RIWAYA:BALAA
MTUNZI: Ibrahim GAMA
SEHEMU YA KWANZA
Mahabusu na
Wafungwa
simamaaaaa, kofiaaaaaa towaa! Selo
salama kabisa Bwana
mkubwa , tupo tayari
kwa mafungio.
Tunafungiwa
mahabusu mia mbili , na
wafungwa watano,
jumla miambili na
tano,
Selo namba Mbili
mkuu Ilikuwa ni sauti ya
Nyapala wa
Kimahabusu, katika
Gereza la Mahabusu la
Segerea, akiwainua
mahabusu waliokuwa wamekaa kitako,
wakiwa katika mistari
ya watu kumikumi,
huku wakiwa vidari
wazi, yaani wamevua
shati na fulana zao, tayari kwa kufungiwa
ndani ya Selo, muda
huo
ikiwa ni saa kumi
alasiri
juu ya alama!!! Askari Magereza,
mwenye zamu yake ya
kufungia, akiwa na
askari wenzake
wengine
wapatao kumi, alikuwa
makini na kifimbo
chake, akiwahesabu
wale mahabusu,
waliokuwa wakiingia
ndani ya Selo, kwa mwendo wa mbio,
mmoja baada ya
mwengine, hadi mtu
wa
mwisho kuingia ndani
ya Selo ile, ambae ni Nyapala wa Kifungwa
aliposema kwa sauti,
akithibitisha ile
hesabu,
aliyoitoa Nyapala wa
Kimahabusu! Hapa salama kabisa bwana
mkubwa, tunafungiwa
wafungwa watano, na
mahabusu mia mbili,
jumla mia mbili na
tano, selo namba mbili
bwana
mkubwa! Baada ya
kuingia ndani,
ya Selo ile, ambayo
imepewa uwezo wa kulala watu wasiyozidi
hamsini, lakini
wanalazwa Mahabusu
hadi mia tatu,
kutegemea na wingi
wa wahalifu, hasa kipindi
cha sikukuu, na
mwisho
wa mwaka!
Askari magereza,
aliifunga kufuli nje ya mlango wa Selo ile,
kisha akaja askari
mwingine
kuhakikisha ,
kama kufuli ile
imefungwa sawasawa! Askari
wale walifungia
kwa utaratibu ule, hadi
walipomaliza kufungia
Selo namba tisa,
ambayo ndiyo ya mwisho
kufungiwa katika
upande ule wa
Rumande
wing, katika Gereza
lile. Ndani ya Selo ile
namba
mbili, maarufu kwa
jina
la Spear, ambayo
ndiyo imepangwa mahususi
kwa ajili ya kuchukua
Mahabusu wageni,
ambao kwamba huwa
ndiyo mara yao ya
kwanza, kuingia gerezani. Hivyo Selo ile
ndiyo pekee
iliyoteuliwa
na Afisa usalama, ili
wageni wa jela
kupewa maelekezo na taratibu
za kuishi ndani ya
Gereza! Alisimama
kijana
mmoja, aliekuwa na
cheo cha askari Selo, na kupiga makofi.
(ASKARI
SELO NI MSAIDIZI WA
NYAPALA NDANI YA
SELO ) Na mara kimya
kikatawala Selo nzima! Hiyo ndiyo taratibu ya
kutaka utulivu, watu
wanyamaze ili itolewe
taarifa ndani ya Selo.
Na baada ya utulivu
kupatikana, Yule Askari Selo akasema. Oyaa
sikia hiyoo. Kama
wewe
unajijuwa umeingia
leo
ndani ya Gereza, au uliwahi kuingia
ukatoka
na leo umerudi tena,
twende mbele kule
ukapate maelekezo.
Sasa wewe kaa usitoke
mbele, halafu
uyakanyage uone hapa
unapigwa Salala, kisha
kwa Meja nakupigisha
Rungu nyingi! Na humu
utaita taa hadi ishuke
chini ikufate (SALALA)
alikuwa anamaanisha
kofi la mgongo,
linalopigwa kwa mikono
miwili, kwa Mahabusu
aliekosa kufata
taratibu!.
