hapa na pale ya kifamilia, ni kawaida, lakini safari hi ilizidi, maana mume wangu ratiba zake zikawa hazieleweki sio kama ilivyokuwa awali, tukawa tunabishana, lakini kwangu nilichukulia ni mambo na kawaida tu.

Basi siku moja nikapokea simu kutoka kwa huyo rafiki yangu, akaniambia kuwa anajiandaa kuondoka kwenda Zanzibar, kuna mambo muhimu anatakiwa kuyafuatilia

‘Mambo gani mbona mapema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Kuna jambo natakiwa kwenda kulifanya, natakiwa kukabidhi kabidhi ofisi, kwani inawezekana nikasafiri kwenda kusoma nje ya nchi…niliwahi kukuambia kipindi fulani kuwa niliomba kwenda kusoma, sasa imetokea kipindi hiki na mimi siwezi kuachia hiyo nafasi,…’akasema nilitaka kumuuliza na mtoto vipi, nikasita yeye akasema

‘Na uzuri..haitakuwa muda wote, nitaweza kulea na kusoma, mfadhili wangu kasema hilo halina shida..kwahiyo sitakuwa na muda wa kukabidhi, nikimaliza likizo yangu ya maternity, yawezekana nikaondokea huku….’akasema

Ilinisthua kidogo, ikizingatiwa kuwa mtoto bado mdogo, sikumuulizia sana kuhus mtoto,…. kwasababu hapa kati kati tulifikia sehemu hatuelewani na yeye kabisa, alichoka na maswali yangu na hata kufikia kusema niache kumfuta fuata masiha yake na mtoto wake.., kauli hiyo ikaniudhi sana, ikabidi kweli nimuache na maisha yake. Hata hivyo kiukweli, sio kwasababu hiyo, ila sikuwa na muda wa kukutana naye mara kwa mara, majukumu yalizidi sana.

Tuliongea kidogo kwenye simu …tukamaliza hivyo tu, na sikuweza kumpigia tena , na siku mbili baadae akapiga yeye, nahisi ni pale aliponiona nipo kimia, akasema;

‘Rafiki yangu vipi, nilijua utakuja, kabla sijaondoka, si nilikupigia simu jamani, sawa najua labda, bado umenikasirikia,… lakini utakuja kuelewa tu, baadae, …ila nilikuwa na ombi moja kwako, kwa vile wewe nyumba yako ina nafasi naomba baadhi ya vitu vyangu nije kuviweka kwako maana hizi nyumba za kupanga nikiondoka, vitakuwa havina usalama kabisa....’akasema

Kiukweli mimi sikuwa na hasira kihivyo, hasira zangu ni za hapo kwa hapo..na ukiniudhi naweza kufanya jambo kubwa hapo hapo…baada ya hapo, mambo yamekwisha, ila …kiukweli naweza kufany ajambo baya huwezi amini,..mimi kwa hilo nilishaliondoa nafsini kwangu sikuwa na kinyongo na yeye,..nikasema hakuna shida, nyumbani kwangu ni kwake, nikazidi kumsisitizia kwa kusema;

‘Wewe ni rafiki yangu bwana, hakuna haja ya kuniomba, hapa ni nyumbani kwako pia, watoto wanakuulizia kila siku, wewe lete vitu vyako na wewe kama mkataba umekwisha kwenye hiyo nyumba haina haja ya kulipia tena, njoo ukae hapa, mapak siku ukiondoka, ...’nikamwambia.

‘Hapana, sina maana hiyo, na sitaweza kufanya hivyo, urafiki wangu usiwe mzigo kwako, umeshanisaidia mengi sana, kiasi kwamba najihisi vibaya, na ..hata sijui nitawezaje kulipia hayo,…. ninachokuomba kwa sasa ni hilo tu....’akasema.

‘Sawa hamna shida, wewe vilete wakati wowote utakapopata nafasi, au nikipta nafasi, hata kama wewe haupo ninaweza kuja au kutuma gari likaja kuvichukua haina haja ya kusumbuka sana, ila nitajitahidi nije kabla hujaondoka..’nikasema, nikiwa na mambo yangu mengi shughuli zangu, na sikutaka kuongea naye zaidi, hasa kuhusu maisha yake alishasema hataki nikikutana naye tuyaongelee maisha yake, hasa kuhusu mtoto na aliyezaa naye.

Kesho yake nikapata nafsi nikaona nimpitie kidogom, nijua kinachoendelea, na kama vitu hivyo sio vingi, na kaviandaa, basi ninaweza kuondoka navyo, kwa kukodi gari, sikutaka kumpigia simu, mimi mwenyewe nikaenda nyumbani kwake…kwa mbali niliona gari kama ya mume wangu, lakini sikuwa na uhakika kama ilitokea kwake, au ilikuwa inapita tu, na mume wangu alikuwa kwenye mkutano.

‘Hivi mkutano ulishamalizika,..au kuna mtu kamtuma na gari lake…?’ nikajiuliza, nikataka kupiga simu kwake, lakini ikaingia simu ya mteja wangu muhimu, nikajikuta naipokea kwanza, na nilipomaliza kuongea naye , nikiwa nimesimamisha gari nyumbani kwa rafiki yangu,..nikawa nimeshaua kumpigia simu mume wangu

Rafiki yangu alikuwa kasimama mlangoni kwake kunikaribisha, nikamsogelea tukasalimiana kama ada yetu, nikaingia ndani na swali la kwanza likawa hili.

‘Mtoto kalala…?’ nikamuuliza

‘Ndio….’ Akasema ile ya kulazimishwa, sio sauti kama ile niliyo-izoea, halafu akauliza

‘Hujakutana na….’akasita,kwani simu yake iliita, akaisikiliza kwanza kwa muda, akasema

‘Nimekuelewa hamna shida, lakini niache kwanza, sitaki, sikiliza, nilikuelezea, msimamo wangu basi…’akasema na kukata simu.

Alionekana kama ana hasira na hataki kuongea, akawa kama anataka kuniambia jambo lakini anasita, nilihisi hivyo, ila na mimi nikasimamia kwenye msimamo wangu kuwa sitamuuliza tena kuhusu maisha yake na mtoto, …kwa jinsi alivyo nilijua ana tatizo.

Baadae mtoto akawa analia, kwahiyo akaenda kumchukua, na kumnyonyesha alipomaliza, akanipa nimpakate ili aniandalie kinywaji, ndivyo tulivyozoeana , nilitaka kujiandalia mimi mwenyewe, maana anajua mimi ni mpenzi wa sharubati ya baridi,… lakini akasema hapana

‘Wewe mpakate mtoto ..hujamshika tokea siku ile….’akasema na mimi sikukataa nikamchukua mtoto.

Unajua mtoto wa mwenzako hakawii, sasa anageuza macho, anangalia, na sura halisi inaanza kuonekana, sura haikujificha alikuwa akifanana kila kitu na watoto wangu, maana watoto wangu wanafanana, ni wale mapacha wanaofanana kwa kila kitu, mimi akilini nikaweza hitimisho kuwa rafiki yangu atakuwa atakuwa katembea na mdogo wa mume wangu. Hata hivyo sikuweza kuvumilia nikamwambia;

‘Hapa sasa haijifichi kitu, lakini tuyaache hayo, lini unaleta hiyo mizigo, au nitafute mtu tupakie, kukurahisishia kazi…’nikasema

‘Haijifichi nini, usianze yale mazungumzo tena, nimefikiria kwa makini nimeona, ni bora iwe hivyo, libakie kama tulivyokuliana basi… sasa ibakie utakavyofikiria wewe inatosha,..’akasema.

‘Hamna shida, isiwe taabu, sasa unasemaje…?’ nikamuuliza

‘Nilitamtafuta ,mtu, kuna mambo sijayaweka sawa, kuna mtu ananisumbua akili yangu, sipo sawa, ila nimeshukuru kuwa umafika….’akasema

‘Ok, sawa mimi naondoka…’nikasema

‘Kuna kitu nilitaka kukuambia, lakini bado sijawa na uhakika, nataka nipate ushahidi halafu tutaongea….’akasema

‘Kuhusu nini….?’ Nikauliza

‘Nataka uwe na amani na hili jambo tulimaliza kabisa….’akasema

‘Jambo gani…?’ nikamuuliza

‘Kuhusu huyo mtu niliyezaa naye….’akasema

‘Sijakuelewa bado…na usiumize kichwa chako kabisa,..kama hutaki nijue haina shida, ..mimi nakujali sana, sitaki uumie, uwe na wakati mgumu kwa ajili yangu,…mimi nina amani kabisa, sina kinyongo na wewe, naahamu una sababu yako muhimu tu y akufany ahivyo….’nikasema

‘Unajua mimi linanisumbua sana, nimejaribu kuliwazia tukio zima la siku ile sijaweza kulithibitisha,…sijawa na uhakika ilikuwaje…’akasema

‘Tukio gani…?’ nikamuuliza

‘La kuipata hiyo mimba….’akasema

‘Mhh..sikuelewi, ...usinidanganye rafiki yangu..wewe sio mtu wa kubakwa, wewe sio mtu wa kufanyiwa tendo bila rizaa yako, nakufahamu sana, kwa hilo usinidanganya....’nikamwambia, ni kweli rafiki yangu ni mbabe, mjasiri na anajiamini, anaweza kupambana na midume, hata kama ni kwa kupigana ngumi.

‘Kwakweli siku ile, nilizidiwa, na sijui kwa vile nilitaka iwe hivyo, ndio maana sikujali, hata hivyo nikuambie ukweli, sikuwa nimepanga itokee hivyo, sio siku ambayo nilisema leo nataka nikafanye hivyo, hapana, ...ilitokea tu , na huenda ilipangwa iwe hivyo, kwa kifupi siwezi kukumbuka siku ile nililewa...’akasema.

‘Ulilewa, ulianza lini kunywa…?’ nikamuuliza

‘Siku hiyo hiyo…na nilijuta …na mara pili, nikarudia tena, ..na kilichotokea ndio nikasema sitakunywa tena,…najuta…’akasema

‘Wewe mtu…..ina maana ukinywa pombe…na wewe uliwahi kuapa kuwa katika vitu ambavyo hutaweza kuvitumia kimojawapo ni pombe…?’ nikamuuliza
 
SEHEMU YA 16

‘Nimevunja miiko mingi sana ya kwangu, na kila nilichokifanya kwa kuvunja miiko yangu nimekuja kupata matatizo makubwa..hadi sasa sina amani…’akasema

‘Ilikuwaje maana wewe mwenyewe ndio umenichokoza, nilipanga nisikuulize tena, lakini umelianzisha wewe mwenyewe, utanieleza au niondoke, na nikiondoka sitaki tena kuniambia kuhusu maswala yak ohayo…’nikasema

‘Sawa kama umeamua hivyo, mimi nitakuambia ilivyokuwa siku ile, na wewe mwenyewe utajaza,…na naomba usije ukanilaumu,....maana wewe mwenyewe ndiye uliyenishauri...’akasema na mimi nikafurahi tukakaa na kuanza kuongea, na yeye alianza kusema hivi;

Siku uliponipa ushauri wako, moyo wangu ulianza kuwa na shauku, …nikawa na hamu sana ya mtoto kuliko siku zote,….nikawa nawaza sana kupitiliza mpaka watu wakanifahamu kuwa nina mawazo…niliwazia nikiwa nimempakata mtoto wangu, na hasa wawe mapacha….nilipata shida sana....’akatulia kidogo.

‘Unakumbuka ulivyoniashauri, nimtafute yoyote hata awe mume wa mtu nifanye naye tendo kwa minajili ya kupata mtoto, na nilijiuliza nitamuendeaje mwanaume bila..unajua mume ndiye anakutongoza, au sio..sasa nitakuwaje na uso usio na aibu….haraka nikasema kwanza labda nitafuta kitu cha kuniondoa aibu,…’akasema.

‘Ndio ukaenda kulewa…kwenye mabar, au ilikuwaje…nashindwa hata kukuelewa, kwanini usingeliniomba ushauri nikakuelekeza jinsi gani ya kufanya…’nikasema

‘Unajua rafiki yangu, kinachonishinda kwa hivi sasa ni kuhusu shemeji…’akasema

‘Nani, huyo bwana mliyezaa naye…?’ nikamuuliza

‘Ndio.....’akasema.

‘Kasemaje…? Nikamuuliza.

‘Ndio, kaniomba sana, tena sana hata kulia, hata kunipiga magoti, kuwa nisimwambie yoyote kwa sasa iwe siri kubwa kwani kuna mambo kayagundua yanaweza kumleta matatizo kwenye familia yake….’akasema

‘Ni sawa,…hata mimi nilikushauri hivyo, je labda mkewe keshamuhisi vibaya au….?’ Nikamuuliza

‘Anasema…kuna mambo yake ya kifamilia, ambayo hataki yaharibike, na ikigundulikana kuwa ana …mtoto nje, atayaharibu..ok, mimi nilion ni jambo la maana, kama na yeye kakubali iwe hivyo itakuwa ni heri kwangu…ila kwa masharti kuwa anataka mtoto atambulikane kuwa ni kwake kwa siri..hapo ndio tukaanza kukorofishana,...’akasema.

‘Unakubali nini na unakataa nini, kosa umelifanya wewe mwenyewe, kwanini toka mwanza usingelimdanganya kuwa mimba sio yake,..hii inaonyesha kuwa ulitaka afahamu, na huenda ulifanya hivyo kwa dhamira fulani ambayo unaogopa kuniambia...’nikasema na yeye akainama chini kuashiria kuwa kauli yangu umemgusa moyoni.

‘Kwa hali kama hiyo nimeona nisimwambae yoyote ....shemeji kaniomba na mimi nikamuahidi iwe hivyo, kwa masharti kuwa na yeye asinifuate fuate tena..lakini naona yeye kaanza kuvunja ahadi, kila siku hodi, na mbaya zaidi ananunua vifaa vya mtoto..sipendi, na ndio maana ilipotokea nafasi hiyo ya kusoma mimi nikaikubali kwa haraka sana, na sijamwambia kuwa mimi nakwenda kusoma nje....’akasema.

‘Kwahiyo eeh, unajua mimi unaniweka kubaya, …mimi naona nikuache na mambo yako, kwani kila hatua unanitamanisha intake kumfahamu huyo shemeji, na hutaki kuniambia ni nani…tuyaache kama ulivyosema au…?’ nikamuuliza nikiwa nimekunja uso kwa hasira.

‘Mimi nitakuambia jinsi ilivyotokea siku ile...au niache maana wewe unakimbilia kumjua huyo shemeji lakini hutaki kujua ilitokea vipi, nataka ufahamu ilivyotokea, ili uone kuwa sikuwa nimekusudia siku ile,…japokuwa tulipanga iwe hivyo, lakini sio kwa huyo na …hata sijui, nisemeje ndio maana nataka nikuelezee ilivyo kuwa na sio alzima nikutajie kwua ni nani...’akasema

‘Sawa hebu elezea, uonavyo wewe… maana na wewe sasa unajifanya mtunga tamithiliya, wengine hawapendi vitu virefu, sawa mimi sijali ila unipe kitu cha ukweli, sio hadithi za kubuni...’nikasema kutoka moyoni hadi hapo sikuwa na dhamira yoyote mbaya dhidi yake, sikua na wazo kuw ahuyu mtu anaweza kunifanya chochote kibaya, yaani sijui kwanini ilitokea hivyo, maana pamoja ya kuwa ni rafiki kwangu mimi nilishamweka kuwa ni ndugu yangu…moyo wangu umejengwa hivyo kuamini watu.

‘Baada ya ule ushauri wako, nikajikuta nakutana na wanaume wale ambao wana watoto ninaowapenda, nilijipangia kama karatiba fulani, ..ni ngumu lakini…kwahiyo ikawa inatokea awali, kwa huyo na yule lakini ghafla ikaja kubakia kwa huyo mtu mmoja, bila hata kukusudia,…

Cha ajabu sio kama awali wengi wakinialika kwenye chakuala cha jioni, inaishia kula na kunywa kidogo basi, tunaagana imekwisha, nahisi walishanisoma, na wengi hawakutaka kuniomba tufanye lolote zaidi ya hapo, ni ile raha ya kukaa na mimi kula kuongea, inaishia hapo tu,…na mimi sikuweza kushinikiza ili lifanyike hilo tendo, siwezi, ningalianzaje..na hata kwenye akili yangu bado nilikuwa na shaka...’akatulia.

‘Kwahiyo baadae ndio akabakia huyo mmoja ambaye hutaki kumsema, japokuwa mimi nimeshamfahamu kuwa ni nani, au sio… shemeji yangu wa ukweli.. au sio..?’ nikamuuliza huku nikicheka.

‘Ndio, sijui ilitokeaje, …ilikuwa kila nikienda kupoteza mawazo, shemeji yumo..ni kama ananifuatilia nyuma, utafikiri alikuwa ananilinda, au hata sijua ni kwanini alikwua akifanya hivyo, na ndiye niliyekuwa nikijaribu kumkwepa kuliko wengine, lakini haikuwa rahisi, kila nikitaka kutoka shemeji yupo nyuma, akiona sina mtu, anakuja kunipa pambaja,…nikaanza hata kuogopa, nikifahamu ukaribu wangu na mkewe, na familia kwa ujumla....’akasema.

‘Ok,…tuendelee..’nikasema.

‘Lakini mimi naona tuache tu kuyaongelea haya,…’akasema

‘Umeshaanza, siwezi kuondoka mpaka uelezee, hapo utaniuzi, hatutaelewana…’nikasema

‘Sawa, ngoja niendelee, maana hata mimi sijawa na uhakika, ni kwanini litokea hivyo na je ni yeye kweli,..nachanganyikwia ndio maana sina raha na kwanini ilitokea siku zote mbili, ilikuwa kama….haa, hata sijui nisemeje,....’akasema.

‘Sawa endelea ilikuwaje, ...kwani naiona hiyo sasa ni tamithilya fulani , kuna kitu unanificha na nitakigundua tu,...’nikasema.

‘Ofisini kwangu kupo karibu sana na ofisi za shemeji..’akasema.

‘Ok…ni sawa, ...ndio maana ilikuwa ni rahisi sana, kwako wewe ..mmh najaribu kujiuliza ni nani pale anafanana na mume wangu, mbona wengi wanaofanya kazi pale nawafahamu hata huyo mdogo wa mume wangu yupo karibu sana…ok..na upande huo wa pili yupo mume wangu,…, sasa naanza kuelewa, tuendelee..’nikasema na yeye akaniangalia huku akijaribu kutabasamu lakini uso ulikuwa umejaa huzuni.

‘Ndio ni kweli ndio maana ilikuwa ni rahisi sana kwake.., kuniona nikitoka, na niliona kama kadhamiria kufanya hivyo, na mimi hata nilivyojaribu kumkwepa ikawa haisadii, nikaona isiwe shida, kwanza ni mtu ninayemwamini hawezi kunifanyia lolote baya na anafahamu kabisa kuwa mkewe ni mtu tunayefahamiana sana naye...’akasema.

‘Mhh, ndio nafahamu si mlikuwa mashoga kipindi fulani na mkewe.., nikafikia kukukanya kuwa huyo mwanamke haaminiki, anajaribu tu kuficha ule ubaya wake , ili uone ni kawaida tu…maana kama angelikuwa rafiki wa ukweli, asingelikuibia mchumba wako, …mara nyingi marafiki wanaweza kuwa hivyo, unatakiwa rafiki awe kweli rafiki mnayeaminiana, ambaye huwezi hata kumdhania ubaya, au sio..?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukubali, hakusema neno

‘Ni kama mimi na wewe, mtu hawezi kuniambia kitu kibaya kuhusu wewe, najua huwezi kamwe kunifanyia mabaya, kama mimi nisivyoweza kukufanyia mabaya, mtu kama humfanyii mwenzako ubaya, huwezi kufanyiwa ubaya, au sio..itakuwa ni ajabu sana wewe ukinifanyia ubaya, au sio…....’nikasema na yeye akatabsamu na kusema.

‘Mhh, mabaya kama yepi tena rafiki yangu, wakati mengi tunafanyiana baada ya kushauriana…?’ akaniuliza

‘Kama aliyokufanyia yule rafiki yako, mtu unamuamini, halafu anakuja kukuibia mchumba wako…kiukweli inauma, kuibiwa mume au mke, unajua inatokea kama nilivyokushauri,au sio, na huwezi kumfanyia rafiki yako, mpendwa,, ni lazima utafanya mbali kabisa,…maana kama ni rafiki yako, mtaumizana sana…’nikasema

‘Mhh…hapo sasa…’akasema, akijikuna kichwa, halafu akajaribu kutabasamu na kusema;

‘Nimewaza sana hili…..naona bora ….nikuambie tu, ilivyotokea…’akasema

‘Ikawaje hebu endelea bwana, acha kusua sua, usinipe ugonjwa wa moyo….’nikasema

‘Basi kutokana na hali hiyo, kuwa mke wake namfahamu, ni mtu tunaheshimiana, nikaona nisimzalilishe, maana kama unavyonifahamu, huwa simkopeshi mtu, huwa siogopi mtu, kama sitaki sitaki...naweza nikamtolea nje mbele za watu akabakia kuzalilika na nisingeliweza kufanya hivyo kwa shemeji....’akasema.

‘Ni kweli mimi nakuaminia,ndio maana hilo lililotokea siwezi kuamini kuwa lilitokea bila ya ridhaa yako, wewe utakuwa ulikubaliana nalo, vinginevyo kuna kitu unanificha, na sipendi unifiche kitu, maana nikigundua, haaa..weee, si unanijua nilivyo, mume wangu mwenyewe ananiheshimu kwa hilo, ananiogopa, ndio maana anajitahidi kuwa mkweli kwangu, kama nilivyo kwake...’nikasema.

Hapo akatulia kidogo kama anawaza jambo, baadae akaendelea kunihadithia…

‘Ikawa kila nikitoka kwenda kula jamaa huyu hapa, nikitoka kwenda kazini, jamaa huyu hapa, ikawa kila siku nakutana naye, nikajikuta sina raha, na hata yeye akaliona hilo,…lakini akaniambia niwe na amani, atajitahidi kuhakikisha hatuvunji heshima yetu, …kiukweli hata lile wazo likafutika, sikutaka tena,… lakini moyoni...nilikuwa unanijia ule ushauri wako,na nikawa natamani ufanye kazi, lakini sio kwa huyo mtu, mume wa mtu, siku zinasogea...’akatulia kidogo.

‘Endelea…nina muda kidogo…ila najiuliza kwanini ulipoteze muda kwa huyo mtu, maana hapo ulikuwa unajichora kwa watu, walikuona, wanakuona au sio, kwahiyo hadi hapo wana ushahidi bayana ….hapo eeh, uliharibu…’nikasema

‘Kwa vile ni jamaa, ambaye…ni..ni .. shemeji yangu, sikuona tatizo, na ..unajua nisingeli…mkatalia hata chakula, japokuwa awali nilikuwa nafanya hivyo….’akasema

‘Ok nimekuelewa, sasa nikuulize katika wanaume wote wewe uliona huyo ndiye anakufaa au kwa vile ulihisi atakuzaliwa watoto sawa na wakwangu au…?’nikauliza

‘Kiukweli ndio hivyo, kama ungelianiambia nichague ni nani wa kunipa mimba, kama hakuna kikwazi, mimi kutoka moyoni, ningelimchagua yeye....lakini kutokana na ukaribu ulivyo hapana, sikupenda litokee kwake, lakini ndio hivyo, watu husema litokee ili liwe fundisho,...kwakweli hadi sasa siwezi kuamini, sikujua kabisa kuwa nitakuja kuzidiwa kiasi hicho…ni pombe, sitarudia tena…’akasema.

