NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA
Sehemu ya Ishirini.
“Yupo wapi?”
“Nawaona vijana wawili wakiwa wamesimama, mmoja yupo ndani ya kibanda cha simu na mwingine yupo nje, Benjamin ni huyu aliyekuwa ndani, aliyekuwa nje simfahamu,” alisema kijana huyo aliyejiita Genius.
Alichokisema Bwana Swan ni kuunganishwa kwa kompyuta ile katika televisheni kubwa iliyokuwa ndani ya chumba hicho huku akimtaka kila ofisa wa FBI aliyekuwa humo ndani aangalie kile kilichokuwa kikiendelea.
Sehemu iliyoandikwa Location ikiwa na maana ya eneo ilionyesha kwamba ilikuwa ni Macberth 25W, sehemu ambayo ilikusanya watu wenye maisha ya kati katika Jiji la Boston, huko ndipo ambapo huyo Benjamin alipokuwa.
Kumuona tu hawakuridhika, waliamini kwamba wangeweza kutorokwa kwani huyo Benjamin hakuwa mtu wa kawaida hata kidogo. Walichokitaka ni kumfahamu mtu ambaye alikuwa naye, alikuwa nani na alikuwa akiishi wapi.
Hiyo wala haikuwa kazi kubwa, alichokifanya Genius ni kuivuta sura ya Harry, akaruhusu sura kadhaa zianze kupita katika kompyuta yake huku ikiitafuta sura ya mwanaume huyo aliyekuwa pamoja na Benjamin.
Ilikuwa kazi kubwa, kila mtu aliyekuwa ndani ya jengo hilo alikuwa kimya, Bwana Swan alibaki akiwa amesimama, mkono wake mmoja ulikuwa mfuko na mwingine aliupeleka katika shavu lake, alikuwa akifuatilia kwa ukaribu sana.
Zaidi ya sura milioni mbili zilipita kwa kasi kubwa mno, ndani ya dakika ishirini, kompyuta ikasimama katika sura moja na kujiandika 100 MATCH kwamba sura ya mtu huyo ilifanana na huyu aliyekuwa ametafutwa.
“Ni nani huyo?” aliuliza Bwana Swan, jamaa mwingine akachukua kalamu na karatasi.
“Anaitwa Harry Hoff, kijana mwenye asili ya Ujerumani, anaishi jijini Boston, nyuma namba 278 katika Mtaa wa Vivien View Barabara ya St. Peters, anasoma katika Chuo cha Kikuu cha Harvard,” alisema Genius, maelezo ya wananchi wote wa Marekani, data zao zilikuwa zimechukuliwa kutokana na vitambulisho wa taifa walivyokuwa wamepewa.
“Safi sana...ninahitaji maofisa kumi waende huko anapoishi Harry. Hakuna kuua, mnachotakiwa ni kuwapata wote wakiwa hai,” alisema Bwana Swan na maofisa wote kuitikia na hivyo kuanza kwenda huko.
****
Vivian hakuwa na raha, moyo wake ulikuwa na majonzi tele, hakuamini kile kilichotokea kwamba mpenzi wake alikuwa akitafutwa kila kona huku sababu kubwa ikiwa ni kufanya mauaji.
Alijua kwamba hakuwa muuaji bali kulikuwa na mtu ambaye alifanya mauaji, hakumfahamu na hivyo ndivyo alivyowaeleza maofisa wa FBI lakini hakukuwa na mtu aliyemuelewa.
Aliruhusiwa kwenda nyumbani, hakukukarika, kila alipokaa, alimkumbuka mpenzi wake tu. Maofisa wa FBI hawakutaka kumuacha, walihakikisha wanamfuatilia kila hatua.
Nje ya nyumba hiyo kulikuwa na gari lao, ndani ya gari hilo kulikuwa na kompyuta nyingi pamoja na kamera zilizokuwa na uwezo wa kupiga picha na kuona kile kilichokuwa kikiendelea ndani.
