Mattaka wa ATCL arejeshwa Bima kuwa mjumbe wa bodi
Exuper Kachenje na Leon Bahati - Mwananchi
MKURUGENZI wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka, ameula tena, baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Bima ya Taifa (NIC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Fedha na Uchumi, kupitia msemaji wake, Ingiahedi Mduma, Mattaka ni mmoja wa wajumbe watano wa bodi hiyo ambayo uteuzi wake ulifanywa na Waziri wa wizara hiyo Mustafa Mkulo.
Mattaka ni mmoja wa wajumbe wa timu iliyoteuliwa kulichunguza shirika hilo la bima, kabla ya kufanyiwa mabadiliko ambayo uteuzi wake katika timu hiyo ulizua maswali kutokana na kuliongoza ATCL iliyokuwa na matatizo lukuki yakiwemo ya kufungiwa kufanya safari zake,
Aidha, Rais Jakaya Kikwete alimteua Balozi Charles Mutalemwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Shirika hilo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Aprili 21, 2009.
"Rais wa Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Balozi Charles Mutalemwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe 21 aprili, 2009," ilisema sehemu ya tarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Waziri wa Fedha na Uchumi alimteua Justine Mwandu kuwa kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NIC kuanzia Aprili Mosi, 2009.
Kabla ya uteuzi huo Mwandu alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya kiufundi wa Idara ya kusimamia shughuli za bima (ISD).
Wajumbe wengine wa bodi ya NIC mbali ya Mattaka ni Michael Mhando, Agnes Bukuku, Kate Bandawe na Charles Kilasile.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, bodi hiyo itafanya shughuli za usimamizi wa NIC pamoja na urekebishaji wa shirika hilo.