Steve Dii
JF-Expert Member
- Jun 25, 2007
- 6,402
- 1,241
Yaliyo wakuta viongozi kadhaa wa CCM hivi karibuni naona sasa yameanza kuwakuta wapinzani (walau huyu mmoja!), kama jinsi habari ifuatayo inavyosema. Je, demokrasia hapa inafanyakazi ipasavyo au...?!
SteveD.
Source link: HabariLEO.Mbunge wa Chadema azomewa mkutanoni
Makubo Haruni, Tarime
HabariLeo; Thursday,October 18, 2007 @00:02
MBUNGE wa Jimbo la Tarime, Chacha Wangwe (Chadema), juzi alikumbana na wakati mgumu na kulazimika kukatisha mazungumzo yake na wananchi wa Kijiji cha Nyakunguru baada ya kumzomea wakimtaka ashuke jukwaani.
Wangwe alikumbana na dhahama hiyo katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Stanley Kolimba baada ya Mbunge huyo kumfukuza Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji na kufunga ofisi. Aliitisha mkutano huo mahsusi kuelezea taratibu za kufuatwa wakati wa kumfukuza kiongozi wa serikali ya kijiji anapokuwa anatuhumiwa kwa jambo lolote.
Katika ufafanuzi, Mshauri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoani Mara, Laxford Miyaye alisema njia zilizotumiwa na Mbunge huyo kumfukuza Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakunguru, Abel Maginga na kufunga ofisi yake kwa tuhuma mbalimbali, haukuwa sahihi.
Alisema kiongozi anapotuhumiwa ni lazima kwanza ajadiliwe na Kamati ya Serikali ya Kijiji na apewe nafasi ya kujitetea mbele ya Mkutano Mkuu wa kijiji ndipo uamuzi utatolewa. Miyaye alieleza kuwa mkutano wa Mbunge alioufanya Septemba 26, mwaka huu na kuamua kumfukuza mwenyekiti huyo uongozi na kufunga Ofisi ya Serikali ya Kijiji ni kinyume cha taratibu za uendeshaji.
Baadaye Wangwe alipata nafasi ya kutoa maoni yake na kueleza msimamo wake kwamba uamuzi alioufikia ni sahihi na ndipo wananchi walipomcharukia na kumtaka aache mazungumzo yake wakipiga kelele wakisema, wewe ni mchochezi, hatutaki mambo yako, toka hapo hatuna haja na uongo wako.
Licha ya Mbunge huyo kuwa mkali na kuwaambia wafunge midomo yao wamsikilize, walisisitiza hawamtaki na kamwe hawatamsikiliza. Hali hiyo ilimfanya Mbunge huyo wa Chadema atamke kwa hasira kuwa msinibabaishe, kwanza mimi hamkunichagua.
Baada ya kutoa kauli hiyo, aliketi chini kwa vile Mkuu wa Wilaya Kolimba aliingilia kati kuwatuliza wananchi hao walioonekana kuwa na jazba, huku Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Tarime, Constantine Bandola akisaidiana na Polisi wengine kutuliza ghasia, ingawa hakuna aliyejeruhiwa kwani vurugu zilizokuwapo zilikuwa za maneno ya kuzomea tu.
Mbunge Wangwe na wakili wa kujitegemea, Tundu Lisu, walilazimika kuondoka eneo hilo kwa gari kwenda katika uwanja wa ndege katika Kijiji cha Kewanja na kupanda ndege ya Kampuni ya Barrick Tanzania kurejea Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Trasias Kayenzi alikwenda kufungua ofisi ya mwenyekiti huyo wa kijiji na wananchi hao walimbeba juu mwenyekiti wao hadi ofisini hapo.
Hapo ndipo mkutano huo ulipofungwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime aliyewataka wananchi kufuata sheria katika uamuzi wa kuwaondoa viongozi madarakani. Tuhuma zilizokuwa zikimkabili mwenyekiti huyo ni pamoja na kutosoma mapato na matumizi ya kijiji, kuuza ardhi ya kijiji kwa Sh milioni 6.2 kwa Kampuni ya Barrick Tanzania.
SteveD.