Leo tarehe 18 Mei ni Siku ya Kimataifa ya Jumba la Makumbusho. Mwaka 2026 ni mwaka maalum – unaoashiria miaka 70 tangu China na Afrika zianzishe uhusiano ya kidiplomasia, pia ni “Mwaka wa Mawasiliano ya Kitamaduni kati ya China na Afrika.” Vile vinavyohifadhiliwa kwenye majumba ya makumbusho vinazungumza kimyakimya: mazungumzo ya ustaarabu kati ya China na Afrika hayajawahi kukoma.
Katika jumba la makumbusho ya Ibn Batouta huko Tangier, Morocco, ramani kubwa inaonyesha safari za msafiri huyo wa karne ya 14 aliyetembea kwa miaka 30 hadi kufika na China. Aliandika kwamba meli za China ni kama kasri baharini, bandari ya Quanzhou ilitiwa nanga na meli elfu, biashara ya Guangzhou haikukoma mchana na usiku, na Hangzhou ilikuwa kama bustani ya peponi. Huu ni uangalizi wa makini wa ustaarabu wa Kiarabu kuelekea ustaarabu wa China.
Miaka 600 baadaye, meli za Zheng He zilifika pwani ya Afrika Mashariki. Tofauti na wakoloni wa Ulaya, Zheng He alileta kauri, hariri, na chai – sio bunduki na utumwa. Kama alivyosema Profesa Amany Farouk wa chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri, “Zheng He aliacha hisia ya kina kwa Afrika – biashara ya amani.”
Katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Kenya, vipande vingi vya kauri kutoka magofu ya Lamu, Malindi, na sehemu nyingine vinathibitisha mtandao wa biashara uliodumu kwa karne nyingi. Kauri hizo sio tu zilikuwa ishara ya hadhi kwa watu wa tabaka la juu waishio sehemu za pwani, bali pia ziliwekwa kwenye kuta, milango, na mapambo ya makaburi, zikichanganyika na usanifu wa Kiafrika. Katika jumba la Makumbusho la People Palace mji mkongwe, Zanzibar, ukuta mmoja unaoonyesha kauri kutoka enzi za Yuan hadi Ming za China, na hata watafiti wanawaza kuwa labda upendeleo wa rangi ya buluu-nyeupe pwani ya Afrika Mashariki unahusiana na kauri ya buluu-nyeupe ya China.
Mawasiliano hayakuwa ya upande mmoja. Aprili mwaka huu, Jumba la Makumbusho la Sanaa la China lilionyesha vinyago vya mbao kutoka Afrika, vikielezea hali halisi za familia, kazi, na sherehe barani Afrika. Wasomi wa China wamegundua kufanana kwa kushangaza kati ya vinyago vya usoni vya Afrika na vinyago vya usoni vya makabila madogo madogo ya China. Na katika majumba mengine ya makumbusho nchini China, baadhi yao yanaweka vinyago kutoka Afrika pamoja na michoro ya jadi na vinyago vya usoni vya China, na hivyo kubadilisha jinsi watazamaji wa China wanavyoielewa Afrika.
Leo tukiangalia nyuma, hizo kauri na vinyago ni zawadi ambazo ustaarabu wa binadamu ulitafutana kwa njia ya upepo wa Bahari ya Hindi. Wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika unapotimiza miaka 70, na mwaka huu umeitwa “Mwaka wa Mawasiliano ya Kitamaduni,” wale mashahidi wakimya katika majumba ya makumbusho wanatuambia: daraja kati ya ustaarabu halijawahi kuhitaji kujengwa kutoka mwanzo – limekuwepo kwa muda mrefu na linangoja tu tupate kuligundua upya.