Mauaji yaliyojaa utata

Smart911

JF-Expert Member
Jan 3, 2014
55,176
2,000
NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA

Sehemu ya Ishirini na Nane.

Maswali yake yalikuwa magumu lakini Benjamin alijitahidi kujibu kwa uelewa mkubwa, baada ya kuulizwa maswali hayo na kumaliza, hapo ndipo akakaa, watu wote wakata kuona Bwana Seppy naye akiulizwa maswali.
Hilo halikuwa tatizo, akasimama na kuelekea kizimbani. Mtu wa kwanza kabisa kumuuliza maswali alikuwa wakili wake, maswali aliyoulizwa yalikuwa mepesi na yale ya kumuweka katika wakati mzuri wa kushinda kesi, wakili huyo alipomaliza, akasimama na Donald kusimama.
“Unaitwa nani?” aliuliza Donald huku akimwangalia Bwana Seppy usoni mwake.
“Naitwa David Seppy...”
“Sawa. Una akili?” aliuliza Donald.
“Unasemaje?”
“Una akili?” alirudia swali lake.
“Ndiyo nina akili!”
“Unajua kwa nini upo hapa?”
“Ndiyo mheshimiwa! Nipo hapa kwa sababu nimesingiziwa kwamba nimeua,” alisema Bwana Seppy.
“Umesingiziwa au umeua kweli?”
“Nimesingiziwa kwa kuwa kama ningekuwa nimeua, basi hata alama za vidole vyangu zingeonekana,” alijitetea.
“Mshtakiwa ambaye ni Benjamin anasema kwamba wewe ndiye uliyehusika katika mauaji hayo na wewe ndiye uliyemuita na kumpa kazi hiyo ili akaue, ni kweli?” aliuliza Donald.
“Si kweli!”
“Unamjua Benjamin? Ushawahi kuonana naye kabla?” aliuliza Donald.
“Hapana! Sikuwahi kuonana naye kabla.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Tarehe kumi na mbili mwezi wa sita, simu yako ilitumika kutuma ujumbe mfupi kwenda namba +56 890 672 88 ambayo inamilikiwa na mtu anayejulikana kwa jina la Petterson Edward ambaye ulikuwa ukimuita kwa jina la Dracula, ujumbe huo uliuandika kwamba kulikuwa na mtu ambaye alitakiwa kuuawa mara moja, huyo si mwingine bali ni Carter, ni kweli?” aliuliza Donald.
“Si kweli!” alijibu Bwana Seppy baada ya kukaa kimya kwa muda.
“Mheshimiwa hakimu, naomba niwekewe televisheni na kompyuta kwa ajili ya kuletea ushahidi ulioshiba kabla ya shahidi wa mwisho kabisa ambaye ni David kuja na kuthibitisha yote yaliyotokea,” alisema Donald.
Bwana Seppy alipolisikia jina la David, akayapeleka macho yake kwa Dracula ambaye alikuwa ndani mahakama ile, alichanganyikiwa kwani taarifa ya mwisho ilisema kwamba mtu huyo alikuwa ameuawa, je, ni David yupi ambaye alikuwa akizungumziwa mahali hapo.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, harakaharaka televisheni ikaletwa mahali hapo, laptop ikaunganishwa na simu simu aina ya iPhone aliyokuwa nayo Donald na kisha kuanza kuonyesha ushahidi wa kila kitu kilichokuwa kimetokea.
“Kama nilivyosema, ushahidi umeonyesha kufanya mawasiliano hayo kama inavyoonekana, ujumbe huo ulitumwa kutoka namba hii, naomba kuuliza, je, hii namba ni yako au si yako?” aliuliza Donald huku akimuonyeshea namba Bwana Seppy katika televisheni.
“Ni yangu!”
“Kuna mtu aliwahi kuishika simu yako na kutuma ujumbe pasipo kujua?” aliuliza.
“Hapana!”
“Sawa. Mnamo tarehe kumi na tisa mwezi wa tisa, ujumbe wa mauaji ulitumwa kutoka katika simu yako kwenda katika namba ileile na ulisema kwamba ni lazima Todd Lewis auawe kwa sababu alikataa kuweka mkataba na wewe ambao ungemlipa kiasi kidogo cha fedha, hivyo kama kisasi ukaamua kumuua kwa kutuma watu, je, ni kweli?” aliuliza Donald, Bwana Seppy akabaki kimya, alianza kuweweseka huku akiangalia huku na kule.
“Uliidanganya dunia kwamba Benjamin ndiye aliyekuwa akifanya mauaji. Hiyo haikutosha, pia ulitumia njia hizohizo kuwaua watu wengine na kumfanya Benjamin kuingia matatani. Na kwa faida ya mahakama ni kwamba ulikuwa ukiweka noti kila sehemu uliyoua ili iwe vigumu kugundulika ila noti hizo zilikuwa na maana kubwa.
