Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

Aiseeee ndio nini hiki kuwa mstaarabu basi
 
SEHEMU YA 85

Alipoamaliza kuyafikiria sana maisha yake akaondoka na kwenda chooni, huko, akajisaidia kete za madawa ya kulevya aliyokuwa amewekewa tumboni na kukiflashi choo kwa maana kwamba hakutaka kuyachukua kwa kuwa alitaka maisha yake yawe upya tena, yawe safi na amuabudu Mungu kwa hali na mali.

Siku iliyofuata akaanza safari ya kuelekea nchini Marekani. Hakutaka kuondoka kwa ndege jijini Marseille, alichokifanya ni kupanda basi ambalo lilimpeleka mpaka Monaco ambapo huko ndipo alipopanda ndege na kuelekea huko.

Ndani ya ndege, mawazo yake yalikuwa katika maisha yake tu, bado aliendelea kuumia kupita kawaida, hakuacha kulia, moyo wake uliendelea kuwa kwenye majuto kiasi kwamba kuna wakati alijiona kuwa na dhambi nyingi kuliko hata shetani mpaka kuhisi kwamba hata kama angefanya kitu gani Mungu asingeweza kumsamehe.

“Mungu naomba unisamehe!” alisema Fareed wakati ndege ikikata mawingu kuelekea Uingereza kabla ya kuunganisha na kuelekea nchini Marekani.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 86

Fareed alifika nchini Marekani majira ya saa 10:30 jioni. Hali yake hewa ilikuwa ni baridi kali, katika sehemu kubwa ya Jiji la New York kulikuwa na theluji kitu kilichomfanya kuwa kwenye wakati mbaya mno.

Akaondoka uwanjani hapo kwa kuchukua teksi ambayo ilimpeleka mpaka katika Hoteli ya Queen Cleopatra ambayo haikuwa mbali sana kutoka katika uwanja huo. Alipofika, akakifuata kitanda na kutulia.

Bado kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, akili yake ilichanganyikiwa kupita kawaida. Maisha aliyokuwa amepitia yalikuwa machafu yaliyomfanya kulia sana.

Hakutaka kumwambia mtu yeyote kwamba aliamua kuyabadilisha maisha yake, hata Asteria alipokuwa akimtumia meseji kwa njia ya WhatsApp au hata kumpigia hukohuko hakuwa akipokea simu kwani alihitaji muda wa kuwa peke yake, Mungu ayasafishe maisha yake na kuishi maisha matakatifu.

“Nilisikia kwamba Yesu alikufa kwa ajili yetu wanadamu! Alisulubiwa ili tupate ukombozi, kwa kupigwa kwake, sisi tumepona. Mungu naomba unisaidie, uusafishe moyo wangu kwa damu ya Yesu,” alisema Fareed huku akiwa kitandani, hakuishia hapo, akatoka kitandani hapo, akapiga magoti na kuanza kusali kwa maneno aliyoyafahamu yeye kwani hakuwahi kuingia kanisani hata mara moja.

Sala yake ilichukua dakika tano, alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa, aliuona upendo wa Mungu mpaka kumtoa mwanaye wa pekee kuja duniani kwa ajili ya maisha ya wanadamu lakini mwisho wa siku wanadamu hawakutaka kuyabadilisha maisha yao akiwemo yeye.

Alisikia hukumu kubwa moyoni mwake, alikuwa akilia na wakati mwingine alikipiga kifua chake kwa maumivu makali mno kwani hakuamini kama alikuwa amefanya uovu mkubwa kiasi hicho.

“Mungu! Naomba unisamehe! Mungu, mimi ni mwanadamu, nimekutenda dhambi, moyo wangu unalia, unahuzunika na kuumia, sikustahili kukutendea hay. Mungu! Nisamehe, usafishe moyo wangu,” alisema Fareed huku akiendelea kulia kama kawaida.

Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kutubu dhambi zake, ulipofika usiku akalala huku akisubiri asubuhi ya kesho aende katika Kanisa la St. Peter ili kuungama dhambi zake kwa padri aweze kusamehewa.
 
SEHEMU YA 87

Akalala, alipoamka hakutaka kuendelea kubaki hotelini, akachukua mkoba wake na kuelekea katika kanisa hilo ambalo nalo wala halikuwa mbali kutoka mahali pale alipokuwa.

Alipofika, hakukuwa na watu wengi kanisani, kulikuwa na watu watatu tu ambao walikaa kitofautitofauti wakisali na kusoma Biblia. Akaa kwenye kiti na kisha kupiga ishara ya msalaba na kupiga magoti.

Hapo kanisani, akaanza kulia tena, bado moyo wake ulichoma mno, maovu mengi aliyokuwa ameyafanya kipindi cha nyuma yalikuwa yakijirudia kichwani mwake kama mkanda wa video kitu kilichomuumiza kupita kawaida.

Alipomaliza, akatoka na kwenda kule kulipokuwa na chumba cha kuungamia dhambi zake ambapo akakuta kiti kikiwa karibu na kidirisha kidogo kilichokuwa na wavu ambapo ndani ya chumba kile kulikuwa na padri aliyekuwa na kazi ya kusikiliza dhambi za watu waliokuja kuungama.

Fareed akakaa kwenye kiti kile huku akilia. Akaanza kumsubiri padri Luke ambaye akafika mahali hapo baada ya dakika mbili kupita.
“Karibu sana mtoto wa Mungu!” alisema padri Luke.
“Nashukuru padri!”

“Niambie, unataka kumwambia nini BWANA?”
“Nimefanya dhambi nyingi. Nimekuja kuungama,” alisema Fareed huku akiendelea kulia.
“Zipi hizo?”

Hapo ndipo alipoanza kumuhadithia Padri Luke dhambi zake alizokuwa amezifanya. Alikuwa akilia kwa uchungu. Hakutakiw akuficha kitu chochote kile, alimwambia kila kitu kilichotokea katika maisha yake, jinsi alivyoanza kufanya mchezo wake wa ushoga mpaka pale alipofikia, alimwambia jinsi alivyolala na wanaume na kuwachezea alivyotaka.

Padri Luke alikuwa kimya akimsikiliza, Fareed aliungama dhambi zake na mwisho wa siku padri kumwambia kwamba Mungu alimsamehe dhambi zake zote na siku inayofuata alitakiwa kurudi kanisani hapo kwa ajili ya kupakwa mafuta ya baraka kwani alikuwa akiingia katika maisha mapya ya kumuabudu Mungu.
 
Back
Top Bottom