siku zote alikuwa wapi huyu!? 😕
Mbunge wa CCM naye akerwa na wawekezaji katika migodi
* Awakoromea mbele ya Waziri Mkuu Lowassa
Na Mkinga Mkinga, Mara
Kutoka Gazeti la Mwananchi
MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, amewashutumu wawekezaji katika migodi ya madini mkoani Mara kuwa wanahamisha rasilimali hiyo na wakiwaacha wananchi wakiwa masikini, huku wakichangia kiasi kidogo kwenye maendeleo ya jamii.
Alisema licha ya kuchimba madini ambayo yanawapatia fedha nyingi, mchango wao katika jamii hauendani na kile wanachokivuna kwenye mgodi hiyo.
Mbunge huyo alisema kinachofanyika ni kuhamisha madini hayo na kuwaachia wananchi umaskini mkubwa.
Akizungumza katika ziara ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kukagua shule za sekondari zilizojengwa na mbunge huyo kwenye Kijiji cha Busegwe, Mkono alisema mchango wa wawekezaji hao ni kidogo sana.
"Katika mkoa mzima huwezi kuona shule nzuri kama nilizojenga mimi, hata ukienda shule zilizojengwa na hao wawekezaji," alitamba Mkono huku Lowassa akiwa amekaa kimya.
Mkono amekuwa akipinga kiwango kidogo cha michango ambacho kimekuwa kikitolewa na wawekezaji katika mendeleo ya jamii kama ujenzi wa shule na vituo vya afya kuwa, hailingani na thamani ya rasilimali wanayovuna.
Mbunge huyo aliwahi kususia makabidhiano ya Sh240 milioni kutoka kwa wawekezaji, akidai kuwa hataki kuona uchafu ukifanyika mbele yake kwa sababu hajui umiliki wa migodi hiyo pamoja na uliokuwa jimboni lake la Buhemba.
?Sitaki kuona uchafu huo unafanyika mbele yangu. Maana hiyo mikataba mimi siijui, hata ule wa mgodi wa Buhemba, ambao uko jimboni kwangu sijui unamilikiwa na nani,? alinukuliwa Mkono wakati akisusia kushuhudia makabidhiano hayo kati ya Kampuni ya Barrick Gold Tanzania na halmashauri za wilaya ambako kuna migodi yake.
Wilaya zenye migodi inayomilikiwa na kampuni hiyo ni Tarime, Kahama na Biharamulo.
Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, anahoji uhalali wa kiwango cha dola 200,000 zilizoainishwa kwenye mikataba kwa ajili ya halmashauri husika na anapendelea kupitia upya mikataba kabla ya kupokea fedha hizo.
?Kisheria kukubali kidogo ina maana umekubali moja kwa moja, hapa huwezi baadaye ukataka watoe fedha zaidi,? aliendelea kunukuliwa Mbunge huyo.
Wakati mbunge huyo akitoa shutuma hizo, kuna sakata linaloendelea kati ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kuhusiana na kusainiwa mkataba wa mgodi wa Buzwagi nje ya nchi. Mgodi huo pia unamilikiwa na Kampuni ya Barrick.
Sakata hiyo imesababisha Zitto kusimamishwa shughuli za ubunge baada ya kuwasilisha hoja binafsi bungeni, akitaka kuundwa kwa Kamati Teule kuchunguza mchakato wa mkataba huo.
Tangu kuibuliwa kwa tuhuma hizo, kumekuwa na maelezo yanayokinzana kuhusiana na ufafanuzi juu kwa upande wa Barrick na Waziri Karamagi, huku wakichanganyana kwenye tarehe za mchakato hadi kusainiwa London, Uingereza.