‘Hebu kwanza nikuulize yule jamaa anakunywa, unajua mimi simpafahamu vyema maisha yake, na unijuavyo huwa sifuatilii maisha ya watu wengine hata mke wake hatupo karibu kihivyo, japokuwa ni mke wa shemeji yangu…?’ nikamuuliza


‘Anakunywa lakini sio kihivyo….’akasema

‘Mhh, hawa wanaume jameni…. unajua nilikuambia hata mume wangu anakunywa, lakini akiwa na wazee, watu wa heshima wa dini, anajifanya mtu wa dini sana, na kupinga ulevi,....mimi nafahamu siri yake, uzuri wake hata akinywa huwezi kufahamu, anajitahidi sana kujificha…, nimemkanya sana tabia hiyo ya kunywa pombe…, yeye anasema anakunywa kwa dharura, na kidogo sana…’nikasema

‘Wanaume wengi wapo hivyo….sioni ajabu kwake,…’akasema.

‘Ilikuwa sio sana kama ilivyotokea baada ya kunipa huo ushauri, mwanzoni nilikuwa nakutana naye, anaiomba tukale chakula pamoja, tunaongea,…ananishauri kuhusu maisha, ni nani angelipenda awe mume wangu,…nikawa nimezoeana naye sana, nikiwa sina raha, yeye anipa ushauri , lakini sikuwa na wazo jingine lolote dhidi yake, na yeye alilitambua hilo...’akasema.

‘Mambo ya shemeji hayo , nafahamu sana ulichompendea, ni kw vile kwanza ni mtanashati,…. mrembo kama mume wangu, wanafanana sana, na mume wangu, kwahiyo nahisi ndio sababu ulimpendea hivyo au sio..?’ nikamuuliza..

Kwanza akaniangalia kwa makini, halafu akawa kama anasita kunijibu baadae kwa shingo upande, akiwa kainamisha kichwa akasema…..

Nb….naona inazidi kuwa ndefu na muda umekwisha, ngoja niishie hapa kwa leo


WAZO LA LEO: Urafiki wa kweli ni ule wa kuangalia athari za kila jambo kuwa unalolifanya halitamkwanza mwenzako,... ni hilo litafanikiwa pale utakapojiuliza je, kama nitafanyiwa mimi jambo kama hilo nitafurahia au nitachukia. Tukiwa na tabia hiyo ya kuchuja matendo yetu kwa wenzetu nina imani kuwa hatutachukiana, tukumbuke kuwa ubaya kwe wenzetu unauma kama vile tungelifanyiwa sisis, kwani mkuki sio nguruwe tu, na kwa binadamu mchungu.
 
SEHEMU YA 17

‘Kumpenda kwasababu hizo,…mhh…naomba uwe na stahimili…sitaki nikujibu swali lako kihivyo…hilo la kupenda lipo wazi,…maana mengine yanaweza kuja kuwa kuni,…lakini si wewe mwenyewe umetaka, na nataka nikisafiri niwe na amani, au sio…sasa mimi nakuomba unisikilie kwa makini…nikuelezee ilivyotokea, …tafadhali…’akasema

‘Sawa uonavyo wewe uwanja ni wako, au sio…..lakini mimi nimeshajua kuwa ni nani unayemzungumzia, ni nani baba wa mtoto wako, hilo sina shaka,..na hata mume wangu japokuwa hataki kuliongelea hilo, eti anadai hayo ni mambo yetu hayamuhusu, lakini kwa namna fulani, anakubaliana na wazo langu….’nikasema.

‘Ina maana mlinijadili, ..si ulisema hutaongea naye sana kuhusu siri zetu…?’ akaniuliza

‘Tuliongea, yale ya kawaida, si lazima mtu aulize baba wa mtoto wako ni nani, na lazima wengi wataniuliza mimi, kwa vile mimi ni rafiki yako, na nimeshajipanga jinsi gani ya kuwajibu,..lakini kwa mume wangu nilitaka nichukue tahadhari, jinsi gani ya kumjibu, umenielewa hapo…’nikasema

‘Ok, sawa…’akasema

‘Kwani hajafika kukuona…alisema akipata muda atafika kwako, hajafika…?’ nikamuuliza

‘Keshafika…’akasema

‘Mhh, alikuuliza….kuhusu mtoto…?’ nikamuuliza

‘Mhh…ndio…lakini …tuliongea, …’akasita

‘Najua, …mume wangu sio muongeaji, sana, hawezi kukudadisii kivile, baba yake ni nani, una matarajio gani, mengi anajua tumeshaonge, namfahamu sana..’nikasema


‘Sawa….utakuja kuelewa huko mbele ya maelezo yangu, kama utavuta subira…’akasema

‘Aaah, kama leo umeamua kunisimulia ukweli, nipo tayari kuvumilia mpaka umalize, nitafurahi sana…moyo wang utatulia,…’nikasema;

Tuendelee na kisa chetu…

***********

‘Basi siku ile, ya tukio la kwanza ilikuwa kama bahati mbaya, au ndio niseme ilipangwa itokee hivyo, kwani siku ile kulikuwa na sherehe ya kampuni yetu, huwa tunafanya hivyo mara kwa mara kwa namna ya kujitangaza, na kuwapa pongezi wafanyakazi kwa kazi fulani iliyofanikiwa….’akasema

‘Na sherehe kama hizo, familia inawajali sana familia na wafanyakazi, maana bila ya wao, wafanyakazi hawawezi kufanya kile walichofanya, tuna msemo hapo kazini kwetu kuwa juhudi ya mtu huanzia, nyumbani kwake…waingereza wanajua sana kuwale wafanyakazi wao…wajanja sana….’akasema

‘Ni kweli hata mimi najitahidi kuwafanyia hivyo wafanyakazi wangu….’nikasema

‘Basi kila mtu alipewa nafasi ya kuwaalika wanandoa wenza wao, na kama huna mwanandoa mwenzako, basi uje na mpenzi wako anayetambulikana, sio muhuni tu,…na wengi wanajulikana, hakuna siri hapo kazini kwetu,..au kama huna hata mpenzi, basi tulipewa nafasi ya kuja na hata ndugu yako..ilimradi kuwe na namna ya kupongezana kifamilia, na kijamii zaidi…’akasema.

‘Na wewe ukamualika nani, …hahaha, najua ulimualika yeye, au sio…?’ nikajikuta nimemuuliza hivyo…nitamani asema ndio, ni yeye, lakini haikuwa hivyo….ila akilini mwangu nilishajua kuwa ndio huyo ninayemfikiria mimi.

‘Sasa cha ajabu siku hiyo sikuwa na mtu wa kumualika,..unajua tena wapenzi wangu walishaoa,..na nilikuwa kivyangu zaidi,…na siku hiyo,..sikuhitajia mtu, nilikuwa na yangu kichwani…’akasema

‘Mhh..kweli hilo…’nikasema

‘Kabisa kabisa sikutaka kuwa na mtu, nilikuwa nimetingwa na mawazo yangu maana siku zinakwenda, lile zoezi tulilolipanga halifanikiwi,…naona kama wanaume wannikwepa, na ninaokuwa karibu nao, siwezi kufanya nao…yaani ikawa shida, na sikutegemea kuwa itakuwa vigumu hivyo.

‘Yah..kiu ukikidhamiria inakuwa hivyo…’nikasema

‘Ila kwa siku hiyo, kiukweli… nilitaka nisiwe na mtu karibu yangu anayeweza kunigusa…kunipa mawazo..nilitaka niwe peke yangu …, nilitaka hata kuwepo nisiwepo kwenye hiyo shughuli…, lakini ningeonekanaje na mimi ni mmoja wa mabosi wa vitengo, hapo nilipoajiriwa,,

Kwahiyo siku hiyo nikaingia kwenye ukumbi kivyangu, sikuwa muongeaji siku hiyo niliwaambia wenzangu kuwa sitaongea kabisa, ..niliwaambia naumwa, …najisikia vibaya, na wenzangu walinielewa, wao wakaongea, walichoongea, na akili haikuwa hapo kabisa....’akasema.

‘Wakati nimekaa naongea na wafanyakazi wenzangu, ..kikiwa ni kipindi cha kula na kunywa,…wenzangu wakawa wananitambulisha familia zao, na wale waliokuja na watoto wao wakawa wananionyesha watoto wao,..basi hapo ndio nilikuwa sipataki…sio kwamba siwapendi watoto, wewe mwenyewe unanielewa, ila hisi fulani ndani kwa ndani…’akatulia

‘Nakuelewa sana…’nikasema

‘Mtu akiwa ana familia, ..anaweza hata kujingiza kwenye shirki, sio kwamba anataka,…maana inaumiza ndani kwa ndani, na huwezi kuelezea hilo labda liwe limeshakufika…

Basi, wakawa wakinionyesha watoto wao, najitahidi kuwaonyesha ile hali yangu ya kupenda watoto lakini moyoni naumia,…na mpaka ikafika muda…, najiuliza ni kwanini, wote hapo tupo umri mmoja wana familia zao, na wengine nimewazidi, lakini wameshabahatika kuwa na familia zao, kwanini mimi....kwakweli niliumia sana, hadi nikajikuta machozi yananitoka,...na kabla sijaonekana nikainuka …

‘Nilikimbilia washroom, kunawa nikiwa na maana nikitoka huko, sirudi tena kwenye sherehe, naondoka zangu kulala, na siku hiyo sikutaka kabisa kugusa kilevi, nilishadhamiria kuacha kilevi kabisa, niwe huru, niwe tofauti..…,

Sijui nilikaa muda gani, ila nililia sana,…sijui,..nilimlilia mungu wangu..sana, na kama mtu angeliingia akanigusa,..sijui…nilikuwa sio mimi… na nilipohakikisha machozi yamekwisha, nikatoka mle ndani,…, nikarudi pale mezani kwangu kwa nia ya kuchukua mkoba wangu, niondoke zangu…lakini haikuwezekana.

‘Kwanini…?’ nikamuuliza

*********
‘Wakati nimetoka chumb cha kunawa, niliona mtu mgeni mezani kwangu…’akasema

‘Mhh, hapo hapo,….’nikasema

‘Tulia basi…’akasema

‘Kwasababu alinipa mgongo sikuweza kumtambua kwa haraka, na akilini mwangu sikutaka …kuongea na mtu, kwahiyo sikutilia maanani, nikawa nakwenda mwendo wa haraka kwenda kuchukua mkoba wangu, na sikutaka kuaga…’akasema

‘Ok…’nikasema

‘Pale nilihisi machozi kama yanataka kunitoka tena,..nikajikaza ki-kike…na..niliposogea nikashikwa na butwaa, sikutarajia kabisa,…’akasema

‘Una maana ni …huyo bwana’ko...?’ nikajikuta nimemuuliza maana kwa muda ule nilikuwa nimetekwa na hisia za huruma, kama nilivykuambia awali rafiki akiumizwa na jambo ni kama mimi niliyeumizwa, kwahiyo hata mimi pale nilitamani kulia, lakini nikawa namuuliza maswali ilikupotezea….

Kiukweli usichanani kwetu ilikuwa hivyo, ikitokea tatizo la kuumia, kulia, kuhis jambo kwa mwenzangu na mimi nakuw ahivyo hivyo..sijui ilikuwaje, kwa watu wasiotufahamu wakituona walihisi sisi ni mapacha…maana kama ni tukioa la kulia, tutalia sote…mmoja akiwa na furaha, basi tunafurahi sote, …kwahiyo maneno yake hayo hapo yalinifanya nitoe machozi na mimi….sasa uone kiasi gani tulivyokuwa tumeshibana.

Yeye hakujibu hilo swali mara moja…, muda huo alikuwa kimia kidogo, nahisi alikuwa akiwazia mbali,..basi ili kumpa unafuu, nikauliza swali la kumtoa hapo alipo

‘Si huyo bwanako mliozaa naye, au…?’ nikauliza hivyo kumchochea, nafahamu hapendi kuambiwa hivyo, na kweli, akainua kichwa na kuniangalia huku akisema kwa jaziba;
 
SEHEMU YA 18


‘Huyo sio bwanangu bwana,…mume wa mtu atakuwaje bwana’ngu, …!’akasema kwa sauti ya kukereka…!

‘Nauliza ni huyo aliyekupa huo ujauzito, au huyo unayefikiria kuwa ndiye aliyekupa mimba…, maana awali umesema huna uhakika,…na mpaka sasa hujaelewa, nakushangaa, ina maana ulipewa madawa ya kulevya au ilikuwaje …..hahaha mtu wewe, yaani wanificha hata mimi, haya ngoja tuone unataka nini ….?’ Nikamuuliza, hapo akatikisa kichwa tu.

‘Sio hivyo rafiki yangu, hujui nipo kwenye wakati gani sasa, unajua ..nilijua baada ya kumpata huyu mtoto, akili yangu itatulia,…nilijua kila kitu kitakwenda sawa,..lakini nashangaa sana,…nakuwa na wakati mgumu kuliko…lakini yote haya ni sababu ya ….anataka mambo ambayo …we acha tu…’akasema

‘Una maana gani hapo…?’ nikamuuliza

‘Nitakuja kukuambia tu…., wewe si unataka nikuambie…u-ukweli, subiria sasa, ila nakuomba tafadhali uwe na subira,…tafadhali sana, wewe ni rafiki yangu na hili tulilipanga pamoja, au sio..’akasema

‘Kwanini unasema hivyo..?’ nikamuuliza nikimuangalia moja kwa moja usoni, yeye akanikwepa na kuangalia pembeni.

‘Lakini si wewe umeamua tuvunje yale makubaliani yetu moja baada ya jingine…ulisema iwe siri, sasa unataka nikuambie ukweli, haya, au niache…?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho ya kutia huruma

‘Ndio, nataka uniambie kila kitu,…wewe ndiye ulianza kuharibu, sasa endelea, nautaka sana huo ukweli,…, wewe ni rafiki yangu nilijua utaniambia tu,…huwezi kunificha jambo hata siku moja, … au sio....ila kauli yako inanipa mashaka, nahsi kuna jambo baya lilikutokea unaogopa kuniambia kuwa labda na mimi nitaumia, usijali, wewe niambie tu..…haya endelea, mimi sina wasiwasi na wewe, wewe ni ndugu yangu, kama kuna jambo limekutokea, siwezi kukutupa kamwe, niambie tu ilikuwaje…’nikasema

‘Mhh, wewe wasema tu, kwa vile hujausikia huo ukweli…lakini sina jinsi inabidi nikuambie tu…ila sitakuambia ni nani , ni wewe mwenyewe utamfahamu…kutokana na maelezo …sasa utakaloamua, sina jinsi…’ akasema na kugeuka pembeni.

Niliwaza huyu mtu ana maana gani, nikajikuta nasema

‘Wewe endelea bwana…acha kuniweka roho juu…’nikasema

‘Kumbe mjamaa alishafika muda, kwani nilimkuta anakula, sikujua kuwa nilichelewa sana chomba cha kunawia mikono, ni kweli nilichelewa nikiwa nimezama kwenye mawazo, mawazo ya mitihani niliyo nayo…ok, ndio hivyo….’akasema

‘Basi nikamkuta jamaa anakula...pembeni kilevi…nikajua ehee…kazi ipo leo,..sijui ni nani alimualika, maana mimi sijafanya hivyo, …japokuwa wengi pale ofisini walishaniona nikiwa naye, na wanajua ni nani kwangu, …na sijawahi kusikia mtu akiniongelea vibaya dhidi yake, maana wanamuheshimu sana…na, wanamfahamu kuwa ni mtu mstaraabu tu…’akasema

‘Yule..hahaha, mstaarabu, au maana ya ustaraabu hamuijui nyie, acha bwana, hata wewe unamuita hivyo,…hahaha, ..labda , kwasabbu ulishapenda, utasemaje, ukipenda chongo utaita kengeza au sio, hahaha, hata hivyo sikulaumu,…’nikasema

‘Ndio kupenda, nilipenda, kama nilivyowahi kukuambia awali lakini nilishaweka mpaka, kwa vile ni mume wa mtu..nielewe hapo….’akasema

‘Nakuelewa sana, mimi ninachokataa ni kumuita eti mstaarabu,…hana hiyo sifa kabisa,…labda, maana mtizamo wa watu, unatofautiana,…nikuambia kitu, na nilishawahi kukuambia, unakumbuka nilikuwambia huyo jamaaa alifanya nini kwangu…ananitongoza mimi, shemeji yake mke wa kaka yake, nilichomuambia hajawahi kurudia tena…’nikasema.

‘Mhh…sawa nakuelewa, ulishaniambia bwana, hayo tuyaache, …ngoja niendelee au…?’ akaniuliza

‘Sawa endelea, …lakini usimvike sifa hiyo ya ustaarabu, hamtoshi….’nikasema

‘Utakuja kuelewa tu kwanini nasema hivyo…’akasema

‘Sawa endelea….’nikasema


‘Kwanza, nilitaka nigeuze , niondoke, ..kabla hajaniona, lakini macho ya watu, waliniona na yeye alipoona watu wanaangalia upande wangu, akageuka akaniona..ikawa haina jinsi, …nikasalimiana naye, naye akanikaribisha nikae utafikiri yeye ndio mwenyeji, mimi nikamwambia najisikia vibaya nataka kuondoka.

‘Aaah,…mimi nipo nitakupa dawa…’akaanza utani wake, unajua kuna kitu kimoja nilimpendea, anajua kumfariji mtu…na hata kama ulikuwa huna raha, utatulia tu, mna bahati sana mlioolewa….’akasema

‘Hata mume wangu ana tabia hiyo, ila kuna muda, akiwa na mambo yake, …hataki kusema, anaumia ndani kwa ndani, yeye akikuona upo huna raha, atakudadisi mpaka basi, lakini yeye, akiwa hana raha, ngumu kujua labda awe anataka kukuambia, anasema kuna mambo mengine ya kiume, sio lazima kumsumbua mkewe, basi, mimi najionea sawa tu, ila kiukweli hatufichani, …ndio hivyo tena, siku hizi, sijui uzee…’nikasema

‘Eti uzee, unanitisha mimi, una uzee gani….’akasema

‘Mkiishi sana na mwenzako, unajionea kawaida, hata ile …raha ya usichana inakuwa haipo, utaolewa utajionea wewe mwenyewe…’nikasema

‘Basi mimi nikazidi kumsihi kuwa najisikia vibaya yeye aendelee tu, …mimi naondoka kurudi nyumbani,…unajua alisema nini….’akawa kama anauliza

‘Yaani hiyo tabia gani,…mimi mgeni wako nimekuja, kwa ajili yako…, mwenyeji wangu unataka kuondoka, haiwezekani, kaa angalau kidogo, nimalize kinywaji, ..na hiki chakuka, ..au niaviache…?’ akauliza akiashiria kwa mkono pale mezani, uzuri pale mezani hakukuwa na mtu mwingine, watu walishajichanganya huku na kule,

‘Hapana wewe endelea tu wapo wengine mtaendelea nao, usiwe na shaka jisikia upo nyumbani…’nikasema sasa nikidhamiria kweli kuondoka.

‘Mimi wengine siwajui, nimekuja kwa ajili yako…nimekuja kukupongezeni, …na mimi ninayemfahamu hapa ni wewe…au nimekosea kuja, basi kama unaondoka, nikuombe kitu kimoja, wewe si unaumwa, subiri nimalizie hiki kinywaji nitakupeleka nyumbani kwako, vinginevyo ukae, au…?’ akaniuliza

Basi nikaona sio vizuri..nikaa kidogo, na yeye akaendelea kunywa, nilishangaa kumuona shemeji akinywa kwa pupa siku hiyo ,… sio kawaida yake, ni kama alikuwa na kitu kinamkera,…hata sielewi… mpaka nikaingiwa na wasiwasi , kwanini anakunywa hivi.…’akasema

‘Lakini yule ni mlevi, anakunywa sana, hata kaka yake aliniambia, labda akiwa kwako ndio anajivunga, haya ikawaje, …?’ nikamuuliza


‘Nikamtahadharisha kuwa kunywa kwa namna ile mimi sikupendi, anaweza akazidiwa ikawa shida kwangu, nikamwambia mimi naondoka,….akanizuia, akisema hii moja basi, hii moja basi..basi moja baada ya nyingine…’akasema.

‘Hapana shemeji…mbona leo hivi….?’ nikamuuliza

‘Usijali, siku moja moja, nafanya hivi, ili akili yangu iwe sawa,…nataka nikirudi nyumbani sisumbui kichwa changu tena, nalala tu, sitaki shida,..na leo sijisikii kwenda nyumbani, sitaki, na..na mambo yangu ya kufanya mengi ofisini, ikibidi nitenda kulala ofisini…’akasema

‘Shemeji mimi nakuhofia wewe, imetosha…’nikasema

‘Mhh, wanaume jamaani…., mimi sioni ajabu hata mume wangu kuna kipindi ilikuwa hivyo, mpaka nikawa sielewani naye, hasemi tatizo ni nini, anarudi kalewa, na ilikuwa sio kawaida yake, sijui, wakati mwingine najilaumu maana hizi kazi zinanifanya nakuwa mbali na mume wangu, ndio hivyo…’nikasema

‘Mhh, yawezekana, ndio maana ilitokea hivyo...’akaguna na kusema hivyo

‘Endelea na kisa chetu, nilitaka tu kukuambia kuwa hayo ya ulevi ni kawaida ya wanaume, hasa waliopo kwenye ndoa ...usijali sana, na wala usimwazie sana mtu kama huyo, kama kakupa ulichokitaka mpotezee, haya niambie ikawaje baadae naona muda umekwenda sana, ..’ nikasema.

‘Basi, aliendelea kunywa, na mimi sijui ikatokeaje, akanishawishi, nilianza na mimi kunywa kidogo, kidogo ooh… akawa ananiongelesha kunichkesha, utani, nakunywa, nakunywa,..weeeh, akili ikabadilika, nikawa nami nazipupia, …japokuwa kiukweli nilijitahidi kujizuia,…’akatulia

‘Mhh, kumbe…naanza kuipata picha….’nikasema
‘Basi bwana, ikafikia muda nikaanza kujisahau na mimi nikawa nakunywa kupitiliza, ila nikabakiwa na akili kidogo ya kukumbuka, hapo nikaingiwa na shaka..huyu mtu kalewa hivi atakwendaje nyumbani, sikujijali mimi, maana najua nitapara msaada kwa wenzangu, huwa wanafanya hivyo wakiona mmoja kazidiwa kwa kilevi,a pombe mbaya jamani...’akasema.

‘Nikatoka kidogo, kwenda `wash-room’ …nikampigia ndugu yake mmoja, ili kama akizidiwa ahakikishe anamchukua na kumfikisha nyumbani kwake…’akasema

‘Ok, namfahamu sana yule ndugu yake, wanasema eti ni mapacha, sio mapacha ila wamepishana kidogo sana, kama miezi tisa hivi au pungufu ya hapo kidogo…, sijui ilitokeaje mama yao alishika mimba mapema, ..ndio hivyo tena, bahati mbaya, kwahiyo wanakaribiana sana, sio mapacha wale…’nikasema.

‘Nikampigia simu…kumbe alikuwa naye karibu tu, …akasema anatuona nisiwe na wasiwasi...’akasema.

‘Mhh, hata mume wangu akilewa mara nyingi anamuita mdogo wake aje amchukue...hilo ni kawaida kwa wanaume wengi, na wadogo zake kuna kipindi wanakosana na kaka yao kuna kipindi wanaelewana, damu ni nzito bwana asikuambie mtu ....’nikasema.

‘Ndio..naelewa hayo sana…’akasema

‘Ok, sasa ikawaje...?’ nikamuuliza.

‘Yaani baada ya kurudi mezani, akili hayo iliganda, sijui nilikunywaje,..sijui ilitokeaje, mengi nimekuja kuhadithiwa,…maana ninachokumbuka ni wewe kuwa kichwani mwangu na wazo lako hilo, kila mara unanighasi, ukisemaa…sasa fanya lile jambo wakati ndio huu… usimwachie huyu ..mshawishi, ...ukishindwa hapo basi tena..’

