Sio mbaya tukapata kidogo kuhusu Mr Donald Trump ...

Donald Trump, rais mteule wa Marekani ambaye anatarajiwa kuapishwa leo tarehe 20 Januari mwaka 2017, ni tajiri anayemiliki majumba mengi na ambaye amekuwa mtangazaji wa kipindi cha maisha ya uhalisia kwenye runinga.

Amekuwa mtu anayeangazia sana ushindi katika maisha yake na alikuwa tangu mwanzo amesema ni lazima afanikiwe katika kupata tuzo kuu duniani, kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.

Kwa wafuasi wake, ndiye anayeweza kuleta ufanisi kwa Marekani.
Kwao, huyu ni tajiri shupavu anayeweza kusuluhisha matatizo yote ya nchi ambayo wanahisi yameshusha hadhi ya Marekani duniani.
Wengi wao ni raia wa Marekani wafanyikazi hasa wenye asili ya Kizungu na walio na maisha ya kadri.

Sasa ndoto ya kisiasa ya BwTrump imetimia, kinyume na matarajiyo ya wengi.
Ni ushindi ambao umetajwa kuwa wa kihistoria katika siasa za Marekani.
Trump ameamua kuvunja desturi ya siasa za Marekani kwenye kampeni.
Aliwatusi wanawake, raia wa Mexico, Waislamu na yeyote yule aliyemkera wakiwemo wapinzani wake 16 aliokabiliana nao katika mchujo wa Republican.

Mwanasiasa huyu alisafiri kwa ndege ya binafsi aina ya Boeing 757 kwenye mikutano yake ya kampeni. Alivutia umati wa watu na waandishi habari sawa na nyota wa mziki.
Yeye aliongoza katika kuangaziwa katika taarifa za runinga kuwaliko wapinzani wake wote kwa pamoja katika mchujo wa Republican.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, taarifa za Trump kwenye runinga zilileta dola bilioni mbili, bila yeye kugharamia.
Mwanzo wa kampeni za mchujo, swali kubwa lilikua ikiwa kura za maoni zilizomueka Trump kifua mbele zingemuwezesha kuzoa kura halisi?

Baada ya kushindwa mchujo wa kwanza na Ted Cruz katika jimbo la Iowa, Trump alijikwamua na aliendeleza ushindi ambao haungeweza kuzimwa ambapo aliwapiku wapinzani wake katika majimbo ya kwanza ya New Hampshire na South Carolina. Aidha Jumanne Kuu ya tarehe 1 mwezi wa Machi, alizoa ushindi katika majimbo saba kati ya 12 ambako mchujo ulifanyika.
Mwisho alishinda katika majimbo saba zaidi ikiwemo Indiana.
Swali sasa likawa kama atafanikiwa katika kura ya urais hapo mwezi Novemba, hasa baada ya kura za maoni kumuonesha mara nyingi akiwa nyuma ya Clinton.

Donald Trump alizaliwa Juni 14 mwaka wa 1946, mjini New York, akiwa mtoto wa tano kati ya watoto sita.
Babake Fred alikuwa tajiri aliyemilki majumba na babu zake Trump walikua wahamiaji kutoka Ujerumani.
Mamake Mary alikua mzaliwa wa Scotland.

Tangu utotoni, Trump alikuwa mtundu na wazazi wake walimpeleka shule ya msingi iliyofadhiliwa na jeshi mjini New York.
Baadaye alifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania, kitivo cha elimu ya biashara mwaka wa 1968.
Alifanya kazi katika kampuni ya babake ambaye aliendesha biashara ya kuuza nyumba kwa raia wa kipato cha kadiri, viungani mwa New York
Aliwekeza katika biashara kubwa ya ujenzi na kuweza kujenga mojawapo ya mijengo ya kifahari zaidi nchini Marekani. Alifanikiwa kutokana na sera ya kiuchumi iliyowekwa na utawala wa Reagan miaka wa 1980.
Kuna tofauti kuhusu utajiri hasa wa Trump. Aliwahi kuambia tume ya uchaguzi kwamba anao utajiri wa kima cha dola bilioni 10. Hata hivyo jarida la Forbes limenadi kwamba utajiri wa Trump haufikii juu ya bola bilioni 4.5.
Lakini unapotembea barabara kuu za Manhattan, kampuni ya Trump imeweka mabawa yake kwa majumba ya kifahari yaliyofuatana.
Yapo mahoteli, viwanja vya mchezo wa gofu, makazi ya kifahari, majumba ya kamari kutoka Carlifonia hadi Mumbai nembo yake ikiwa ni Trump.
Ameandika Riwaya kadhaa kuhusu biashara, huku umaarufu wake uking'aa zaidi katika makala yanayoelezea maisha halisi, "The Apprentice," katika runinga ya NBC. Hata hivyo alitupwa nje ya makala hayo baada ya kutoa kauli zilizowakera raia wa Mexico
Asanteni