SEHEMU YA 49
Wakafika hotelini, Mickey hakutaka kuwa na haraka, aliamini kwamba huyo alikuwa wake hivyo alichokiifanya ni kumuacha huku akimpa dola elfu mbili na kuondoka zake pasipo kufanya kitu chochote kile.
Fareed alichanganyikiwa, alipoingia hotelini, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mwanaume huyo tu.
Hakuamini kama kweli alikuwa amefanikiwa kuwa na mtu aliyekuwa na pesa, ambaye hakuwa mchoyo kama alivyokuwa Mickey.
Akaanza kuwa msumbufu, kila wakati alikuwa akimpigia simu mwanaume huyo na kumuuliza alikuwa akiendeleaje, alitaka kuonana naye na kumpa haki yake na si kutumia pesa zake tu.
“Tutaonana tu mpenzi kabla sijarudi Australia! Utakuwa na nafasi usiku wa leo nikufuate twende klabu?” aliuliza Mickey.
“Yeah! Tena nitakuwa mpweke sana. Naomba uje kunichukua mpenzi!” alisema Fareed.
“Sawa. Nitakuja!” alisema Mickey na kukata simu.
Usiku huohuo Mickey akafika hotelini hapo, hakutaka kuchelewa, akamchukua Fareed na kuondoka naye. Walizungumza kama wapenzi, aliongea kama mwanamke na hata mapozi aliyokuwa akiyafanya pale kitini alipokaa alikuwa kama mwanamke.
Saa 8:12 usiku Mickey akamrudisha Fareed hotelini na kisha kuondoka zake. Njiani, hata kabla hajafika katika hoteli aliyochukua chumba, akachukua simu yake na kupiga upande wa pili ambapo baada ya sekunde kadhaa, ikapokelewa.
“Umefikia wapi?” iliuliza sauti ya upande wa pili.
“Kila kitu kipo poa. Kama itawezekana basi kesho tumuue,” alisema Mickey.
“Haina shida. Waambie wenzako kesho mfanye hayo mauaji! Au subiri mpaka nije. Kesho jioni nitaingia, nitahakikisha namuua kwa mkono wangu,” alisema mwanaume upande wa pili na kisha kukata simu.
Je, nini kitaendelea?