‘Mimi nipo kichwani mwako….?’ Nikamuuliza kwa kushangaa

‘Nakuona mbele yangu, ….nakusikia kichwani mwangu, unanishurutisha, nifanye kile tulichopanga nikifanye,…..akili ilikuwa sio yangu,…pombe mbaya, jamani..sitaweza kulisahau hilo…na yaliyotokea hapo, hapana….’akashika kichwa

‘Ikawaje sasa….?’ Nikauliza nikiangalia saa yangu

‘Nilijikuta nipo kitandani kwangu, nilivyofika, sijui…na wakati nazindukana, mara mlango unagongwa,…nikasema nikiwa nimejichokea ‘nani wewe, fungua mlango…mlango upo wazi,’

Mara mlango unafunguliwa taratibu, anayefungua anaonekana kama anaogopa,..halafu kama ana uhakika, akafungua mlango kabisa,

Mtu niliyemuona pale mlangoni, alinifanya nipandwe na hasira, sijui kwanini, nikasimama kwa hasira nikitaka kumfukuza, ..oh, najikuta nipo kama nilivyozaliwa..

‘Nani sasa…yeye, kwanini umkasirikie, na …ina maana hukukumbuka kilichotokea usiku….?’ Nikamuuliza

‘Sasa subiri kwanza, unajua ni kwanini nilikasirika, na huyo aliyeingia unamfahamu ni nani…?’ akaniuliza

NB: Naishia hapa kwa leo, kili imechoka kidogo


WAZO LA LEO: Kiukweli pombe kwa wanyaji huwezi kuwaambia kitu, lakini pombe ni sababu kubwa ya maasi,…imekuwa ni kichocheo cha kuharibika maadili, kuharibu ndoa..na kuharibu afya za watu, …wengi wanasema kuna faida ndani yake, lakini ukilinganisha faida na hasara , hasara ni nyingi zaidi. Nawausia wenzangu na kujiusia mwenyewe tuachane na ulevi…ewe kijana ewe mwanandoa, kulewa sio suluhisho la matatizo, bali ni kuahirisha tu tatizo kwa muda, tusijidanganye kuwa pombe inaondoa mawazo.
 
SEHEMU YA 19


‘Huyo aliyeingia alikuwa ni nani, si huyo shemeji au…huyo aliyekufanya sasa una mtoto, si ndio huyo, hutaki kuniambia lakini mimi nimeshamfahamu...si ndio huyo, mdogo wa mume wangu au sio?’ nikamuuliza

‘Hapana....'akasema

'Ni nani sasa.mbona sikuelewi...?' nikamuuliza

'Alikuwa mdogo wa huyo jamaa,…'akasema

'Mdogo wake...!!!'nikasema kwa mshangao

'Ndio, na tena kaingia huku kafunga taulo, kiuonini, …na tabasamu tele mdomoni, kama vile nilikuwa naye usiku kucha,....na sasa ana...yaani mimi nilihisi kama kutapika, nikawa na hisia za ajabu,..nikawa nahisi huenda walinifanyia kitu kibaya hao watu…’akasema

‘Mbona sielewi, na huyo..unayemuita shemeji...alikwenda wapi, ina maana watakuwa walishirikiana hapana hawawezi kufanya hivyo, sio watu wabaya kiasi hicho au…?’ nikauliza

‘Kwa muda huo akili ilikuwa hivyo, inadhania hivyo....sikuelewa kitu kwa muda ule, si unajua tena ukiamuka kutoka usingizini, , …hapo ilivyo, akili yangu ilinifanya nielewe hivyo kuwa walishirikiana,...'akasema

'Lakini sio kweli...'nikasema

'Mhh...ngoja niendelee...maana hadi sasa nahisi hasira,...kama ilivyokuwa siku ile, nilipomuona huyo mtu, akili yangu ikajawa na ..., hasira chuki, ..nahisi kuzalilika,..na hasa pale nilipogundua kuwa nipo kama nilivyozaliwa, nikarudi kitandani na kunywea, na huku akilini nikijiuliza kulitokea kitu gani..na kama kuna kitu kilifanyikabasi watu hao, watakuwa wametangaza vita na mimi,….mimi sio mtu wa kuchezewa hivyo…’akasema

‘Kaka ameshaondoka, ,…alisema nije nikuangalie kama umeshaamuka..na kama unahitajia lolote uniambie niweze kukusaidia, ..’akasema na sikumjibu kitu, na jamaa akataka kusogea kuja pale kitandani, nikainua kumuangalia kwa chuki, akasimama, hakusogea tena.

'Eeeh, imekuwa hayo...'nikajiukuta nimesema hivyo.

'Nilimuambia kwa ukali, kwa ishara ya mkono,....

'‘Naomba utoke humu ndani kwangu kwa haraka…’nikasema, kwa msisitizo

‘Oh,….imekuwaje sasa…ok.ok…hakuna shida,… ila nilitaka kuhakikisha tu kuwa upo salama, mimi nitaondoka tu,…sina nia mbaya, kwanza hata mimi nahitajika nyumbani haraka, si unajua tena…’akasema

‘Na ole wenu,….kama mlinifanyia chochote kibaya, mtanitambua kuwa mim ni nani….’nikasema

‘Kibaya, ....!!! Hapana,...shemeji.... yote yaliyofanyika kwa ridhaa yako, …na ok, mtaongea na kaka, mimi ngoja nikavae, niondoke , hamna shida, ….’akasema akirudi kinyume nyume karibu ajigonge mlangoni

‘Kwa ridhaaa yangu….’nikajikuta nimesema hivyo, na wakati huo mjamaa alishatoka ndani kwangu,

Nilijikagua,....kiukweli, sikuwa na hali mbaya....ila nilisi vibaya tu...na nikaona iliyo bora ni kwenda kuoga...basi nikaenda nikaoga, huku nikiwaza na kuwazua,,,, kilichotokea jana ni nini,...je sijafanya mambo ya aibu...

Na maji yalipomwagika mwilini ndio nikaanza kumbukumbu, ...akili ikianiz kwenye sherehe,....oh, nikahema, ...nikawa najidadisi, je sikufanya jambo la aibu mbele ya wafanyakazi wenzangu pale ukumbini...hapana....hilo nalikumbuka vyema, je baada ya hapo….

‘Oh mungu wangu…’nikajikuta nikisema hivyo na kurudi kitandani,...kujilaza, uzuri siku hiyo ilikuwa ya mapumziko...na nilipotulia vyema ndio taswira ya tukio nzima ikaanza kunijia akilini…

**********

Nilianza kukumbuka, kuwa nilikunywa kupitiliza, na hata tulivyofika nyumbani ilikuwa ni kwa shida, kama isingelikuwa huyo mdogo wake shemeji sijui ingelikuwaje, japokuwa nay eye alikuwa kalewa pia, lakini sio sana, …

Tulipofika nyumbani, gari likisimama , kwa muda ule sikujua tumefika, nikawa nafoka, kwanini kasimamisha gari, dereva ambaye ni mdogo wa shemeji akasema tumeshafika, …basi nikawa najitahidi kutoka kwenye gari, ni mshike mshike..hata nilipotoka nje,..mmh, sikua vyema nayumba.

Hapo nikajua wataondoka wataniacha …nilianza kutembea kuelekea ndani huku nayumba, shemeji naye huyo, akawa keshateremka kwenye gari...akawa ananifuata naye hivyo hivyo, anayumbe, akanishika nikawa najaribu kumkatalia asinishike,..uhimili wa miguu yetu ukahindwa,... sote tukaserereka chini.

'Hahahaha...kama nilikuwepo....'nikacheka

‘Sasa wewe vipi…’nikasema, nikimuambia shemeji, hapo kanilalia, .. tukaishia kucheka, hapo tumelala chini, na mdogo wake shemeji ndio akaja kutusadia kusimama mmoja mmoja..., haya…mzobe mzobe hadi ndani kwangu...pombe mbaya jamani, narudia tena kauli hiyo...'akasema

‘Haya ondokeni…’nikasema tulipoingia ndani…

‘Haondoki mtu hapa….leo tunalala hapa hapa…’akasema na mdogo mtu akashangilia, ujue wote hao wana wake zao, wanafamilia zao...

Kwa muda huo hata sikutaka kubishana nao...macho manzito, yanatamani kulala tu..., mimi nikakimbilia chumbani kwangu…nashangaa mjamaa naye huyu hapa, kaniganda, na tukajikuta tupo kitandani kwangu…kilichotokea hapo,..aaah, hata siwezi kuongea, maana ilikuwa kama sinema fulani …’akasema.

‘Hongera,…ikawaje sasa maana mlilewa, iliwezekana siku hiyo...sizani , maana mlikuwa bwiii..au ilikuwaje...?’ nikamuuliza

‘Mhh, kwani hapo nakumbuka, siwezi kukuficha, sikumbuki sikumbuki ndio maana hadi sasa najiuliza.., …..ila kumbukumbu za baada ya hapo zipo,…'akasema

'Unanificha...'nikasema

'Kunaaaah, ....muda, ndio... nahisi ilikuwa usiku sana, nilishituka,…akili kidogo zilikuwa zimerudi, kichwa kinaniuma kweli..,..najikuta kuna mtu kalala pembeni yangu…hapo natamani,..sijui kutapika, kichwa, kichwa...’ akasema

‘Hahaha…pole sana nyie mwafikiri pombe ina mema, ..ni shida, sijui kwanini mnaendekeza kunywa..haya ikawaje..?’ nikauliza

'Kichwa, kichwa kinauma,...'nikalalamika, na jamaa akajizoa zoa, na kwenda kuniletea maji, akaniuliza nina ..dawa ya maumivu,...nikamwambia ipo ...akanichukulia nikanywa, nikatulia kwa muda, baadae kikapoa kidogo.

‘Hapo...., akili zimesharudi, nikamwambia aamuke aondoke..lakini akasema hawezi kuondoka usiku huo,…nikatoka kujisaidia, vyoo ni ndani kwa ndani, lakini , nikawa na wasiwasi, nikaelekea varandani, ..nashangaa kuna mtu kalala kwenye sofa.

Nikaanza kukumbuka pale ilivyokuwa, hapo hapo nikamuamusha mdogo mtu, ili waondoke.., lakini shemeji hakukubali, akasema hawezi kuondoka usiku huo hata hivyo alishamuambia mkewe atalala kazini…nikaona isiwe shida, ..sijui ilikuwaje, nakumbuka nilisikia kiu, nikataka kunywa kitu…nikasikia shemeji akisema

‘Bwanamdogo mpe kinywaji atulie…’akasema

Kweli mdogo mtu akaniletea kinywaji, nikanywa, …haikuchukua muda,...nahisi kama kilevi kilikuwa sio cha kawaida, maana nililegea ..hata sijui ilikuwaje,ila nahis kuna mambo yalifanyika tena hapo..sina uhakika, …ukumbuke hapo ilikuwa varandani, sasa naamuka asubuhi, najikuta nipo kitandani kwangu, nimelala, nipo kama nilivyozaliwa, je ilitokea nini..na hapo sikumbuki vyema imekuwa mtihani kwangu,…’akasema

‘Ikawaje sasa, tuache hizo pazia unazoweka, hazina maana kwangu, ilikuwaje…?’ nikauliza

‘Ikawaje, ikawaje, ikawaje... ..ndio hivyo, asubuhi, huyu mdogo mtu nikamuambia aondoke, nikabakia peke yangu….’akasema

‘Mhh,… wanaume hawa bwana, …nakumbuka siku moja mume wangu alikuja na mdogo wake, naye akiwa amelewa bwii, sikutaka hata kuongea naye, nikamwambia alale huko huko sebuleni,….sikutaka shida, …kama huyo yupo hivyo, achana naye, ilimradi kakupatia mtoto basi inatosha, mwanaume mlevi ni tatizo, anaweza kukuleta magonjwa…’nikamwambia.

‘Nikuulize kitu samahani lakini..kwani shemeji ana tatizo gani?’ akaniuliza. swali lake lilikuwa kama kitu cha kushitukiza ni kitu sikutarajia kuulizwa, nikawa kama nimeshtuka, nikajikuta nikisema;

‘Nani shemeji, mume wangu kakuambia nini…?’ nikaamuuliza

‘Ndio mume wako..., naona kama …ana matatizo, wewe ni rafiki yangu, na lako ni langu, niambie ukweli …kuna tatizo gani kati yenu wawili?’ akaniuliza

‘Matatizo ni ya kawaida tu..leo hili kesho lile mimi nimeshajizoelea tu, kwani umemuonaje, sizani kama alipokuja hapa mliongea kitu, au kwanini unaniuliza hivyo…?’ nikamuuliza

‘Hapana,....mmh, ... mimi si ninaona tu…alivyo, sio yule shemeji niliyemzoea, anaonekana hana raha kabisa…nahisi kuna tatizo kati yenu wawili , niambie ukweli....’akasema

‘Ungemuuliza yeye kwanza,...maana mpaka unauliza hivyo si ina maana mlikaa mkaongea au...na ni shemeji yako,..kwanini hukumuuliza...'nikasema

'Aaah, ina maana hutaki mimi kukuuliza mambo yako...'akasema

'Sijakuambia umefanya vibaya,.... mimi nimemuuliza anasema yupo sawa,..hebu jiuliza kama wewe mtu baki umemuona hivyo, je mimi ninayeishi naye,…kiukweli mimi sitaki kujisumbua tena kichwa changu, maana nina mengi ya kufanya,..hayo nakuomba tuyaache tu nitayamaliza mimi mwenyewe, kwa muda wake,..., nashukuru kwa kuliona hilo…’nikasema

‘Mhh, nahisi kuna tatizo kubwa sana linalomsumbua shemeji..., jaribu kuwa naye karibu, sio vizuri rafiki yangu, mimi nawajali pia...’akasema rafiki yangu huyo.

‘Unafikiri,....mbona nalifanyia kazi...nimeshaliona hilo, na yeye,...nimeshajaribu kumdadisi,... hasemi,... sasa nifanyeje, na sitaki hata kumuuliza zaidi, …kwa hivi sasa nimeamua akili yangu yote kwenye mambo ya kimaendeleo , kwa ajili ya familia yangu basi, muda utafika nikiona mambo yamekaa vyema nitalijadili, na yeye aniambie kwanini hataki kusema ukweli, ana tatizo gani…’nikasema

‘Kama ni hivyo huyo mtoto wa kiume mtampataje…?’ akaniuliza swali ambalo, pia lilitoka na kunifanya nishtuke, sio kwamba ni swali la ajabu, lakini nakumbuka kauli hiyo aliwahi kuitamka mume wangu, wakati tunazozana, ilinijia tu hivyi, lakini sio kwa kudhania ubaya...

Nakumbuka katika kuzozana zozana na mume wangu, kuna kipindi alitoa kauli hiyo...

‘Mke wangu, hivi kwa hali kama hii, ..tutapataje huyo mtoto wa kiume,…kila siku uko na kazi nyingi, umechoka,…unanifanya nifanye hata nisiyodhamiria kuyafanya,…’akasema
 
SEHEMU YA 20

Kiukweli kauli hiyo ilinifanya niwe kwenye wakati mgumu, kama binadamu, kama mwanamke, nilihisi kweli nimekosea, lakini hata hivyo kama mwanamke nilihitajika kubemebelezwa, sio kwa vile mimi ni mke wake basi iwe hivyo, ni mambo ya ndani sitaki kuyasema zaidi,, lakini kiukweli …hayo niliwaza tu, sio kwamba niliongea na rafiki yangu.

Pale mimi nikasema;

‘Achana naye…kama yeye kaamua hivyo..., na kaona hiyo ndiyo starehe yake ya kulewa, na pombe ndio kila kitu basi aendelee, sitaki tena kumuingilia, sana muda utafika lakini sio kwa sasa, kwa sasa kuna mambo yananiumiza kichwa...'nikasema

'Hilo ni muhmu sana rafiki yangu....'akasema

'Nikuambie kitu, mimi sio mtoto mdogo, ...kulikuwa na wakati wa hayo....sasa hivi sisi ni watu wazima, lazima tuwe ni kipaumbele cha kujali ni nini baadae,...sasa nikimueleza mwenzangu haelewi, sawa, ana mambo yake..lakini...hajayatilia maanani kihivyo....'nikasema

'Lakini ulisema kuwa anajitahidi kwa kazi, ndio maana kafungua ofis yake...'akasema

'Sasa hiyo ni baada ya kuongea sana..na akicheza atashindwa,...kama ataendekeza pombe, najua yeye ulevi wake ni pombe, sizani kama ana ulevi mwingine,...kwa hivyo, basi...naona ni sterehe yake, nimemuacha aendelee nayo...'nikasema

'Aakirudi inakuwaje...mnalala pamoja...?' akanuliza swali jingine lililonifanya sasa nicheke sana.

'Hahaha, wewe sasa nona unataka kuvuruga ajenda yetu,....hahaha, kwanin unaniulza hivyo...nikuambie tu kwa vile wewe ni rafiki yangu...kwa muda sasa.., nimeamua kumsusa hata kulala naye tuna muda, hata tunaishi hivyo hiyo ni siri yangu nakuambia wewe tu kwa vile ni rafiki yangu,…na nilishamwambia akirudi kalewa, asilale na mimi chumba kimoja, sipendi harufu ya mipombe…na siku akiwa safi, aaha, hamna shida anakuja tunalala, lakini ndio hivyo, tupo tupo tu,….’nikamwambia.

‘Rafiki yangu hilo ni tatizo, jaribu kumuuliza vyema, kwani tatizo ni nini,..nahisi mume wako ana tatizo, mimi kama rafiki yngu nakuomba ulifanyia hilo kazi kabla hujachelewa, sizani kama unataka uwe na mke mwenza….utakuja kujuta, ukiwa umechelewa, hali kama hiyo sio nzuri.., utampoteza mume kwa hali hiyo, huenda ana tatizo linamsumbua na mtu wa kumsaidia ni wewe mke wake...’akaniambia

‘Hahahaha,unanichekesha, eti mke mwenza, hahaha..ajaribu..kama ni kuoa, aoe, mbona nilishamuambia hilo, ila asifanye siri...nikaja kugundua,...na leo, kweli umenichekesha, Hivi nikuulize, unajifanya unafahamu saana maswala ya ndoa, wewe ngoja utakuja kuolewa, utakuja kuyaona haya wewe mwenyewe, ..ndoa nyingine ni ndoa,kuna matatizo chungu mbovu, ...., lakini sisi wanawake tunavumilia mengi,.we yaache tu..’nikasema

‘Hata kama sijaolewa, lakini mengi ni ya kibinadamu , nayafahamu tu…’akasema

‘Unafikiri mimi sijafanya juhudi, nikuambie kitu, ndoa..sio ..yeye akiwa na hamasa zake aje akuvamie tu, mimi ni mwanamke, nahitajia kubembelezwa, nahitajia, hali itakayonifanya nisahau mengine ya kikazi,..na hilo halianzii,..kitandani tu…’nikasema

‘Mhh..hapo unanitisha ...ok, labda nikuulize hapo... unataka kusema nini, mbona shemeji mimi namuelewa sana, nakumbuka ulishawahi kuniambia, umempata mwanamume anayejali, anayejua kubembeleza, au ulikuwa ukinidanganya…’akasema

‘Ilikuwa…ghafla, mambo yalipojiongeza, majukumu ya hapa na pale, unaelewa, hali nayo ikabadilika,…tukurudi nyumbani kila mtu na laptop yake, shughuli mtindo mmoja, ..mengine ni uhalisia, hata hivyo, ..siwezi kumlaumu au yeye kunilaumu, lakini pia, yeye anawajibika, kulibadili hilo…’nikasema

‘Mhh..mnatakiwa muwajibike wote, ..rafiki yangu shemeji ni mtu mnzuri sana, …anajali, nahisi wewe ndio hutaki kulifahamu hilo, au kwa vile unacho, ukiwa nacho unaona ni kitu cha kawaida tu..’akasema

‘Unajifanya unamuelewa sana kuliko mimi au..ni kweli, unalolisema, alikuwa hivyo, lakini sio hivi sasa..nahisi keshonja kwingine, na mimi sina muda wa kupoteza kumdadisi, ila nilimuambia, …kama atakuja kufanya jambo kinyume na ndoa yetu, ajue tumeshamalizana….’nikasema

‘Una maana gani…?’ akaniuliza
‘We tuyaache hayo, ….muhimu nataka nihakikishe jambo lako limekwisha, halafu nitayamaliza ya kwangu nionavyo ni sahihi…na najiuliza sana, kwanini umefikia kuniuliza haya yote..maana hayahusiani na tatizo lako au sio…?’ nikamuuliza

‘Nimeuliza tu…kwa vile nimemuona alivyo, na sizani nimekosea kukuulizia hayo, kaam uanavyonijali mimi, ndivyo ninavyokujali wewe…’akasema

‘Ni kweli,..ila yasikuumize kichwa, mimi mwenyewe ni mipangilio yangu, kuna haya mambo ya kikazi yakikaa sawa, nitatafuta mtu wa kuyafanya, na mimi nitakuwa kariu na familia yangu, hilo nimeshaliona, lakini kwa sasa, ngoja, nione ni kitu gani anakihitajia,..ila, siku nikigundua ana kimada nje,..ohooo..huyo na yeye nitakachowafanyia, watakuja kunikumbuka….’nikasema


‘Mhh, kama ni hivyo utanifanya mimi niogope kuolewa, na hilo litawafanya wanaume wengine wapate mwanya wa kutoka nje ya ndoa…mpaka hapo naogopa, na hata …sizani kama nahitajika kuongea zaidi…’ akaniambia.

‘Usiogope, kuolewa kwa vile umesikia hayo kutoka kwa ndoa za watu , ndoa za watu hazina utaratibu maalumu kuwa yule akiwa hivi na wewe utakuwa hivi, kila mmoja ana utaratibu wake wa kuishi, na mwsho wa siku wote wawili mnakubaliana na hali halisi iliyopo, muhimu msifichane, msiwe na ajenda za siri, zinazovunja ndoa....’nikasema.

‘Lakini mimi nina imani nikiolewa nitahakikisha kuwa mimi na yeye kwanza tunapeana masharti ya jinsi gani ya kuishi, na kama nikihisi kuwa kuna tatizo nitamuuliza mpaka aniambie, kwani sitafurahi aje kutembea nje ya ndoa, na chanzo kiwe ni mimi....vinginevyo, nisijue …. ’akasema.

‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa mimi ninaweza kuwa chanzo, kuwa mimi ndiye nimemfanya mume wangu alewe , awe hivyo, au.. ..kama ana tatizo angeliniambia basi, moja kwa moja, mimi si mkewe, kwanini aone uzito kuniambia, eeh,.., ukiona anaficha kitu, ujue hataki kukuambia, mimi namfahamu sana,…vinginevyo mimi siwezi kumuingilia maisha yake aliyoamua kuwa nayo, muhimu mimi mwenyewe naweza kuishi maisha yangu...’nikasema.

‘Mhh, haya bwana, kama ulivyosema ndoa kila mtu na utaratibu wake, na mimi nimejifunza kutoka kwa wenzangu sizani kama nitafanya hayo makosa,...maana mengine hayavumiliki, ...na wasiwasi wangu najiuliza kama likitokea tatizo hapo ni wa kulaumiwa, na je ni nani wa kuumia, kama sio sisi wanawake, hebu lifikiria hilo rafiki yangu....’akasema..

‘Achana na mume wangu, hebu tuendelea na hili tatizo lako, likimalizika la kwako litanipa nafasi ya kuendelea na mambo mengine, …ilikuwaje baada ya hapo,...?’ nikamuuliza.

‘Yaliyoendelea ni kama unavyoona, ....kwanza baada ya tukio hilo tulikaa kama wiki hivi hatuonani, na tulipoonana akawa ananionea aibu,..na mimi halikadhalika, na hatukuweza kubahatika kuliongelea hilo tukio hata siku moja, na ikawa kama vile tukio hilo limetushitua, sote wawili…’akasema

‘Mhh, lakini ulisema ilitokea mara ya pili au…?’

