Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 80

Belleck alikuwa ametulia, masikio yake yalikuwa kwenye simu yake, alitaka kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea nchini Ufaransa, alitaka kujua kama tayari Fareed alifanyiwa upasuaji na kutolewa kwa kete za madawa ya kulevya au kitu hicho hakikuwa kimefanyika.
Alisubiri sana, tangu Fareed afikishwe ndani ya hospitali, aliambiwa kwamba angepigiwa simu na kupewa kila kitu kilichokuwa kimeendelea lakini mpaka saa moja na nusu bado hakuwa ametaarifiwa kitu chochote kile.

Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilitokea, hakutaka kuvumilia, hapohapo akachukua simu yake na kupiga upande wa pili, simu ilipopokelewa, akaambiwa kila kitu kilichokuwa kimetokea.
“Kwa hiyo Dk. Wtason hayupo?” aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo mkuu!”

“Atatuchelesha, ingieni ndani na mmuue kisha zitoeni hizo kete, hakuna haja ya kuendelea kumsubiri muda wote,” alisema Belleck na kukata simu.
Ilikuwa ni amri, vijana hao hawakutaka kuendelea kumsubiri daktari huyo, walitaka kufanya kile walichokuwa wameambiwa. Fareed alikuwa ndani ya chumba kile, haikuwa kazi kubwa kuingia na kumuua kisha kulipasua tumbo lake na kuzitoa kete alizokuwa amezimeza.

Wakaufuata mlango kwa lengo la kuufungua, haukufunguka, ulionekana kufungwa kwa ndani. Kwa kuwa hiyo haikuwa hospitali kubwa sana, hakukuwa na wagonjwa wengi wala madaktari hivyo kuanza kuupiga mlango huo kwa lengo la kuuvunja na kuingia, tayari walipewa agizo kwamba mtu huyo auawe hivyo hawakuwa na msalie mtume.
*
*

“What are you doing?” (mnafanya nini?) lilisikika swali kutoka kwa mwanamke aliyekuwa nyuma ya watu hao waliokuwa wakijaribu kuuvunja mlango ule wa chumba alichokuwemo Fareed.

Vijana wa Belleck wakageuka nyuma na kumwangalia mtu aliyewauliza swali hilo. Alikuwa nesi wa hospitali hiyo, kibonge, aliyevalia gauni refu jeupe huku kichwani akiwa na kikofia kidogo cha kilichoonesha kwamba alikuwa muuguzi.

Bastola zilikuwa mikononi mwao, kitendo cha mwanamke huyo kuziona bastola hizo, hakutaka kubaki mahali hapo, akaanza kukimbia huku akiwaita polisi kwani alijua kwamba watu hao hawakuwa watu wazuri hata mara moja.
 
SEHEMU YA 81

Ilikuwa ni hatari kwao, walijua kwamba hospitalini hapo kulikuwa na polisi, walijua fika kwamba walimiliki bastola zile kimagendo, wakaogopa na kuhisi kwamba kungekuwa na jambo baya, walichokifanya ni kukimbia mahali hapo kwenda kujificha kwani kama wangekutwa na polisi waliokuwa wakiitwa, maisha yao yangekuwa hatarini.

Fareed alikuwa ndani ya chumba kile, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alitamani hata kama kungekuwa na mlango wa kuingia darini, aingie na kujificha huko lakini alipoangalia, hakukuwa na malngo huo.

Bado kitasa kiliendelea kutekenywa, mule ndani alikuwa akiogopa mno, alikosa amani na muda wowote ule alikiona kifo chake kikiwa mbele yake. Wakati akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya ndipo akasikia sauti ya mwanamke yule ikiwauliza wanaume hao, badala ya kujibu swali waliloulizwa, wakaanza kukimbia huku mwanamke huyo akiwaita polisi.

Ghafla, ukimya ukatawala mahali hapo, akaona nafuu moyoni mwake, hakutaka kubaki ndani, aliamini kwamba hakukuwa na mtu yeyote nje ya chumba hicho hivyo alichokifanya ni kuchukua mkoba wake uliokuwa na nyaraka zake za kusafiria na kuufungua mlango,akachungulia nje ya chumba kile, kweli hakukuwa na mtu hivyo kuanza kutoka.

Alifanikiwa, hakukuwa na hatari yoyote ile, hakutaka kusubiri, alijua kabisa kwamba kuendelea kusubiri mahali hapo ingekuwa hatari kwa maisha yake hivyo akaondoka kwa kupitia mlango mwingine, kwani kama asingefanya hivyo ilikuwa ni lazima kuuawa mahali hapo.

Akaondoka mpaka nje ya hospitali ile. Akaanza kutembea kuelekea sehemu iliyokuwa na magari mengi yaliyokuwa yamepaki. Alikuwa akijifichaficha kwani mahali hapo hakukuonekana kuwa na amani kwa maisha yake.

Akafika sehemu moja iliyokuwa na kiukuta na kutulia hapo. Macho yake alikuwa ameyaelekezea kule kulipokuwa na mlango wa kutokea katika jengo la hospitali hiyo, akawaona wale wanaume wawili wakiwa sehemu wamesimama, alijua dhahiri kwamba walikuwa wakimsubiri yeye.
 
Back
Top Bottom