SEHEMU YA 79
Lilipofika saa moja, Fareed akashtuka kutoka katika usingizi aliokuwa nao. Kitu cha kwanza kabisa baada ya kuyafumbua macho yake ni kuangalia mahali alipokuwa.
Aligundua kwamba palikuwa ni hospitalini, hakukumbuka ni kwa namna gani alifika mahali hapo lakini baada ya kukaa na kukumbuka kwa sekunde kadhaa, akakumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Akakurupuka kutoka kitandani pale, ile haikuwa sehemu salama, alijua fika kwamba kama asingeondoka ndani ya chumba hicho ilikuwa ni lazima kupasuliwa tumbo lake na kutolewa kete za madawa ya kulevya zilizokuwa tumboni mwake.
Hakutaka kuona hilo likitokea, ilikuwa ni lazima kuondoka hospitalini hapo, akateremka kutoka kitandani, akaufuata mlango lakini hata kabla hajaufungua, akawasikia watu wakiwa wanaongea kwa nje.
“Mmh!” alijikuta akiguna.
Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, akarudi kitandani pale na kutulia, kichwa chake kilimuuma, alitamani hata kupitia katika mlango mwingine lakini kitu kibaya kwake ni kwamba hakukuwa na mlango wowote zaidi ya ule waliokuwa wakiutumia.
Minong’ono ile ya watu bado iliendelea kusikika kutoka nje ya chumba kile, aliogopa, kwa jinsi alivyoona, ilikuwa ni lazima watu hao waingie ndani kumwangalia kwani hakujua daktari alikuwa mahali gani.
Alichokifanya ni kuusogelea mlango na kisha kuufunga kwa ndani, hakutaka mtu yeyoite aingie ndani ya chumba kile na kumkamata, alijua kwamba angekufa, ila hakuwa tayari kuona akifa siku hiyo.
“Ni lazima nifanye kitu!” alisema lakini hata kabla hajafanya kitu hicho, akasikia kitasa cha mlango kikianza kutekenywa kwa ajili ya kufunguliwa lakini haukufunguka kitu kilichowafanya kuanza kuugonga kwa lengo la kuuvunja.