(Kuita taa, ni
kusimama wima kisha unanyoosha
mikono yako juu
usawa
wa taa ilipo unafumba
na kufumbua vidole
vyako mithili unamwita
mtu kwa ishara ya
mkono!)
Mahabusu arubaini
waliinuka, na kuenda
mbele, ili kupata maelekezo kwa Yule
msaidizi wa Nyapala
au Askari Selo, kama
anavyopenda kuitwa
hivyo!
Walipokuwa wote wamekaa na Selo,
ikiwa
katika utulivu, yule
askari Selo, alianza
kwa
kuwajulia hali wale wageni! Habari zenu
wezi?! Na wale
wageni
ambao siyo wote
walioingizwa gerezani
kwa kosa la wizi, lakini waliitikia kwa pamoja
Poa Mwizi!
Kisha Yule Askari Selo,
akaendelea. Sema
nini,
humu ndani ya Selo tunataka heshima,
tuwaheshimu viongozi
wetu kwani wao
ndiyo
jicho la askari
Magereza. Askari wao wamelala
majumbani kwao, sisi
tumefungiwa humu
ndani kama kuku!
Yule
Askari Selo alikuwa akizungumza huku
akiwatazama, wale
Mahabusu wenzake
waliokuwa wamekaa
mbele yake ili
kutambua kama walikuwa
wanamuelewa
sawasawa! Baada ya
kuridhika kuwa
wanamsikiliza
akaendelea. Humu ndani ya Selo yetu
namba mbili, tuna
viongozi ambao
mnatakiwa
muwafahamu, ambao
wanastahili heshima! Ambao ni Nyapala wa
kimaabusu, na Nyapala
wa Kifungwa. Mkisha
pewa maelekezo
mtaoneshwa mahali
walipo ili muwatambue.
Yule askari Selo
alisimama kidogo,
kisha
akaendelea. Pia tuna
kiongozi mwengine mwenye cheo cha
Bwana Afya humu
ndani
ya Selo. Yeye ndiye
anaetugawia maji ya
kunywa humu. Kwani bila ya yeye kuwepo
na
kugawa maji katika
utaratibu, tungeweza
kugombea na asiye na
nguvu asingeweza kudiriki kunywa maji!
Pia yupo kiongozi
mwengine mwenye
cheo cha Kilina, yeye
anahakikisha vyoo
vinakuwa safi, na kwa kuwa maji ni tatizo
katika Gereza letu la
Segerea, ukisha
kwenda
haja kubwa, kuna
fimbo pale pembeni tunaiita
mchokocho.
Unatakiwa
baada ya kwenda haja
kubwa, utapiga
mchokocho, kwa maana
ya kuponda kinyesi
chako, hadi kilainike
kiwe uji, ili uweze
kutumia maji
machache kuondosha kinyesi. Sasa
wewe nenda kanye
kisha usipige
mchokocho uone
utakachofanywa!
Humu ndiyo mwana ukome
jeuri uache kwenu!
Yule askari Selo
alisimama kidogo
kuzungumza, kwani
alisikia minongono ikizidi na kufanya
kelele kutoka kwa
baadhi ya
mahabusu wenyeji,
waliokuwa hawana
habari kabisa kama wapo jela, walikuwa
wakiongea na kucheka
kama hawana kesi
zinazowakabili! Mara
makofi yalipigwa na
Nyapala wa Selo, na ghafla Selo yote ikawa
kimya kama
hakukuwa na watu
mle ndani ya
Selo! Kisha Yule
Nyapala akazungumza kwa
ukali.
Oyaa sema nini
mnazingua bwana,
wenzenu
wanaelekezwa kaeni kimya, nyie
mmeshakuwa
vijelajela,
mnakwenda na kurudi
humu nje hamna
maisha hamkai, siyo
mnatupigia
kelele bwana, sasa
nateuwa Kihelehele
akamate kesi, sasa
wewe kaidi, halafu ukamatwe na
Kihelehele
unapiga kelele uletwe
kwangu uone, wewe
ndiyo utakuwa funzo
kwa wenzako mimi nimeletwa na kesi
yangu humu, sikuja na
mtu!