‘Ya pili, si ilikuwa siku ya pili yake, nikawa nahisi kuumwa, kumbe ni hiyo mipombe, akaja akaniambia dawa twende kunywa tena,..nikagoma, akanisihi mpaka nikakubali, ikaja kutokea kama vile…aliyetusaidia ni huyo huyo ndugu yake…’akasema

‘Una hatari wewe…’nikasema

‘Basi baada ya hapo,…nikaona atanizoea vibaya, nikaanza kumkwepa, akipiga simu sipokei, nikawa sasa siendi kula chakula cha mchana,nikingia ofisi nakuja a chakula changu, sitoki hadi jioni, na nikitoka najivunga kutoka na mmoja wa wafanyakazi ninaofanya nao....siku zikaenda...’akasema.

‘Mara nikaanza kuhisi mabadiliko...nikashituka, mwezi wa kwanza wa pili sijaona siku zangu, nikaona oohoo,… ngoja nikapime, kupima, nikaambiwa hongera..una mimba.....’akatulia.

‘Oh…ikawaje…?’ nikamuuliza

‘Ikawa hivyo hivyo, namkwepa kuliko, awali, lakini ikafikia muda, hali inanivuta natamani kuonana naye, ..lakini sitaki nionekane na watu, nahisi aibu fulani hivi…basi siku moja akanitumia meseji kuwa hana raha,…bila kuniona hataweza kwenda nyumbani kuna kitu anataka kuniambia

‘Kitu gani….?’ Nikamuuliza

‘Mhhh…nilishindwa hata kumuelewa, kumbe alikuwa na ajenda ya siri, …na sijui kwanini ilitokea hivyo, ndio maana rafiki yangu nakukanya,..ndio mimi sijaolewa, ndio mimi sina uzoefu wa ndoa, lakini wanaume wengine wanafikia kufanya mabaya kutokana na jinsi tunavyoishi nao, tunawajenga,..tunawafanya wafanye hivyo,…tuweni makini sana…’akasema
‘Hebu niambia alitaka kukuambia nini, maana mimi nataka kuondoka, naona unanifanya nijihisi siwajibiki, wakati wewe hujui mengi ya ndoa,..ipo siku nitakueleza, sio kweli kuwa mimi nimefikia kuyafanya hayo bila sababu, lakini mambo mengine ya ndoa, …hayazungumzwi….’nikasema

‘Basi kwa vile hali hiyo ilinizidi, nikawa natamani nimuone tu, awe karibu yangu, awe akiongea, awe kinibembeleza…yaani nakuwa na raha, na kuwa na amani, na akuiondoka, nakuwa muogoa, naogopa, ni hali tu ilinitokea hivyo…basi, nikamkubalia siku hiyo aje, …na hiyo ikawa imekaribisha mimi na yeye kuwa karibu tena

‘Sasa alipokuja siku nyingine ndio, akaniambia lake la moyoni….na hilo ndilo likafanya ajue kuwa mimi nina uja uzito….’akasema

‘Alikuambia nini…?’ nikamuuliza na yeye, akasimama maana mtoto alikuwa akilia, na mimi simu yangu ikawa inaita…

‘Alikuambiaje…?’ nikamuuliza nikiangalia ni nani anayenipigia, kumbe, … alikuwa ni mume wangu, nikamwambia rafiki yangu;

‘Tafadhali kidogo…niongea na shemeji yako…’nikasema

Nikawa sasa naongea na mume wangu , huku rafiki yangu akiniangalia kwa makini, ni kama ana shauku kufahamu naongea nini na mume wangu

‘Njoo nyumbani haraka…’ilikuwa sauti ya mume wangu kwenye simu

‘Kuna nini…?’ nikauliza, na mume wangu akakata simu…kutokana na sauti yake hiyo, nikajua kuna tatizo, kwahiyo sikutaka tena kuendelea na rafiki yangu, nikasema

‘Rafiki yangu, tutaendelea baadae , nataka kufahamu, alikuambiaje, au ..alikuambiaje…ok..ngoja niondoke….tutaongea siku nyingine si bado upo,….?’ Nikamuuliza

‘Kesho naondoka…’akasema

‘Basi nitakuja, …nahisi nyumani kuna tatizo…’nikasema na kukimbilia nje, kuondoka..

NB: Naishia hapa kwa leo,

WAZO LA LEO: Ndoa ina siri zake nyingi sana, na iliyo wajibu, ni wanandoa wenyewe kujaribu kuzikabili changamoto zao, na kufiachiana siri zao, kwa kadri wawezavyo, kwani siri nyingine ni mtihani mungu anawajaribu…ni changamoto za kuvuka daraja…
Ni vyema kwa wanandoa, mkawa kitu kimoja kwa kuyajadili matatizo yenu, ni aibu kama wanandoa kama mtakuwa mkilalamika kwa watu wengine kuhusu mambo yenu ya ndani, ambayo mengine ni siri za ndoa, kwanini msiulizane, mkaangalia tatizo lipo wapi…kumbe yawezekana ni kitu kidogo tu… Tuweni makini kwa hili. Tumuombe mola azilinde ndoa zetu atuongoze tuwe kizazi chema.
 
SEHEMU YA 21


Basi niliondoka hadi nyumbani, namkuta mume wangu kazidiwa shinikizo la damu, ikabidi nifanye jitahada nyingine za kumuita docta, hakutaka nimpeleke hospitalini, akaja docta, akasema kweli shinikio la damu lipo juu, kwahiyo apate dripu…

Baadae hali ikawa shwari, ikabidi nikae naye kumuhoji hili na lile, nilichelea kuongea naye maswali yanayoweza kumtatiza hata docta alinionya kwa hilo, lakini kuna swali lililokuwa kichwani mwangu;;

‘Nikuulize kitu samahani lakini..kwani shemeji ana tatizo gani?

‘Ndio mume wako, naona kama …ana matatizo, wewe ni rafiki yangu, na lako ni langu, niambie ukweli …?

‘Hapana, mimi si ninaona tu…alivyo, sio yule shemeji niliyemzoea, anaonekana hana raha kabisa…’akasema

‘Mhh, nahisi kuna tatizo kubwa sana linamsumbua, jaribu kuwa naye karibu, sio vizuri rafiki yangu, mimi nawajali pia..

Kumbukumbu hizo ziliuteka ubongo wangu, na kiukweli sikuwa na amani kabisa..,Japokuwa mpaka hapo sikuwa na wazo baya dhidi ya rafiki yangu…ila nilianza kuamini kweli mume wangu ana matatizo..na hilo ndilo nililipa kipaumbele, vipi nitaweza kumsaidia mume wangu, maana hiyo hali iliyojitokeza ikiendelea hivyo, kweli naweza kumpoteza mume, …niliwazia zaidi kwenye afya yake

Basi nilipoona mume wangu katulia, na anaongea vizuri, nikamuuliza

‘Hivi mume wangu, hebu niambie,…. kuna tatizo gani linalokusumbua…?’ nikamuuliza

Mke wangu matatizo ni ya kawaida tu, …tulishayaongea haya,…na mimi sitaki ukwazike kwa hilo, na sijui kwanini leo hali yangu imekuwa hivi,..nijitahidi isitokee tena, lakini kuna mambo mengi yamenizonga, lakini yataisha tu, nitayamaliza kwa vyovyote iwavyo…’akasema

‘Huo ni ugonjwa, halafu unasema utajitahidi isitokee tena, na tatizo hilo, ninavyoona sio bure, nahisi kuna kitu kinakusumbua,…sasa usipotaka kunishirikisha mimi, eeh, hebu niambie,…ni nani mwingine anaweza kukusaidia, zaidi ya mkeo …’ nikamwambia.

‘Usijali mke wangu,…wewe endelea na kazi zako tu, najua una mipangilio yako mingi sana, …, na sitaki mimi niwe sababu ya kukukwamisha…’akasema

‘Hujanisaidia kwa hilo, maana sasa sitaweza kufanya kazi zangu kwa amani, nitakuwa na mashaka muda wote, usiponiweka wazi…utanifanya na mimi nianze kuumwa.

Basi nikaanza kuwa karibu na mume wangu na kumuomba samahani kama mimi ndiye chanzo cha hayo yote, na siku moja akaniambia;

‘Mke wangu, uwe na amani, najua yametokea mengi, ambayo huenda hata mimi sikupenda yatokee, lakini isiwe sababu ya wewe kukatisha shughuli zako, muhimu ufahamu sijapenda yatokee, na kuumwa kwangu hata mimi ninaanza kuogopa, inabidi nibadilike..’akasema

‘Ni kitu gani kinachokusumbua, hebu niambie kwanza…?’ nikamuuliza

‘Kifupi hakuna…nimeshazoea, na…hakuna tatizo, …’akasema na sikuweza kuwa na amani tena…hasa nikikumbuka zile kauli za rafiki yangu, na sasa ninaona kweli mume wangu ana matatizo,…

Kwasababu ya hayo matatizo, nikawa sina muda wa kumfuatilia rafiki yangu tena, kumbe alishaondoka kwenda Zanzibar.

Na siku baadae nikamtembea rafiki yangu, katika kupoteza mawazo, na katika kuongea tukajikuta kwenye yale mazungumzo yetu, tukafikia pale pale…nikamuuliza

‘Unajua siku ile tulipoongea ukanipa ushauri kuwa niwe makini naweza kumpoteza mume wangu, imenifanya nianze kujirudi, nimewaza sana, naona kweli nitakuja kuumiza mume wangu…’nikasema

‘Nilikuambia lakini…sasa kwanini unaendelea kufanya hivyo, na je mume wako anaendeleaje…?’ akaniuliza

‘Hajambo hajambo kabia…na huwezi kujua ni yule siku ile nilimkuta kitandani akiwa kama kapoteza fahamu, ..shinikizo la damu ni baya… siku ile hata mimi niliogopa, maana alikuwa kama anataka kukata roho…’nikasema

‘Oh,… lakini ni nini tatizo…?’ akaniuliza

‘Mpaka leo sijafahamu…na hata sielewi, unajua kuna kauli alisema…lakini sio sababu nahisi kuna jingine..lakini hizo kauli zimenifanya niwaze tu, …japokuwa sizani kama zinaweza kuwa ndio sababu..’nikasema

‘Kauli gani hizo mbona huzitaji…?’ akaniuliza

‘Unajua kuna kitu, …mume wangu anatamani sana, kimojawapo ni hicho, ya kuwa anatamani kupata mtoto wa kiume…na kingine ambacho hatusikilizani, yeye bado, anapenda ujana ujana,….hajui kuwa umri umekwenda…hilo sijui wanaume wengi kwanini haalioni…mzee mzima bado upo na mambo ya vijana.., mimi namemuambia sina muda huo…’nikasema

‘Mhh kwanini unafanya hivyo, unafanya makosa, maana mume wako ni mwenza wako mwatakiwa mshirikiane, mfurahishane, sasa kama anataka hivyo akaende wapi, ndio maana wanakimbilie mitaani, ..hili hulioni wewe…?’ akaniuliza

‘La kujiuliza ni hili mambo hayo, eeh yana faida gani kwetu, kwa umri huu…sawa kama ni watoto tutapata tu,….mungu akipenda, … ila nilitaka nimalizane na mipangilio yangu ili tukianza kuzaa, nisiwe na hangari hangari nyingine ndio mpangilio wangu, nimejifunza kwnye mimba hiyo ya kwanza, …na hilo nilishamuambia…’nikasema

‘Ina maana hilo ndilo la kufanya usiwe karibu naye,…hilo ndilo linakufanya usitimize haki za ndoa, ambazo ndio msingi wa ndoa au …’akasema

‘Unasema nini.., nani kakuambia kuwa sitimizi haki za msingi za ndoa..?’ nikamuuliza kwa mshangao.

‘Nakuuliza sio nasema mimi, nakuuliza wewe, na …’akasema na kabla hajamaliza nikasema;

‘Umeyajuaje hayo,….!! Kwani aliwahi kukuambia hivyo, kuwa sijamtimizia hayo…aah, naona sasa unaingilia mambo yasiyokuhusu…’nikasema

‘Lakini rafiki yangu rejea mazumgumzo yetu tuliyofanya siku ile, kwani hukuwahi kunigusia hilo,…. au unafikiri mimi nakuzulia au urafiki wetu una mipaka sijakuelewa, …’akasema

‘Ok,…ok… basi labda niliwahi kukudokezea hilo.., sawa, nimekumbuka nilikuambia …hata hivyo hilo mimi nimeshaliona, na nilikuwambia nitalifanyia kazi, kwahiyo lisikuumize kichwa, umenielewa…’nikasema

‘Sawa, ….ni heri ulifanyie kazi, na kiushauri, kama kuna yaliyotokea yakakukwaza, au kama kuna kitu, jaribu kukiweka kapuni, kitupe… nakuomba uyasahau yote mabaya ya nyuma,…hali umeshaiona, hali hiyo inaashiria kuwa , sasa hivi uwe karibu naye, na…nahisi inaweza ikaleta heri ukifanya hivyo.., tusameheane tu, maana mengi yanafanyika ili tu, kutimiza adhima…’akasema

‘Nimekuelewa,…’nikasema

‘Unajua nilitaka nikisafiri niwe na amani, niwe nimeacha kiula kitu ni shwari..nisiwe na kitu moyoni mwangu kwako, na wewe kwangu…’akasema

‘Hilo lisikutie shaka, hebu kwanza nikumbushe, siku ile tuliishia wapi…’nikasema

‘Siku ipi tena….mmh, yale tuachane nayo bwana…ndio maana nataka tuhakikishe tumeridhiana, hakuna …jambo la kuumizana kichwa, na ukweli wote, nshakuambia au sio…’akasema

‘Hapana hujambia,..ukweli wote.., maana nakumbuka siku ile ulisema…, alipokuja kwako,…kuna kitu alikuambia ndio kikafanya yeye agundue kuwa una mimba, ni kitu gani miliongea…?’ nikamuuliza

‘Hahaha, na wewe bwana,….hahaha, unajua wakati mwingine nacheka, lakini wakati mwingine najiuliza hivi hili jambo litafikia mwisho tusahau , isije kuleta matatizo huko mbeleni,…na ikileta .. itakuwaje…maana nimejaribu kila njia unielewe, lakini sizani kama utanielewa, kwa hali kama hii…unakuwa mdadisi kwa kitu ambacho ulikanya wewe mwenyewe kuwa jambo hilo liwe siri….sasa labda mimi naona nikuambie kila kitu iwe iwavyo…’akasema

‘Sawa lakini hapo …kuna kitu sijakuelewa…’nikasema

‘Rafiki yangu, hebu nikuulize kwani unataka nini zaidi,..unataka matatizo, unatakaje ili iweje, …wakati mwingine naona ni bora tukae kimia, wakati mwingine naona ni bora niweke kila kitu kwenye meza, ..lakini sitaki kuumizana , sipendi kabisa…’akasema

‘Kwa hivi sasa bora uniambie kila kitu tu, maana ukiacha ndio utanipatia shinikizo la damu, maana nimekuwa nikijiuliza, na…nilitaka hata niende kuonana na mdogo wa shemeji ili niwe na uhakika fulani, kuna maswali yana nijia, na mimi nataka nimuulize, lakini siwezi kufanya hivyo mpaka nipate ridhaa yako,…wewe huelewi tu, …wewe ni kama mdogo wangu lazima niwe na uhakika na ulichokifanya, ili likitokea la kesho, niweze kuwa na majibu, ukumbuke kuna leo na kesho…’nikasema

‘Kwahiyo unataka nini hasa, na upo tayari kwa …mimi siwezi kuwa na uhakika na wewe, maana hili linaweza likawa sababu, na mimi sitaki, unielewe hapo, eeh, mmh…nasita kidogo hapo…’ akasema

‘Swali lipo pale pale… ikawaje, usitake tuzunguke,…. huyo shemeji alifahamu vipi kuwa wewe una mimba, na ni kauli gani ilikyokufanya hata wewe ufikie kumwambia, au ilikuwaje…unajua, nimeanza kuandika kitabu changu, natunga true story ya maisha yetu mim na wewe vyema…hahaha, huwezi amini mengi yaliyotokea kati yangu na wewe nimeshayaandika…’nikasma

‘Unasema kweli…?’ akauliza

‘Ndio..ni pale ninapokuwa sina kazi,..akili imetulia huwa naandika, yale yaliyotokea kama hadithi fulani hivi,…sasa hivi nipo kwenye hilo tukio, naona lina maswali mengi yasiyokuwa na majibu, na sehemu hiyo nimeiita, ‘ukweli baada ya ushauri kwa rafiki yangu..’.

‘Mhh, ushauri kwa rafiki yako, ambao umeleta matatizo au, itakuwaje sijui….’akasema

‘Matatizo aah, nani kasema, hakuna kitu kama hicho, ni ushauri ulioleta matunda ya kuleta faraja…huoni sasa una mtoto, usiseme hivyo….’nikasema

***********

‘Kama nilivyokuambia, kuna muda nilikuwa natamani yeye awe anakuja, au nimpigie simu tuongee naye, nikifanya hivyo, nikasikia angalau sauti yake, kama hakuweza kufika, najihisi raha, nakuwa na amani fulani… lakini wakati huo sikutaka hayo yajulikane na watu.., sikutaka watu wanione nikiwa naye tena, naona aibu kuliko wakati wote, nilihisi kama watu watanigundua kuwa ndio yeye…’akaanza kusimulia

‘OK…sawa endelea…’nikasema

‘Siku hiyo alifika akiwa hana raha, nikamuuliza tatizo nini…akasema hakuna kitu ni mambo ya kawaida tu,..ni mambo ya kifamilia zaidi…’akasema

‘Kama huniambii, sitakuwa na amani, siku hizi sijisikii vizuri, nataka wewe ukija uwe na furaha, na kama huna furaha ..ni bora usije ,..na usiponiambia tatizo lako, ni bora uondoke..’nikasema na moyoni nijiuliza hivi kweli akifanya hivyo si nitaumia sana, na mimi nataka awe karibu yangu.

‘Ina maana muda huo mimba bado imejificha,..bado mapema au sio..?’ nikamuuliza

‘Kitumbo bado ile yasana,… ila kimeshaanza kutuna, na mimi sijui kwanini, nilianza kuvaa nguo pana mapema, ..kama Madera…kitu ambacho wengi walianza kunihoji nakawa nawapa majibu yao, na nikazoeleka hivyo kuwa nimebadilika, siku hizi sio yule mdhungu tena…ilinisaidia, hata dalili zozote zisionekane mapema, na siku baada ya siku …tumbo likaanza kukua…’akasema
 
SEHEMU YA 22



‘Safi kabisa, ulicheza hapo maana hata mimi sikuwahi kukushuku awali…’nikasema

‘Nataka unizalie mtoto wa kiume…mjamaa alipofika alisema hivyo…’akasema

‘Mungu wangu alikuambia hivyo…?’ nikauliza nikihema, muhemo, kama vile kauli hio inanihusu mimi.

‘Ndio alisema hivyo na mimi kauli hiyo ilinishika kwa mshangao, lakini sikutaka kujionyesha, nikacheka kweli

‘Kwanini unacheka, akaniuliza…?...’akasema

‘Unanishangaza, ina maana kukuita hapa, umenifanya mimi kama hawara wako,..nilishakuambia yaliyotokea siku ile, mimi sikuyataka na yaninipa wakati mgumu sana, na..na..kwanza ole wenu nilitaka kuwashitaki, mlichonifanyia wewe na ndugu yako, sitaweza kuwasamehe..’nikasema

‘Kitu gani, mbona sikuelewi…?’ akasema

‘Tuyaache hayo…na umesema nini…?’ nikauliza kama vile sijasikia

‘Natamani wewe unizalie mtoto, lakini awe wa kiume..’akasema

‘Nikuambie kitu, hilo kamwambie mkeo, sio mimi…’nikajifanya kuwa mkali,

‘Sikiliza,..najua hata wewe unataka mtoto, nimesikia hivyo..,..unatamani uwe angalau na mtoto, hata mimi naliunga mkono, maana umri unakwenda au sio, sasa hebu tulia basi…’akasema na mimi muda huo nilikuwa nasimama nahisi kichefu chefu

‘Ni nani kakuambia upuuzi huo…’nikasema nikigeukia upande wa pili leso mdomoni.

‘Wakati mwingine wanawake mpo hivyo, kama hujaolewa kwa muda..umekaa na unahisi umri utakusuta..na sio siri kila mtu anatamanikuwa na mtoto, hata wewe itakuwa hivyo,…hilo lipo wazi, sasa nisaidie na mimi nikusaidie…’akasema

‘Nikusaidie..wewe si mume wa mtu jamani, unataka nini…?’ nikamuuliza na mengi yakaendelea hapo ikawa tena hatuelewani…’akasema

‘Mengi yapi..?’ nikauliza

‘Tulibishana sana kuhusu hilo la mimi kumzalia mtoto, eti tena wa kiume,…hivi hilo si alitakiwa aongee na mkewe…anyaway, tulibishana hapo, na sijui ikatokeaje, nikaanza kujisikia vibaya, kutapika, nikakimbilia washroom, kumbe alinifuatilia kwa nyuma, sasa wakati natapika, ikafikia muda, nikasema;

‘Kama mimba ni hivi, bora …nizae mapema tu..hiki kikombe kinipite…’nikasema na huku nyuma yangu nikasikia akisema;

‘Kumbe una mimba…’akasema,..nilishtuka, karibu nizimie, na akaja haraka kunishika ili nisidondoke, na alipohakikisha nipo salama akasema;

‘Oh, sasa niambie ukweli,…kumbe una mimba , kumbe ni kweli…mmh, nishathibistha inatosha, sasa niambie ukweli ni yangu au kuna mwingine…’akasema

‘Mimi sio Malaya bwana…’nikasema

‘Ndio maana nauliza isije kuleta matatizo..najua mimi nimeshatembea nawe, sina uhakika na mwingine je ni ya kwangu au kuna mwingine…?’ akaniuliza

‘Mimi sijui, maana mlichokifanya wewe na ndugu yako siku ile mimi sijui, mimi sijui na sitaki kujua, niache, ushaiharibu siku yangu , ondoka…’nikasema

‘Basi natosha, ninachoomba kwa mungu awe mtoto wa kiume…’akasema hivyo, na hakutaka kukaaa sana, akaondoka akiwa anaonekana ana furaha usoni , sio kama alivyokuwa amekuja.

‘Kwahiyo hebu kwanza nikuulize kuna jambo nilitaka niwe na uhakika nalo..hivi ulipogundua kuwa una mimba, ulikwenda kupima wapi, maana nataka mambo haya yawe kwenye kumbukumbu zangu, hapo kasema, ‘kumbe ni kweli’…’nikasema.

‘Kwanini unauliza hivyo…ina maana kweli kuna kitabu unatunga, au unataka jambo kama ushahidi fulani, ushahidi wa nini…?’ akaniuliza.

‘Nimeshakuambia naandika tu kujifurahisha, nilianza kama mzaha tu, lakini kadri siku zinavyokwenda naanza kufurahia,… na hasa hii kadhia, kuna muda.. inaniacha kwenye maswali mengi ya kutaka kujua zaidi,..unajua tena…na hata hivyo ni kawaida yangu kuwa na kumbukumbu, na usinifikirie vibaya, kwanini nafanya hivyo, au hupendi, niwe naandika, kama hupendi nitaacha tu…’nikasema

‘Ok.. nilikwenda kupima kwenye ile hospitali iliyopo karibu na kazini,…na nilifanya hivyo kwa vile sikuwa na amani, nilikuwa sijisikia vibaya vibaya, hali ambayo sijawahi kuihisi kabla, huko kupoteza siku zangu , inatokea mara kwa mara kwahiyo haikuwa ni sababu…hata hivyo wakati naenda kupima, nilikuwa kama siamini, maana …kama tukio lilivyokuwa ilikuwa kama ni ndoto…na sikuweza kuwa na uhakika, niweke hivyo tu…’akasema

‘Hukuwa na uhakika gani kuwa ni nani kati ya hao ndugu wawili au si..…au hukuwa na uhakika kwa vile..haiwezekani ulisema ..kitendo kilikuwepo au sio, … hapo usinidanganye kitu…mpaka hapo nahisi kuwa kuna kitu unanificha, halafu unajinasa mwenyewe hiyo kauli ‘sikuwa na uhakika..’nikasema

‘Nimekumbuka kitu…siku ile nilipokwenda kupima nilikutana na docta ambaye nafahamiana naye, naye kuna kipindi tulikuwa naye karibu baadae ndio akaoa, nikaachana naye,…sasa nikuchekeshe kitu,....’akasema.