Mbali na hivyo, waliendelea kufuatilia mpaka mawasiliano ya simu zake, kuanzia ile ya mezani mpaka ya mkononi kwani waliamini kwamba msichana huyo alikuwa na nafasi ya kuwasiliana na mpenzi wake ambaye alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba kipindi hicho.
“Nini kinaendelea?” aliuliza Bwana Swan ambaye aliwagawa vijana wake sehemu mbalimbali.
“Bado tunaendelea kufuatilia, tunamuwekea ulinzi wa kutosha huyu msichana wake,” alijibu ofisa mmoja.
“Simu zake?”
“Tumeziwekea ulinzi pia.”
“Sawa.”
****
Maofisa wa FBI wakaelekea nyumbani kwa Harry, walikwenda na gari lao, ilikuwa asubuhi sana muda ambao waliamini kwamba hata watu hao hawakuwa wameamka, walitaka kuwavamia na kisha kumchukua mtu wao ambaye aliwatesa sana huku usiku uliopita tu akiwa amefanya mauaji katika hoteli moja huko Los Angeles.
Walifika katika nyumba hiyo huku wakiwa na bunduki zao mikononi mwao, waliamini kwamba wangeweza kumpata kwani kwa jinsi walivyoona siku iliyopita, wawili hao wangeendelea kuwa ndani ya hiyo nyumba na ilionyesha kwamba kwa kipindi kirefu Benjamin alikuwa mahali hapo ila tu hawakuwa wakijua hilo.
Walipofika nje ya nyumba hiyo, kitu cha kwanza kabisa walichokifanya ni kuizunguka nyumba hiyo na ndipo mmoja wao akaanza kuugonga mlango na kutaka kufunguliwa.
Nyumba ilikuwa kimya, japokuwa alipiga kelele na kusema “FBI, FBI” lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyefungua mlango. Hawakutaka kuendelea kubaki hapo ndani, walikuwa na hofu kwamba inawezekana Benjamin angekimbia hivyo walichokifanya ni kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa kuuvunja mlango.
Bunduki zilikuwa mikononi mwao, walioingia hawakuwa wao peke yao bali kulikuwa na askari wa SWAT ambao kazi yao ilikuwa ni kuvamia sehemu zilizokuwa na hatari, yaani kule ambapo kulikuwa na watu waliokuwa na silaha nzito, walitumika hao kwa ajili ya kuwalegeza kwanza.
Ndani, hakukuwa na mtu, walijaribu kuingia humu na kule, walitembea huku na kule lakini hawakukuta mtu yeyote. Mwisho kabisa wakaamua kukifuata chumba kimoja, kilikuwa chumba cha Harry, walipokifikia, wakaingia ndani, hawakumuona Benjamin, mtu pekee waliyemuona humo alikuwa Harry.
“You are under arrest....” (Upo chini ya ulinzi...) alisema ofisa mmoja huku wote kwa pamoja wakimnyooshea bunduki Harry ambaye aliamka na kuanza kuwaangalia.
“What the hell is going on?” (Nini kinaendelea?) aliuliza huku akiwaangalia.
Hawakutaka kumjibu swali lake, walichokifanya ni kumshika na kumlaza chini kisha kumfunga pingu huku wakimtaka kuwaambia mahali alipokuwa Benjamin.
“Benjamin, I don’t know where he is,” (Benjamin, sijui yupo wapi) alisema Harry huku uso wake ukionyesha tabasamu pana.
“Tell us where he is,” (Tuambie yupo wapi)
“I dont know men, he left last night,” (Sijui jamani, aliondoka usiku uliopita) alijibu Benjamin, kwa kumwangalia tu, alionyesha dhahiri kwamba aliwadanganya.
****
Benjamin alikuwa kama mtu mwenye machale, usiku wa siku hiyo hakulala, alibaki macho huku akiwa na wasiwasi mno, alijua kama kulikuwa na kitu ambacho kingetokea hivyo asingeweza kulala kabisa.
