KUMBE BRUNO NI CHAGUO LA RONALDO
OLE Gunnar Solskjaer amekiri kuwa amezingatia ushauri wa Cristiano Ronaldo kwenye usajili wa kiungo fundi wa mpira, Bruno Fernandes.
Kocha huyo wa Manchester United, Solskjaer amenasa huduma ya Fernandes kwenye dirisha la Januari na tangu alipotua kwenye kikosi hicho cha Old Trafford amekuwa moto na kubadili kila kitu.
Staa huyo amekuwa mchezaji muhimu kwa Man United ndani na nje ya uwanja, wakati huu wakifukuzia nafasi kwenye Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, wakibakiza mechi tatu tu kwenye Ligi Kuu England kufahamu hatima yao.
Wakati mabosi wa benchi la ufundi la Man United wakimjadili kiungo huyo, Solskjaer alisema kumtazama Fernandes pekee yake haikutosha kufahamu ubora wa mchezaji huyo, hivyo alimtumia Ronaldo kwa ushauri kabla ya kumsajili dirisha la Januari.
“Tulikuwa na maskauti wetu makuu waliomfuatilia, tulimfanyia uchambuzi yakinifu na kujiridhisha kwa kila kitu. Lakini, kumwona pekee yake haikutosha kufahamu ubora wa kipaji chake,” alisema Solskjaer.
“Hapo tukawa tunahitaji kuuliza wachezaji wenzake, pengine wale waliopata nafasi ya kucheza naye kwenye timu ya taifa, hapo ikawa rahisi kwangu kuzungumza na Cristiano. Niliwasiliana na Patrice Evra, nikawasiliana na Cristiano na kutoa mapendekezo yao ya kumsajili Fernandes katika namna nzuri.”
Ubora wa Fernandes tangu atue Man United umekuwa moto, akihusika kwenye mabao kibao kwa maana ya kufunga na kuasisti. Lakini, kocha Solskjaer amemsifu kutokana na namna alivyozoea kwa haraka mazingira na utamaduni wa Old Trafford.
“Jamaa ana kipaji, hakika. Unaona kabisa ubora wake na kwamba amekuwa akilifanya hilo kwa mwendelezo,” alisema kocha huyo wa Man United na kuongeza. “Anapiga krosi, anapiga asisti, anafunga na anapiga penalti. Anafanya kila kitu ndani ya muda mchache tu.”