‘Nichekeshe…’nikasema

‘Kumbe yule docta ni best sana wa shemeji….’akasema

‘Shemeji,…una maana huyo bwana’ko…?’ nikauliza

‘Na wewe bwana…sio bwanangu huyo..,..mwishowe utazoea hiyo kauli, mimi siipendi…’akasema

‘Samahani, naongea hivyo kwa vile tupo wawili wala usiwe na shaka…’nikasema

‘Sasa nahisi..au nilihisi huenda waliwahi kuongea kuhus mimi, kuwa nina mimba, nahisi hivyo kwa vile siku nilipokwenda kupima,..jana yake, au siku baada yake, nakumbuka, mjamaa aliniuliza…. , japokuwa hakuwahi kuniambia kuwa kagundua kuwa nina mimba..na nijuavyo aligundua hilo baada ya siku hiyo wakati alipokuja, na kuanza kuongea hayo kuwa anataka nimzalie mtoto…’akasema

‘Mhh, ...mambo ya huyo shemeji hayo….yanafanana sana na mambo ya mume wangu, , unajua hata wakati naandika, nikawa najiuliza huyo mtu ni nani, sura ya mtoto inafanana na familia yangu, ina maana huyo baba yao, eeh, atakuwa anafanana na mume wangu, …na na…hili tena,….unajua mume wangu ni rafiki mkubwa wa huyo docta wa pale…walisoma wote…’nikasema.

‘Ndio hivyo….mmh, sasa…mmh, unajua yote haya ni kutokana na ushauri wako, nisingelifikia hatua hiyo, wakati mwingine nafikia kujilaumu ni kwanini nilikusikiliza, ….usinielewe vibaya hapo kuwa sikuupenda huo ushauri wako.., ila nasema haya kwa vile naona kila hatua kuna mtihani fulani na naona inaweza ikafikia sehemu…hata sijui itakuwaje……’ akasema

‘Ni wasi wasi wako tu….unafikiri, unajua hayo yote nayafahamu na …kukushauri kwangu sikuwa na nia mbaya, nilijua haya yanaweza kutokea hivyo..na mimi nitayapokea kwa jinsi yalivyo, siwezi kukulaumu kwa lolote lile, unasikia,.., kwahiyo, wala usiwe na shaka kabisa…’nikasema

‘Kwahiyo unataka kusema nini hapo.., kuwa unajua ni nani, na huna shaka lolote kwa hilo…yaani hutanifikiria vibaya , tukaja kukosana…?’ akaniuliza

‘Hebu nikushauri kitu, hebu kwanza nihakikishie kwa huyo shemeji ni nani , ili niweze kupanga jinsi gani ya kumweka sawa, mimi nataka nije kuonana naye, ili niliweke hili jambo sawa, sawa..’nikasema

‘Mhh..kumbe bado…’akasema

‘Ni hivi…ninachoogopa ni wewe unaweza ukavuruga huu mpango kabisa…, wewe unachukulia hili jambo kirahisi tu, hujui ni jinsi kwenye mwenye mume atakavyojisikia akiligundua hilo, unataka mim nije kujuta kwanini nilikushauri, sitaki itokee hivyo kamwe, unasikia,...sasa nataka uniambie ukweli huyo shemeji ni nani?’ nikamuuliza.

‘Na wewe bwana , hapa nilijua unasema umeshamfahamu, na ulijua kitu kama hicho kinaweza kutokea,…ulikuwa na maana gani,..mimi naona haya tuyaache tu, yasije kukutia presha?’ akasema

‘Mimi nishakuambia ..kwa hisia zangu ni huyo mdogo wake mume wangu, kwasababu nyingi tu, kuanzia kufanana watoto na tukio zima kama ulivyoliezea, na , naaeeh…sioni mtu mwingine anayefanana na hivyo,… labda uniambie wewe, ni nani huyo, na kwanini…eeh, unaona ugumu kunihakikishia kuwa ni yeye, …mimi siwezi kufanya lolote, maana hanihusu kwa sana, japokuwa ni mume wa mtu,…hawa wanaume jaman…’nikasema.

‘Lakini…mbona umesahau kuwa ulinishauri hivyo, ukisema hawa waume jamani, unanishutumu na mimi au…’akasema

‘Ndio hivyo, ila …ukweli upo pale-pale, inauma sana, tena, sana, sijui ikitokea kwangu kama nitaweza kuvumilia, mimi aah, ..mimi siwezi,…ndio maana nilitaka nimfahmu huyo mtu ili madhara yasizidi kuendelea, umenielewa hapo…nataka niongee naye,nitajua jinsi gani ya kumweka sawa,…haya niambie ni nani huyo mtu….?’ nikamuuliza


‘Ni shemeji jamani…nimeshakuambia ni shemeji’akasema, na kusimama, kama anataka kuondoka,…sijui kwenda wapi, akageuka kuniangalia na mimi nikawa nimemuangalia, tukawa tunatizamana…


Kiukweli mpaka hapo bado mimi sikuwa na tashwishwi yoyote mbaya, maana kwa hilo neno ‘shemeji’ ndivyo alivyo kuwa akimuita huyo jamaa yake tangia awali, na nikajua anamuita hivyo kutokana na mimi, kuwa ni mdogo wa mume wangu…lakini bado naona kama anaogopa kunibainishia hilo, na kwa namna hiyo akazidi kunipa hamasa.

‘Hahahah, nilijua tu, kwahiyo sasa umenihakikishia, kuwa ndio yeye, au sio….marafiki wawili wana waume kutoka familia moja, japokuwa…wewe unapita tu, hahaha…kiukweli, nimefurahi, japokuwa,…mmh, namuonea huruma sana mke wake….’nikasema na mara ujumbe wa simu ukaingia kwenye simu yake, akausoma, na mara kwa haraka akasimama, akiangalia kule mlangoni, sikusikia sauto ya gari…kwahiyo sikuwa na mashaka kuwa kuna mtu kaja…

‘Unajua, …kuna mgeni anataka kuja, na sikutaka akukute hapa, wewe au mtu mwingine, na huyu mtu kawahi kabla ya muda,ujuo wako sikuwa na …..sasa sijui kwanini, mbona hivi…’akasema akijaribu kupigia simu, nahisi kwa huyo mtu, lakini naona simu ilikuwa haipokelewi..

‘Kwani una nini, mbona huna amani , ni nani huyo mtu…?’ nikamuuliza

‘Hata sijui itakuwaje…na nilishamuambia asije hapa mpaka nimpe nafasi, au aniambie kabla, sasa anajileta tu, mbona huu mtihani.’akasema sasa akiangalia mlangoni


‘Kwanini, mimi si rafiki yako…na huyo shemeji,…niambie ukweli..’nikasema

‘Ndio yeye….’akasema

‘Safi kabisa, …hilo sasa niachie mimi, wala usiwe na shaka,…na kwa vile mume wangu hajui kuwa nipo hapa, ..nitamtumia ujumbe kuwa nimepitia mahali, sitamwambia kuwa nipo hapa, nataka hili jambo tulimalize leo hii, au sio…’nikasema

‘Ina maana mume wako, hajui kuwa upo hapa, umekuja huku bila kumuambia, kwanini lakini, …?’ akaniuliza kama ana hamaki

‘Nilikuwa na kikao na muwekezaji mmoja, na bahati kikao hakikufanyika kwahiyo yeye anafahamu nipo kazini..mimi kwa hasira…maana huyo muwekezaji kanipotezea muda wangu maandalizi, halafu analeta ujumbe mwishoni kuwa kaahirisha kuja..ameniboa kwa kweli,…’nikasema

‘Mhh….’akasema akiangalia simu yake naona alitarajia kupata majibu fulani lakini hayaji.

‘Sasa sijamfahamisha mume wangu kuwa nimetoka, ngoja…nimtumie ujumbe…’akasema akiandika ujumbe kwenye simu…akatuma na kusema

‘Leo simu ya mume wangu haipo hewani, kulikoni…’nikasema

‘Labda kwa vile…’akasema na kusita….kwani mlango uligongwa


‘Huenda ni shemeji,...mungu wangu…’akasema

Nikiwa natabasamu tele mdomoni macho yangu yakaelekea kule mlangoni, nimuone huyo shemeji, akilini kwangu najua ni huyo huyo, mdogo wa mume wangu….shemejiiiii…

Nikamtupia jicho la pembeni rafiki yangu nikamuona akiwa anahangaika hana amani kabisa, sikuelewa ni kwanini, labda ni kwa vile hakutaka nikutane na huyo shemeji, lakini kwa muda huo sikujali, nilijua nitalimaliza nikikutana na huyo mtu, sasa nilimuona kama anataka kwenda kule mlangoni,...huku mkono mmoja kashikilia mdomoni…!!!


WAZO LA LEO: Tunapopeana ushauru, au tunapotoa ushauri tuhakikishe hicho tunachokifanya tuna uhakika nacho, kiimani ya kweli(kwenye dini zetu), au kiutarataibu uliokubalika na jamii zetu, ili matokeo yake yasije kutuathiri sisi wenyewe au kuonekana watu wa ajabu katika jamii zetu. Lakini muhimu tuangalie je mola analiridhia hilo, je ningelifanyiwa mimi ningerizika nalo…
 
SEHEMU YA 23


Mlango wa geti la nje uligongwa ndio,…!

Sio mlango wa nyumba yenyewe, maana hiyo nyumba imezungukwa na geti, , nina uhakika ni geti hili la nyumba anayoishi rafiki yangu…nikamtupia jicho rafiki yangu huyo,….nikamuona, akitoa macho kuangalia kuelekea kule mlangoni…

Ni kweli atakuwa huyo mgeni wa rafiki yangu, maana nilisikia sauti ya mlango wa geti ukilia,…geti linafunguliwa, sasa kuashiria kuwa huyo mtu kaamua kulifungua hilo geti yeye mwenyewe hapo ina maana gani, kuw huyo mtu kazoea kufika hapo, anapajua vyema.

Hapo ikawa kama kamchokoza rafiki yangu huyo, nahisi rafiki yangu hakutaka kabisa huyo shemeji tuonane naye mimi, kwa jinsi nilivyomuona akihangaika, na kwa jinsi alivyobadilika sura, usoni alionekana kutahayari…, mpaka nikamuonea huruma,…lakini nikawa sijali, kwanini …mimi sina nia mbaya, hanielewi tu…

‘Kwanini unapata shida hivyo, mkaribishe mgeni…’nikasema lakini rafiki yangu alibakia akiwa kashika kichwa, akiniangalia kwa macho yenye huruma, au…kama anataka kulia…


‘Hapana, sio leo jamani..sijajiandaa kwa hili, nahisi imekuwa ni haraka sana, …nahisi hatari…unasikia, rafiki yangu, wewe pitia mlango wa nyuma uondoke, sitaki matatizo hapa nyumbani kwangu, najua kabisa itakuwa hivyo….’akasema akishika kichwa.


‘Kwanini…mbona sikuelewi…’nikasema nikimuangalia kwa macho ya kujiuliza na yeye akawa ananikwepa kabisa kuniangalia machoni.

‘Tafadhali fanya hivyo….nitakuja kukuambia ni kwanini…lakini kwa hivi sasa ili kuepusha shari..ili , nisivunje uaminifu..unajua aliniomba tena sana nisije kumsema kwa watu, hadi muda muafaka ufike,…na nikifanya hivyo, ..na yeye…unanielewa hapo, haya nenda pitia mlango huo wa nyuma…’akasema

‘Mimi siendi mahali, lao nataka hili jambo lifikie mahali na mimi, niwe na amani , nahisi kuna …sijui nisemeje, unanifanya nianza , kama nilivyokuambia nitunge kitabu, sasa ni kwanini, maana matendo yako, kauli, zako zinanihamasisha nifenye hivyo, kifupi nahisi kuna kitu unaficha, ambacho ni zaidi ya hilo tulilokubaliana, sasa ningeliomba umkaribishe huyo mgeni, najua tutayamaliza,….’nikasema

‘Hapana, nielewe nina maana yangu kubwa sana, najua itafika muda hili itabidi liwe hivyo, lakini sio kwa leo, sio kwasasa…nakuomba mimi ni rafiki yako, niamini ninalokuambia…yanayotokea, na kauli zako…hapana, na iwe hivyo tu..ila nitakuja kukuelezea kila kitu..unajua, nitaumia sana ikifikia mahali pabaya….’akasema na mimi nikataka kusimama

‘Unataka kufanya nini sasa ?’ akaniuliza

Mimi nikamtizama kwa macho ya kujiuliza, akilini nilishadhamiria kitu, lakini sina uhakika nacho, na alipoona kweli nataka kuchukua hatua akasema

‘Rafiki yangu, ndugu yangu sivyo kama unavyofikiria wewe, tulia kwanza unataka kwenda wapi…nielewe maana hata mimi nilivyokuwa nikitegemea, imekuwa sivyo kabisa, nahisi nahitajia muda zaidi wa kulitafakari hili nisije kuleta hatari…..!’ akasema akiwa kasimama mbele yangu kama kutaka kunizuia


Mimi pale nilishikwa na butwaa, sikumuelewa kabia, ni kwanini anafanya hivyo,..nikabakia kumuangalia, uso ukiwa na maulizo mengi, kujiuliza kwingi, ..baadae nikasema

‘Mhh..hatari…hatari gani….mbona unanichanganya, au hatupo sawa tena,nieleze rafiki yangu kama kuna kitu kibaya kimetendeka nielewe mapema, hivi unanitesa kabisa, wewe hujui tu,…hapana mimi bado nakuamini, mimi bado nipo na wewe, usiwe na wasiwasi bwana…achana na mafikira potofu,…nikuambie ukweli, mimi nina hamu sana ya kumuona huyo shemeji yangu..’nikasema

‘Utamuona…kwanza ushamuona sana..ila kwa sasa naomba nipo chini ya miguu yako tafadhali…’akasema akiashiria kutaka kupiga magoti.

‘Unajua sijakuelewa, kwanini..…kila siku ni …shemeji, shemeji, nataka nimuone huyo shemeji, hata kama yupoje, labda unahisi hadhi yake haiendani na wewe labda, kama kweli sio huyo ninayefikiria mimi,… labda umekuja kutembea na mtu, asiyekustahili labda hivyo..mim hilo sijali kabisa , ilimradi kakupa kile ulichokitaka na mimi ndiye msiri wako…’nikasema

‘Hapana, sio hivyo…ninasababu nyingine kabisa, ya nia njema, …nielewe hivyo tu…’akasema

‘Mhh..mimi hapo sitakuelewa kabisa.., leo…eeh, hakuna jinsi, lazima nimuone huyo mtu, kama kaja yupo huko nje, mwambia aingie ndani, tuyamaliza hapa hapa…’nikasema na yeye akabakia kimia

‘Sasa unaogopa nini, mtu yupo huko nje, anasubiria, unajua naanza kuingiwa na wasiwasi, kitu ambacho sikuwa nacho dhidi yako, na hizi eeh…kauli zako zinanipa mashaka, ..kwanza najiuliza kuna hatari gani, kuwa itakuwaje, kuwa nitatoa hii siri nikimfahamu au..hahaha, mimi nimeshamfahamu, muite tuyamalize leo hii, ili na mimi niwe na amani..’ nikasema

‘Siwezi kufanya hivyo, for the sake of our friendship….kwa minajili kwa kuwa hata yeye mwenyewe hataki, na kama angelijua nipo na mtu asingelifika kabisa,…alishaniomba na akafikia kunitisha, kuwa ni..iwe siri yetu,…’akasema

‘Kukutisha kwa vipi….?’ Nikamuuliza

‘Bwana wewe liache kama lilivyo… na sijui kwanini unang’ang’ania hivyo, wakati hata wewe mwenyewe ulitaka iwe hivyo…hapana, acha tu, iwe hivyo hivyo.., nakuhakikishia muda utafika kila kitu kitakuwa bayana, ikibidi….’akasema na mimi nikatikisa kichwa kukataa.

Hapo akageuka kuangali mlangoni, …uzuri mlango ulifungwa..kuna namna ukifunga mtu wa nje hawezi kufungua, mpaka mtu wa ndani labda uwe na ufungua…sasa sikujua kama aliuegesha tu,…

Nikawa naangalia kule mlangoni nikitamani huyo jamaa aingie, lakini nahisi alikuwa kasimama, anasubiria mwenye atoke, au kahisi kuna …na mara nikasikia sauti ya viatu vya mtu kukaribia mlangoni …ka-ka-ka-ka..huyo mtu kavaa viatu vinavyotoa sauti,

Nakumbuka kuwa hata leo mume wangu wakati anaondoka kwenda kazini alikuwa kavaa viatu vinavyotoa sauti ukitembea, nikamwambia hivyo viatu vinavyotoa sauti sio vya kisasa, abadilishe, lakini hakutaka, siku ya leo alisema alivitamani kuvivaa viatu vyake maana vinamkumbusha mbali.

‘Bebii…upoooh…’nikasikia sauti ikasema kutoka nje…..

‘Bebii…..’nikajikuta nikisema hivyo, akili ikanipeleka mbali kabisa, hivyo ndivyo mume wangu alizoea kuniita, kipindi hicho, mambo hayajawa mambo, na sikumbuki tena kuniita hivyo,…na, mbona hata sauti ni kama …hapana…mmh,

Unajua nilihis moyo ukinienda mbio nikishindana na nafsi yangu, sikupenda kamwe nafsi inishinde, ..lakini hata hivyo, hata huyo mdogo wa mume wangu ana sauti kama hiyo, isipokuwa ya kwake inakwaruza-kwaruza hivi, hiyo imetoka sawa sawa naya mume wangu.

Na hata kufikiria hivyo, sio kwamba nilihisi kuwa ni mume wangu yupo huko nje, hapana siwezi kudanganya, akili yangu ilinizidi kunipa tashwishwi ya kumuona huyo mtu anayefanana mambo mengi na mume wangu.

‘Mume wangu yupo ofisini sio…’nikajikuta nasema hivyo kwa sauti ndogo.

Rafiki yangu akanitupia jicho aliposikia nikiweweseka hayo maneno, na ni kweli..nilikuwa na uhakika kuwa mume wangu yupo ofisini kwao, ana kikao muhimu sana, asingeliweza kuja huku,…ndio maana alizima hata simu yake kuchelea kusumbuliwa.

Sasa kwanini moyo wangu ukashtuka hivyo, niliposikia sauti hiyo, inayofanana nay a mume wangu, na kwanini kauli hiyo neno hilo, liwe sawa sawa na neno alilopenda kulitumia mume wangu enzi mapenzi yamepamba moto....hapo nikagwaya...

Lakini atakuwa ni shemeji tu huyo….

**************
‘Kumbuka ahadi yetu, kumbuka kuwa wewe ndio uliyenishauri hivyo, na naomba iwe hivyo ...nataka tukubaliane, ili lisije kuleta shida baadaye…’.

Nikiwa nasubiria rafiki yangu amkaribishe mgeni wake, nikahisi maneno hayo yakijirudia rudia kichwani mwangu kama onyo…na mara mtoto akaanza kulia,…na muda huo rafiki yangu yupo mlangoni, anataka kufungua mlango,

Mtoto alipolia akageuka kumuangalia, na akaniona mimi nasimama kwenda kumuhudumia, akawa na amani akashikilia kitasa kunyonga mlango ufunguke

Mimi mtoto alipolia kwa haraka nikasimama na kuelekea pale alipolazwa huyo mtoto, alikuwa kwenye kitanda chake chandarua , nikamkagua na nikaona kakojoa, kwa haraka nikaanza kumbadilisha, na kuwa muda huo akili ikawa kwa mtoto sikuwa na muda tena wa kuangalia kule mlangoni, ila nilisikia sauti kwa mbali ikisema;

‘Upo peke yako, …sijakuelewa, nauliza upo peke yako…mbona hunikaribishi ndani..?’ sauti hiyo niliisikia kwa kuunga unga, sikuweza kubahatisha vyema, maana kulikuwa na kelele za tv,na kulikuwa na kitu kama upepo nje, ulikuwa unapita, sikuweza kusema hiyo sauti inafanana nanni, sio ..kama ile ya awali alipotamka neno bebii, …na mara kukawa kimia.

Mtoto akawa kalala , basi mimi nikasimama sasa, sasa namuangalia rafiki yangu, sisikii wanachoongea kama wanaongea itakuwa ni sauti ya chini sana,…hapo nikatamani nisikie wanachoongea, nikatembea taratibu kuelekea huko mlangoni

Nikasogea taratibu, hadi nikakaribia mlango, na nilipofika , kwanza nilikuwa na nia ya kuwaingilia, na kumkaribisha huyo mgeni, lakini nilipofika hapo nafsi ikataka kusikia wanachokiongea,..na kwa muda huo rafiki yangu alikuwa kazama kwenye mazungumzo na huyo mtu, na nilichoweza kusikia kwa muda ni haya maneno, yalikuwa ya kuwewesa zaidi kiasi kwamba huwezi kuyasikia vyema, alisema ;

‘Kama upo peke yako unaogopa nini…’ni sautiya chini sana….kiasi kwamba sikusikia alichoongea zaidi

‘Wewe nenda, siku ya leo sio nzuri, muhimu unielewe, …ondoka haraka sana,..mimi hapa nipo peke yangu, lakini muda wowote anaweza kufika mtu, nielewe hivyo, kwaheri…oh..’akasema rafiki yangu na kutaka kuufunga mlango, na sasa akageuka, na kunikuta nipo nyuma yake, alishtuka, ..na kunitolea macho yenye dalili ya uwoga fulani hivi

‘Oh, ulikuwa unani…sikiliza…?’ akauliza kwa mashaka
 
SEHEMU YA 24

‘Vipi, mbona haingii…’nikasema, na akiniashiria nikae kimia, kwa vidole, akisema,
Sshiii…huku akitikisa kichwa, na mkono mmoja bado umeshikilia mlango ina maana hataki huyo mtu huko nje ajue kuwa kuna mtu ndani…lakini mimi nikajifanya sijamsikia, nikasogea karibu sasa nikitaka kufungua huo mlango.

‘Haya baadae nitakuja,…’sauti huko nje ikasema, hiyo sauti nikaisikia, sauti hiyo iliyonifanya nishtuke kidogo, lakini sio saana, maana haiwezi ikanihakikishia nilichokifikiria kwa muda, nikajikuta nikisema;

‘Mhh..ni nani huyo anaongea sauti kama ya mume wangu..?’ nikauliza

‘Ni shemeji…’akasema rafiki yangu akionekana kuwa na wasiwasi, na sasa akawa kasimama kati kati ya mlango kunizuia nisiweze kufungua mlango na kutoka nje.., huku akiniangalia machoni kwa yale macho ya mtu aliyetoka usingizini, au alikuwa analia, …au mashaka…hivyo!

Mimi nilimuangalia kwa mashaka, ...na sasa kitu kama hasira zilianza kujijenga, ni kwanini rafiki yangu mwenyewe ana nifanyia hivyo, kwa vyovyote iwavyo rafiki yangu hataki nimuone huyo mtu, ni kwanini… na inawezekana ikawa sio huyo shemeji…, na kama sio shemeji atakuwa ni nani..au anaweza akawa ndio yeye, lakini hataki tuonane naye uso kwa uso..ni kwanini…, labda kutokana na jinsi walivyoelewana. Hata hivyo, ..