Alikesha, mpaka mwanga unaanza kuchomoza asubuhi, alikuwa macho, akatoka kitandani na kwenda jikoni ambapo akaandaa kahawa na kisha kuelekea sebuleni kuangalia televisheni.
Kipindi hicho televisheni ndiyo ilikuwa faraja yake, hakuwa na cha kufanya, hakuwa na uhuru wa kufanya kitu chochote kile, alipokuwa kwenye televisheni, ndiyo ulikuwa muda wa kujua kitu gani kilikuwa kikiendelea katika ulimwengu aliokuwa akiuogopa.
Mara kwa mara alijiona kwenye televisheni, alikuwa mtu maarufu kwa sababu ya matukio yaliyokuwa yametokea. Watu wengi walihojiwa, kilio chao kilikuwa ni kumuona Benjamin akikamatwa na kufikishwa mahakamani na kisha kushtakiwa kwa makosa ambayo dunia nzima ilijua kwamba aliyafanya.
“Ila kwa nini huyu mzee anafanya hivi?” alijiuliza pasipo kupata jibu.
Akasimama, akaanza kutembea ndani ya sebule ile huku akiwa na mawazo lukuki, aliongea peke yake kama kichaa, akatoka pale alipokuwa mpaka katika dirisha kubwa, akafungua pazia na kuanza kuangalia nje.
Alitamani kuwa huru, aliwaona watu wakitembea barabarani huku wakiwa wamejiachia, alitamani na yeye kuwa vile lakini ilishindikana kabisa, hakuweza kuwa huru kama watu wale walivyokuwa huru kipindi kile.
Wakati akiwa amesimama katika dirisha lile ndipo alipoliona gari moja likija na kusimama karibu na eneo la nyumba ile barabarani. Kwanza akaanza kuwa na wasiwasi, hakutaka kujipa uhakika kwamba watu waliokuwa ndani ya gari hilo walikuwa watu wazuri, akagundua kwamba kulikuwa na kitu.
Hakutaka kuwa na wasiwasi mwingi, akasubiri kuona ni watu gani wangeteremka kutoka ndani ya gari lile. Wakati akiwa amelikodolea macho, likatokea gari jingine ambalo kwa ubavuni liliandikwa S.W.A.T.
Harakaharaka wanajeshi waliokuwa na mavazi yaliyoandikwa S.W.A.T wakatoka ndani ya gari lile, walikuwa na bunduki kubwa hasa AK 47 ambazo ndizo zilikuwa maalumu kwa kazi yao.
Mavazi yao, yalikuwa yale mazito ambapo tumboni mpaka kifuani walikuwa na vazi jingine lililokuwa na uwezo wa kuzuia risasi. Benjamin alipowaona watu hao, hakutaka kusubiri, alijua fika kwamba walikuwa mahali hapo kwa ajili yake.
Hakutaka kujiuliza, wanajeshi wale na FBI tayari walianza kuelekea kule ilipokuwa nyumba ile, aliamini kwamba kama angekwenda jikoni na kutoka nje kupitia mlango wa nyuma, angechelewa na hivyo kukamatwa, wazo pekee lililomjia kichwani ilikuwa ni lazima aingie ndani ya ‘chimney’.
Sebuleni hapo kulikuwa na sehemu maalumu ambayo nyumba nyingi za Marekani na Ulaya au hata sehemu zenye baridi kali huweka kama jiko kwa ajili ya kuchoma kuni na kuleta moto ambapo moshi wake ulipita katika bomba kubwa lililokwenda juu ya bati na kupotelea huko.
Yeye alitaka kuingia katika bomba hilo, halikuwa kubwa sana lakini lilitosha kwa mwili wake kuenea kwani hakuwa mnene ila alikuwa mrefu. Hakutaka kuchelewa, haraka sana akaelekea katika sehemu ile, kulikuwa na kuni, akazisogeza pembeni na kisha kuanza kujiingiza, hakuanza kukiingiza kichwa, alibinuka na kuanza kuiingiza miguu yake kwenda kwenye bomba lile kwa juu.