“Ile noti ya Dola, alama yake ambayo inawakilisha S, ile Euro ambayo inawakilisha fedha ya Ulaya, ile Paundi iliyowakilishwa na P, na mwisho ile Yuen iliyowakilishwa na Y, inaunganisha jina lako la SEPPY, je, bado unataka kubisha hapo?” aliuliza Donald huku akimwangalia mzee huyo usoni. Bwana Seppy akabaki kimya.
“Wiki kadhaa zilizopita, kulikuwa na mauaji ya msichana Stacie, mauaji hayo yalifanyika jijini Los Angeles mnamo majira ya saa nne usiku huku alama za vidole zikionyesha kwamba ni Benjamin ndiye aliyehusika, saa tano usiku kupitia kamera za CCTV zilizokuwa Boston zilimuona Benjamin na hivyo polisi kwenda kumkamata.
“Swali langu ni hili! Kama ni Benjamin ndiye aliyekuwa amefanya mauaji ya Stacie, je, alitumia usafiri gani kutoka Los Angeles mpaka Boston na wakati kutoka sehemu hizo kwenda nyingine hutumia muda wa saa tatu kwa usafiri wa treni na saa mbili na nusu kwa usafiri wa ndege? Wewe ndiye uliyefanya mauaji hayo, na bahati mbaya sana ulishindwa kujipanga kwa kutumia saa yako,” alisema Donald huku akiifunga faili lake.
Bwana Seppy alibaki kimya, alikuwa akitetemeka mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo, alimwangalia Donald huku akionekana kuchanganyikiwa.
Minong’ono ilianza kusikika hapo mahakamani, kesi ilionekana kuwa nyepesi mno kwa upande wa Benjamin. Wakati Donald akilifunga faili lake, hapohapo akamuomba mheshimiwa jaji kumruhusu kumleta shahidi wa mwisho, huyo shahidi wa mwisho akaruhusiwa kuingia hapo mahakamani, kitu kilichomshtua Bwana Seppy, ni David na msichana Vivian wakaingia.
“Aliuawa, nini kinaendelea?” alijiuliza Bwana Seppy, hapohapo akaona huo ndiyo mwisho wake.
“Mheshimiwa jaji, naomba tumpe nafasi shahidi, hii ni kesi nzito ambayo inahitaji ushahidi wa kutosha kwani kama shahidi hatotoa ushahidi wake hapa mahakamani sasa hivi, anaweza kuuawa kwani hata alipotajwa kwamba yeye ni shahidi, alitekwa,” alisema Donald na kumuomba hakimu, hapohapo David akapanda kizimbani na kuanza kutoa ushahidi wake.
“Mheshimiwa jaji, mara baada ya rafiki yangu Benjamin kupata tatizo, aliniomba nimsaidie ili kujua kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia, ilikuwa kazi kubwa na nzito lakini kwa kutumia kompyuta yangu, niliweza kufanikiwa kunasa ushahidi wote ambao niliukabidhi kwa Donald.
“Kwa kifupi ni kwamba Bwana Seppy amehusika katika mauaji. Baada ya kujua kwamba mimi ndiye shahidi kwa kuwa data zote ninazo, akawatuma watu waje kuniteka, wakaniteka na kunipeleka katika jumba moja lipo sehemu fulani.
“Huko nikakutana na huyu msichana, Vivian ambaye ni mpenzi wa Benjamin, alinihadithia kilichotokea baada ya kutoroka. Tulipotoroka, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumtafuta Donald ambaye akatupeleka katika jengo la FBI ambapo tulipewa hifadhi kwani bila kufanya hivyo, tungeuawa.
“Ila mbali na kufanya mauaji ya watu hao, nadhani pia anatakiwa kushtakiwa kwa kufanya mauaji ya maofisa wa FBI kwani wakati amewatuma vijana wake kumteka Benjamin, waliua maofisa wa FBI na kumteka Vivian,” alisema David.
David alizungumza mambo mengi yaliyokuwa yametokea, kila alipokuwa akizungumza, watu walikuwa kimya wakimwangalia tu, jaji McRegan alikuwa akiandika kila kitu kilichokuwa kikihitajika kuandikwa. Mpaka David ananyamaza, alikuwa ameridhika na ushahidi.
Jaji akabaki kimya, watu wote walikuwa wakimsikilizia yeye ni kitu gani angezungumza baada ya kupewa ushahidi uliojitosheleza. Hakutaka kutoa hukumu moja kwa moja, alichokifanya ni kuliita jopo la wazee wa baraza, wakaomba muda wa dakika ishirini kwa ajili ya kuijadili kesi hiyo.
