Warioba; Tusiruhusu Kashfa zitugawe
Na Yahya Charahani
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameonya dhidi ya utamaduni wa kuchafuliana majina ulioibuka miongoni mwa jamii kwa kuwa utakapokomaa utasababisha wananchi kusahau mambo ya msingi na kusababisha vurugu.
Akizungumza jana ofisini kwake Oysterbay, Dar es Salaam Jaji Warioba alisema, amestushwa na utamaduni huo ambao unaonekana kukomaa kiasi cha kumgusa mtu muhimu kama rais.
"Nimeulizwa maswali mengi baada ya kutoka 'orodha ya mafisadi', nimeipata, lakini ninachoweza kusema hakuna jipya katika orodha ile, zaidi ya kupakana matope, kwani orodha ile inafanana kabisa kimtiririko tuhuma zake na orodha mbili zilizopita,"alisema.
Alisema ameona yaliyoandikwa katika ile orodha inayoitwa 'list of shame' mengine yamemstua sana, nchi ikifikia kumtaja rais ni fisadi imefika mbali, na kwamba mtu hawezi kutoa tuhuma kama hizo mpaka awe na ushahidi mzito usioacha shaka.
Alisema rais ni alama ya taifa na kwa maana hiyo mtu anapomtaja rais kuwa fisadi na kisha akaendelea kujigamba kuzungumzia juu ya hilo hatimaye ina maana hakutakuwa na uongozi wa taifa, itakuwa ni hatari.
Alitoa mfano kama tuhuma za namna hiyo zinaendelea ina maana kuwa wananchi wanaweza kukosa imani na serikali yao suala ambalo ni hatari na halitakiwi kufumbiwa macho.
"Unapomtaja rais kama fisadi unakuwa na unataka kufanya wananchi wakose imani na serikali yao suala ambalo ni hatari, wananchi watakimbilia wapi kama wanayetaka kumkimbilia naye anachafuliwa," alisema.
Hivi karibuni Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Willibrod Slaa, aliwataja vigogo 11 wengi wao wakiwa katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne kwamba ni mafisadi waliohusika na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za umma.
Miongoni mwa waliotajwa na Dk Slaa akishirikiana na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, ni makatibu wakuu wawili, mwanasheria pamoja na viongozi wengine waliokuwa katika serikali ya awamu ya tatu.
Dk Slaa aliwataja vigogo hao wiki iliyopita katika Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa vyama vya upinzani katika mikoa 11 ya Tanzania, ikiwa ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa mwezi uliopita katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia tuhuma, Jaji Warioba alishangazwa hata Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutajwa katika baadhi ya ripoti wakati rekodi yake inaonyesha kuwa kafanya mengi mazuri, lakini taarifa zinazotolewa zimelenga tu kumchafua.
Kwa muelekeo ulivyo sasa alisema, inaonekana kwamba kuna njama na jitihada za makusudi za kuchafua majina na kisha kusumbua utawala uliopo kukimbizana na hoja za ufisadi wakati mambo ya msingi yakiachwa bila kutekelezwa.
Alishangaa kwamba kila kukicha viongozi wanatishia kwenda mahakamani suala ambalo linaonyesha kuwa viongozi wanatumia muda huu kujibu tuhuma badala ya kushughulikia masuala ya maendeleo ya taifa.
"Sikatai Mkapa ni binadamu anaweza kuwa na mambo yake, lakini siyo kiasi cha kufuta rekodi yake. Hivi kweli mtu unaweza kweli kufuta rekodi ya Mkapa kwa utendaji wake uliowezesha kushusha inflation ya asilimia 30 alipoingia madarakani hadi tano wakati anaondoka, kisha ukatoa tuhuma za jumla jumla tu, hivi nadhani si sawa," alisema.
Aliorodhesha miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Rais Mkapa ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, uchumi miundombinu na vitu vingine.
Kwa mtazamo wake alisema kuwa, baada ya uchaguzi mambo ya msingi ambayo sasa yangekuwa yakishughulikiwa ni pamoja na uboreshaji wa kilimo, kukabiliana na tatizo la bei za umeme kuwa juu, mfumuko wa bei na vinginevyo, lakini badala ya kushughulika na hayo, suala lililowekwa mbele ni kuchunguza dosari za viongozi.
Hata hivyo aliitaka jamii kutoacha kupambana na viongozi wala rushwa iwapo kunakuwapo ushahidi wa msingi na uthibitisho usioacha shaka, lakini jamii hiyo hiyo isitumie mwanya huo kujineemesha kisiasa.
"Sisemi kwamba viongozi wala rushwa wasiandamwe la hasha, waandameni iwapo mna ushahidi wa kutosha na msiishie kuwataja tu songeni mbele zaidi kuhakikisha haki inatendeka," alisema.
Pia alisema ni muhimu vyombo vya habari na jamii vikasisitiza katika kuwapo utawala bora, lakini si kwa kiwango cha kusahau vipaumbele vingine katika jamii.
Alisema inavyoonekana kama kuna jitihada za makusudi za kuchengesha mambo ya msingi kwa jamii yasishughulikiwe, ili suala liwe ni moja tu kukimbizana na tuhuma ambazo zinatolewa na kisha kutofuatiliwa.
Hali hii anasema Warioba kuwa huenda ikasababisha muda si mrefu masuala yaliyolisumbua taifa kipindi kilichopita yakarudia tena kusumbua, sababu mwelekeo unaonekana ni kukimbizana na kujibu tuhuma.
"Wiki chache zilizopita nilikuwa Mara kwa shughuli za uchaguzi, nikasikia kwenye vyombo vya habari Mungai analalamika watu wanampaka matope eti mara wanamwita si raia, inashangaza sana, hivi kweli mtu kama Mungai anaweza kuhojiwa vitu vya ajabu kama hivi, tunakokwenda siko," alisema.
Aliwachekesha waandishi wa habari pale alipojibu swali aliloulizwa na mmoja wa waandishi wa habari aliyetaka kujua kama alitumwa kutoa taarifa hiyo akajibu : "Sikutumwa na mtu, simo katika siasa, wala serikali mimi ni mtu huru hakuna mtu aliyenituma, nasema ninachokiamini."
Source: Mwananchi
Tag it:?