Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 142

Hilo halikuwa na tatizo, akaruhusiwa na kuondoka huku akiwa na kadi ile mkononi. Alipofika katika chumba cha rafiki yake, akagonga mlango, ulipofunguliwa, akampa kadi na kumwambia ampe Fareed ambaye alitakiwa kukamilisha kazi ya mauaji na kuondoka hotelini hapo.

Hilo halikuwa tatizo, kadi ikachukuliwa, De Leux akarudi chumbani kwake kuendelea kufanya mapenzi na msichana huyo. Huku nyuma, rafiki yake akampelekea kadi ile Fareed ambaye aliichukua na kuufuata mlango wa chumba kile.

Fareed hakuwa mikono mitupu, alikuwa na kisu pamoja na dawa kali ya usingizi ya Microphenon ambayo ilikuwa ikitumika sana katika vyumba vya upasuaji.

Alipoulikia mlango ule, akaingiza kadi, mlango ukafunguka, akaingia ndani.
Belleck na mpenzi wake walikuwa wamelala, kabla ya kufanya chochote, akaanza kupulizia dawa ile ya usingizi ambapo baada ya kuwaingia wote wawili, wakapitiwa na usingizi mzito, tofauti na ule waliokuwa nao.

Kwa haraka sana Fareed akamfuata Belleck pale alipokuwa, akamshusha na kumuweka sakafuni, akanza kumchomachoma visu vya tumbo. Damu zilitoka lakini hakujali, alichoma mara kadhaa, akauacha mwili wa mwanaume huyo chini na kuuburuza kidogo hali iliyoifanya damu ile kutengeneza michizrizi sakafuni pale.

Hakutaka kuondoka hivihivi, akachukua kalamu na karatasi kisha kuandika maneno mafupi yaliyosomeka C'est fait yakiwa na maana ya kukamilika kwa jambo au ‘done’ kwa Lugha ya Kiingereza.
Fareed hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, kwa haraka sana akatoka na kuelekea chumbani kwa rafiki yake, De Leux ambapo akampa ile kadi na yeye kuichukua na kumpeleka mwanaume huyo ambaye bado alikuwa akiserebuka na msichana yule chumbani kwake.

Alipopiga hodi tu, De Leux akafungua mlango, akapewa kadi ile na kisha kurudi kitandani. Mpaka mambo hayo yote yanafanyika, Natalie hakujua kitu chochote kile, alichukulia kawaida, hakujua kama mwanaume huyo alichukua kadi na kwenda kufanya mauaji ndani ya chumba kimoja humo.
 
SEHEMU YA 143

Williams akapewa taarifa kwamba kila kitu kilichotakiwa kufanyika, kilifanyika. Moyo wake ulikuwa na furaha kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa akimchukia kipindi hicho kama alivyokuwa Belleck.

Akampa pongezi zake, hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alimuaidi kumpa kiasi cha dola milioni kumi, haraka sana akamuhamishia kiasi hicho mpaka kwenye akaunti yake kwa mategemeo kwamba kama atamuua basi kiasi kile kingeweza kuchukuliwa kirahisi ndani ya saa arobaini na nane.

Ilipofika asubuhi, hawakutaka kuendelea kukaa ndani ya hoteli hiyo, muda wao ulikuwa umefika na hivyo wote kuondoka hotelini humo. Safari yao ilikuwa ni uwanja wa ndege, tayari rubani alikuwa ameandaliwa na alikuwa na taarifa kwamba ilikuwa ni lazima warudi kuelekea nchini Marekani.

Walipofika uwanja wa ndege, wakapanda ndege na safari ya kurudi nchini Marekani ikianza. Huko, Williams akamtumia ujumbe mfupi De Leux kwamba Fareed hakutakiwa kufika nchini Marekani salama, ilikuwa ni lazima auawe njiani na kutupwa katika Bahari ya Atlantiki kitu ambacho kwa mwanaume huyo, jinsi alivyokuwa na ubavu, hilo halikuwa na tatizo lolote lile.

“No problem,” (hakuna tatizo) alijibu De Leux huku akiachia tabasamu. Wakati huo ndege ilikuwa njiani, ndiyo kwanza ilikuwa ikielekea katika anga ya bahari hiyo ambapo mauaji yalitakiwa kufanyika ndani ya ndege.

Alichokifanya ni kuwaambia wenzake kwamba piga ua mwanaume huyo alitakiwa kuuawa ili kuficha siri.
**** Hali ya hewa ilibadilika ghafla, mawingu mazito yakaanza kujikusanya angani kumaanisha kwamba mvua kubwa ingenyesha muda mfupi ujao.

Kila mtu alikuwa na hofu kwamba mvua ya siku hiyo ingekuwa kubwa kuliko zote ambazo ziliwahi kutokea nchini Ufaransa.
Watu wa idara ya hali ya hewa nchini Ufaransa walitoa angalizo kabla kwamba siku hiyo mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ingeweza kunyesha hivyo watu wote walitakiwa kujiandaa.
 
SEHEMU YA 144

Miungurumo ya radi ilikuwa ikisikika kila kona, watu wengi waliogopa na kujifungia ndani. Kabla ya mvua hiyo kuanza kunyesha, upepo mkali ukaanza kuvuma.

Ulikuwa mkubwa uliosababisha maafa makubwa kiasi kwamba wengine wakasema kwamba upepo kama huo mara ya mwisho ulivuma mwaka 1956 ambapo uliacha madhara makubwa kwa watu kufa na mali nyingi kuharibiwa.

Watu wengi waliogopa, katika viwanja vya ndege, hazikuruhusiwa kupaa kwani hali ilitisha sana na hata kwa ndege ambazo ziliondoka, kila mmoja alikuwa na hofu kwamba zingeweza kuanguka na kulipuka.

Miongoni mwa ndege zilizoondoka ilikuwa ile ndogo binafsi aliyokuwa Fareed na wenzake. Walipanga kumuua ndani ya ndege lakini kabla ya kufanya kile walichoambiwa wakifanye, ndege ikaanza kuyumba huku na kule.

Upepo ulikuwa mkali mno, rubani aliyekuwa akiiendesha ndege ile alichanganyikiwa, alijitahidi sana kuiweka sawa lakini ilishindikana kabisa. Ilikuwa katika usawa wa bahari, upepo mkali uliendelea kuvuma huku mawingu yakiwa yametanda kila kona.

Wote wakajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wao na hivyo ilikuwa ni lazima wajiokoe.
“Tunakufa…” alisema De Leux huku akionekana kuchanganyikiwa, hata wazo la kumuua Fareed likapotea.

Akaanza kuelekea mpaka kule alipokuwa rubani, akamuuliza juu ya hali iliyokuwa ikiendelea, akamwambia kwamba walikuwa usawa wa bahari, mita mia moja na ilikuwa ngumu kurudi kwani yeye mwenyewe alishindwa kabisa kuiweka sawa ndege hiyo.

“Kwa hiyo?”
“Hatujui tufanye nini! Tusalini sala zetu za mwisho!” alisema rubani, hakuona kama wangeweza kupona kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyejiona kuwa salama, kila mmoja aliona kuwa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.

Wakachukua maparachuti yaliyokuwa katika viti vyao kwa ajili ya kurukia baharini ambapo kulionekana kuwa salama kwa maisha yao.

Nje, hakukuwa na mwanga wa kutosha, mawingi mazito yalitanda na upepo mkali uliendelea kuvuma kama kawaida.

Chini, hawakuona kitu kwani mawingu yale yalianza kushuka chini kutokana na upepo huo uliokuwa ukiendelea kuvuma kama kawaida.
 
Back
Top Bottom