Nyapala baada ya
kusema maneno yale,
akamteuwa mtu mmoja
wakuitwa Dubwi
Santana, ambae katika
jela na Selo ile,
aliaminika kuwa mnaa
sana! Akapewa kazi yakuwa Kihelehele
akamate kesi! Dubwi
Santana alisimama
akazungumza.
Santana hapa,
nishapewa rungu na Nyapala, kuanzia sasa
hakuna kuzungumza
hakuna kumokee!
(KUMOKEE NI KUVUTA
IWE BANGE AU SIGARA)
Hapa ni mwendo wa kimya hadi Nyapala
atengue cheo changu,
bwanabwana wewe
unaejifanya unanijua,
ukataka kuniletea
shobo, mbona nitakuzingua,
mie nuksi halafu
sijasingiziwa! Mie ni
mwizi na nje naiba
kweli yaani wazazi
wangu wenyewe hivi mie kuwa huku wao
wanaombea nisitoke
sasa wewe zingua
uone
mbona
nitakukomesha, kwanza mie sina
ndugu
humu nimekuja peke
yangu na kesi zangu!
Askari Selo endelea
kuwapa maelekezo hao
mafresh huku hakuna
Briman wala Blue
yeyote
atakaezingua hawa ni
wanyonge tu, wanaranda nje siyo
humu hawa
wachumba
tu!!!
Baada ya Dubwi
Santana kupiga mikwala mingi,
Selo ikarejea katika
utulivu mkubwa. Na
yule
askari Selo Baada
yakuona wale mahabusu
wageni walikuwa
wapo
makini kumsikiliza,
akawataka wale
mahabusu kila mmoja akifika kwa Nyapala
wa
Selo ataje kesi yake
kama alivyosomewa
mahakamani, pia ataje
mahakama ilipo kesi yake, na jina la
Muheshimiwa Hakimu
wake, aliemsomea
shitaka.
Oyaa hapa usiseme
nimesingiziwa, taja kesi
yako kama
ulivyosomewa
mahakamani, kesho
mtapoitwa kwa ajili ya
kuandikisha urithi, utaulizwa kesi yako na
askari magereza. Sasa
wewe ukisema
umesingiziwa kesi,
utachezea rungu hadi
magoti yajae maji hayo tumeelewana?
Yule askari Selo,
alizungumza huku
akimalizia kwa swali.
Na
wale mahabusu wageni
Fresh case wote kwa
pamoja wakaitikia
kwa
pamoja ndiyooo.
Yule askari Selo, alimfata
Nyapala wa
Kimahabusu, na
kumwambia.
Kiongozi wezi wapo
tayari kwa kukuona,
nimeshawapa
maelekezo, hivyo
nawaleta waje
wakutambue na
wewe uwatambue! Yule
Nyapala wa Selo
namba
mbili, alimuashiria
askari Selo wake,
awalete wale wageni ili
azungumze nao. Na
mara moja ikatendeka
hivyo wale Mahabusu
wageni, wakawa
wanatazamana uso kwa
uso na Nyapala wa
Selo.
Habari zenu? Nyapala
wa Selo aliwasalimia
wale wageni wa Jela, na
baada yakuitikiwa
akaendelea kusema.
Poleni sana ndugu
zangu, nawasihi mfate
taratibu za gereza, mtatoka salama bila
kupigwa hata kofi,
lakini
kama mtakaidi yale
mliyoelekezwa,
mtaumia kwa vipigo na
kupata ulemavu wa
Rungu za askari
Magereza. Mkiwa
humu
ndani gerezani, ondoweni kabisa
mawazo ya wake na
wachumba wenu
mliowaacha nje! Hao
mkiwafikiria sana
mtaumiza nafsi zenu bure. Kwani huku
unatakiwa ufikirie kesi
yako iliyokuleta humu
tu acheni kabisa
kuwaza
vitu ambavyo vitawaletea msongo
wa
mawazo. Jela
kajengewa binaadam
na
hata wale ambao sasa hivi wapo nje wakiwa
raia wema na huru,
nao
pia ni mahabusu na
wafungwa
watarajiwa! Kwani wanaweza siku
yoyote wakaletwa
gerezani bila
kukusudia!
