Kifo cha Mwenyekiti wa Demokratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila jana alfajiri kwa ajali ya gari kimetajwa kuwa ni mwendelezo wa vifo vya aina hiyo vilivyowakumba wanasiasa wa Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni.
"Aliondoka hapa Ijumaa kwenda Njombe kumnadi mgombea wetu wa ubunge , Nicodemus Atoswege na walipata ajali katika kijiji cha Msolwa, Chalinze. Ndani ya gari hilo pia alikuwa Mchungaji Mgaya, Ni huyu ndiye aliyetoa taarifa za awali za ajali na kifo hiki" Alisema Katibu Mwenezi wa DP Mwambichoka Ferous.
Wanasiasa na vifo vya ajali:
Julai 27, 2008, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Chacha Wangwe, alifariki dunia kwa ajali ya gari liliyozua utata mkubwa katika maeneo ya Panda mbili mkoani Dodoma. Kabla ya kifo kile , Wangwe aliyekuwa akielekea Dar es salaam kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa mkongwe, Bhoke Mnanka alikuwa kwenye malumbano na uongozi wa CHADEMA, wakati huohuo alikuwa amepania nafasi ya juu ya uongozi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani. Katika ajali hiyo , alifariki yeye huku mtu mwingine aliyekuwa naye, Deus Malya akinusurika , hivyo kuzua maswali mengi.
Oktoba 24, 2007 , kada na Mbunge wa CCM, Salome Mbatia , alifariki kwa ajali ya gari akiwa njiani kwenda Songea kusaka kura za ujumbe wa NEC ya CCM. Utata katika ajali hiyo ya Salome uliibuka kwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA wa wakati huo, Zitto Kabwe, naye alikuwa njiani kwenda Songea kwa shughuli za kikazi. Wakati huo Zitto aliyekuwa kwenye mgogoro wa ndani na CHADEMA, alisimama kwa muda Njombe na kuliona gari lake, likipita hapo na muda mfupi baadaye alikuta limepata ajali.
Mbunge mwingine wa CHADEMA aliyefariki kwa ajali za namna hiyo ni Regia Mtema huku mwezi uliopita , mgombea ubunge wa CHADEMA huko Lushoto, Mohamed Mtoi , naye alifariki dunia kw ajali ya gari. Marehemu Mtoi anatajwa kuwa, alikuwa na misimamo ndani ya CHADEMA kama waliyokuwa nayo Zitto Kabwe na Chacha Wangwe.
Chanzo: Raia Tanzania
Tafakuri: Tutakumbuka kuwa siku za hivi Karibuni, marehemu Mtikila alijitokeza waziwazi kwenye vyombo vya habari na kusema, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA), Edward Ngoyai Lowassa ni fisadi na hafai kuwa rais wa nchi hii. Marehemu Mtikila alienda mbali na kusema nchi za wengine kama CHINA, LOWASSA angeshanyongwa kwa sababu ya kujihusisha na ufisadi.
