Manji yu mahututi arejeshwa hospitali
na Dina Ismail
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MFADHILI wa klabu ya Yanga na mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuph Manji, amerejeshwa hospitali na hali yake ni mbaya.
Manji, Jumatatu wiki hii, alianguka ghafla nyumbani kwake, Upanga, akisumbuliwa na malaria iliyopanda kichwani, alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa uchunguzi na juzi asubuhi aliruhusiwa, baada ya kupata nafuu.
Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu zilizokuwa zimepatikana, Manji anasumbuliwa na malaria iliyokuwa imepanda kichwani, ikiambatana na msongo wa mawazo na kufanya kazi muda mrefu pasipo kupumzika.
Hata hivyo, juzi majira ya saa 4 usiku, akiwa nyumbani kwake Upanga, jijini Dar es Salaam, mfadhili huyo wa Yanga, hali yake ilibadilika ghafla, hivyo kurejeshwa hospitalini Aga Khan.
Baada ya Tanzania Daima kupata taarifa za kurejeshwa kwa Manji hospitalini, ilifika hospitalini hapo na wauguzi kuthibitisha suala hilo.
Habari kutoka kwa mmoja wa wauguzi, ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema Manji alifikishwa hospitalini hapo huku hali yake ikiwa mbaya.
Alisema, kutokana na hali kubadilika mara kwa mara, baada ya kurejeshwa, alipumzishwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu (ICU), ambako alipumzishwa huko hadi jana mchana alipotolewa ICU.
Hata hivyo, Manji bado yu hospitalini akiendelea kupatiwa matibabu katika wodi namba 3 chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.
Kutokana na hali yake, tangu aliporejeshwa hospitalini hapo juzi usiku, amekuwa akila kwa kutumia mpira huku kukiwa na ulinzi mkali kutokana na daktari wake kuzuia watu kumuona, isipokuwa familia yake na wasaidizi wake wa karibu.
"Kutokana na tatizo linalomkabili, ni kama mtu aliyechanganyikiwa, hivyo yuko katika uangalizi wa hali ya juu, ndiyo maana amehifadhiwa katika chumba maalumu," alisema mmoja wa wauguzi.
Habari za kuugua ghafla kwa Manji, zimewatia simanzi kubwa wadau wa Yanga ambao jana walikuwa katika hali ya taharuki.
Akithibitisha kurejeshwa hospitalini kwa Manji, Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega, alisema, ni baada ya hali ya mfadhili huyo kubadilika.
Aidha, Madega amezidi kuwasihi wanachama wa Yanga, kutokuwa na hofu zaidi, ingawa wako katika wakati mgumu kutokana na kuuguliwa na mfadhili huyo.
"Ninapenda kuwatoa hofu Wanayanga wenzangu kwamba taarifa hizi zisiwashitue, kwani kuna watu wanazisambaza isivyo, kwa mitazamo wanayoijua wao, Manji anaendelea kupatiwa matibabu, tumuombee kwa Mwenyezi Mungu apate nafuu haraka," alisema Madega.
Mbali ya kuwa mfadhili wa Yanga na kada wa CCM, Manji ni Mkurugenzi wa kampuni za Quality Group, aliyewahi kuwania ubunge katika Jimbo la Kigamboni na kushinda kwenye kura za maoni, ingawa alienguliwa na vikao vya juu vya CCM.
Tangu aingine mkataba wa kuifadhili Yanga, Manji amekuwa msaada mkubwa kwa klabu hiyo kutokana na kujitolea mamilioni ya fedha hata zaidi ya mkataba. Habari ambazo zilitufikia wakati tunakwenda mitamboni, zilisema kuwa, mfadhili huyo wa Yanga, alisafirishwa kwenda mjini Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.