Kwani siyo wote
tuliyopo humu kama ni waalifu kweli,
wengine
wameletwa kwa
bahati
mbaya tu! Alinyamaza
kusema yule Nyapala akitaka
kufahamu kama
anaeleweka. Baada
yakuona anasikilizwa
barabara, akawataka
wale Mahabusu wataje kesi zinazowakabili
kama walivyosomewa
mahakamani na
Hakimu.
Nataka mnitajie
majina yenu kamili, kesi
zinazowakabili na
mahakama
uliyosomewa kesi
hiyo.
Wale mahabusu wageni,
mmoja baada ya
mwengine, walikuwa
wakitekeleza agizo lile,
hadi kufikia kwa mtu
wa Arobaini alipojitambulisha.
Mimi naitwa
Athumani
Dobe, Mahakama
yangu ni mahakama ya
mkoa Kisutu, Kesi yangu ni
Mauaji, Nashitakiwa
kwa kumuua Mauwa
binti Simba Makupa,
hakimu wangu ni
..!!! Athumani Dobe
hakuweza kutaja jina
la
Hakimu wake, kwani
uchungu ulimjaa
moyoni, donge likamsugua na
machozi yakamtiririka
mashavuni mwake,
kilio
cha kwikwi
kikamshika hatimae akalia kwa
sauti iliyohuzunisha
kuisikiliza! Akazama
katika lindi la mawazo.
Ama kweli mtu mzima
ukimuona analia, basi ujue kuna jambo! Ni
kweli. *******
ZANZIBAR MWAKA
2006.
Upepo mkali ulikuwa
ukivuma kutoka kusini kuelekea kaskazini,
watu wa pwani huita
pepo za Kusi. Mji wa
Unguja ulikuwa safi na
upepo ule ulikuwa ni
burudani kwa watalii wengi waliokuwa
katika
Bandari ya Unguja
kuelekea katika mji wa
Dar es salaam. Wasafiri
wengi walikuwa katika
hekaheka za kusafiri,
katika muda ule wa
Alasiri. Boti ya Sea
Express,
ilikuwa inapakia mizigo
kabla ya kupakia abiria
waliokuwa
wamesheheni pale
Bandarini, wakiwa na
wahaka wa safari. Wale abiria wenye
tiketi wanaosafiri na
boti yetu ya Sea
Express,
kuelekea Dsalaam
mnaombwa kupanda chomboni, muda wa
safari umekaribia.
Sauti
ya kike ya mfanyakazi
wa Boti ya Sea Xpress,
ilisikika katika kipaza sauti na msururu wa
abiria ulielekea katika
boti ile kwa ukaguzi na
kupanda chomboni.
Saa kumi kamili boti ile
ilifunga milango yake, na safari ya kuelekea
katika Jiji la Dar es
salaam ikaanza.
Kaka yangu samahani,
naomba hilo jarida
nisome, kwani kuna hadithi naifatilia humo
yaani sitaki kuikosa.
Ilikuwa ni sauti ya
Abiria
mmoja mwanamke,
aliekuwa amekaa karibu
kabisa na Abiria
mwenzake
mwanaume, huku boti
ikiwa imeanza
safari, ikiitafuta Chumbe
kuelekea bandari
salama!
Ohoo haina shida
soma
tu mimi nitaangalia filamu katika video
pale,
kwani hii filamu ya
KABIKUSH KABIGHAM,
naipenda sana hilo
jarida mie nitasoma
nyumbani. Alijibu
Yule abiria wa kiume
huku
akimkabidhi lile jarida
la Ndoto.
Muhudumu wa Boti ile,
alikuwa akipita na
mifuko ya plastiki
akigawa ndani ya boti
ile, kwani bahari ilichafuka na wale
abiria
ambao siyo wenyeji
wa
bahari, wanaweza
kutapika sana! Hivyo ilikuwa rasmi mifuko
ile
kwa kutapikia.
Alipofika
katika usawa wa Yule
dada aliekuwa akisoma
lile jarida la Ndoto,
Yule
abiria wa kiume
alimchukulia Yule dada
mfuko, yaani alichukua mifuko miwili! Kwani
yule dada alikuwa
amekazana macho
yake
katika jarida lile,
hakuwa na habari ya mifuko.
