SEHEMU YA KUMI
MWANAJESHI ni mwanajeshi tu bila kujalisha kuwa yu mzee ama kijana. Licha ya umri wake kuwa umeenda lakini bado ule ukakamavu wa kijeshi bado ulikuwepo katika damu yake.
Ni kweli alikuwa amedhibitiwa vilivyo na mwanadada yule anayejitambulisha kwa jina la Tz 11 lakini mwanaye alipoingia pale ndani mzee Bosco alijikaza na kujaribu kusema neno lakini haikuwezekana, alikuwa amevunjwa taya yake tayari, alijaribu kusema akaishia kutema damu tu!!
Ama! Damu nzito kuliko maji, Sofia hakuwahi kudhani kuwa ipo siku ataingiwa na huruma itakayompeleka katika kutokwa machozi, aliwahi kuhudhuria misiba mingi lakini hakuwahi kudondosha chozi, sasa anamtazama baba yake mzazi akiwa katika hali ile mbaya anajikuta akitokwa na machozi hasahasa alipomuona mzee Bosco akijaribu kuzungumza lakini akishindwa kabisa.
Sofia alijiongeza, akamsogelea baba yake ili kuona kama kuna lolote anaweza kupata kutoka kwake, wakati huo bunduki yake ikiwa sawia katika kiganja cha mkono wake.
Akainama na hapo mzee Bosco akaukaza mkono wake akachovya damu iliyokuwa imemtoka na kutapakaa sakafuni.
Baada ya kuichovya akajikokota pembeni kidogo hadi katika sakafu isiyokuwa na damu, akaushusha mkono wake ule uliokuwa na damu. Akajikaza kiume akaandika kwa kutumia ile damu aliyoichovya awali.
“TZ 11”
SOFIA akasoma aliyoandikiwa bila kuelewa lolote, mzee wake akamsihi kwa vitendo kuwa atoke nje.
Kuna mambo mengi ya kupuuza katika huu ulimwengu lakini linapokuja suala la nduguyo wa damu tena ambaye ni baba mzazi hapa unaweza ukajikuta ukipuuzia mambo mengi ambayo uliwahi kufundishwa huku ukisisitizwa kuyazingatia bila kujalisha u pamoja na nani.
Sofia alitambua wazi kuwa baba yake amekuwa mwanajeshi kwa miaka mingi na hata alipomwamuru atoke nje basi kuna kitu alikuwa anamaanisha, lakini unaanzaje kutoka nje na kumwacha babako mzazi akiwa anavuja damu huku taya ikimuanguka?
Sofia naye alikuwa muathirika wa hali hii ya kibinadamu, alisita kutoka akamfuata baba yake pale alipokuwa huku akiwa hajui ni kipi cha kufanya, alipofika paler mzee Bosco akajitutumua na kutokwa na teke dogo kwenda kwa mwanaye likampata katika mguu wake.
Sasa akili ya Sofia ikafunguka akatambua kuwa yeye si tabibu hata akibaki pale ndani ni kazi bure tu, alichotakiwa ni kuwaachia matabibu kazi yao na yeye aende kuitafuta maana ya Tz 11.
Akatoka upesi, akamkuta katibu muhtasi akiwa ameuvuta mdomo wake na kuzidi kuifanya ile sura yake isiyokuwa na mvuto kuwa mbaya zaidi.
“Upesi wasiliana na viongozi wako... mzee Bosco anatakiwa kupata tiba ya upesi sana..... nimekuamuru si ombi!!” alizungumza kwa kumaanisha. Macho yake makali yakaulainisha ule mdomo wa yule dada na kuurejesha katika hali ya kawaida kisha ukaingia katika mshangao!!
Sofia hakungoja jibu lolote, upesi akaenda hadi katika mgahawa, alipofika pale mgahawani akashangaa kuona watu wanakurupuka, ni hapo ndipo alipojitazama na kugundua kuwa bastola yake ilikuwa mkononi mwake na jinsi alivyoingia kwa kasi kubwa pale ndani basi ilikuwa si jambo geni hata kidogo kwa hali ile kutokea.