Minong’ono haikuisha hapo mahakamani, kila mtu alikuwa akiongea lake huku wakimtaka jaji amuhukumu Bwana Seppy kifungo cha maisha gerezani au hata kumnyonga kutokana na kile alichokifanya.
Jopo hilo la wazee wa baraza na jaji lilichukua dakika kumi na tisa, likarudi mahakamani. Kabla ya kuzungumza kitu chochote kile, jaji akaanza kuwaangalia watu waliokusanyika ndani ya mahakama hiyo kisha kuyapeleka macho yake kwa Bwana Seppy.
Mwanaume aliyekuwa bilionea, aliyewatetemesha watu wengi kwa ajili ya ubilionea wake, leo hii alikuwa kizimbani huku akituhumiwa kuua watu kwa tamaa zake za fedha.
Mbali na yeye, pia kulikuwa na familia yake, muda wote mke wake alikuwa akilia, hakuwa akiamini kile kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo. Watoto wake waliokuwa na miaka kumi na tisa nao walikuwa pamoja nao, kitendo cha baba yao kufikishwa mahakamani tu kisa aliua kiwahuzunisha wote na hawakutegemea kama kitu kama kile kingetokea.
“Mahakama imejiridhisha kwa kila kitu kilichotokea, ushahidi umekamilika na kila kitu kilichozungumzwa. Hivyo kwa kupitia kifungu namba 113B kilichowekwa mwaka 1893, mahakama haikumkuta Benjamin na hatia hivyo inamuachia huru ila kwa mauaji aliyoyafanya David Seppy, amekutwa na hatia hivyo atahukumiwa kifo kwa kuchomwa sindano ya cyanide mpaka kifo.
“Hii itakuwa fundisho na pia kwa kupitia maofisa wa FBI, imebainika kwamba mmoja wa watu wake ambao walikuwa wakifanya mauaji ajulikanaye kwa jina la Petterson Edward ‘Dracula’ yupo hapa mahakamani akifuatilia kila kitu, hivyo naye atachukuliwa na kujumuishwa katika adhabu hii,” alisema jaji, hakutaka kuendelea sana, akapiga nyundo yake, akasimama na kutoka katika kiti kile.
Mahakama nzima ilikuwa shangwe, watu hawakuamini kama kweli kile walichokisikia ndicho kilichokuwa uamuzi wa mahakama ile. Benjamin hakutaka kusubiri, hapohapo akachomoka na kuwafuata wazazi wake na kuwakumbatia, kwake, ilikuwa furaha tele.
Kwa Bwana Seppy ilikuwa ni kilio kikubwa, hakuamini kile ambacho mahakama ilikiamua, akabaki akilia pale alipokuwa. Hata kabla watu hawajawanyika, tayari maofisa wa FBI walimfikia Dracula na hapohapo kumpiga pingu na kuondoka naye.
Siku iliyofuata, magazeti yote nchini Marekani yalitawaliwa na habari hiyo, kifo cha Bwana Seppy ambaye katika kipindi hicho ndiyo alitakiwa kuanza maandalizi ya kuiaga familia yake kabla ya kutekelezwa adhabu kali ya kifo ambayo ilikuwa mbele yake.
Alilia na kuhuzunika sana lakini hakuweza kubadilisha kitu chochote kile, hukumu ilikuwa palepale kwamba ni lazima afe kama hukumu ilivyosomwa mahakamani.
Benjamin akabadilika na kuwa shujaa, yule mtu aliyekuwa akitafutwa usiku na mchana, akawa mtu aliyekuwa akipendwa na kuzungumziwa kila kona, kila mtu alitamani kuwa karibu naye japo kupiga picha naye kwani hakukuwa na mtu aliyeonekana kuwa shujaa kama alivyokuwa yeye.
Alichokifanya ni kuendelea na masomo yake chuoni na baada ya miaka miwili, akakamilisha miaka yake mitano ya kusomea masuala ya kitabibu na hivyo kuwa daktari katika Hospitali ya St. Monica iliyokuwa Ohio nchini Marekani.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mafanikio yake, hakumuacha mpenzi wake, Vivian, baada ya miaka miwili kukatika, akamuoa kwa harusi kubwa na iliyohudhuriwa na watu wengi maarufu.
Kilichoendelea baada ya hapo, kilikuwa ni historia tu.

MWISHO
Safi sana...

Justice served...


Chapter Closed...


Cc: mahondaw
 

Kanungila Karim

Verified Member
Apr 29, 2016
17,615
2,000
WALE WOOOOOOOOOOOOOOOTE MNAOIFUATILIA HII HADITHI ANDAENI SHILINGI 10,000 YA KUNUNUA KITABU MAANA HII HADITHI HAITOMALIZIKA
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Similar Discussions

Top Bottom