Mbeya: Kikundi cha Ulinzi Shirikishi Kata ya Ifumbo chafanya kazi Kidigitali

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Wananchi wa Kata ya Ifumbo iliyopo Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kupitia Mkaguzi Kata hiyo pamoja na kikundi cha ulinzi shirikishi kilichopo ili kuzuia uhalifu.

Akizungumza Januari 29, 2024 katika hafla ya kupokea na kukabidhi vitendea kazi vya kisasa, redio za mawasiliano (radio calls) na T-shirt kwa kikundi cha ulinzi shirikishi Kata ya Ifumbo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amewataka wananchi wa kata hiyo kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuwafichua watu wanaofanya matukio hayo.

Aidha, mwekezaji ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya G&I inayojishughulisha na uchimbaji madini ndugu Selemani Kaniki amesema kuwa, Kata ya Ifumbo inakwenda kulindwa kidigitali kupitia mifumo ya kisasa ya mawasiliano.
89d8762f-667e-4408-a6ea-e40c5cb4e0bc.jpg

0455696a-fdc5-4226-b760-25e46952bcc1.jpg
"Niliona mbali sana, wananchi wa kata ya Ifumbo wamekuwa wa kwanza kuwa na kikundi cha ulinzi shirikishi kinachotumia redio za mawasiliano (radio calls) kufanya shughuli za ulinzi, nenda popote hutokuta kitu hiki" alisema Kaniki.

Aliongeza kuwa, matumizi ya redio za mawasiliano yanakwenda kuleta ufanisi katika ulinzi wa Kata ya Ifumbo pamoja na vijiji jirani kwani redio hizo zina uwezo wa kushika mawimbi zaidi ya umbali wa kilomita kumi hivyo zimekuja kutatua changamoto za kimawasiliano.
9ad3994a-9c7d-41f0-8575-6a2dace602e9.jpg

b8aeba56-5c47-4a80-afd2-90918e1f608f.jpg

83c95866-f1e8-4a86-b530-7c2eaaa5a3aa.jpg
Naye mkazi wa Kata ya Ifumbo ndugu Charles Mkomolo amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kupeleka Mkaguzi Kata pamoja na kuhimiza na kuhamasisha vikundi vya ulinzi shirikishi hali inayopelekea kuimarika kwa ulinzi na usalama wa wananchi wa Kata hiyo.

Mbali na kutoa vifaa vya ulinzi, ndugu Selemani Kaniki ameahidi kujenga kituo cha Polisi Kata ya Ifumbo ili kutatua changamoto ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita zaidi ya 45 hadi kituo cha Polisi Chunya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga kupitia hafla hiyo amekabidhi ramani ya kituo cha Polisi kwa uongozi wa Serikali Kata ya Ifumbo ili kuanza maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ikiwa ni pamoja na kutoa eneo la mradi wa ujenzi.
 
Back
Top Bottom