SEHEMU YA 103
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua kile kilichotokea ndani ya piramidi, watu waliendelea kuingia na kutoka kwa siku hiyo lakini baada ya saa mbili, sauti na mwanamke ikasikika kutoka ndani, kila mtu alishtuka, mbali na kupiga kelele hizo, akatoka huku akihema kwa nguvu.
Kila mtu alimwangalia, alionekana kuona kitu cha ajabu ndani ya piramidi hilo. Polisi na wasimamizi wakamfuata na kumuuliza kilichokuwa kimetokea, akawaambia kwamba aliona maiti ya mtu mmoja ndani ya piramidi lile kitu ambacho polisi na wasimamizi walikataa lakini wakataka kwenda ili kuhakikisha kwa macho yao.
Wakaelekea huko, kile walichoambiwa ndicho walichokiona, waliuona mwili wa mwanaume ukiwa chini, ulichomwa kisu huku ukiwa umeburuzwa na kuacha michirizi ya damu sakafuni.
Picha iliyoonekana iliwaogopesha.
Kutokana na mwanga hafifu uliokuwa humo wakashindwa kumgundua mara moja hivyo kuchukua tochi na kummulika, napo hawakumgundua lakini baada ya kuona kadi zake za kibiashara ndipo wakagundua kwamba mtu huyo alikuwa Keith, bilionea mkubwa.
“Ni Keith! Yule bilionea wa Marekani!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Si unamuona!”
Hawakujua ilikuwaje mpaka mwanaume huyo kuuawa ndani ya jengo hilo kubwa.
Walibaki wakiulizana, alivyoonekana ni kwamba hakuuawa muda mrefu uliopita kwani hata michirizi ya damu ile haikuwa imeganda, ilikuwa damu mbichi kabisa hali iliyoonyesha kama wangeamua kumtafuta muuaji, hakuwa amefika mbali.
Wakaondoka na kuelekea nje, katika geti la kuingilia, walitaka kufahamu mwanaume huyo aliingia na nani ndani ya piramidi lile. Wakapitia majina na kugundua kwamba aliingia na mwanamke aliyeitwa kwa jina la Maria Ogabugu.
“Yupo wapi?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hebu tukaangalie kwenye kamera!”
Hilo ndilo walilolifanya, wakaenda katika chumba kilichounganishwa na kamera ndogo za CCTV zilizokuwa mahali hapo, walitaka kuona tangu kipindi watu hao walipoingia, na kama mwanamke huyo alikimbia, ilikuwaje?
Itaendelea.....