Ilikuwa kazi kubwa lakini haikumsumbua sana, hakuchukua sekunde nyingi, akafanikiwa kuingia ndani ya bomba lile na kutulia, masikio yake yalikuwa ni hapo sebuleni, tangu maofisa wa FBI walipoanza kuugonga mlango na kuuvunja, yeye alikuwa ndani ya bomba lile sebuleni pale huku akisikiliza kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Maofisa wa FBI walijua fika kwamba Harry alikuwa akijua mahali alipokuwa Benjamin ila hakutaka tu kuwaambia ukweli. Walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka kituoni.
Huko wakamuingiza ndani ya chumba cha mahojiano na kuanza kuzungumza naye, walitaka aeleze ukweli mahali alipokuwa Benjamin, vinginevyo wangemfanya kitu kibaya.
“Nina haki ya kusikilizwa pia,” alisema Benjamin kwani tayari aliona maofisa wale walikuwa wamekasirika.
“Sawa. Benjamin yupo wapi?”
“Sijui! Kwani nyie wa nini?”
“Amefanya mauaji!”
“Hapana! Benjamin hakuwahi kuua,” alisema Harry.
“Usibishane na sisi, aliua na hata jana aliua pia,” alisema ofisa huyo.
“Jana kuna mauaji yalitokea huko Los Angeles, wote mnasema kwamba Benjamin ndiye aliyehusika, si ndiyo?” aliuliza Harry.
“Ndiyo!”
“Sawa! Kwenye maelezo yenu mlisema kwamba jana usiku mliniona nikiwa naye, ilikuwa saa tano usiku, si ndiyo?”
“Ndiyo!”
“Mauaji yalitokea saa nne na nusu, si ndiyo?”
“Ndiyo!”
“Sasa jamani! Huyo Benjamin awe ameua saa nne na nusu usiku, atatumia usafiri gani kutoka Los Angeles mpaka hapa Boston kwa mwendo wa nusu saa? Kwa ndege haiwezekani, alitumia usafiri gani sasa?” aliuliza Harry huku akiwaangalia maofisa wawili aliokuwa nao humo ndani.
“Labda niwaulize kitu kimoja. Nyie mnaamini Benjamin ni yupi? Yule aliyefanya mauaji huko Los Angeles au huyu aliyekuwa pamoja nami?” aliuliza Harry. Maofisa wakabaki wakiangaliana tu.
Alichokisema Harry kilikuwa ni ukweli mtupu. Kutoka Los Angeles mpaka hapo Boston ilikuwa ni mwendo wa saa moja na nusu kwa ndege, sasa ilikuwaje huyo Benjamin afanye mauaji Los Angeles halafu ndani ya nusu saa aonekane jijini Boston? Hilo likawapa wakati mgumu maofisa hao, hawakujua washike lipi, kama Benjamin alionekana hapo Boston majira ya saa tano usiku, je aliyefanya mauaji saa nne na nusu usiku huko Los Angeles alikuwa nani? Wakabaki na maswali kibao.
****
Dunia ilikuwa ikijiandaa kwa ajili ya kumuona msichana mrembo ambaye angeibuka kidedea katika Mashindano ya Miss Dunia ambayo kwa kipindi hicho yalitegemewa kufanyika jijini Texas nchini Marekani.
Watu walitaka kushuhudia ni msichana yupi angeibuka mshindi kwani wasichana wote ambao walitegemewa kushiriki walikuwa wale warembo, waliowavutia watu wengi nchini mwao.
Kila mtu anawa na uhakika kwamba msichana Angelica Sanchez kutoka nchini Mexico angechukua taji hilo lililokuwa likishikiria na mrembo kutoka nchini Venezuel, Maria alejandro.
Kwa kumwangalia, Angelica alikuwa msichana mrembo mno, alikwenda juu, hipsi zake zilionekana vilivyo, alikuwa na sura nzuri uliopendezeshwa na vishimo viwili vilivyokuwa mashavuni mwake. Muda wote, alikuwa kwenye tabasamu pana kana kwamba hakujua maana ya kukasirika.