Upesi akaihifadhi ilebastola na kisha akaelekea katika meza aliyomuacha Pocha...
Pocha hakuwepo!!
Alimngoja kwa dakika tano zaidi lakini hakuonekana.
Hofu mpya ikatanda!!
Lakini hofu ile haikudumu sana, Pocha akarejea asijue kuwa Sofia anakabiliwa na tatizo jipya.
“Ulienda wapi Pocha na tuliagana kuwa unabaki hapa mpaka narejea?” Sofia alihoji kwa ukali.
“Kuna rafiki yako mmoja hapa nilikuwa nimemsindikiza hapo nje kidogo...”
“Rafiki? Nilisema nina rafiki huku?”
“Aah! Hapana iola kuna kitu ameniagiza kwako nikaona si vibaya nikimsindikiza walau nimjue kidogo tu....” alijitetea Pocha na kisha akaendelea kuzungumza huku akiona hasira ya Sofia waziwazi.
“Amesema amependa ulivyomuangalia.... neno lake hilo likanivuta zaidi kwake kujua kulikoni... nafsi yangu imejikuta tu!!.... na mwisho akasema ukija nikusalimie...”
“Pochaa! Unaongea sana niambie ni nani?”
“Tz 11” alijibu Pocha kwa uoga kiasi.
Jibu lile likamweka Sofia katika bumbuwazi... akakumbuka maneno ambayo aliandikiwa na mzee wake kwa kutumia damu, ni jina hilohilo....
Sasa Sofia akagundua kluwa Pocha analo jambo la muhimu zaidi ya alivyokuwa anajenga ghadhabu juu yake. Akamuhoji Pocha kwa utulivu juu ya huyo Tz 11.
Pocha akaelezea kuwa ni binti fulani mrembo tu halafu mdogomdogo.
Majibu ya Pocha yakamvuruga Sofia, binti mdogo mdogo anawezaje kumvunja taya mzee jasiri na imara kama Bosco.
Mtihani ukaanza kuwa mgumu, sasa haikuwa tena kwa usalama wa Pocha pekee bali kwa ajili ya baba yake.
Na hakuna aliyehitajika zaidi ya Tz 11.
Ni huyu ambaye angeweza kutoa majibu yote.
_____
TOFAUTI na nyakati nyingine ambazo familia ya Caro huwa na furaha sana pindi Caro anaporejea kutoka London kuja kuwasalimia, safari hii furaha haikuwa kubwa sana.
Kuna jambo ambalo lilikuwa linawatatiza na mwenye majibu alikuwa ni Caro peke yake, walipanga kuwa muda utafika na watamuuliza ni kitu gani ambacho muheshimiwa Lucas huwa anaenda kufanya uingereza. Na wakati huo walikuwa wamejiandaa kumuuliza iwapo anaifahamu nambari ya simu ile ambayo ilitumika kuzungumza na mama Caro kisha kumweleza juu ya muheshimiwa.
Mpasuko uliokuwepo haukuwa mdogo, Edwin rafiki yake Lucas na mume halali wa mama Caro alikuwa anahisi kuwa huenda mkewe alikuwa na mahusiano na Lucas nd’o maana akapigiwa simu ile na kuelezwa kuwa amekaa tu mwenzake anaenda London kufaidi maisha na binti mwingine.
Mama Caro alizipinga vikali shutuma zile na yeye akataja hisia zake kuwa yawezekana kabisa Mheshimiwa Lucas ana mahusiano na mtoto wake wa kike Caro!!
Hivyo ni neno la Caro ambalo lingeweza kurejesha amani katika nyumba hiyo.
Baada ya kupokea zawadi kadha wa kadha kutoka kwa Caro hatimaye wadogo zake caro na ndugu wengine waliwapisha watatu hawa sebuleni kwa kile ambacho baba caro alidai ni mazungumzo muhimu.
