SoC03 Mbegu ya uzalendo kwa watoto: zao la uwajibikaji na utawala bora kwa taifa

Stories of Change - 2023 Competition
Jun 6, 2023
6
7
Nimezaliwa mwaka 2013 katika wilaya ya Muleba na kulelewa na bibi yangu kipenzi, Bi.Khadija. Bi.Khadija alipenda sana kusoma na muda mwingi aliutumia kusoma vitabu vilivyoelezea utawala bora na namna babu zetu walivyo pigania uhuru lakini pia alipenda kusoma magazeti.

Siku moja nikiwa nje nachemsha chai ilisikika sauti iliyojawa na uzuni ikiniita, hakua mwingine bali Bibi yangu kupenzi. Nilipomkaribia alinitazama kwa unyonge kisha akasema sina budi kuyasema haya mjukuu wangu maana samaki mkunje angali mbichi na uzalendo husaidia kazi ya utawala bora kisha akameza fundo la mate.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa bibi aliendelea kwa kusema mjukuu wangu nimekuita kukuasa juu ya uzalendo maana wewe ndio taifa la kesho.

Mjukuu wangu kutokana na kamusi uzalendo ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini na kujitoa kwa ajili ya nchi yake kwa msingi wa kikabila, utamaduni, siasa au historia. Na uzalendo ukizidi kwa kiasi cha kulitetea taifa huitwa uzalendo kipofu au uzalendo bubu. Mfano wa watu wazalendo Tanzania ni Hayati Mwl J.K.Nyerere, Hayati Edward Sokoine, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na nje ya mipaka ya Tanzania ni Hayati Nelson Mandela, Hayati Nkwame Nkuruma. Hakika waliupenda na kuuishi uzalendo kwa manufaa ya taifa. Ili uwe mzalendo kuna kanuni zake.

Upendo kwa nchi yako ni kitu kikubwa cha kuzingatia pindi unapotaka kuwa mzalendo. Sio kuwaachia tu viongozi kuipenda nchi na raia kukaa pembeni wakisubiri viongozi wakosee ili walalamike la hasha hii inajumuisha watu wote kuipenda nchi yao kulingana na sehemu waliopo. Katika kitabu cha Patriotic Leadership In Demcracy kilichoandikwa na Haig Patapan, 2014 amejaribu kuelezea kuwa upendo kwa nchi hurahisisha kazi ya utawala.

Uaminifu na kujitoa kwa wananchi na viongozi ni msingi mkubwa wa uzalendo. Watoto wakilifahamu hili tangu chini itasaidia kuwajenga katika misingi ilio bora ili kulinda mali na nyaraka za nchi. Kwasababu jukumu la utawala bora si la viongozi pekee bali na wananchi kwa ujumla. Steven B. Smith kwenye kitabu chake cha Reclaiming Patriotism In An Age Of Extremes amejaribu kuelezea katika sehemu ya kwanza namna uzalendo na uaminifu huchochea utawala bora.

Ushiriki wa kiraia katika nyanja mbalimbali kama kupiga kura, kuheshimu sheria za nchi, kulipa ushuru na hata kuhudumia jamii ni hoja nzito ya uzalendo inayotakiwa kuangaliwa na jicho la ukaribu na raia maana ushiriki wao katika kupiga kura, kufata sheria za nchi na kulipa ushuru huwasaidia sana viongizu katika swala zima la utawala kwasababu makosa yatapungua na viongozi watatumia muda mwingi katika masuala ya maendeleo na si kutatua migogoro.

Ukosoaji wa kujenga na uboreshaji. Hakuna binadamu alie umbwa mkalimifu wote hukosea na tunapokosea tunastahili kukosolewa lakini kwa namna ilio bora na huo ukosoaji uwe wa kujenga kwa taifa na sio wa kumlega mtu binafsi. Mfano dhahili ni jamiiforums unaweza wafatilia kupitia tovuti yao ya ww.jamiiforums.com lakini pia katuni za Masoud Kipanya kupitia akaunti yake ya Instagram wamekosoa lakini kwa nia ya kujenga na kuboresha.

Uzalendo ni pamoja na kutunza urithi wa baba zetu kama historia ya nchi, mila na mafanikio ndo maana serikali imejenga makumbushi na maeneo ya kumbukumbu ya taifa. Lakini hii haiishii hapo tu bali kulindaa maliasili ya taifa na kushiriki katika kuchangia sera zitakazo linda maslahi ya taifa.