Huyo ndiye alikuwa gumzo kipindi hicho. Tangu alipochukua taji la urembo nchini Mexico, kila mtu alitokea kumpenda, kampuni mbalimbali zinazojihusisha na mambo ya mitindo ikamtafuta, yeye alijiona mrembo, watu wengine wakamuona mrembo lakini makampuni hayo yaliona fedha.
Walijua kwamba kama wangemtumia msichana huyo katika matangazo yao mbalimbali, wangepata fedha nyingi, hivyo wakaingia naye mikataba mingi kwa kutegemea kuwa angeweza kuchukua taji hilo.
Mbali na Angelica, pia kulikuwa na msichana aliyeitwa Jenny Chu, msichana kutoka nchini China, alikuwa mrembo, alisoma na kuwa na PhD ya udaktari, hakuangalia elimu yake, alichokuwa akikiangalia kilikuwa ni masuala ya urembo tu, tangu zamani aliwaahidi wazazi wake kwamba kuna siku angekuwa mrembo wa dunia, na muda huo, aliona ndiyo kipindi chenyewe.
Kulikuwa na wasichana wengi, japokuwa wengi waliwafikiria wasichana hao warembo lakini wakasahau kwamba mbali na wasichana hao kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa mrembo mno, inawezekana kuliko wote hao, msichana huyo aliitwa Stacie Lawrence.
Kwa kumwangalia msichana huyo kutoka nchini Australia, alikuwa mrembo haswa, sura ya kitoto, lipsi pana kidogo, macho ya goroli, shingo ya upanga, aliumbika, alijua kutembea, yaani kwa kumwangalia harakaharaka, ingekufanya kudhani kwamba umekutana na mzimu wa mwanamke mrembo kuliko wote, Cleopatra.
Stacie hakuwa mzungumzaji, alikuwa kimya, alionekana kama kuwa na wasiwasi, hakuonekana kujiamini kabisa. Alikuwa msomi, alikuwa na PhD ya mambo ya uandishi, alitamani kusoma lakini pia alipenda sana mambo ya urembo na huo ukawa ndiyo muda wake wa kukamilisha kile alichokuwa akikiota kila siku.
Alimuogopa msichana Angelica kwa kuwa alitangazwa sana, hakuwa na uhakika kama angeweza kushinda kinyang’anyiro hicho, kila wakati alipokuwa akimuona Angelica, alitamani kumsogelea na kumsalimia kisha kumwambia kwamba alitamani sana kuwa kama yeye.
Hakujua watu walimfikiria vipi. Wasichana wengi waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho walimpa ushindi, alionekana kustahili hata zaidi ya Angelica ambaye mara kwa mara alikuwa akipigiwa promo kutoka sehemu mbalimbali.
Wasichana wengine wakashindwa kujizuia, walimsogelea na kumwambiia wazi kwamba alikuwa mrembo, kila msichana alitamani kuwa kama yeye lakini kila alipoambiwa, aliwajibu kitu kimoja kwamba inawezekana hawakumuona Angelica.
“Unajua wewe mzuri sana,” aliambiwa na msichana Priscilia, mrembo kutoka nchini Italia.
“Nani? Mimi?”
“Ndiyo! U mrembo sana...”
“Hapana! Labda hujamuona Angelica...”
“Nimemuona lakini wewe, hakika unastahili kuwa mshindi katika shindano hili,” alisema msichana Priscilia.
Kwa kumwangalia, alionekana kutokutania, alimaanisha kile alichokuwa akikizungumza. Hiyo haikuwa kwa msichana huyo tu, alipoondoka walimfuata wasichana wengine na kumwambia jinsi alivyokuwa mrembo.
Alipoambiwa, alijisikia aibu, hakujiamini hata kidogo. Kwa Angelica, tayari alianza kuona wivu, jinsi wasichana wengine walivyokuwa wakimzungumzia Stacie, moyo wake uliuma kupita kawaida.
