Miaka ya 80, 90 hadi 2000 Dar ilikuwa inachangamshwa na ngoma mbali mbali za kitamaduni, je wewe unakumbuka ngoma ipi?

6 Pack

JF-Expert Member
Apr 17, 2022
1,826
4,074
Enzi hizo ilikuwa ukienda Kinondoni kuanzia ijumaa hadi jumapili maeneo mengi yalikuwa yakitawaliwa na ngoma ya sindimba, ambayo inasemekana asili yake ni huko mkoani Mtwara na wenyeji wa ngoma hiyo ni wamakonde haswa wale waliochanjwa chale.

Siku hizo hizo za ijumaa hadi jumapili ilikuwa ukienda maeneo ya mabibo unakutana na sangula ambayo inasemekana asili yake ni huko Morogoro na wenyeji wa ngoma hii ni kabila la wapogoro wanaopatikana katika wilaya ya Mahenge.

Ukitoka huko ukisema usogee sogee hadi maeneo fulani fulani ya mburahati unakutana na dundo la kingoni ambalo nimelisahau jina lake. Aisee ikipigwa hiyo hakuna mngoni ambae atakaa chini hadi mwisho wa ngoma.

Ukisema ujielekeze manzese, buguruni, temeke, mwananyamala kisiwani, tandale na maeneo mengine ya uswahilini huko ilikuwa ni ngoma za wenyeji wa mkoa. Namaanisha wazaramo na vanga lao au wakizunguka na mdundiko karibu mkoa mzima wa Dar es salaam.

Kama na wewe ulikuwepo zama hizo ni ngoma gani nyingine uliishuhudia mtaani kwako ambapo sasa hivi ni nadra kuiona?

Enzi hizo tulikula raha kweli kweli, tofauti na leo kumuona Diamond elfu 50.
 
Back
Top Bottom