Mjukuu wangu uzalendo ni neno pana sana haliishii hapo tu bali lina husisha pia ushiriki wa kimataifa katika kukuza uhusiano kwa manufaa ya taifa kwa ujumla, usawa katika utoaji wa elimu na maarifa, kutunza amani, umoja na mshikamano, uwajibikaji wa kijamii na hata utatuzi wa migogoro kwa amani.

Kipindi Bi.Khadija akiniambia hayo alitokea jirani yetu na kuanza kumuuliza kwanini ananielezea hayo ingali mimi bado mdogo na hapo ndipo bibi alipo endelea kwa kusema
Mbegu ya uzalendo ukiipanda kwa watoto, itawasaidia watoto kujengwa na hisia ya utambulisho kwa nchi. Ambayo huchagiza kuupenda na kuuishi utamaduni na historia ya nchi tangu utotoni. Hii itasaidia kuthamini utamaduni na historia ya nchi maana huwezijua uendapo kama hujui utakapo.

Watoto wakipandikizwa na mbegu ya uzalendo itasaidia kuthamini na kudumisha maadili ya kidemokrasia. Maadili ya kidemokrasia ni kama uhuru, haki, usawa na haki za binadamu ambapo watoto watatakiwa kufundishwa juu ya faida ya utawala bora na kuwa raia hai ambaye anajitoa katika mambo ya kijamii na ya kiserikali. Watoto wanatakiwa kufahamu kuwa dunia inatambua unachokifanya na itakuzawadia kulingana na matendo unayoyafanya. Kwa mfano heshima anayopewa Hayati J.K.Nyerere ni matokeo ya matendo aliyoyafanya nyuma na kuwahimiza sana watoto ili kuyafanya yalio ya haki kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Uwajibikaji na ushiriki wa kiraia ni kitu cha msingi kikipandwa kwa watoto ili kuwajenga tangu utotoni kujitolea katika huduma za kijamii na uhifadhi wa mazingira. Kwa mfano jamii imekua ikihimizwa juu ya upandaji wa miti na kuzuia ukataji. Jambo amblo hata watoto wanatakiwa kushiriki kwa vitendo kwa manufaa ya kizazi kijacho. "Panda mti, zuia kukata mti" (RC.Kindamba, 2022). Hii itasaidia kujenga hisia kali kwa watoto juu ya kuchangia vitu chanya kwa jamii.

Lakini pia, mbegu ya uzalendo itasaidia kujenga umoja wa kitaifa na ustahimilivu. Uzalendo huleta umoja wa kitaifa na ustahimilivu kwa pamoja ambapo ikipandwa vyema kwa watoto itasaidia kujenga upendo tangu chini na kwa kuwa huwezi kumdhuru mtu umpendaye basi itadumisha utawala bora na kujenga umoja katika kipindi kigumu. Mfano katika kipindi hiki kigumu cha kufanya maamuzi makini juu ya mkataba wa DP world kiwango cha umoja kama taifa na ustahimilivu unahitajika kwa hali ya juu ili kufanya maamuzi ambayo hayatokuwa na lawama badae.

Zaidi, watoto watajisikia fahari na motisha juu ya taifa lao na hii itasaidia kupunguza idadi ya watanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi kwa manufaa ya taifa lingine na kupetaza rasilimali watu nchini huku izo juhudi na ujuzi zikiitajika sana nchini kwa maendeleo na utawala bora ujumla.

Mwisho bibi alituambia waandisha wa habari na vyanzo vyote vya mawasiliano wanasehemu kubwa katika kuotesha mizizi ya uzalendo kwa watoto na taifa kwa ujumla itakayo pelekea utawala bora kupitia kwa taarifa wanazotoa. Hivyo serikali inabidi itathimini utengenezaji na utekelezaji wa sheria zinazo wahusu waandishi wa habari zisiwanyime uhuru katika kutoa taarifa na aina ya taarifa. Huku pia waandishi wa habari wakitambua madhara na ukubwa wa sehemu yao katika taifa na kusimamia misingi yao ya kazi kwa ufasaha itasaidia kupanda mbegu ya uzalendo kwa watoto na kuzaa zao la watu wajibikaji na utawala bora kwa taifa la badae.
 
Back
Top Bottom