Walikaa kambini huku wakiendelea na mazoezi kama kawaida, saa zilizidi kukatika, siku zikaenda mbele mpaka siku ya tukio kufika. Kila mtu alitaka kuona msichana Angelica akichukua taji hilo na kuwa mrembo wa kwanza kushinda kutoka nchini Mexico.
Wakati Angelica akiendelea kuwa gumzo ndipo watu wakafanikiwa kumona msichana Stacie. Kwanza kila mmoja akashtuka, hawakuamini kile walichokiona, hawakuamini kama kulikuwa na msichana mwingine mrembo hata zaidi ya Angelica ambaye alikuwa gumzo.
Mioyo ya watu ikaanza kubadilika, ikatoka kwa msichana Angelica na kuhamia kwa Stacie, watu wakaanza kumtafuta katika mitandao mbalimbali, picha zake, urembo wake ukawadatisha sana, hakukuwa na aliyeamini kama dunia hiihii ingekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Stacie.
Watu wakaanza kutumiana picha za msichana huyo katika mitandao ya kijamii, kila mtu aliyemuona Stacie katika picha zile, alitaka kumuona uso kwa uso kwani mioyo yao ilikataa kabisa kwamba katika dunia hiihii, kipindi hikihiki kungekuwa na msichana mrembo kama Stacie.
“Ni lazima nitakwenda kutazama kinyang’anyiro,” alisema jamaa mmoja, alikuwa ameshika simu yake akimwangalia Stacie.
“Si ulisema hauendi!”
“Nitakwenda, nimebadili mawazo,” alisema jamaa huyo.
Watu walitaka kuona ushindani mkubwa kutoka kwa wasichana wawili warembo, mmoja kutoka nchini Australia na mwingine kutoka nchini Mexico. Kila kona, wawili hao walawa gumzo, japokuwa kipindi cha nyuma Angelica alikuwa akizungumziwa sana lakini katika kipindi hicho upepo ukabadilika kabisa, hakuzungumziwa Angelica peke yake bali alizungumziwa Stacie, tena kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele, aliendelea kusikika zaidi.
“Unahisi nani atachukua ushindi?”
“Mmh! Wala sijui manake nishanchanganyikiwa!”
Watu walisubiri mpaka pale kinyang’anyiro kilipoanza. Mwana huo, watu walifuatilia kinyang’anyiro hicho kuliko vipindi vingine vyote, kila kona, watu walikuwa wakifuatilia katika televisheni zao na kitu kilichokuwa kikiwavuta zaidi ni urembo wa wasichana hao wawili.
Vipengele vyote vikapita na mwisho wa siku mshindi kutarajiwa kutangazwa. Katika tatu bora alibaki Stacie, Angelica na mrembo mwingine kutoka Afrika Kusini, ThandiMbokani.
Ukumbi mzima ulibaki kimya, mtu aliyetakiwa kutangaza matokeo, akasimama, akachukua matokeo kutoka kwa majaji na kisha kusimama, hakuanza na mtu wa kwanza, alianza na mtu wa tatu.
Lilipotajwa jina la Thandi, kila mtu alikaa kimya, walilitegemea hilo, walijua kwamba msichana huyo angeshika nafasi hiyo na mbili za juu zingekuwa kwa hao warembo waliowafanya watu wengi kujaa ndani ya ukumbi huo.
Mtangazaji, hakutaka kutangaza kwa pupa, alitaka kila mtu awe na presha mahali hapo, kwanza akarekebisha tai yake, akajikoholesha, akafanya mambo mengi yasiyokuwa na msingi ili kuwafanya watu kuwa na presha ndani ya ukumbi huo.
Kila mmoja alikuwa akimwangalia, mapigo yao ya moyo yalikuwa yakidunda sana, wote walikuwa na mshindi wao mioyoni mwao, walitaka kumsikia mtangazaji huyo alikuwa nani kwani kama ni urembo, wote walikuwa warembo japokuwa msichana Stacie alizidi kidogo.
Je, nini kitaendelea