Walipobaki watatu, wasijue kabisa kuwa mchezo wanaotaka kuucheza tayari umechezwa kimataifa na matokeo yalikuwa wazi, wakajaribu kuucheza tena.
Baba Caro akamuuliza Caro ju ya maisha yake jijini London na ukaribu alionao na muheshimiwa.
Caro hakushtushwa na tuhuma zile kwani ni siku mzili zilizopita alizungumza na Lucas na kuamua nini hatma ya mahusiano yao, wakaamua kuwa yaendelee kuwa ya siri la ili kuondoa utata huo basi wauzunguke mbuyu na kuwachota akili wazazi wake.
Caro akatumia fursa ile kuumaliza mchezo kisayansi.
“Naishi vizuri sana na ninafanya kazi zangu kwa mafanikio, Mheshimiwa huwa tunaonana naye mara moja moja kuna muda anakuja London na hatuonani kabisa, kuna mfanyakazi mwenzangu aliniambia kuwa mheshimiwa ana mchumba wa kizungu maeneo ya jiji la Liverpool, hivyo huwa anakuja na kuishi pale. Ujue ninapoishi mimi na kufanya kazi ni mbali sana kutoka Liverpool, hivyo sikutilia maanani na hadi sasa sitaki kujishughulisha na mambo yake... ujue wanaume wote naona tabia yao moja tu, labda wewe tu babab yang undo siwezi kukusemea lakini pale London hii ni tabia mtu anakuwa na mke pale London halafu jijini Manchester ana familia nyingine... ila tafadhali sana sina uhakika na hizi tuhuma sitaki kuitwa ushahidi, sitaki kuchanganywa kabisa kwa sasa nipo na maisha yangu...” alijibu kwa kirefu akiwa ametulia kabisa.
Jibu lake liliupooza moyo wa mzee wake pamoja na kuutuliza kabisa mtima wa mama yake.
Majibu ya kupangwa yaliyofanyiwa mazoezi ya kutosha!!
Jibu likairejesha amani!
Hawakujua kabisa kuwa mtoto wao alikuwa akiwachezea shere!
_____
Baada ya kutoka katika mgahawa wa magereza Tz 11 alitoa taarifa kwa bosi wake wa Nairobi akamueleza kila kitu alichoelezwa na Luteni mstaafu Bosco.
Akamueleza kuwa Bosco alikuwa akimfuatilia Manfredy Gregory kwa sababu alienda pale gerezani kumuulizia Pocha!
Akaelezea zaidi kuwa hata Bosco mwenyewe hajui ni kwa nini Pocha anafuatiliwa.
“Ulifuatilia na kumjua Pocha ni nani?” alihoji mwanadada wa Nairobi.
“Haikuwa katika makubaliano yetu mkuu... hiyo ni biashara tofauti kabisa!” alijibu kikaidi Tz 11.
Mwadada wa Nairobi akatokwa na tusi zito kwa lugha ya kiingereza, kisha akamuuliza anahitaji kiasi gani ili aweze kuifanya kazi kikamilifu.
Tz 11 akaitaja bei yake, dada wa Nairobi akamwambia aende kufuatilia huyo Pocha ni nani na kwa nini anatafutwa na Manfredy Gregory ‘Chopa’.
Tz 11 akaingia kazini tena....
_____
Umbile la mwanadada aliyezengea zengea katika mgahawa wa magereza ulivutia macho ya yeyote yule anayependa kutazama.
Dada yule alichukua nafasi huku marashi yake nayo yakisumbua pua za wanusaji wengi katika namna ya kuvutia na si kukera.
Muhudumu alifika na kumsikiliza haja yake, akaeleza kuwa anahitaji maji baridi makubwa. Muhudumu akaomba pesa yule dada mrembo akalipia.