Kwanza nilitaka nirudi, niyaache kama yalivyo, lakini nafsi ikasema, kwanini ..kwanini niyaache , hapana, ni lazima nihakikishe huyo ndiye kama ninavyofikiria, na kwanini nisimuone, ni kwanini nisimuone tukaongea naye, haya mambo niyaweke sawa yaishe tu, nina imani nikionana naye nikaongea naye, yataisha tu..nataka nimuone huyo, she-she…shemeji….

Hapo sikuwa na simile, nikasogea na kuubandua mkono wa rafiki yangu pale mlangoni, na kumpiga kikumbi cha kumsukumiza pembeni…, ili asogee, na hakulitazamii hilo, akapepesuka na kutaka kudonoka chini, mimi hilo sikujali, nikavuta mlango, ukafunguka…

Nje…hakuna mtu…lakini hisia zinanifanya nihisi kuna mtu, ila simuoni..yupo wapi..!nikageuka huku na huku , sioni mtu…

‘Mhh…haya..’nikasema hivyo tu

**********

‘Mbona hivi rafiki yangu, imekuwa ugomvi…’akasema sasa yeye akiwa kasimama mlangoni, akinitizama kwa mashaka,..

Muda huo ndio naangaza huku na kule kumtafuta huyo mtu kwa macho lakini huyo mtu haonekani,…haiwezekani huyo mtu ayeyuke hivi hivi, haiwezekani kwa muda huo mfupi awe keshafika getini na kutoka nje,..hapo nikataka kuhakikisha, nikatembea hatua chache kuelekea getini, lakini sikuona mtu.

‘Amekwenda wapi huyo mtu uliyekuwa ukiongea naye…?’ nikauliza

‘Nani, …keshaondoka bwana…?’ akaniuliza na kusema hivyo, sasa akionyesha uso wa kunishangaa mimi. Nikamtizamaa weeh, na kutikisa kichwa.

‘Hahaha, haiwezekani, …huyo mtu anapaa au….yupo wapi huyo shemeji….nataka nionane naye…kakimbije haraka hivyo na kutoka nje, haiwezekani, yupo wapi…’nikasema na nikaona kama uso wa rafiki yangu ukinawiri, ni kama vile alitarajia nitaongea kitu kingine kibaya, lakini akakuta nimeongea kitu ambacho hakikumkwaza, akasema;

‘Utamuona tu ndugu yangu..subira huvuta heri, njoo ndani tuongee , tumalizane, maana leo sina amani, natamani niondoke leo hii hii nikakae huko Zanzibar, mpaka siku yangu ya kuondoka kusoma ifike.., lakini haiwezekani, mambo ya visa bado hayajakamlika…lakini sikufukuzi, njoo ndani tafadhali…’akasema

‘Kweli ni bora niondoke zangu, huna maana wewe kabisa…yaani leo, sijui hasira zangu zimekwenda wapi..haya bwana fanya utakavyo, naona …aah, sijui kwanini,…mimi ninavyokujali na kukupenda malipo yake ndio haya, baya bwana…lakini…hiyo lakini iweke moyoni, ipo siku nitaimalizia,..’nikasema sasa nikitaka kuondoka

Nikakakumbuka kuwa nimeacha mkoba wangu ndani,…uone mambo ya mweneyzimunu yalivyo,..nikarudi ndani kwa haraka, muda huo nishakasirika nataka niondoke tu hapo.

Mimi kwa haraka nikarudi kuelekea ndani, ila haraka, uso umeshakasirika, hata nampita rafiki yangu anaonekana kuogopa labda nitafanya kitu..yeye kasimama kwa tahadhari,, akionekana hana amani…mimi sikutaka hata kumuangalia machoni.

Nilipofika ndani, mtoto alikuwa kaamuka, nikamuona anavyochezesha-chezesha vimkono vyake pale alipolazwa, nikavutika kumuangalia…unajua tena ukiwa na hulka ya kupenda watoto…, keshaamuka macho yake yamefunguka, ananitizama, kama vile ananiona na hapo hapo taswira za watoto wangu wakiwa wadogo zikanijia akilini.

Kila ninapomuangalia huyu mtoto , nawaza mengine ambayo siyataki, nahisi kama ni mtoto wangu, nahisi..kufanana…na… lakini hainijii akilini, na naishia kuhitimsha kuwa baba wa huyu mtoto atakuwa mdogo wa mume wangu…hivyo tu na kujiaminisha kwa msimamo wangu huo. Mungu mwenyewe ndiye anajua..

Nilisimama pale kwa dakiki kadhaa nikimkagua huyo mtoto kwa macho, kabla sijageuka kuondoka, na mara huko nje nikasikia sauti ya viatu kama mtu anakimbia, tatatatata…sauti ya viatu…ni sauti ile ile…atakuwa ni huyo jamaa kumbe alikuwa hajaondoka, atakuwa alijificha sehemu kwanini sikuwa makini kukagua upande wa nyuma wa hiyo nyumba,

Hapo, hapo…nikamuangalia rafiki yangu kwa macho yaliyojaa hasira, na kwa haraka nikawa nimeshauweka mkoba wangu mkononi, na sasa najiandaa kuelekea mlangoni, ili niweze kumuwahi huyo mtu, na rafiki yangu alikuwa hajaondoka pale mlangoni, malngo upo nusu wazi, lakini kaushikilia, na aliponiona akajua nataka kufany anini, akaufunga mlango na kuendelea kuushikilia…, kasimama kati kati ya mlango.

Nikamsogelea nikiwa na haraka nataka kutoka lakini safari hii alikuwa kajizatiti, akawa hasogei, hata baada ya kumsukuma anipishe nipite..na huko nje nilisikia mlango wa geti ukifunguliwa na najua atakuwa keshaondoka, kiukweli kitendo hicho kilinikwanza kweli……sasa ikawa kama shari, tunasukumana, na bado hataki mimi nitoke…baadae nikafanikiwa nikamtoa pale mlangoni, nikafungua mlango na kutoka nje,…nilishachelewa.

‘Kwanini unanifanyia hivi lakini, kwanini, ..?’ nikamuuliza sasa akiwa kasimama pale mlango akiniangalia tu kwa mashaka..baadae akasema

‘Ni bora nusu shari kuliko shari kamili, ni bora tu, iwe hivi, ili nisije kuharibu…najua utakuja kunielewa baadae, ..samahani sana rafiki yangu, nakuomba unielewe hivyo, sina nia mbaya kabisa, natimiza masharti yetu tuliyowekeana, na ahadi niliyoweka na huyo mtu, haitapendeza kabisa, nikifanya kinyume chake, nielewe hivyo tu, samahani sana rafiki yangu…’akasema

‘Kwahiyo kumbe ni kweli…eeh,’nikasema huku nikitikisa kichwa changu

‘Kweli kuhusu nini..nimeshakuambia huyo ni shemeji, hutaki kunielewa,sasa bora iwe hivyo hivyo tu…., na ukweli ndio huo, nimetimiza kile tulichokipanga, ni wewe sasa unayetaka kuharibu, sijui kwanini unataka kujisaliti mwenyewe…’akasema

‘Shemeji ..shemeji,…, hata mimi ninao wengi tu… haya kaaga na huyo shemeji yako na sitaki tena kumuona, ila ole wako, litokee tatizo, unasikia, ole wako…si unanifahamu nilivyo, na usifikiri nimekata tamaa, …nitamfahamu tu, huwa sishindwi jambo …haya kwaheri…’nikasema na kuanza kuondoka..

Nikageuka nyuma, nikamkuta rafiki yangu kasimama mlangoni mwa nyumba anapoishi,..bado ananiangalia kwa mashaka, ..mimi nikatikisa kichwa kama mtu anayesikitika, sikusema kitu zaidi…nikaanza kutembea kuelekea kwenye geti na hapo simu yangu ikaita.

Nilipoangalia mpigaji, nikagundua ni namba ya docta , huyu ni jirani yangu, sikutaka kuipokea kwa muda ule.., sijui kwanini. Docta ni mtu ninayejuana naye sana, na mara nyingi hunipigia simu tunaongea naye sana, huyo kwa viwango naweza kumweka kwenye nafasi ya marafiki zangu ninaoaminiana naye sana.

Kwa muda ule sikutaka kuipokea simu yake maana mara nyingi akinipigia tunaishia kuongea mengi sana yaliyopita, kutaniana…kwahiyo nikadharau, kwa vile akili yangu haikuwa sawa, nikakata simu

Baadae alipopiga tena, nikajua kuna jambo, nikapokea

‘Upo wapi zilipendwa…’ akasema kiutani, najuana naye kiukweli

‘Acha utani wako, nipo kwenye …jambo muhimu, tutaongea baadae, naelekea nyumbani…’nikasema, yeye akasema niende kwake.

‘Nije kwako kuna nini…?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Pitia hapa ni muhimu tuonane…kama unaelekea nyumbani…’akasema

‘Sawa…’nikasema , lakini sikuwa na shauku , na moyoni nilipanga nisipitie kabisa, namfahamu , tumezoeana kihivyo …nitakuelezea baadae ni kwanini nimezoeana naye hivyo

Nilielekea pale nilipoweka gari langu na kumlipa huyo kijana ambaye ninamuamini sana, nikaingia kwenye gari, na wakati nataka kuondoka, yule kijana akasema

‘Shemeji naye alileta gari lake, nilisafishe … , lakini hakusubiria nimalizie kusafisha, anaonekana ana haraka sana, ameondoa gari kwa haraka sana, sio kawaida yake….’akasema

‘Shemeji gani…?’ nikamuuliza na mara honi ikapigwa nyuma ya gari langu, kulikuwa na gari lilikuwa linataka kuingia, basi,…sikuweza kuongea na huyo kijana, ikabidi nisogeze gari langu mbele kwanza, na nilipomaliza, nikafungua kiyoo cha gari, kutizama nje, kumtafuta huyo kijana, nikamuoana anaongea nawateja wake, nikaona isiwe taabu…nikapandisha kiyoo changu kuanza kutoka nje ya eneo lile.

Nikabakia kwenye kitendawili,..ni nani shemeji, ..ni kwanini rafiki yangu ananificha, kuna nini hapa….akili ilikuwa bado imefungwa kabisa….huwezi amini, ilikuwa hivyo…

Wakati nakaribia nyumbani, nikaona nipitie supermarket, ninunue vitu fulani,…lakini nilihisi moyo wangu ukiwa hauna amani, sijui kwanini,..hata hivyo nikasema labda ni hayo mawazo, ya rafiki yangu…nikasimamisha gari…,lakini akili ikawa haitulii…

‘Huyu kijana kasemaje, ‘shemeji naye alileta gari..’ naye shemeji, rafiki yangu shemeji..shemeji, shemeji….si alisema shemeji, au sikumsikia vyema, huyu shemeji atkuwa ni nani, ni mume wangu, hapana, mume wangu yupo kazini,…ana kikao muhimu sana, hawezi kutoka, aliniambia, hatatoka kazini mapema..

Nikataka kumpigia simu mume wangu, ili nihakikishe,…lakini nikaona nitamsumbua tu, sasa hivi atakuwa kati kati ya mikutano yake…nikaachana na wazo hilo, nikaingie hapo, sokoni-duka, na kununua vitu nilivyovitaka.

‘Oh, nimekumbuka , huyo atakuwa ni shemeji… mdogo wa mume wangu ..’nikasema kwa suti, niliwazia hivyo kwasababu huyo kijana kipindi fulani nilifika akawa analisafisha gari langu na mara mdogo wa mume wangu akafika, na aliponiona akasema

‘Shemeji kumbe umeniwahi, basi ngoja amalize, na mimi nitafutia, vipi shemeji hatuonani…’akasema na tukawa tunaongea, na huyo kijana alipomaliz kusafisha, akafika na kusema

‘Shemji zamu yako…’alipotamka hivyo sisi tukacheka,…basi akawa kila akionana na huyo shemeji yangu anamuita hivyo shemeji…sasa sijui kuwa alikuwa na maana ya huyo shemeji au la…mmh, shemeji, shemeji..hapa kuna kitu, kimejificha, nah ii itakuwa ufungua wa kuupata ukweli.

Sikuwa na tabia ya kumdhania mtu vibaya,… hasa mume wangu, au huyo rafiki yangu, niliwaamini sana, kutokana na jinsi tulivyoishi,…mume wangu ni mwaminifu sana, na namuamini kwa hilo,sikuwa na shaka naye hata kidogo, licha ya tabia hiyo ya kulewa, ambayo ilianza baadae tu…hata sijui ni kwanini, lakini binadamu bwana….

Kiukweli hadi hapo sikutaka kuingia na dhana mbaya dhidi ya mume wangu, wala rafiki yangu…ndivyo nilivyokuwa, utaniona ni mtu ajabu lakini , sijui nisemeje, na ilinisaidia sana kuwa na tabia hiyo kipindi , hadi lilipotokea hili tukio.


Mimi mwenyewe ili kulimaliza hilo akilini, ili nisije kuingiwa na shetani mbaya wa dhana chafu, nikahitimisha kichwani kwangu kuwa, huyo aliyefika pale nyumbani kwa rafiki yangu atakuwa ni mdogo wa mume wangu, na kwa kujiridhisha tu, nitarudi kwa huyo kijana tena kumuulizia vyema au nitakwenda kwa shemeji, yaani mdogo wa mume wangu. Hilo nikalimaliza hivyo kichwani. Lakini bado nikasema;

‘Huyu rafiki yangu kuna kitu ananificha..na hicho kitu ni zaidi ya tulivyokubaliana, na nafsi yangu haitatulia mpaka nikigundue, nitakigundua tu,..’


Wakati huo naendesha gari kulekea nyumbani….mara simu yangu ikaita, na kuangalia nikakuta ni mmoja wa wateja wangu , nikaipokea simu, muda huo ndio nataka kuingia kwenye gari,

‘Unasemaje,…nini, ajali, …wewe una….hapana, sijasikia,…ndio naelekea huko, wapi lakini…’ nikahisi kitu kama kikigonga kichwani, kizungu zungu,…sikujitambua, baadae nafungua macho najikuta nipo nimelala chini, watu wamenizunguka.

‘Ajali….!!!’ Nikajikuta nimesema hivyo, kwa haraka nikainuka kutaka kuingia kwenye gari langu.



WAZO LA LEO: Ni kweli tunahitajia kitu, ni kweli tunataka kupata lakini je ni sahihi kupitia njia ambayo sio sahihi, kwa vile tu, muda umekwenda, kwa vile upo kwenye shida, kwa vile tu…je unauhakika utakipata na kuishi muda wa kukifaidi hicho kitu…..tuwe makini na mambo tunayotenda huku tukiangalia uwepo wetu hapa . Tumuombe mungu atupe hekima ya kutafakari mambo kabla ya kuyafanya Aamin.
 
SEHEMU YA 25


‘Ajali….’ Ilikuwa kauli yangu ya awali pale nilipozindukana, sijui kwanini hali hiyo ilinitokea,..kupoteza fahamu,…mmh.. nilijiuliza pale bila kujua sababu ni nini,.. labda ni kuchoka tu, mambo yamekuwa mengi kupitiliza…, niliinua uso na kuwaangalia watu , maana walishafika kuangalia kuna tatizo gani, …haikuchukua muda mrafu hiyo hali.

Bahati nzuri, nahisi ni dakitari, alikuja kutokea hapo kwenye hilo jengo la soko-duka, alikuwa kavalia nguo za kidakitari, hilo jengo ni kubwa lina ofisi nyingi na mojawapo ni dispensary. Na kuwa huo alikuwa kachuchumaa karibu yangu, na akawa ananiangalia tu, huenda alishanichunguza nikiwa nimepoteza fahamu

Mimi kwa haraka nikajaribu kusimama,…nikajikuta narudi chini,.. nilihisi kizungu zungu kidogo, huyo docta akanishika mkono, kunisaidia, nikaa vyema, nikawa najifunika vizuri, kushusha gauni vyema….

‘Upo ok.., unajisikiaje sasa..?’ akaniuliza na mimi nikawa kimia, nikitafakari, kuvuta fikra.

‘I hope so, nipo ok…’nikasema

‘Mhh, unahitajika kutulia kwanza, naona hali yako bado haijawa sawa, unahitajika mapumziko kidogo, sijaona tatizo lolote kubwa kwako, lakini ni vyema, ukafika hospitali kwa uchunguzi zaidi, hapo ndani kuna zanahati, nahudumia hapo, kama hutojali unakaribishwa...’akasema huyo docta?’ akaniuliza

‘Nipo ok…nahisi hivyo, natumai, hunidai kitu…’nikasema

‘Hamna…sijafanya lolote, nilikukagua tu Je utaweza kuendesha gari mwenyewe…, au tumpigie mume wako simu,au jamaa yako, simu yako hii hapa, tukusaidie kumpigia…?’ akauliza huku akiwa kashikilia simu yangu, nahisi waliichukua wakitafuta namba ya jamaa yangu yoyote.

‘Hapana….niko ok..’ Ni alipotaja kuhusu mume wangu, ndio akili ikafunguka, nikakumbuka ile simu niliyopigiwa na hapo hapo kwa haraka nikaingia kwenye gari…

‘Ahsante sana kwa huduma yako,….’nikasema

‘Hamna shida, uwe mwangalifu tu, na nazidi kukushauri fika hopsitali, usizarau hilo laweza kuwa chanzo cha tatizo , na huwezi kulijua mpaka ukapimwe…’akasema huyo docta na mimi nikawasha gari na kuanza kuondoka.

Niliendesha gari langu kutoka eneo hilo, na muda huo sikuwa na wazo la kuangalia vitu vyangu kama vipo salama,..sikuwa na wazo la kuangalia simu yangu ambayo, alinikabidhi huyo docta niliweka pembeni ya kitu,..kumbe simu yangu …ilikuwa imezima..watu wananipigia wanipati.

Nilipokaribia eneo la nyumbani kwangu ndio nikakumbuka kuwa dakitari alisema nipitie kwake,… lakini niliona haina umuhimu kwa muda huo, kwanza nifike nyumbani kwangu, nijue kinachoendelea,…maana mpigaji simu, nakumbuka alisema,..

‘Kuna ajali, gari la mume wako limepata ajali, lakini hayupo….haonekani…. , tunahisi huenda kaimbilia nyumbani kwake… watu wanamtafuta haonekani sijui wapi alipo….’nilikumbuka hiyo sauti.

‘Ajali halafu yupo nyumbani, haonekani wapi alipo…?’ nikajiuliza tu, hata sijui nifanyeje, lakini muhimu nikaona nifike nyumba kwangu kwanza, nianzie hapo.

Ndio nikakumbuka simu yangu, nikaichukua na kuiwasha sijui kwanini ilizimika, maana chaji ipo ya kutosha, nia yangu nikujaribu kumpigia mume wangu… lakini ujumbe nyingi zikaanza kuingia, kuashiria kuwa watu wengi walikuwa wakinitafuta, nikapokea simu iliyokuwa inaita kwa muda huo.

Alikuwa ni docta jirani yangu….

‘Upo wapi…’ akaniuliza kwa haraka hivyo

‘Nipo , ndio nafika kwangu…’nikasema,

‘Ok sasa ni hivi, fika hapa kwangu mara moja ni muhimu sana, mume wako yupo hapa,…’akasema

‘Yupo salama lakini…?’ nikauliza

‘Ndio…anaendelea vizuri…mengine utayajua ukifika hapa….’akasema.

‘Haya…nakuja…’nikasema

Nikarudisha gari nyuma, maana sio mbali na kwangu, tunatenganishwa na bara bara na ukuta…

‘Umeshafika…’akanipigia tena docta, nilishangaa kwanini kapiga tena kwa haraka, nikaanza kuhisi kuna tatizo kubwa.

‘Nimeshafika eneo la getii ya nyumba yako....vipi kuna maendeleo gani…maana huyo mtu aliyenipigia simu, alisema kaona kama gari la mume wangu limepatwa na ajali, …lakini sizani kama ni yeye, kwani ninafahamu yupo kazini, yupoje mume wangu, ni yeye, kaumia, …’nikasema.

‘Sawa ingia ndani, tutaongea ukifika, hajambo….’akasema.

‘Nataka kujua ni kweli docta, niambie yupoje..?’ nikauliza.

‘Mume wako ni kweli kapatwa na ajali..…, na yupo hapa nyumbani kwangu, ...’akasema

‘Kwanini hajaenda hospitali, …?’ nikauliza

‘Ukifika tutaongea, kama ni kwenda hospitali..au la…wewe ukifika unaweza kusaidia hilo, maana mwenyewe hajataka kwenda hospitalini ...’akasema

‘Mhh..haya nakuja…’nikawa najiuliza imekuwaje, nijuavyo mume wangu alikuwa kazini, sasa hiyo ajali ilitokeaje, na wapi…nikawa najiuliza.

Basi nikaingia nyumbani kwa docta


************
‘Oh, shemeji bora umewahi kufika, naona uliendesha kwa mwendo usio wa kawaida, msifanye hivyo....’akasema jirani yetu huyo mmoja, ambaye nahisi aliniona wakati naingia na gari kwa mwendo wa kasi.

‘Mumeo ni kama unavyomuona kapatwa na ajali mbaya sana, kwa jinsi nilivyoambiwa na watu, …na ameponea kwenye tundu la sindano,hapa tumempatia huduma ya kwanza , hata hivyo alitakiwa awepo hospitalini kwa hali jinsi ilivyo...cha ajabu mumeo amekataa kata kata tusimpeleke hospitalini,…’akasema

‘Kwanini jamani, hili sio swala la kuhitaji yeye kukubali au la, docta, rafiki yako huyo, unambembeleza kwa hilo…?’ nikauliza

‘Yeye alisema afikishwe hapa nimpatie huduma ya kwanza, anahisi hana tatizo,..’akasema

‘Kwahiyo..?’ nikauliza

‘Muhimu afikishwe hospitalini haraka iwezekanavyo, ...’akasema docta.

Mimi sikuelewa, kwanini mtu apatwe na ajali ya gari, watu badala ya kumpeleka hospitali, wanamleta huku nyumbani kwa docta,...labda, au sijui alikuwa na maana gani kutibiwa nyumbani.

‘Shemeji kwa hali ilivyo, tunahitajika tumuwahishe hospitalini, hatuwezi kumsikiliza tena yeye, na kwa vile wewe upo, utawezesha hili, tulishapigia simu gari la wagonjwa linakuja,,....’akasema docta.

‘Haya, mimi sioni kwanini tusubiria hilo gari la wagonjwa, si tunaweza kumbeba hadi kwenye gari langu,au…?’ nikauliza

‘Gari la wagonjwa linakuja na kitanda cha kumlaza, …isije kuleta matatizo mengina lakini kwa vile limechelewa, basi tumbebe tu, awahishwe hospitalini…’

Nilimuangalia pale alipolala, shati ni vipande vipande…uso umevimba, na michubuko…

‘Sasa hivi kapatwa na usingizi kwa dawa nilizompa…’akasema docta

‘Basi abebwe hivyo hivyo, afikishwe hospitalini…’nikasema

‘Ni kweli, lakini lazima atazindukana, na ataweza kuhisi maumivu kwa sasa , alikuwa kama kachanganyikiwa alivyoletwa hapa…’akasema

‘Kwahiyo aliletwa kumbe…?’ nikauliza

‘Kuna mtu alikuwa anamsaidia, alikuja naye, wakati mimi nataka kutoka nje..kiukweli alikuwa akitembea kwa shida sana, na muda huo hajaanza kusikia maumivu bado, nahisi sasa ataanza kuyasikia, nimempa dawa za kutuliza maumivu zitasaidia kidogo…’akasema

‘Mhh, ...huyu mtu ana hatari kweli…angelifika hospitalini kwanza, kwa hali hii jamani anakuja kutibiwa nyumbani kama mhalifu…’nikasema,

‘Hayo hayana maana kwa sasa, hakuna haja ya kusubiria hilo gari la wagonjwa, tulionelea kama gari la wagonjwa lingelifika mapema, tungeliweza kumfikisha hospitalini bila kukwazika na foleni, na kuzidi kulete athari mwilini.’akasema docta.

