SEHEMU YA 137
Hakuwa na uamuzi mwingine zaidi ya huo na safari ilitakiwa kufanyika usiku. Fareed akajiandaa na baada ya siku mbili, magari mawili ya kifahari yakafika hotelini hapo na kumchukua kisha kumpeleka uwanja wa ndege.
Moyo wake ulikuwa na hofu, hakuamini kama angefika salama huko kwani kila kona alikuwa akitafutwa na FBI ambao hawakutaka kuzisambaza picha zake, walimtafuta kimyakimya ili asishtukie kama anatafutwa kumbe mwenzao alikwishajua hilo kitambo.
Uwanja wa ndege, hakupitishwa mlango wa kawaida, ndege ilikuwa ni ya binafsi tena ya bilionea mkubwa duniani, hivyo hata mlango aliopitishwa ulikuwa ni wa VIP na ilikuwa vigumu kumgundua kwamba alikuwa yeye.
Mpaka anakaa katika kiti ndani ya ndege hiyo, akashusha pumzi ndefu, hakutegemea kama ingekuwa kazi nyepesi namna hiyo.
Huku nyuma, bilionea Williams alikuwa akifanya mawasiliano na watu wake waliokuwa Ufaransa, alitaka kupata data zote kuhusu bilionea huyo, kwamba alikuwa akiishi katika hoteli gani na ratiba yake ya siku ilikuwaje.
Hilo halikuwa tatizo kwa vijana wake, kwa kuwa walikuwa huko na mtu huyo alikuwa maarufu, wakapata data zote na kumtumia na hivyo na yeye kumtumia Fareed ambaye baada ya kuzipokea, akamshukuru Mungu.
“Sasa kazi itafanyika,” alimwambia Williams kwenye simu.
“Ukikamilisha! Nakuahidi kukupa dola milioni kumi.
Huyu mpumbavu ananinyima sana usingizi,” alisema William huku akiwa na uhakika kwamba ilikuwa ni lazima mwanaume huyo ammalize Bilionea Belleck.
Ila la zaidi, alitaka kuona bilionea huyo akifa na yeye kumuua Fareed kwani kama angemuacha, siri ingeweza kuvuja. Ili siri itunzwe ilikuwa ni lazima hata naye Fareed afe.