Mazingira yale hayakuwa mageni kwa mteja huyu ni muda mchache sana uliopita alikuwa ametoka kuhudumiwa.
Kwa jinsi alivyojiweka alijuwa waziwazi kuwa wanaomtazama kimatamanio ni wengi sana na yupo ambaye atapenda kujitoa muhanga kati ya wengi wale wanaomtamani.
Hata kabla hajamaliza kufikiria ni nani ambaye atajipeleka katika himaya yake, tayari aliisikia sauti ya kiume ikimuuliza iwapo wanaweza kuketi wote.
Dada yule akatabasamu vizuri huku akiyaruhusu meno yake mawili ya mbele kuonekana.
Yule bwana akaketi kindakindaki akijiona ndiye aliyebarikiwa kupita wateja wote.
Binti yle alimtazama kwa chati, akagundua kuwa alikuwa ameketi na askari wa kawaida kabisa katika ile meza.
Alijua kitakachofuata baada ya hapo ni kusifiwa kuwa yeye ni mrembo sana na mambo mengine kemkem ambayo aliyazoea tangiapo.
Maaskari kwa tamaa!!! Naji asiyejua....
Kweli akaanza kutoa sifa kedekede, binti yule naye akazipoe kwa utulivu, wakazungumza mengi huku yule binti naye akimsifia kuwa anafurahisha sana kuzungumza naye.
Bwana yule alikuwa anakwepa sanakujitambulisha kazi yake lakini hakujua kuwa yule binti tayari alikuwa anjua kila kitu licha ya kwamba alivaa nguo za kiraia.
“Yaani hapa kuna kaka yangu alikuwa anaendesha pikipiki jana akagonga kibanda cha mama mmoja hivi basi pikipiki yake imekamatwa ndo najiuliza atakuwa kituo kipi. Hapa ninamtafuta askari mmoja hivi anisaidie....” binti alimueleza yule bwana.
“Unamjua kwa cheo chake au majina kama unajua jina lake nambie maana mimi hapa ni mzoefu sana nawajua watu....” alijibu akiendelea kuficha kazi yake katika namna ya kizembe.
“Dah! Kaka yaani hapa ni kama vile natwanga maji kwenye kinu, hata nikiomba kusaidiwa naona maelezo yangu hayajitoshelezi kabisa...” alijibu yule dada akionyesha kukata tamaa.
“We sema tu dada, huwezi kujua labda hata unanitafuta mimi hapa..” alisema yule bwana.
“Kwani na wewe ni askari?” mwanadada alimuuliza huku akionyesha kushangaa, yule bwana akafadhaika kuwa janja yake ilikuwa imefikia ukingoni ikabidi akiri tu nkuwa hiyo ndiyo kazi yake.
“Sawa basi mimi namtafuta mtoto wa luteni nani sijui.. Bosco eeh! Luteni Bosco nimeambiwa huku nd’o naweza kumpata yaani nikimpata huyo naamini kaka yangu atatoka maana nimesoma naye shule moja ya sekondari na kiukweli hapa mjini bila kujuana..... utaishia kulia kila siku.” Alijieleza kwa utulivu.
Yule askari akaguna kisha akafikiri kwa muda kiasi.
“We unamfahamu mtoto wake ukimuona?” askari akamuuliza.
“Hata ikiwa usiu wa manane nitamjua yule binti...” alijibu kisha akatabasamu.
“Dah! Hapa dada labda tu mimi niangalie uwezekanowa kukusaidia lakini kama ni ishu ya Luteni Bosco kuna tatizo alipatwa presha ikawa imepanda amepelekwa hospitali hapo Muhimbili na bila shaka watoto wake wote watakuwa hukohuko....” alijibu kwa sauti ya chini.
Yule dada akatoa maelezo ya uongo kabuisa juu ya huyo kaka yake aliyekamatiwa pikipiki, kisha akampatia ile namba ya simu yule askari ikiwa kuna lolote basi ampe taarifa.
