SoC03 Mfumo tiba ukosefu wa ajira nchini

Stories of Change - 2023 Competition

The Future 85

Member
Jun 23, 2023
6
6
Ajira ni kazi au shughuli ambayo mtu anafanya kila siku na kujipatia kipato kwa ajili ya kujikimu na kufanya maendeleo binafsi na nchi kwa ujumla. Mazingira wezeshi ya upatikanaji wa elimu (elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari), elimu ya kati vyuo vya kati na elimu ya juu (serikali inatoa mikopo kwa wanachuo) imepelekea uzalishaji mkubwa wa wasomi na wahitimu wengi nchini, hivyo kupelekea uhitaji wa ajira kuwa mkubwa kupindukia (janga) na ikizingatiwa mfumo wetu wa elimu unawaanda wahitumu kwa ajili ya kuajiliwa zaidi kuliko kuajiriwa.

Mh. waziri mkuu mstaafu Edward Ngoyai Lowassa alisema "ukosefu wa ajira ni bomu ipo siku litaripuka". Sasa tunashuhudia kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa kubwa sana la vijana kuhitimu vyuo na kuishia mtaani kwa kukosa ajira. Serikali kwa nafasi yake inajitahidi kuajiri lakini kwa wingi wa wahitimu bado ajira hizo zimekuwa ni chache, wingi wa wahitimu kila mwaka katika ngazi tofauti tofauti za elimu imekuwa kubwa na inazidi kuongeza ongezeko la uhitaji wa ajira kulinganisha na nafasi za ajira zinazotolewa kwa mwaka, kwa ufupi unaweza kusema ni mbingu na ardhi yani haviendani kabisa (hakuna uwiano).

Mh. Rais Samia Suluhu Hassan, alisema uhitaji wa mikopo kwa vijana ni mkubwa kulinganisha na uwezo wa serikali kutoa mikopo, hii inamaanisha mahitaji ya vijana na wahitimu kwa ujumla ni makubwa kuliko uwezo wa serikali kuajiri lakini kutoa mitaji wezeshi ili hawa vijana kujiajiri, na tukizingatia vijana wengi wanatoka katika familia za hali ya chini kiuchumi hivyo ni ngumu kupewa mtaji maana hata wazazi wenyewe wamekuwa wakipata wakati mgumu kiuchumi kusomesha. Ni njia ya kibunifu pekee ambayo kwa kuratibiwa vyema inaweza punguza hadi 80% au zaidi ya tatizo la ukosefu wa ajira na mitaji kwa vijana na wahitimu.

Ajira ya masaa maalum/Ajira ya mapokezano (Part Time/Shift Employment). Ni mfumo ajiri ambao vijana na wahitimu wa vyuo wataajiriwa kwa ajira ya kudumu serikalini kwa utendaji wa masaa maalum (part time) au utendaji wa mapokezano (shift) kwa kiwango wastani cha mshahara. Mfumo huu unatoa nafasi kwa mwajiriwa kuajiriwa mahala pengine popote (sekta binafsi) kwa kuzingatia utaratibu wa ajira yake ya kudumu (yani ajira ya serikalini).

Lakini pia ni mfumo rafiki kwa kutatua changamoto ya vijana wengi kukosa ajira na mtaji kwani kupitia mshahara kijana ataweza tengeneza mtaji wake yeye mwenyewe na kuweza kuanzisha au kufanya shughuli zingine kiuchumi na kukuza kipato zaidi, lakini pia mfumo huu ni rafiki kwani unawezesha mwajiri kutumia muda wake wa ziada kuendesha na kusimamia shughuli zake kwa ukaribu, kwa maana inampatia mwajiriwa nafasi ya kushughulika na mambo mengine kiuchumi kwa ule muda ambao anakuwa nje ya ofisi.

Kiafya mwajiriwa anapata muda wa kutosha kupumzika hivyo kumfanya kuwa na ufanisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yake. Lakini pia unatoa fursa ya waajiriwa kupata muda wa kutosha kukaa na familia tukizingatia siku hizi wazazi wamekuwa wanakosa muda wa kutosha kukaa na familia zao sababu ni kubanwa na majukumu.

Mifano hai tunaona kiutendaji kupitia ajira za madaktari, wauguzi, ajira za ulinzi, lakini pia katika elimu tunaona katika ngazi ya elimu ya juu wahadhiri wanafanya part time employment kwa kufundisha vyuo 2 au zaidi na wakati mwingine bado ni waajiriwa wa serikali ,lakini pia somo1 kufundishwa na wahadhiri 2 hadi 3 kwa kugawana topics. Hivyo hata katika elimu ya chini (msingi na sekondari) serikali kupitia mfumo huu inauwezo wa kuajiri somo 1 walimu 3 ambao watagawana topics za kufundisha na siku za kufundisha kama ambavyo imekuwa ikifanyika hasa kwa shule binafsi.

Mfumo huu utaipunguzia serikali mzigo mzito wa kushindwa kutatua tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwani itaondokana na mfumo wa kuajiri mtu 1 kwa nafasi 1 kwa gharama kubwa, hivyo inaweza ajiri watumishi 3 kwa gharama ambayo kwa mfumo uliopo ana ajiriwa mtu 1 kwa nafasi 1 kwa maana mshahara wa kumlipa mtumishi 1 unaweza kugawanywa kwa watumishi 3 kwamba serikali italipa kiasi wastani (reasonable payment) kwa maana wahatakuwa wakifanya kazi siku nzima (full time employment). Mfano kama mwajiriwa 1 analipwa mshahara laki 9, serikali inaweza ajiri watumishi 3 kwa mfumo wa part time/shift employment na kuwalipa mshahara wa laki 3 kila mmoja.

Serikali ifanye uratibu mzuri wa mfumo huu bila kuathiri vigezo na masharti ya kuajiri, ubora na viwango vya elimu, uwezo kiutendaji wa watumishi, uendeshaji wa awali wa ofisi. Haina maana kwa kuwa lengo ni kupunguza janga la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu basi utaratibu wa kuajiri usizingatiwe. Vijana wengi wako mtaani wana uwezo mkubwa kiutendaji ila changamoto ni uchache wa nafasi zinazotangazwa na serikali (ajira za sandakalawe anaepata na apate). Ni kheri kugawana hicho kidogo kuliko kukosa kabisa.

Serikali inatumia gharama kubwa kuweka fedha katika sekta ya elimu ili kupunguza ukali wa gharama kwa wananchi wake kupata elimu, hivyo ione umuhimu wa kuwatumia wataalamu hawa inaowazalisha amabao ni nguvu kazi ya taifa. Vijana tupo tayari kutumika kitaaluma katika ujenzi wa Taifa letu kiuchumi.
 
Back
Top Bottom