SEHEMU YA 60
Mkewe akaingia chumbani humo, akamfuata mumewe na kumuuliza kuhusu mtu huyo. Hakumficha, alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea, jinsi alivyowaona watu wabaya wakimtupa baharini kwa lengo la kumuua, lakini kwa kuwa aliwaona, akaenda kumuokoa akiwa amezamishwa ndani ya maji.
“Alhamdulilah!” alisema mkewe huku akiangalia juu na kuinua mikono yake kama ishara ya kumshukuru Mungu.
Hapo ndipo alipoanza kupata matibabu, katika kipindi chote hicho, mke wa mzee aliyekuwa Ahmedi hakuwa akijua kama mtu aliyepelekwa nyumbani kwake na mumewe alikuwa mwanaume, alikuwa na muonekano wa asilimia mia moja wa kike.
Aliharibika vibaya kwa nyuma, mzee Ahmedi aliligundua hilo lakini hakutaka kumwambia mke wake, alikuwa kimya huku wakati ambao mwanamke huyo hakuwepo nyumbani, alichukua nafasi hiyo kumtibu nyuma kulipoharibika vibaya.
Waliendelea kumuhudumia nyumbani hapo mpaka siku mbili baadaye aliporudiwa na fahamu. Kitu cha kwanza kabisa baada ya kufumbua macho ni kuanza kuangalia huku na kule, alishangaa mahali alipokuwa, hakukumbuka chochote mpaka alipotulia kwa dakika kadhaa na kukumbuka kile kilichokuwa kimetokea kabla ya kuwa mahali hapo.
Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama kweli Keith alimfanya hivyo, moyo wake uliumia, alitakiwa kuuawa lakini aliokolewa na mwanaume huyo mvuvi ambaye alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Fareed hakutaka kuondoka nyumbani hapo, alitulia, wiki moja baadaye alipojisikia afadhali, akaaga na kuondoka zake kurudi nchini Tanzania. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, kifua chake kikajaa kisasi, hakukuwa na kitu kilichomuumiza kama kubakwa na vijana wa Keith ambaye hakuridhika na kutaka kumuua.
Alipofika nchini Tanzania, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, akaelekea nyumbani kwake ambapo huko akampigia simu Asteria, baada ya kusikia sauti ya Fareed hakuamini, akamwambia kwamba angekwenda nyumbani hapo kuzungumza naye, alitaka kujua ni kitu gani kilitokea.
Ndani ya dakika thelathini tu mwanamke huyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo, alimkumbatia Fareed, hakuamini kama mwanaume huyo alikuwa hai, alijua kwamba alikufa.
“Nilikufuata mpaka Dubai,” alisema Asteria.
“Ikawaje?”