SEHEMU YA 82
Hakutoka mahali hapo, aliendelea kusimama na baada ya dakika kadhaa akamuona Dk. Watson akiteremka kutoka katika gari lililoingia sekunde chache, alipowaona wale vijana, akawafuata, akazungumza nao kwa sekunde kumi, ghafla wote wakaanza kukimbia kuelekea ndani.
Alijua fika kwamba walimpa taarifa kuhusu yeye, hakutaka kusubiri mahali hapo, haraka sana akachomoka pale alipokuwa na kuelekea nje ya hospitali hiyo ambapo baada ya kufika huko, akachukua teksi na kuondoka mahali hapo.
*** Dk. Watson na vijana wale wakafika mpaka ndani ya chumba kile, walishtuka, hakukuwa na mtu yeyote yule, Fareed ambaye walimuacha humo hakuwepo.
Walichanganyikiwa, hawakuamini kile walichokuwa wamekikuta. Wakaanza kumtafuta kila kona ndani ya hospitali hiyo lakini mtu huyo hakuonekana.
Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya, hawakujua mahali alipokuwa ameelekea, hawakujua ni jinsi gani wangemwambia bosi wao, Belleck ambaye alikuwa akisubiri taarifa ya kifo cha Fareed kwa hamu kubwa.
“Yupo wapi?” aliuliza Dk. Watson.
“Hatujui! Ila tulimuacha humu ndani!”
“Sasa yupo wapi?”
“Hatujui!”
Walimfikiria Belleck, alikuwa mwanaume makini aliyetaka kuona kila kitu alichoagiza kikifanyika kwa haraka sana. Alitaka mtu huyo afe lakini la zaidi aliyataka madawa yake ya kulevya ambayo yalikuwa na thamani kubwa mno.
Hawakujua angefanya nini kama wangempa taarifa kuwa mwanaume huyo alimimbia, aliwatoroka wakati nesi alipopiga kelele kwa kuhisi kwamba walikuwa watu wabaya.