Ilikuwa ni ndoto ya mchana askari yule kuipata namba ya dada yule mrembo.
Lakini ilikuwa ushindi mkubwa zaidi kwa yule mwanadada kwa kufahamu fika kuwa mzee Bosco amekimbizwa Muhimbili na mtoto wake atakuwa hukohuko.
“samahani jina nisevu nani” askari alimuuliza.
“NIchagulie lolote tu.. lakini ukikosa kabisa nisevu TZ 11” alimaliza kujibu huku akiwa amempa mgongo yule askari.
Akatoweka pale na sasa alikuwa nauhakika wa kumfahamu Pocha kupitia mtoto wa luteni Bosco.
Hakuwa akijua kabisa kama Sofia ndiye mtoto wa luteni. Hivyo alitarajia wepesi kabisa katika kuufanikisha mchezo wake.
______
KITENDO cha kuambiwa na Pocha kuwa kuna mwanadada ametuma ujumbe kuwa amependa macho yake jinsi alivyomuangalia, ujumbe huu ulikuwa na maana ya kawaida kabisa kwa Pocha ambaye hakuna kitu alichokuywa akikijua, na mwanadamu yeyote yule wa kawaida angeweza kuutafsiri ujumbe huu moja kwa moja vilevile, lakini kwa mwanadamu asiyekuwa wa kawaida huu ulikuwa ujumbe mzito sana.
Naam! Sofia naye hakuwa mwanadamu wa kawaida!
Aliielewa maana ya mtu wa kariba yake kusema ameyapenda macho yake, hii ilimaanisha kuwa mtu huyo amemtambua ujuzi alionao na anatamani wakabiliane.
Sasa baada ya kukabiliana na wahalifu nchini uingereza alipokuwa katika masomo kwa vitendo hili linakuwa jaribio la kwanza kabisa kwa mwanafunzi huyu aliyebobea katika mamabo ya upelelezi wa kimataifa na mapigano ya aina zote, aidha kutumia silaha ama la!!
Kuanzia alipopewa taarifa ile na Pocha aliongeza umakini huku akizifuata kanuni zote zlizofundishwa kambini na zile alizojifunza kulingana na matukio aliyokuwa ameyapitia.
Macho ya yule binti waliyetazamana naye ndicho kitu pekee alichokuwa anakikumbuka ili kumtambua adui yake, zaidi ya hapo hakuwa akikumbuka kitu kingine hivyo umakini wake mkubwa kabisa aliutilia katika kuyatazama macho ya raia anaopishana nao, zaidi ya yote alijitahidi wasitambue ikiwa alikuwa anawatazama.
ANMA KWA HAKIKA kila mjanja ana mjanja wake, na pale wanapojikuta ulingoni wajanja wawili basi mjanja mmoja anatakiwa kubuni ujanja wa ziada ili aweze kumshindwa mjanja mwenzake.
Wakati Sofia anawatazama machoni watu ili aweze kumbaini huyo binti wa kutisha anayejiita Tz 11, yeye Tz 11 alikuwa ameyafunika macho yake miwani kubwa ya jua yenye mahadhi ya kike.
Hakufanya hivi kutokana na kwenda na wakati japokuwa alikuwa amependeza, alifanya hivi ili kujiweka katika uhalisia usiokuwa wake kwa wale ambao labda waliwahi kuonana naye kabla ya tukio lolote lile.
Hadi anafika pale Muhimbili alikuwa ameyaziba macho yake, alipita jirani kabisa na Sofia aliyekuwa makini kutazama macho ya watu ili ajue nani hatari kwake.
Maskini Sofia alikuwa amezidiwa ujanja, Tz 11 akaingia moja kwa moja hadi mapokezi. Hapo alihitaji kujua ni wapi alipolazwa mzee Bosco.
Lengo kuu likiwa kumuona mtoto wake ambaye ndiye anayefahamu juu ya Pocha!!
_____