SEHEMU YA 131
Lilikuwa tukio kubwa lililoishtua dunia, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kweli Marekani ingeweza kulipuliwa kama ilivyotokea.
Kila mtu alishangaa kwani kwa jinsi nchi hiyo ilivyokuwa imejiwekea ulinzi tangu kulipuliwa kwa maghorofa ya biashara ya WTC, hakukuwa na aliyeamini kwamba kweli magaidi wangeweza kuilipua nchi hiyo kwa mara nyingine.
Watu zaidi ya elfu moja mia tano wakasadikiwa kufa katika tuki hilo huku maelfu wakijeruhiwa vibaya. Ndani ya dakika chache tangu tukio hilo litokee, magari ya zimamoto yakafika mahali hapo yakiongozana na magari kadhaa ya wagonjwa.
Polisi wakaweka kamba ya nyano iliyoandikwa ‘Do not cross’ yaani Usivuke huku ni polisi tu na watu wa afya ndiyo walioruhusiwa kwenda ndani ya kituo kile kulipotapakaa miili mingi ya watu.
Mambo yote hayo yalikuwa yakiendelea huku Fareed akiwa chini, hakujitambua, pale alipokuwa, kwa jinsi alivyokuwa amerushwa, ilikuwa vigumu kuamini kama mtu huyo alikuwa mzima.
Yeye na majeruhi wengine wakachukuliwa na kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu huku nyuma waandishi wa habri wakiendelea kukusanyika katika eneo hilo la tukio kwa ajili ya kuripoti kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Gari halikuchukua muda mrefu likafika katika Hospitali ya St. Joseph Medical Centre iliyokuwa hapohapo Pennsylvania ambapo mara baada ya magari kuingizwa ndani, machela zikaletwa, majeruhi wakapandishwa kwenye machela hizo kisha kupelekwa ndani.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa Fareed kukaa ndani ya hospitali hiyo. Matibabu yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Baada ya saa kumi na mbili, akarudiwa na fahamu, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Mahali pale palikuwa ni hospitali, hakujua alikuwa amefikaje, aliangalia huku na kule, kwa juu, dripu ilikuwa ikining’inia huku mwili wake ukiwa na maumivu makali kiasi kwamba alishindwa hata kugeuka.