SoC04 Misingi bora ya malezi, Tanzania bora

Tanzania Tuitakayo competition threads

Mercy Clemence

New Member
Mar 12, 2024
1
1
MALEZI YENYE MISINGI YA KUMCHA MUNGU, UWAJIBIKAJI NA KURIDHIKA.

Katika miaka ya sasa hivi wazazi wengi wamekua wakijikita sana katika shuguli za utafutaji kiuchumi ili kukidhi mahitaji ya familia zao na kupelekea upande wa malezi kwa watoto kutotiliwa mkazo na wazazi kama miaka ya zamani. Hali hii Imepelekea wazazi wengi kuwaacha watoto wao na wasaidizi (wadada wa kazi) kwa muda mrefu na kukosa muda wa kukaa nao na kuwafundisha kuwajibika katika kazi ndogondogo za nyumbani ambazo ni msingi mkubwa kwa watoto katika kuwa wawajibikaji katika shughuli nyingine kubwa hapo baadae katika Maisha yao binafsi.

Elimu ya darasani (nadharia) pekee haitoshi kumjenga mtoto kuwa muwajibikaji bali kazi za vitendo pia kama vile kulima bustani za mbogamboga, kupika, kulisha mifugo, kumwagilia maua na nyinginezo zina uwezo wa kumjenga mtoto kuwa na maono ya kuwajibika na kujikita katika mojawapo ya kazi anazofundishwa nyumbani hapo baadae kama vile kuwa mkulima au mfugaji. Kuwaachia wasaidizi wa kazi za nyumbani kuzitekeleza wenyewe sio msingi mzuri wa kuwajenga watoto.

Kuna tatizo kubwa la ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo katika nchi yetu, tatizo hili linaweza kuanza kutatuliwa kwa kuanzia kwenya ngazi ya familia kwa njia ya malezi yenye msingi wa uwajibikaji kwa watoto. Mtoto anapohimizwa kufanya kazi ya bustani haitakuwa ngumu kwake kuwa na wazo la kuwa mkulima hata wa mbogamboga katika eneo dogo pindi atakapomaliza chuo jambo ambalo litaweza kumsaidia kujikimu mahitaji yake wakati akiwa anatafuta kazi yenye maslahi mazuri yatakayomsaidia katika Maisha yake.

Maisha yana matukio mengi kama ajali na vifo. Ninatamani kuona katika nchi yetu wazazi wanabeba uhalisia huu na kuwafundisha watoto kazi za mikono ili wawe na ujuzi endapo wasipokuwepo katika dunia hii watoto wao waweze kuendelea kuyamudu Maisha yao ya kila siku. Ni ukweli usiopingika kuwa wazazi wakiweka misingi ya kumcha Mungu, kuwajibika na kuridhika katika malezi hatutakua na vikundi vya vijana wezi “panya road”, mabinti wanaojiuza “madanga” na vijana wa kike na kiume wanaojihusisha na ushoga, utapeli, uvivu na tabia nyingine nyingi ambazo hazikubaliki katika jamii.

Katika msingi wa kumcha Mungu, mtoto atajifunza mambo mengi sana kama vile Mungu hubariki kazi za mikono (Zaburi 90:17), mtu asipowajibika ipasavyo atakua masikini (Mithali 10:4) pia asiyewajibika hana haki ya kula (2Timotheo 3:10). Kuwa na ufahamu wa ukweli kama huu katika umri mdogo kunamhamasisha na kumjenga mtoto kuwa na mawazo ya kutaka kuwa na ujuzi wa mambo ya ziada na sio wa darasani pekee.

Ninatamani kuona katika nchi yetu wakati watoto wakilelewa katika misingi hii na wazazi pia wawe mfano wa kuigwa. Baba na mama wote wawajibike ipasavyo asiwepo mmojawao ambaye hajishughulishi na kazi yoyote ya kiuchumi. Lakini pia katika mgawanyo wa majukumu nyumbani wazazi wawe na usawa wa kijinsia yaani isiwepo kazi ya mtoto wa kiume na mtoto wa kike kwani kukiwa na mgawanyo wenye mtazamo huu utapelekea kuwa na matabaka katika majukumu kati ya mwanaume na mwanamke hapo baadae.

Kwa kupitia misingi hii katika malezi kutaibua usawa wa ushiriki katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii kiujumla na kuleta maendeleo jumuishi katika taifa letu.

Sisemi kuwa wazazi hawawajibiki ila ninachotamani kuona ni mkazo zaidi uendelee kuwekwa katika suala la malezi ya watoto katika misingi ambayo itajenga taifa bora kwani watoto wa leo ni viongozi wa kesho hivyo wasipolelewa katika misingi ya kumcha Mungu, kuwajibika na kuridhika watakapokuja kuwa viongozi tutegemee kuwa watakuwa viongozi wasio waaminifu, wapokea na watoa rushwa, wahujumu Uchumi, wenye kukubali ushawishi wa watu wenye nia ovu za kuingiza tamaduni zisizofaa katika jamii zetu, wezi na tabia nyingi ambazo sio sifa za viongozi bora.

Viongozi wahusika waratibu semina, warsha na makongamano mbalimbali ambayo yatakuwa na lengo la kuwahimiza wazazi katika malezi bora na pia matukio yatakayohudhuriwa na watoto yenye lengo la kuwajenga katika misingi hii kwa manufaa ya taifa. Viongozi wa dini watumie nafasi zao kuwakumbusha wazazi maandiko matakatifu yanaelekeza mambo gani ya msingi katika suala zima za malezi ya familia wao wenyewe wakiwa mfano wa kulea watoto wao katika misingi bora ili wafuasi wao waone kwa vitendo yale wanayowaelekeza.

Tanzania yenye maendeleo inawezekana pale ambapo tutakuwa na viongozi wenye misingi ya Kumcha Mungu, Uwajibikaji na Kuridhika. Misingi hii haipatikani popote isipokuwa kwenye chimbuko lao ambalo ni familia sehemu pekee panapoweza kuwa na malezi yenye misingi hii. Wazazi wawekeze malezi yenye misingi hii mitatu kwa taifa bora litakaloongozwa na wacha Mungu, wawajibikaji na wenye kuridhika.
 
tatizo hili linaweza kuanza kutatuliwa kwa kuanzia kwenya ngazi ya familia kwa njia ya malezi yenye msingi wa uwajibikaji kwa watoto. Mtoto anapohimizwa kufanya kazi ya bustani haitakuwa ngumu kwake kuwa na wazo la kuwa mkulima
Sahihi kabisa.

Kuwa na ufahamu wa ukweli kama huu katika umri mdogo kunamhamasisha na kumjenga mtoto kuwa na mawazo ya kutaka kuwa na ujuzi wa mambo ya ziada na sio wa darasani pekee.
Ukweli mwingine ni mtu anayetaka kuwa mkubwa baina ya wote ni atakayeweza kuwatumikia hao wote. Mfano bakhresa analisha maandazi na chapati nchi nzima kwa nini asiwe mkubwa? Great person.

Misingi hii haipatikani popote isipokuwa kwenye chimbuko lao ambalo ni familia sehemu pekee panapoweza kuwa na malezi yenye misingi hii. Wazazi wawekeze malezi yenye misingi hii mitatu kwa taifa bora litakaloongozwa na wacha Mungu, wawajibikaji na wenye kuridhika.
Hakika, umelitambua chimbuko na tunashukuru kwa kutujulisha na sie.
 
Back
Top Bottom