Na Saed Kubenea
RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, ni mmoja wa viongozi waliochotewa fedha kutoka kampuni ya Meremeta, MwanaHALISI imegundua.
Kulingana na nyaraka mbalimbali zilizopo, Mkapa alichotewa dola 780,000 za Marekani (karibu Sh. 1 bilioni) kutoka akaunti ya kampuni hiyo iliyopo benki ya NBC, tawi la makao Makuu.
Ingawa haijajulikana mara moja fedha hizo zililipwa kwa kazi gani hasa, imebainika kwamba zilipelekwa kwenye akaunti binafsi ya Mkapa iliyopo Geneva, nchini Uswisi.
Ugunduzi wa malipo haya mapya, unazidi kuonyesha ukwasi wa rais mstaafu wa awamu ya tatu, baada ya kuthibitika alijiingiza kwenye ujasiriamali na kuanzisha kampuni yeye na mkewe, Anna, akiwa bado Ikulu.
Vilevile, Mkapa alilipwa kiasi cha Sh. 600 milioni na Benki ya NBC, zikiwa ni fedha za mkopo usiokuwa na dhamana yoyote. Fedha hizo alizitumika kununua nyumba na baadaye hati ya nyumba hiyo ikawa dhamana.
Mkapa ambaye hajajitokeza kuzungumzia hadharani tuhuma hizo, anatuhumiwa pia kwa kushirikiana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, walijimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa bei ya kutupa.
Tuhuma hizi na nyingine zinaongeza uzito kwenye hoja ya kutaka Mkapa achunguzwe na vyombo husika kuhusu mwenendo wake alipokuwa kiongozi wa taifa (1995-2000), na ikithibiti afunguliwe mashitaka mahakamani.
Kampuni ya Meremeta imekuwa kitovu cha mvutano mkubwa miongoni mwa watendaji wa serikali juu ya nani hasa mmiliki wake.
Wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja amesema Meremeta ni kampuni ya serikali, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu, amekana akisema kuwa kumbukumbu za BoT hazionyeshi ukweli wa hilo.
Profesa Ndulu aliyeteuliwa Gavana mapema mwaka huu baada ya kuondolewa Dk. Daudi Ballali kutokana na msukumo wa ufisadi wa Sh. 133 bilioni uliofanywa kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu mwaka 2005-06, amesema Meremeta haimo katika orodha ya makampuni ya serikali.
Msimamo wa Prof. Ndulu wa kutoitambua kampuni ya Meremeta iliyochotewa mabilioni ya shilingi na Wizara ya Fedha kupitia BoT, unaungana na ule wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.
Utouh alisema hajawahi kuikagua kampuni hiyo kwa kuwa si mali ya umma.
Agosti mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, aliliambia Bunge kwamba Meremeta ni kampuni ya serikali na kuongeza kuwa ilifilisiwa na shughuli zake kupelekwa kwa kampuni mpya ya TANGOLD Limited.
Kampuni ya Meremeta ilikuwa inachimba dhahabu katika mgodi wa Buhemba, mkoani Mara.
Kungundulika kwa malipo kwa mstaafu Mkapa, kunazidi kupanua wigo wa viongozi waliojilimbikizia fedha zenye utata nje ya nchi, baada ya Shirika la Upepelezi la Makosa makubwa ya Jinai la Uingereza (SFO), kugundua kiasi cha dola 1 milioni (sawa na Sh. 1.2 bilioni) zinazomilikiwa na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge.
Fedha hizo zinazohisiwa kuwa ni mlungula uliotolewa kufanikisha ununuzi wa rada ya kijeshi iliyonunuliwa na serikali ya Tanzania mwaka 2002, zimehifadhiwa katika kisiwa cha Jersey, Uingereza.
Utata wa kampuni ya Meremeta na malipo yaliyogunduliwa karibuni, unazidi kumtumbukiza Mkapa katika uovu uliofanyika wakati wa utawala wake uliosababisha hujuma kubwa ya fedha za umma na raslimali za taifa.
Wakati Karamagi akisema shughuli za Meremeta zilisitishwa mwaka 2005, nyaraka za benki zinaonyesha hadi mwaka 2006, malipo mbalimbali yalikuwa yanafanyika kupitia akaunti za kampuni hiyo.
Miongoni mwa malipo yaliyopitia Meremeta ni yale yaliyotoka kampuni ya TANGOLD yaliyofanyika Mei 2006. Meremeta ilipokea pia fedha kutoka kampuni nyingine yenye utata ya Deep Green Financial Limited.
Malipo mengi katika makampuni haya yalifanyika wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Mbali na malipo haya kufanywa kwa rais mstaafu Mkapa na makampuni ya TANGOLD na Deep Green, malipo kama hayo yalifanyika pia kwa kampuni ya mawakili ya Imma Advocate ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, ni mmoja wa wamiliki wake.
Makampuni yote mawili (TANGOLD na Meremeta) yamegubikwa na utata juu ya nani mmiliki. Huku Karamagi akisema TANGOLD inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100, nyaraka zilizopo ofisi ya Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA) nchini, zinaonyesha kampuni hiyo ni ya watu binafsi na ilisajiliwa nje ya nchi.
Wakurugenzi wanaotajwa katika kampuni ya Meremeta, ni pamoja na Andrew Chenge na Daudi Ballali.