Docta akatoa kitanda chake ca kukunja, wakasaidiana kumweka mume wangu kwenye hicho kitanda, sasa alikuwa kilalamika maumivu., wakamtoa nje na kumlaza kwenye kiti cha nyuma cha gari langu, na tukaanza safari ya kuelekea hospitalini.

Ndani ya gari pamoja na docta alikuwepo mtu mwingine na jirani mmoja, na hapo ndio nikaanza kusikia jinsi ilivyokuwa, lakini akili haikuwa sawa kusikiliza wanachoongea….

‘Nimeambiwa hiyo ajali ni ya aina yake, ukiambiwa kuna mtu katoka hapo huwezi kuamini…’akasema

‘Kwahiyo ilikuwaje, uliona ilivyotokea…?’ akaulizwa

‘Hapana , mimi nililiona hilo gari, halina thamani tena…’akasema

Sikutaka kusikia wanachoongea, kwani wanavyozidi kuongea hivyo, ndio nazidi kuogopa, nilitamani kuwaambia wanyamaze..sijui ilikuwa, wakanyamaza hadi tunafika hopsitalini.


Kila nilipokuwa nikimtupia macho mume wangu, wakati sasa anatolewa kwenye gari kuweka kwenye vitanda maalumu vya wagonjwa, ndivyo nilivyoanza kuona kuwa kweli mume wangu yupo kwenye haali mbaya, hali yake ilishaanza kubadilika, alionekana kama anazidiwa, na hapo wasiwasi wangu ukazidi, na hadi anaingizwa hospitalini,sikuwa na amani, nilimuona kama kapoteza fahamu..

Mwili uliniisha nguvu kabisa, lakini nikajitahidi kutembea hadi sehemu ya kusubiria…nilijiuliza tatizo ni nini hasa, ..maana docta alisema mume wangu hajaumia sana. Hapo sikuwa na sababu za kuvumilia, nikamuendea docta, muda huo alikuwa akiongea na simu.

‘Docta kuna nini tena kwa mume wangu....?’ nikamuuliza, na yeye akaniangalia machoni, na hakusema kitu hapo hapo, lakini baadaye akasema;

‘Tutajua baada ya uchunguzi, hivi sasa siwezi kusema lolote, lakini kila kitu kitakuwa sawa....ngoja wakamchunguze na kumpiga x-ray. Na utra sound, tutakuja kufahamu hilo…’akasema, sasa hakusubiria akaelekea huko alipopelekwa mume wangu, chumba cha wagonjwa mahututi.

‘Docta…’nikamuita, nilitaka kumuambia asichelewe kunipa taarifa, sijui kama alinielewa, yeye alinionyeshea ishara kuwa nitulie, nisijali kwa mkono,


**********

Dakitari huyu pamoja ya kuwa ni jirani yetu,pia ni rafiki mkubwa wa mume wangu na alikuwa mpenzi wangu wa awali kabisa ,kabla sijakutana na huyu mume wangu na wazazi wangu walitaka sana niolewe na yeye, lakini mimi nilipingana nao kwani hakuwa ndio chagua langu. Wazazi wangu waliona yeye ndio hadhi yangu, kiuchumi na kielimu.

Kuna sababu za msingi, zilinifanya nisioelewe na yeye, mojawapo ni kuwa mimi nilikuwa nimempenda huyu mume wangu bila kujali hali yake ya kiuchumi. Nilikuwa na sababu zingine tu ambazo hazina umuhimu wa kuzitaja hapa kwa sasa.

Tulikuwa nje sasa tukisubiria,..mimi pale sina amani kabisa…na haraka nikataka nipate angalau mtu wa kuongea naye angalau niwe na amani, ndio nikampigia rafiki yangu simu, nikamwelezea kuhusu ajali iliyompata mume wangu..
 
SEHEMU YA 26


‘Unasema nini kapatwa na ajali saa ngapi…?’ akauliza, kama vile haamini, na mimi nikamuelezea jinsi nilivyosikia.

‘Oh, labda…ilitokea muda ule, na kumbe ndio hiyo watu wanaiongelea, kuwa hajapona mtu kwenye hilo gari, ..nahisi sio hiyo maana wanasema hawezi mtu kupona kwa jinsi gari lilivyo…oh, kwanini aliendesha kwa mwendo kasi, kiasi hicho…’akasema

‘Hata sijui, maana mimi najua alikuwa kazini, na muda ule ni wa kikao, kwasababu niliongea na mtu mmoja alikuwa kwenye hicho kikao chao, hata mpaka natoka pale kwako, najua yupo kwenye kikao, sasa …alitoka saa ngapi..hapo sijui…’nikasema


‘Oh ..na ile kona ni mbaya…’akasema

‘Kona gani…?’ nikamuuliza

‘Acha ile kona ya kutoka kwangu , unaipita hadi ile kona ya bara bara inayokwenda kuelelea kwenu…ndio nimesikia hiyo ajali imetokea hapo, lakini sizani kama ndio hiyo ya she- , …ya mume wako…’akasema, nilisikia mtoto analia, akawa anakat akata maneno.

‘Oh, mungu wangu wakati napita hapo niliona watu wamekusanyika, sikutaka kuangalia, maana nilikuwa na haraka, ina maana…sasa huko alitokea wapi, …mbona kupo kinyume na barabara ya kutokea kazini kwao…?’ nikauliza

‘Labda…alipotoka….hata sijui…hilo tuliache tu…’akasema

‘Hapana,..tuliache kwa vipi, …yaani, muhimu ni kujiuliza huko alifuata nini, na….oh, mungu, ….mungu amjalie apone tu..,..maana hali ilibadilika ghafla tulipofika hapa hospitalini, naogopa kweli rafiki yangu…’nikasema

‘Mhh…muhimu ni hali yake,…hiki kitoto kinasumbua, nakiogesha hapa,…basi, usijali rafiki yangu, mengine hayana tija, atapona tu kwa uwezo wa muumba, …’akasema

‘Ni kweli,…mengine sijui yapi hayo…haya, ndio hivyo rafiki yangu, ni siku ambayo sitaisahau kabisa, maana njiani napo nilikutwa na mikasa, nikiwa soko-duka, nilipoteza fahamu ghafla..’nikasema

‘Ulipoteza fahamu…!!!, ilikuwaje tena jamani… pole, na wewe umezidi kujiongezea mawazo, mengine yaache yatajipa yenyewe, ukitaka kufahamu kila kitu unaweza kuathiri ubongo wako…Haya utanipa taarifa kinachoendelea…’akasema

‘Sawa nitakujulisha..’nikasema na kukata simu.

*************

Baadae docta mmoja akaja, akasema wameshaondoa ile hali mbaya, hakuna matatizo tena, hakuna athari za ndani, kwahiyo mume wangu atapelekwa chumba cha kulazwa wagonjwa wa kawaida, baadae kweli akatolewa huko ICU,

‘Hii ina maana kuwa hana tatizo kubwa…’akasema docta jirani yangu, aliyekuja baadae

‘Kwahiyo tunaweza kwenda kumuona….?’ Nikauliza

‘Ndio..sizani kama kuna kikwazo…’akasema

Tulipofika kwenye hicho chumba alicholazwa mume wangu, tulimkuta kama kalala, kafumba macho, kalala kaangalia juu, nilimkagua kichwani kafungwa fungwa, umebakia uso,..na shingoni kavaliwa dude kuashiria huenda kuna hitilafu shingoni….hiyo ni dalili kuwa kweli alikuwa kaumia, japokuwa alijikaza kuonekana kinyume chake..

Baadae akafungua macho, nikamsogelea nilimuangalia mume wangu pale alipolala, nikahisi machozi yanataka kunitoka…kalala huku kaangalia juu, hakutaka hata kugeuza kichwa kuniangalia, labda hawezi kugeuza shingo,..nikamsogelea pale kitandani, na hapo akajitahidi kuniangalia, kwa kugeuza macho, nikaona machozi yanamtoka…akasema

‘Pole sana mume wangu, mungu ni mwema utapona tu…’nikasema

‘Nisamehe sana mke wangu, ni-sa-sa- mehe…’akasema huku machozi yakiendelea kumtoka, nikachukua leso yangu na kumfuta, sikuelewa, nahsi ni hiyo hali,…hata mimi pale machozi yakawa yananilenga lenga, nampenda sana mume wangu, na kumuona kwenye hiyo hali, niliumia sana, mawazo yalinipeleka mbali sana.

‘Usijali utapona, tu…mume wangu…’nikajitahidi kusema hivyo.

Sasa akafumba macho, akawa anahema taratibu, na hilo lilinipa moyo, kuwa kufumba macho huko sio kwa ubaya, nikasema

‘Mume wangu utapona tu..tuzidi kumuomba mola…, umenielewa eeh, docta amesema hakuna tatizo kubwa…’nikasema, lakini akilini nikawa najiuliza ni kwanini kakimbilia kusema; nimsamehe…labda,…kawaida mtu akiumwa hujua hatapona ndio anaomba msamaha kwa watu, labda…

‘Atapona tu…’nikasema hivyo

‘Ndio atapona docta kasema ni athari ndogo za kuteguka …na ngoja tusubiria vipimo halisi havijatoka kwanza…’akasema docta huyo jirani yangu.

Baadae mume wangu akapitiwa na usingizi, na tuliambiwa tumuache alale, sisi tutoke nja, tukafanya hivyo.

Na wakati tupo nje, ndio nikajaribu kuwauliza watu walikuja nasi, yupo docta , na jirani mwingine na mfanyabiashara aliyenipigia simu, yeye alishafika, wengine yule mwingine tuliyekuja naye alishaondoka, huyu mfanyabiashara anasema yeye alishuhudia hiyo ajali,…

‘Kwani ajali hiyo imetokeaje..?’ nikauliza

‘Imetokea ile kona ya kutoka barabara kuu, kuingia barabara ya mitaa inayoelekea kwako, mume wako alitokea mitaa ya kutokea Uzunguni, mimi nilikuwa barabara kuu naelekea kwingine, nikasikia huko nyuma paaah, mlio wa kuogonga, unajua nilikuwa naendesha sikuona ilitokeaje, nikasimamisha gari, na kutoka nje…’akasema

‘Ina maana ni huu mtaaa wanaouita ‘Uzunguni..’..huko alitokea wapi, …huko si ndipo anapoishi rafiki yangu, mbona mimi nilikuwa maeneo ya huko…, sijamuona ….?’ Nikasema na kuuliza

‘Ndio hivyo..yawezekana alikuwa anaendesha kwa mwendo kasi, nahis alikuwa akiwahi jambo, au angelikuwa mhalifu tungelisema anawakimbia polisi…’akasema huyo mfanyabiashara

‘Mhh, hata sielewi, na hana tabia ya kuendesha gari kwa mwendo kasi..sio kawaida yake…’nikasema

‘Mimi nilijua mlikuwa naye labda…akawa anawahi kitu nyumbani, ..kama ulikuwa maeneo ya huko…’akasema jamaa mwingine.

‘Oh, hata sijui…sikumuona kabisa maeneo ya kule…hakuna mtu aliyemuona,.., labda kwa vile nilikuwa ndani naongea na rafiki yangu..labda kuna kitu alikuwa akikifuatilia, akapitia njia hiyo..akitokea wapi sasa…mmh, hata hivyo ni kwanini akimbize gari hivyo…’nikasema.

‘Ni ajali tu…’akasema docta

‘Kiukweli ana bahati sana, maana ukiliona hilo gari, utasena hakuna mtu aliyetoka humo ndani, halitamaniki, alikuwa kwenye mwendo kasi sana, ..na gari lenyewe baadae liliwaka moto, na hata watu walipouzima, lilikuwa limeshateketea kabisa…’ akasema jirani.

‘Oh, ...niliona ajali hapo njiani wakati nakuja, lakini sikujua ndio hilo ya gari la mume wangu,....,’nikasema

‘Sasa mimi nawashangaa huyo mtu aliyemleta hapo nyumbani kwako docta, badala ya kumkimbiza hospitalini, alikuambia ni kwanini alifany ahivyo?’ akaulizwa docta.

‘Nahisi alichanganyikiwa, na labda hakutaka ijulikane ajali hiyo imetokea wapi, labda maana tunajisema wenyewe tu kuhisia,..sabbu kubwa ni kuwa alichanganyikiwa maana haina maana hapo…, gari si lipo, kama ni wazo hilo, la kuficha kuwa ajali ilitokea wapi…’akasema yule mfanyabiashara.

‘Unajua watu walipofika kwenye hilo gari, walijua wanafika kutoa maiti tu..mimi mwenyewe nilishashika kichwa nilipogundua kuwa ni gari la mumeo…lakini watu walipofika hapo, wanashangaa kuona ndani ya gari hakuna mtu…ina maana huyo mtu alitoka kabla ya kugongana au alirushwa nje ya gari…’akaelezea

‘Na walipoona hivyo hakuna mtu, wasamaria wema wakaanza kuhangaika kutafuta dereva yupo wapi, lakini hakuonekana kabisa…mimi mwenye nahangaika kukupigia, simu inatumika, mara hupatikani mara…baadae ikawa haipatikani kabisa….’akasema huyo mfanyabiashara.

‘Mimi hata sijui….mume wangu jamani, apone tu,..sikujua kuwa ni gari lake wakati napita pale, nilikuwa na mawazo mengi, na kama ni ajali nilitegemea kwingine kabisa sio njia hiyo...’nikasema

‘Gari halithaminiki, hakuna kumbukumbu yoyote ndani,..maana lilikuwa bado haliingiliki, baadae mimi kwa vile nalifahamu ni la nani, taratibu bila kuwaambia watu lolote, nikaanza kufuatilia, kukupigia simu ukawa hupokei, baadae mimi wazo likanijia...

Nikaamua kwenda nyumbani kwanu, na nimefika pale haupo, na mumeo hayupo,,…nikaona hapa, isije ikawa mtu kaungulia ndani ya gari hatukuona vyema, nikataka kurudi tena kuhakikisha,…sasa wakati natoka pale kwenu, ndio nikakutana na jamaa mmoja rafiki yangu, akaniambia, kuwa kakutana na mumeo, yupo kwenye hali mbaya, …kaingia nyumbani kwa docta.

‘Mhh, hapo kwa haraka nikahisi aliruka alipohisi ajali, lakini mmh, yatakiwa uwe mzoefu kweli kama askari, sijui…yaani hapo ni kitendawili mpaka mwenyewe ajae kutuambia…’akasema

‘Hata hatujui alifikaje kwa docta,…..rafiki yangu mmoja alikuwa anapita na gari lake, ndio akamuona yupo nje ya mlango wa docta akiwa kasimama, kashikilia mlango, ..yupo hoi,..kama aliyepatwa na ajali, ana damu, shati limechanika,..ikabidi asimamishe gari kuja kuangalia kuna tatizo gani, ndio akamuona yupo kwenye hali mbaya,… akamsaidia kuingia naye ndani,kwani aliadai aingizwe humo ndani kwa docta.

‘Nikamuuliza alimuachaje …hali yake vipi, maana siamini, mtu katokaje kwenye hilo gari…’akasema.

‘Akasema kumbe docta huyu jirani yenu yupo likizo, walimkuta yupo hapo ndani, basi ikabidi aanze huduma ya kwanza, akaniambia kuwa kamuacha huko ndani akimuhudumia, lakini anaonekana hayupo vibaya, ila ni kama kachanganyikiwa…’akasema

‘ Mhh… mungu mkubwa…’nikasema hivyo. Na mimi ndio nikaingia na kumkuta docta akimuhudumia na kwa muda huo hata docta hakujua kilichotokea, ndio nikamuelezea, nilichokiona huko nilipotoka, na ndio akajaribu kukupigia, naona simu yako ina matatizo,…simu yako haina matatizo kweli…?’ akauliza huyo mfanyabiashara.

‘Haina matatizo, lakini kuna muda ilizima…’nikasema hivyo, sikutaka kuongea zaidi, pale nilikuwa na hamu nirudi ndani nikamuangalia tena mume wangu.

Nikamsogelea docta kumuomba akaombe ili niweze kuingia ndani, nikamuone tena mume wangu.
‘Sawa, hamna shida…’akasema na kuniambia tuongezane, basi tukaenda naye hadi pale alipolazwa mume wangu


Nilipomchungulia mwili wake, nilihisi mwili wangu ukisisimuka sikujuwa kwanini, kwanini kanyoka tu vile…, na muda ule alikuwa kafungua macho, sasa hataki hata kuniangalia machoni, mwili wangu hapo ukafa ganzi, nikawa nasubiria tu hiyo taarifa ya docta nisikie kama ana tatizo au hana...

Pale docta akaongea nilipomuuliza ni kwanini alikuja kwake…


‘Yeye ndiye aliyenipigia simu, na namba tofauti, nahisi alimuomba mpita njia mmoja, mtu wa bajaji…kwa bahati nzuri nipo likizo, kwahiyo nilikuwa hapo nyumbani, nikijua ni tatizo dogo, ndio hivyo akaletwa, kiukweli nilimshauri aende hospitalini, lakini alisema ni muhimu atibiwe hapo nyumbani tu, na nilion akachanganyikiwa, anasema hataki ijulikane kuwa kapatwa na ajali, ..ni kuchanganyikiwa tu huko...

‘Kwanini hataki, wakati keshapata ajali, mmh…?’ nikamuuliza

‘Atakuja kukuambia mwenyewe, ndivyo alivyosema…’akasema docta

‘Kiukweli nilipomfanyia uchunguzi wa haraka haraka na kufanya kile kinachowezekana, sikuona tatizo kubwa la nje, ila…ajali ni ajali, unaweza kwa nje usione kitu, tatizo likawa lipo kwa ndani, na unaona, kumbe kuna athari kwenye uti wa mgongo na shingoni, ngoja tusubiria taarifa za madocta,.. ’akasema huyo docta jirani yangu

‘Uti wa mgongo…umeathirika..mungu wangu ina maana gani sasa ina maana hataweza kutembea tena,..’nikasema nikishika kichwa

‘Usiwe na wasiwasi, …yupo kwa wataalamu..ngoja tusubirie uchunguzi wa mwisho….’akasema docta kunipa faraja


NB: Ndivyo ilivyokuwa hivyo....,



WAZO LA LEO: Mwili wa binadamu una uvumilivu wake, tunahitajika kuutunza sana, na unapouzidishie mambo juu ya uwezo wake, ukiulazimisha sana mwili, hasa kimawazo, tunaweza kujikuta tukipatwa na athari za kiafya. Mazoezi ni muhimu sana ili kuwezesha miili yetu, na akili zetu kubeba mambo kwa mpangilio. Lakini pia tusipende kuulazimisha kupita kiasi…hasa mawazo, mawazo yakizidi sana huja kuleta matatizo.
 
SEHEMU YA 27

Docta amekuwa mfariji wangu mkubwa, tokea enzi hizo, ananifanya nikumbuke mbali sana, maana mara kwa mara nikiwa sina furaha, basi naweza kumpigia simu,tukaongea akaniliwaza, na hata kunipa ushauri, na sijui kwa vile ni docta, lakini hata hivyo tumetoka naye mbali sana, na sehemu katika maisha yangu ndio maana sitaacha kumsimulia kwenye kisa cha maisha yangu….

Kutokana na huyu docta ndio nilijenga na kuiendeleza tabia yangu ya kuamini watu, sio kwa kila mtu lakini wale unaoona wanaaminika, wale marafiki zako wa karibu, waamini, maana na wao watakuamini, yeye ndiye aliyenifundisha jambo moja, kuwa nisipende kuwadhania watu vibaya, maana ukifanya hivyo unajijengea hisia mbaya moyoni mwako, na kujitwika mzigo ambao haujatua kichwani mwako.

Basi wakati nipo hapo hospitalini, docta huyu akawa karibu nami kunipa faraja ili nisahau maumivu ya kumuwaza mume wangu …na kiukweli nilikuwa kwenye hali ngumu sana…mawazo, na yote yaliyotokea siku nzima, yangeliweza kunifanya niathirike kisaikolojia, docta akanipa pambaja, nikahisi sasa nipo na watu wenye kutumania.

Huyu docta ndiye aliyewahi kuwa mchumba wangu, sasa kwanini ilitokea nikamuacha na kuolewa na huyu mume wangu,..ni kisa fulani chenye mazingatio kwa wenye hekima…

Tuendee na kisa hiki

***********


Docta alikuwa pia ni rafiki ya mume wangu, wengi walitarajia angelikuwa nai adui yake mkubwa, baada ya kunyang’anywa tonge mdomoni, lakini haikuwa hivyo,…docta amekuwa seehmu ya kuijenga ndoa yangui kila inapolega lega..

Naweza kusema pia docta ndiye aliyeniingiza kwenye dunia ya mapenzi, alinitoa kwenye ujana na kuniingiza kwenye usichana, nikafahamu ni nini maana ya mapenzi, enzi hizo, nikiwa kwa baba na mama yangu…hutaamini, kinyumbe na walivyotaka wazazi, sikuweza kuolewa naye….

Huyu docta ni nilianza kujuana naye zaidi tukiwa chuoni, huku nyuma, miaka ya utoto, shuleni, … nilikuwa namuona tu, ..kwa vile walikuwa majirani zetu, na ni familia yao ni miongoni mwa familia zilizokuwa na uwezo wa mali, wasomi waliobobea, kwani hata mtoto wao huyu aliweza kusomeshwa nje, kabla hajarudi hapa nchini,

Pamoja na mengine mengi sitaweza kumsahau kabisa katika maisha yangu

Ilivyotokea tunaweza kusema ni mipango ya mungu, maana kipindi nipo na huyu docta , ndio amerudi kutoka ulaya, wakati huo hajawa docta kamili, ndio alikuwa anachipukia, na kwa vile familia zetu zilishibana, aliporudi tu, akawa anakuja kwetu, na akija anakaribishwa vizuri, mtoto wa watu, basi tunakutana naye na kuongea mambo mbali mbali, akanizoea mpaka tukafikia hatua ya kukubalina kuwa wapenzi.

Basi ikawa ni jambo la furaha kwenye familia zetu, maana tupo kwenye daraja moja,…ni maisha yalivyo, kila mti na ndege wake. Familia zetu ikawa imeliidhinisha tamko la kuwa mimi ni mchumba wa docta, kwahiyo yeye aliweza kuja kwetu kunichukua, …unajua tena wao waliishi kizungu zaidi,..basi akija, ndio hivyo tena, ila hali ya wazazi kukuchunga kwake inapungua, ananiombea ruhusa tunatoka kutembea sehemu mbali mbali,…kiukweli mimi sikupenda sana maisha hayo y akujichanganya kwenye majumba ya starehe nk..lakini utafanyaje

Na kitu ambacho kilinifanya nisipende maisha hayo, ni ile hali ya kutizamana, nani kavaa nini, na zaidi pombe, tangia utoto nilitokea kukichukia kinywaji kinachoitwa pombe ya aina yoyote…namshukuru mungu kwa hilo.

Na hata nikiandamana naye kama mpenzi wangu, alifahamu kabisa mimi nipo mbali na ulevi, yeye kunywa kwake, ilikuwa kama kunywa soda, lakini hakuwa anakunywa kuelewa, alikuwa na kipimo chake, sijui kwa vile ni docta.

Ikafikia muda akaanza kunishawishi ili nami niwe nakunywa kama yeye, hapo ndio hisia zetu zilianza kusigishana, na hilo ndilo lilofanya tukaja kukosana kabisa nay eye, lakini haikutokea hivyo tu kwa vile, hapana mimi naweza kukiri kuwa ni mipango ya mungu ilipangwa iwe hivyo.

Kiukweli ilibidi afanye juhudi sana kunishawishi kwa kitu ambacho sikipendi, na sijui kwanini siku hiyo ilitokea nikakubali. Ilitokea siku hiyo, kulikuwa na shughuli za jirani, mmoja wa watu wenye uwezo, waliandaa tafrija kwenye hoteli moja kubwa tu, tukawa tumealikuwa…baada ya mambo mbalimbali, ikawa watu wanakula na kunywa, na hapo mpenzi wangu huyu akaanza kunishawishi, ninywe

Kwa vile niliona ni siku ya furaha, na sikutaka kumuuzi mpenzi wangu, siku hiyo nikasema ngoja nijaribu, nione ina ladha gani, ngoja nijaribu nione hiyo raha wanayoifaidi wenzangu,…ilikuwa ni aibu kwangu na ndio siku niliapa kuwa sitakunywa tena.

