Nina huzuni sana kuona mtu akiandika matusi ya hivi kuhusu nchi yake ya kuzaliwa.
Ama ikiwa yeye anafanya makosa kufikiri hivyo, au ikiwa wengine wamemkosea mpaka kumfanya aseme hivyo, au hata ikiwa ni mchanganyiko wa mawili hayo, bado ni jambo la huzuni sana.
Nimekaa nje ya nchi niliyozaliwa ya Tanzania, hususan Marekani, miaka takriban 20 sasa, na kwa kweli nitakuwa muongo nikisema sijawahi kufikwa na hisia za kuhoji uzalendo wangu kutokana na mwenendo wa uongozi nyumbani, na baadhi ya tabia za kijamii, na pengine kuhoji huko ndio uzalendo wenyewe.
Lakini kamwe sijajisikia kufika kuitukana nchi yangu ya kuzaliwa kwa jinsi hii.
Licha ya hivyo, naelewa baadhi ya sababu za matusi haya na watu kuyachukulia kirahisi.