Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 83

Hawakutaka kuona wakishindwa, waliamini kwamba kama wangemtafuta mtu huyo angepatikana hivyo kuingia mitaani na kuanza kumtafuta. Walitumia saa nne lakini hawakufanikiwa kumpata na muda wote huo Belleck alikuwa akiwasumbua kwenye simu kwa kutaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea.

Walianza kwa kumficha lakini mwisho wa siku walipoona muda umekwenda sana na hawakumpata, wakaamua kumwambia ukweli kwamba Fareed aliwatoroka hospitali.
“Alitoroka?”
“Ndiyo!”
“Aliwatorokaje?”

Wakaanza kumwambia namna mtu huyo alivyowatoroka, alitaka kuwalaumu lakini baada ya kuambiwa mazingira yote jinsi alivyotoroka, akaridhika na kuona kwamba hata kama angekuwa yeye ilikuwa ni lazima kutorokwa kama ilivyokuwa kwa wenzake.

“Ila hakikisheni mnamtafuta hapo. Najua atakuwa hapohapo Marseille,” alisema Belleck huku akiwa na uhakika kwamba mtu huyo hakuwa ametoka hapo Marseille.
“Haina shida mkuu!”

**** Fareed alikuwa ndani ya chumba cha hoteli, moyo wake ulikuwa kwenye majonzi tele, siku hiyo hakujisikia vizuri kabisa. Aliyakumbuka maisha yake aliyokuwa amepitia, jinsi alivyokumbwa na pepo la ngono ambalo lilimfanya kushiriki mapenzi ya jinsi moja.

Moyo wake ulimuuma mno, ulichoma kiasi kwamba hadi machozi ya uchungu yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Alijijua kwamba yeye alikuwa mkosaji, alijua kwamba Mungu alimuumba mwanaume kwa kuwa alikuwa na makusudi naye, hapo akagundua kwamba Mungu hakufanya makosa kumuumba mwanaume bali alikuwa na makusudi mengi.

Alijuta, siku hiyo alijikuta akianza kuyafikiria maisha yake, njia zake mbaya alizopitia, alilia kama mtoto chumbani mule. Nafsi yake ilimuhukumu, ilimwambia kwamba alichokuwa amekifanya kwa miaka yote halikuwa kusudio la Mungu bali la shetani ambaye aliamua kumtumikisha kupitia mwili wake.

Alitaka kubadilika, hakutaka kuendelea kumtumikia shetani, alitaka kubadilika na kuwa mtu mwingine kabisa. Tangu azaliwe, hakuwahi kwenda msikitini wala kanisani, hakujua yeye alikuwa dini gani, alijichagulia maisha yake kuishi hivyo hata alipotaka kuyabadilisha maisha yake.
 
SEHEMU YA 84

Kwa kuogopa maneno mengi ya watu akaamua kuchagua kwenda kanisani, lakini isiwe nchini Tanzania, aliijua mitandao ya kijamii, magazeti ya kidaku ambayo kwa namna moja au nyingine yangemwandika, hivyo kama aliamua kwenda kanisani, basi iwe nchi za hukohuko.

Akalifikiria kanisa kubwa la St. Peter lililokuwa jijini New York nchini Marekani. Lilikuwa miongoni mwa makanisa makubwa ambalo liliwahi kutembelewa na Papa José Kentenich miaka ya 1880.

Padri aliyekuwa akilichunga kanisa hilo aliitwa Mathew Luke. Alikuwa miongoni mwa mapadri waliojulikana nchini Marekani ambapo watu wengi na kumuheshimu huku wengine wakiombea padri huyo achukue nafasi ya upapa siku moja.

Alikuwa mwanaume mpole, aliongea taratibu huku akipenda sana kuonyesha tabasamu pana usoni mwake. Watu wengi walimpenda, uzuri wake wa sura ukawafanya watu wengi kwenda kuabudu katika kanisa hilo.

Mbali na uzuri wa sura aliyokuwa nayo, kitendo cha Papa José Kentenich miaka ya 1880 kuwahi kutembelea huko kikalifanya kanisa hilo kuwa maarufu na wengi kwenda huko kuabudu.

Fareed hakutaka kusikia jambo lolote lile, hakutaka kuzuiwa na mtu yeyote kuelekea huko, alidhamiria kwa moyo wake kwamba ilikuwa ni lazima aende akaungame dhambi zake, Mungu amsamehe kwa yote aliyoyatenda katika maisha yake.
 
Back
Top Bottom