Boti ile ilishika kasi,
kuitafuta bandari ya
jiji
la Dar es salaam
maarufu ikijulikana kwa jina la
Bandari salama.
Mwendo kasi wa boti,
wimbi kali na upepo
wa
Kusi uliokuwa ukivuma
kwa kasi kubwa,
uliitesa
sana Boti ile, kiasi
ilisukwasukwa na
wimbi kubwa, kiasi ikatibua matumbo ya
wasafiri, na wale
wageni wa bahari,
mara
wakaanza kuhisi
kichefuchefu, vilio kwa watoto vikasikika. Yule
dada aliekuwa
akisoma
jarida aliacha kusoma,
akawa amejiinamia
hasemi, mdomo wake ulijaa mate, tumbo
lilitibuka na akahisi
kutapika. Yule abiria
wa
kiume alimpa mfuko
mmoja wa plastiki ili atapikie mle, na kweli
alitapika hadi nyongo!
Ule mfuko ulijaa, na
Yule
abiria wa kiume
akampa ule mfuko mwengine,
nayeye akaenda
kuutupa
chooni ule mfuko
uliojaa matapishi ya
Yule dada! Baada ya kama saa
moja
na nusu, wakiwa
wamebakisha nusu saa
kufunga gati, katika
Bandari salama, Jiji la Dar es salaam lilikuwa
linaonekana kwa
karibu,
wakiwa maeneo ya
kunduchi. Yule dada
sasa akiwa ametulia na
bahari ikiwa imetulia,
akamuomba Yule kaka
simu yake ya mkononi.
Kaka yangu samahani,
naomba niazime simu yako nitume ujumbe
sehemu. Yule kaka
bila kinyongo,
alimkabidhi
simu ile huku nae
akimwambia. Piga kabisa tu, kwani simu
hiyo ina pesa za
kutosha
humo! Yule dada huku
akitabasamu
akamjibu. Asante sana ila
ujumbe
tu mimi unanitosha.
Baada yakusema
maneno yale aliandika
ujumbe wake, kisha akautuma
alipoukusudia, majibu
yakarudi kuwa ujumbe
ule umefika
ulipokusudiwa, kisha
akaufuta ujumbe ule katika simu ile, kule
kwenye sehemu ya
kutuma ujumbe, pia
akafuta na ule ujumbe
uluorudi kuonesha
kuwa ujumbe ule umefika,
na alipomrejeshea
simu
yake Yule kaka,
kukawa
hakuna ujumbe uliobakia katika simu
ile!
Samahani dada
naomba
tufahamiane, Mimi
naitwa Athumani Dobe,
nakaa Mwananyamala
Komakoma,
mwenzangu unaitwa
nani? Yule dada huku
akitabasamu kwa aibu, nae akajitambulisha.
Mimi naitwa Mauwa
Bint Simba Makupa,
nakaa Mtaa wa Swahili
Kariakoo, upande ule
wa pili kama unaelekea
Muhimbili. Alijibu
Mauwa huku akiwa
hamtizami usomi
Athumani Dobe.
Ahaa asante sana bi Mauwa, Unguja kwa
nani wako? Athumani
Dobe, alimuuliza swali
lingine na Mauwa
akamjibu.
Kule ni Kwa Baba yangu
Mdogo anaeitwa
Haruna Makupa,
nimekwenda
kuna kitu kuchukua, na
nilienda juzi leo ndiyo narudi, mimi makazi
yangu ya kudumu ni
Dar
es salaam.
Alizungumza Mauwa
katika utulivu mkubwa. Je nikitaka
kukutafuta
nakupataje?
Athumani Dobe alianza
kurusha ndoana yake,
akakutana na Samaki mbishi! Mmmh mimi
kwetu geti kali, yaani
mimi ni ndani, ndani
na
mie sina muda hata
wa kwenda sokoni! Mungu
akipenda kama hivi
tulivyoonana, basi
naamini tutakutana
tena! Mauwa alimjibu
Athumani, huku akimkabidhi lile jarida
lake la Ndoto, pia
akitoa shukurani kwa
kusoma. ITAENDELEA
KESHO
USIKOSE!!!