SEHEMU YA 129
Baada ya wiki moja kumalizika na mkutano huo kuisha, hakutaka kuondoka nchini Ufaransa, alitaka kuendelea kubaki mahali hapo kwani kulimteka, wanawake wazuri waliokuwa katika Jiji la Paris walimdatisha kichwa chake na hivyo kutamani kuendelea kukaa zaidi.
**** Kila kitu alichokuwa akikifanya ndani ya choo kile, Fareed alikifanya harakaharaka, hakutaka kuchelewa kwani kwa jinsi bomu lile lilivyoonekana, halikuwa limebakiza dakika nyingi kulipuka.
Akaliacha begi palepale chini na kisha kukimbia kutoka chooni hapo, hakutaka kubaki ndani ya kituo hicho kwani aliamini kwamba endapo angebaki basi naye pia angeweza kufa.
Kila mtu alibaki akimshangaa, wengine walihisi kwamba alikuwa mwizi, kwamba aliiba na hivyo kukimbia. Sehemu ambayo ilikuwa ikijifungua kwa kichuma kwenda juu baada ya kuweka tiketi, hakutaka hata ijifungue, akaruka kwa juu na kuelekea nje.
Wakati anafika nje ya kituo hicho kwa kupitia mlango mwingine, mabomu yakasikika yakilipuka na nguvu yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba mpaka wao waliokuwa nje ya kituo kile wakarushwa akiwepo yeye mwenyewe.
Akaangukia katika gari moja lililokuwa limepaki pembeni, watu wengine waliokuwa hapo walikuwa hoi, wengine walikuwa wakiteketa kwa moto, pale alipoangukia ambapo kulikuwa ni kama hatua kumi kutoka pale alipokuwa amefikia, Fareed alikuwa hoi, kichwa chake kilikuwa kikitoka damu, alisikia maumivu makubwa mwilini mwake.
Akajitahidi kusimama, akashindwa, akabaki hapohapo akiwa amelala huku macho yake yakiwa mazito kabisa. Akajitahidi kuuinua mkono wake, akashindwa, kila kitu alichotaka kukifanya mahali hapo alishindwa kabisa.
Kwa kutumia uangaliaji wake wa kwa mbali, akawaona watu wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada, baada ya sekunde ishirini tu akiwa hapo, giza kubwa likayafumba macho yake na baada ya sekunde hizo, akapoteza fahamu na hakujua kitu gani kiliendelea.