Nilikuwa nimekunywa kidogo, kumrizisha mpenzi wangu ambaye kipindi hicho alikuwa ni huyu docta, nilikunywa gilasi moja tu tena kwa kujilazimisha, ilikuwa haipiti kooni, nahisi ni harufu mbaya, nilipomaliza hiyo gilasi moja tena haikumalizika,..,…

Hapo hapo nikaanza kujisikia vibaya, tofauti na ninavyoona wenzangu wakichangamka, mimi nilihisi vibaya kupindukia, niliona kama dunia inageuzwa, inazungushwa, roho imechafuka, tumbo linapanda na kushuka, nataka kutapika lakini hakitoki kitu

Yaani siku hiyo nilijuta ni kwanini nilikunywa,..nilimuona mpenzi wangu kama alitaka kuniua, na muda huo huo, nikamwambia mimi naondoka, siwezi kukaa hapo tena, akanisihi, na kunishawishi, kiukweli anajua kubembeleza, na unajua tena ni mpenzi wangu ikabidi nikae tu…kumrizisha.., na hata aliponishawishi ninywe tena sikukubali, nilimuambia kabisa ukiendelea kunishawishi kunywa hii sumu tutakosana kabisa.

Kwa muda ile nikajitahidi, lakini hali haikuwa nzuri, bado nilikuwa najisikia vibaya,..ikafika muda, siwezi kuvumilia tena, kwani roho ilishachafuka kupitiliza, nikakimbilia chooni, (washing-room), nikamuacha docta na watu wengine wakiendelea kuongea na kunywa, wanajisikia raha zao.., ambazo kwangu mimi ilikuwa ni kero tu.

Nilipokuwa kule hali ikatulia, kidogo cha ajabu sikutapika, kama nilivyodhania nitafanya hivyo,..nikaona labda, hali imetulia, ndio wakati nataka kutoka sasa,natoka chumba hicho cha usafi, nipo mlangoni, nikahisi kizungu zungu,na kama asingelikuwa huyo jamaa kunidaka ningelidondoka vibaya kwenye sakafu….

‘Pole sana dada, ....’akanidaka huyo jamaa na kunisaidia kusimama vyema, lakini sikuweza, mwili ulikuwa hauna nguvu, tumbo linapanda na kushuka, na sikuweza kuvumilia zaidi nikaanza kutapika, na matapishi ya mwanzo yakaenda moja kwa moja kwenye nguo za huyo jamaa.

‘Oooh...pole pole, inaonekana umelewa, wewe..oh, ..tulia kidogo,....’akasema bila kujali kuwa nimemchafua. Na kunisaidia ….

Na hutaamini hakujali kuchafuka kwake, yeye alichojali kwangu ni kunisaidia mimi akanishika vyema, akichelea nisichafuke na yale matapishi niliyomlowesha nayo mimi, ambayo yalikuwa kwenye nguo zake,....na akaweza kunisaidia hadi chooni, ilibidi aingie choo cha wanawake ili niweze kujisafisha,..alipohakikisha nipo sawa, yeye akakimbilia choo cha wanaume kujisafisha, nilijiskia vibaya sana siku hiyo.


Hali ilipotulia nikatoka, kumbe huyu jamaa alikuwa hapo nje akinisubiria, alikuwa keshamaliza kujisafisha, na kukausha nguo zake usingeliweza kujua kuwa nilimchafua, na aliponiona nikitoka akanifuata pale mlangoni, na kuniuliza.

‘Upo sawa sasa,…?’ akaniuliza

‘Ndio nipo sawa, hamna shida, samahani sana, na nashukuru sana…’nikasema

‘Usijali, inatokea tu…na samahani nikuulize ,upo na nani maana naona hiyo hali unahitajia msaada...?’akaniuliza huku akinisogelea, na sikutaka kuongea na mtu, nilichotaka ni kuondoka, na kwenda nyumbani kulala.

‘Nipo na na...’nikasita kusema

‘Na mume wako, au mpenzi wako, off course....’akamalizia na mimi nikakubali kwa kutikisa kichwa, ili nitimize ule usemi wa kubali yaishe, ili aondoke zake, na mimi niende kumuaga docta kuwa narejea nyumbani.

Kiukweli kwa muda ule nilidhamiria kuondoka, sikujali tena kuendelea kukaa kumrizisha mpenzi wangu, wakati hajui kinachonisumbua, yeye aliona ni kwa vile ni mara ya kwanza, basi nitazoea,…hapana sikuzoea na sitaweza kuzoea maishani mwangu.

Nikawa natembea kulekea kule walipo docta na marafiki zake, lakini nlikuwa nayumba, kizunguzungu, yaonekana kichwani bado nilikuwa sipo vyema,na kumbe jamaa yupo nyuma akiwa na mashaka kuwa naweza kudondoka tena,…na alipoona sipo sawa akanijia kwa nyuma na kusema;

‘Basi ni bora nikusaidia hadi kwa huyo mume wako,maana unavyoonekana hujawa sawa, kwanini unakunywa pombe, wakati unaona hazikupendi,.....achana na pombe,pombe zinawenyewe bwana, mimi mwenyewe sinywagi kihivyo, ni kwa dharura tu....’akasema.

‘Sinywi tena...hapana nitaweza mwenyewe…..’nikasema na nikamtupia jicho huyo mtu, na ilikuwa kama ndio namuona kwa mara ya kwanza, nikahisi hali fulani, kama mshituko , ni kama kuna kitu nilikihisi, lakini niliona ni sababu ya pombe, maana mtu mwenyewe simfahamu, lakini nikajiuliza ni kwanini nihisi kitu kama hicho, nikapotezea, na sikutaka kumwangalia tena machoni.

‘Samahani nikuulize,… inakuwaje mume wako asijitokeze, kwani naona kama umekaa huku muda mrefu hajashtuka tu…kama ulikuwa na hali hiyo alitakiwa akujalia, au sio,,? Samahani lakini kama nawaingilia maisha yenu, au....?’akasema kama kuniuliza, hata mimi nililiona hilo , lakini sikujali, na sikutaka huyo docta afahamu kilichotokea.

‘Wenyewe wameshalewa, sizani kama hata wanatambua kuwa nimechelewa huku....na nisingelipenda wanione kuwa nimetapika kwa ajili ya pombe, wala usije ukawaambia hata hivyo nipo safi, haina haja ya wewe kunisaidia nashukuru kwa wema wako huo..na sitakunywa tena hiyo mipombe yao, ....’nikasema.

‘Pole sana....mimi kama ningelikuwa na mpenzi kama wewe, ningeshtuka haraka sana, ulivyochelewa hivyo…sio kwamba namsema vibaya huyo mpenzi wako, lakini kwa hali hiyo alitakiwa awe karibu yako,…mimi hapa naogopa usije kudondoka tena.. sawa, basi tembea mimi nitakufuatilia kwa mbali kuhakikisha umefika salama kwa mume wako, ...’akasema, na kunifanya nifurahie sana wema wake.

‘Hongera ...kama upo hivyo, na mpenzi wako atakuwa na bahati sana…hata hivyo, ni leo tu, mbina mpenzi wangu ananijali sana, sina shaka naye….’nikasema na nikatamani kumwangalia tena huyo jamaa usoni, na nilipomuangalia, akili yangu ikakumbuka kama niliwahi kuiona hiyo sura mahali, lakini sikuweza kukumbuka vyema ni wapi, na lini, sikutaka kuwaza zaidi , nikapotezea.

‘Ina maana hunikumbuki mimi kabisa...?’ akaniuliza na kunifanya nisimame wakati huo nilishaanza kuondoka kuelekea kule walipokuwa docta.

‘Kwani wewe ni nani…?’ nikamuuliza , na hapo ndio nikapa ujasiri wa kumchunguza vyema usoni baada ya kugeuka kumuangalia vyema…hata hivyo sikuweza kumkumbuka kuwa ni nani, akili ilikuwa haitaki kufikiria sana, na sikutaka kufanya hivyo nikasema;

‘Samahani kwakweli sikukumbuki kabisa,..zaidi ya kukufahamu hapa kuwa wewe ni mtu mwema, ...tuliwahi kukutana wapi mimi na wewe, shuleni, au chuoni, au wapi?’ nikamuuliza ili tu kumuonyesha kuwa namjali kwa fadhila zake hizo, lakini sikuwa nataka kuongea...

‘Kweli ukiwa mtu wa chini, ..watu hawakukumbuki kabisa, wewe sio wa kwanza kusema kuwa hunikumbuki, lakini nafahamu ni kwanini...’akasema hivyo.

‘Hapana sio kwa vile wewe ni mtu wa chini, kwanini unasema hivyo, wewe ni mtu wa kawaida mbona, mimi sipendi watu kujishusha, hakuna mtu wa juu na chini, hizo ni hisia potofu, na kiukweli sipendi watu kujifanya hivyo…’nikasema, na nikamwangalia tena kwa makini,japokuwa akili iliona kuwa nilishawahi kukutana na mtu kama huyo, na sio kukutana tu, lakini moyoni nilikuwa kama nimeguswa na hamasa, lakini sikuweza kukumbuka kabisa kuwa huyu mtu ni nani.

Muda ulikuwa umekwenda, sikumuona docta akija ..na sikupenda kumuacha huyu msamaria mwema hivi hivi, nilitaka niondoke akiwa amerizika, sio niondoke aone nimemdharau..hisia za wema wake ziliuteka ubongo wangu, ule ukaribu wake , kunijali, nilimuona kama mtu niliyemzoea….sijui kwanini, yaani kumbe kitu kidogo tu kinaweza kubadili hisia za mtu.

‘Samahani sana, labda kwa vile nipo katika hii hali, ndio maana akili haifanyi kazi vyema, na nisingelipenda kufikiria zaidi, maana kichwa kinaniuma, labda unikumbushe tu, kama hutojali...’nikasema na huku nikikwepa kumwangalia tena moja kwa moja usoni na yeye akaniangalia na kusema;
 
SEHEMU YA 28

‘Mimi ni mtoto wa mzee Mchapakazi…’akasema

‘Mchapakazi…?’ nikauliza, sikuweza kukumbuka ni nani anamuongelea kwa wakati huo..

‘Humkumbuki yule mzee, aliyekuwa mlinzi wa pale nyumbani kweny, na pia alikuwa akiwalimia mashamba yenu na mimi nilikuwa nafika kumletea baba chakula, na siku moja ukanisadia pesa za ada ya shule, kipindi mzee anaomba mkopo kwa baba yako, na baba yako akakataa kumpa hizo pesa..umeshanisahau ehe...’akasema

‘Mungu wangu ndio wewe..mbo-mbona..hapana sio wewe…’nikasema huku nikainua kichwa kumwangalia na mdomo wangu ukabakia wazi kuonyesha mshangao.

‘Ndio mimi …huamini eeh…mlifikiri tumejifia au sio…’akasema

‘Oh, …sio…ila kiukwe umebadilika sana..ooh, nimeshakukumbuka, ..oh jamani , mimi nilikuwa kasichana kadogo kipindi kile,…unajua baada y alile tukio, nilitokea kuwachukia sana wanaume, na nailijiskia vibaya sana kwa yale yaliyotokea, hata hivyo nilitamani nikuone tena, lakini hukuja, nilishaahidi kukusaidia ..kukulipa fadhila ulizonitendea...’nikasema.

‘Kunilipia fadhila , si zilishalipwa na baba yako, au umesahau yaliyotokea..’akasema

‘Usiseme hivyo, wazazi wangu na wao walipokea taarifa tu,..nakubali hawakutaka kuzichunguza,..’akasema

‘Unaweza kuwatetea hivyo, sawa, ni wazazi wako ni lazima useme hivyo…ila kiukweli iliniuma sana kumuona baba yangu anazalilishwa, na sikutaka kurejea tena kwenu, na nikawa nafanya vibarua tu pale waliponiachia jela, na sijui ilitokeaje kesi ikafutwa na kuachiliwa, nilihangaika sana...hadi nikapata pesa za kujisomesha, unakumbuka nilifaulu, na kwasababu ya kufungwa sikuweza kwenda sekondari,…’akasema

‘Pole jamani…nilisikia, lakini aah, mimi sikuweza kufuatilia, maana sikuwepo tena yaliyotokea nyuma nilifanya kuhadithiwa, nilijua yameisha, kumbe..ndio hivyo tusamehe tu, na wazazi wangu…’nikasema

‘Nilipata msamaha, sikufungwa muda mrefu,.. na nilipotoka nilimuomba baba tuhame hapo kijiji kabisa, tukaenda kuishi kijiji cha mbali, huko nikaweza kujisomesha kwa kufanya vibarua...Baba yangu aliumwa sana, naweza kusema ni kutokana na hilo tukio, na kuumwa huko ndio ikawa sababu ya kufariki kwake...’akasema kwa uchungu.

‘Oh, pole sana, ina maana yule mzee alishafariki...?’nilimuuliza nikishikwa na huruma, na fadhaa, na nilitamani nimkaribie ni mkumbatie kumuonyesha jinsi gani nilivyojisikia….kiukweli niliona nina deni kubwa la kumlipa huyu mtu, maana hii ni mara nyingine ananiokoa na kunifanyia huruma…moyoni niliahidi kuja kumlipa kwa kadri nitakavyoweza.

‘Alifariki......ndio mapenzi ya mungu, na mapenzi ya mungu ndivyo yalivyo, na moyoni hatukosi kuwa na sababu..ila kiukweli, baba alinipenda sana, na hali yake hiyo ya kuumwa, na ilianzia pale mama alipofariki , mama yeye alifariki mapema tu, tulipohamia huko,…na,… na hutaamini, baba alikuwa haishi kumkumbuka mama, na hicho ndicho kilichomfanya hali yake izidi kuwa mbayae....na hakupenda mimi niteseke, aliona ni bora yeye akafungwe, aliwaomba sana wahusika afungwe badili yangu...’akasema.

‘Oh, jamani, poleni sana, sizani kama wazazi wangu walifahamu hilo, na ukweli wote wa hayo yaliyotokea…na kwa vile alikuwa mfanyakazi wao kwa muda mrefu wasingelifikia kumfanyia ubaya huo wote…na hata kufariki huko, sizani kama walikuwa na taarifa,..wangeliniambia, na hata wao kufika kwenye msiba, sizani kama wangeshindwa kufanya hivyo, sizani...’nikasema.

‘Baba alikataa kabisa, mama alipofariki, hakutaka kutoa taarifa kwa watu wa mbali, na hata yeye alisema ikitokea akifariki..sisi tufanye hivyo hivyo..maana alishaona dunia haina wema..aliniusia kabisa,.., nisije kuja kuwaambia...na ndivyo ilivyotokea, alizikwa na watu wachache tu…, na wengi hawakufahamu zaidi ya ndugu na jamaa wa karibu tu .....ndio hivyo, lakini mimi sikukata tamaa ya maisha, nikasonge mbele, ....’akasema.

‘Sasa hivi unafanya kazi wapi?’ nikamuuliza.

‘Nipo hapa kwenye hii hoteli nabangaizabangaiza, nilipata tenda ndogo hapa, ndio naifukuzia, ikiisha nakwenda sehemu nyingine, maisha yanakwenda kidogo ninachokipata kinanisaidia, sitaki ile ya kuajiriwa maoja kwa moja, mpaka nikamilishe malengo yangu…’akasema

‘Mungu wangu, imeniuma sana…sikutarajia hili , kweli milima haikutani, ila wanadamu..mmh…sijui nitakulipa nini, sijui nifanye nini ili hayo machungu yaliyokupata yaishe,..sijui, tusamehe tu, mimi na wazazi wangu..’nikasema

‘Ndio maisha sisi watu wa chini kupata kazi inakuwa shida, na sipendi kwenda kuwapigia watu magoti kuwa wanipe kazi, sitaki nizalilike kama alivyozalilika baba yangu, mimi nimeona njia iliyorahisi ni kujiajiri kwa njia hii...hapa leo, keshi kwingine maisha yanakwenda,…..’akasema na hapo nikamwangalia na kumbukumbu za nyuma zikanirejea...

‘Maua unafanya nini huku….?’ Ilikuwa sauti ya docta, na nikageuka haraka na kuanza kutembea kumfuata, nilipomfikia, akaniuliza

‘Ulikuwa na nani muda wote huo…?’ akaniuliza

‘Nilikuwa najisikia vibaya, …sana…’nikasema

‘Utazoea tu,…pombe kidogo tu ndio imekufanya hivyo, ajabu kabisa… tatizo lako hutaki kujifunza, starehe hiyo unaikosa bure, dunia hii kuna starehe gani kama oh, upo ok, lakini samahani, sikuja kukuangalia, kuliko na maongezi nyeti kidogo, nisamahe mpenzi…’akasema akinishika kiunoni kunifanya nisipepesuke.

‘Nipo sawa, haina haja kunishika hivyo, mimi sipendi…’nikasema

‘Ok, ok…samahani nimesahau…haya twende, na yule aliyekuwa karibu yako ni nani..?’ akaniuliza

‘Ni mfanyakazi wa hii hoteli, kanisaidia, sana, maana nilizidiwa kidogo…’nikasema

‘Mhh, ok, sijamshukuru, naona simuoni tena....haya, twende tukaendelee ..wenzangu ndio kumekucha..’akasema, na docta alikuwa hivyo hana hisia mbaya na watu, ndio nilimpendea hivyo, ukimuambia kitu atakuamini, na inaishia hapo.

‘Hapana mimi naondoka…siwezi kurudi tena kule, nahisi harufu za pombe zitaniua,wewe nenda kaendelee tu na wenzako…’nikasema

‘Oooh,..hapana usifanye hivyo,…utaharibu, nitawaambiaje rafiki zangu, kuna mambo muhimu tunaongea pale unajua kazi zangu ni watu, na watu ndio wananiongezea michongo ya maisha..unajua, ...na wale pale ni watu muhimu sana, ni madocta, wamenitangulia, nikiwa nao, najua nitafika sehemu ninayoitaka sana, elimu yangu nataka inifikishe mbali kabisa..’akasema

‘Basi ..ndio maana nasema, wewe nenda kaendelee nao, wala sijali kuhusu mimi, mimi nitarudi nyumbani peke yangu, maana hapa na nyumbani sio mbali, nitafika bila wasiwasi..’nikasema

‘Siwezi kukuacha uende peke yako, na hii ni shughuli muhimu ya majirani zetu haitaonekana vyema tukiondoka, hata wazazi wako hawatafurahi, wakisikia hivyo, hebu lifikirie vyema hili, nikuombe kitu.., vuta vuta muda, tutaondoka pamoja ..’akasema, niliwaza sana baadae nikasema sawa, basi nikarudi pale mezani, lakini baadae nikamuomba mpenzi wangu kuwa nataka nikakae kwenye hewa, nipate upepo,..sijisikii vizuri.

‘Wapi sasa, unaona mambo tunayoyaongea hapa ni muhimu sana, yanaweza kukusaidia hata wewe , kwenye maswala ya ajira, kujiajiri, kuwekeza, unaona, ni mambo muhimu kwenye maisha, leo wazazi, kesho ni sisi, tunahitajika kuchukua hatamu, au sio..umesikia mwenyewe, mimi hatima ya haya ni kuwa ni hospitali yangu kubwa, ndio ndoto yangu…’akasema

‘Usijali, mimi nitakuwa kule sehemu ya kutokea, ..palee , unaona, wamekaa akina mama , na wasichana wasiopenda kujichanga huku,…utakuwa unaniona au sio…’nikasema akakubali, kwa shingo upande, ..kiukweli kwa muda huo, sikutaka kukaa pale na akili yangu ilishaondoka, yaani kuna kitu kilinibadili ghafla, na ..hata sijui ni kwanini.

Nikaenda ile sehemu na kukaa , kulikuwa na watu wengine wasiokunywa wamekaa hapo wanakunywa vinywaji vya kawaida, nikatafuta sehemu nikaa, na nikanyosha mkono kumuashiria docta, kuwa nipo sehemu hiyo, na akanipungia mkono kuwa kaniona..

Sasa ni wakati nimetulia, mara akaja mtu pembeni na kukaa, …sikutaka kugeuka kwa haraka, kumuangalia ni nani, nilikuwa akili yangu imetekwa na tukio kwenye Tv, kuna tamithiliya nzuri inaonyeshwa, na mara sauti ikasema;

‘Kumbe yule ndio mume wako, najua hata yeye keshanisahau, …yupo na akina kaka zetu wa enzi hizo,…mnaoana watu wenye hadhi zenu…’nikashtuka, kumbe alikuwa yule msamaria mwema, nikahisi moyo ukinienda mbio, maana sasa kakaa karibu yangu, nikageuka kuangalia kule alipokaa docta, nikawaona wanaongea na kucheka tu. Hana habari kabisa na mimi…

‘Mhh…sio mume wangu…’nikasema

‘Kwahiyo, kumbe hujaolewa bado…’akauliza

‘Bado ndio tupo mbioni…’nikasema

‘Oh, mungu wangu kwanini hivi lakini…’akasema

‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Unakumbuka ahadi yetu lakini…?’ akaniuliza

‘Ahadi, mmmh…na..ndio na…nakumbuka, lakini…hayo yalishapita au sio ni mud asana, na mambo yamebadilika,…na nishamuahidi docta kuwa ndiye mume wangu mtarajiwa, samahani sana..’nikasema

‘Najua,hamna shida , nilitaka ukumbuke tu hilo, najua huwezi kuolewa na mtu kama mimi,….ila nakuuliza tu…je moyo wako bado upo kwangu, au uliniambia tu kunifurahisha, utoto..lakini hatukuwa watoto kivile, au sio…samahani sana kukuuliza haya, najua umeshampata mtu wa hadhi yako…sizani kama nina maana tena kwako…’akasema

‘Usiseme hivyo, wewe hujui tu….niliteseka sana,…sijui kwanini, na hadi naamua kumkubalia docta, ilikuwa ni baada ya kusikia kuwa wewe haupo hai, walisema ulifia jela au baada ya kutoka kitu kama hicho….’akasema

‘Eti nini…nilikufa…hahaha.., hayo labda waliyatunga wazazi wako,..ili….lakini haina haja, najua, hutaweza kuolewa na mtu kama mimi, nafahamu hivyo,… lakini niliapa kuwa bila wewe sitaweza kuoa tena, ndio maana nikawa napambana ili niwze kufiki hadhi yenu, na nilitaka siku tukikutana unione tofauti, lakini ya mungu mengi tuakutana leo bila kutarajia…’akasema

‘Jamani…..’nikasema hivyo nikigeuka kumuangalia kwa macho yaliyojaa huruma

Na wakati namuangalia, ndio kumbukumbu za nyuma zikaanza kunirejea, na ikawa ndio sababu ya kunibadili kabisa mawazo yangu, hasa kutokana na yaliyotokea siku za nyuma kweli kumbukumbu hubadili maisha…na kutokana na kumbukumbu hizo zikanifanya nimuache docta…haikuwa kazi rahisi, lakini…

NB: Tutaendelea sehemu ijayo. Ilikuwaje, na ina umuhimu gani kwenye hiki kisa, tuzidi kuwepo…


WAZO LA LEO: Tofauti za maisha, tofauti za kipato, tofauti na utawala na wasio kuwa watawala, isiwe ndio sababau ya kuzarauliana, maana huwezi kujua, ni yupi ni muhimu kwenye maisha yetu. Unaweza ukawa na kipato lakini ukawa na mapugufu fulani ambayo yanaweza kujaziliwa na yule unayemuona ni hadhi ya chini, au akaja kukusaidia yule ambaye hukutarajia kabisa. Mola ni mwingie wa hekima anajua ni kwanini maisha yapo hivyo,..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom